Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Sare ya Man City yaamua bingwa EPL? Arsenal wacheka, Dowman aking'ara
Mbio za ubingwa wa Ligi kuu ya England (EPL) zimechukua mwelekeo mpya baada ya Manchester City kulazimishwa sare ya 1-1 na West Ham United katika Uwanja wa London Stadium. Matokeo hayo yanaiacha City ikiwa nyuma kwa alama tisa dhidi ya vinara Arsenal, huku ikiwa bado na mchezo mmoja mkononi.
Sare hiyo imeongeza shinikizo kwa kikosi cha kocha Pep Guardiola, ambaye alikiri kabla ya mechi kwamba kupoteza alama katika mchezo huo kungefanya mbio za ubingwa kuwa ngumu zaidi. Licha ya kutangulia kufunga kupitia Bernardo Silva, City walishindwa kulinda ushindi wao baada ya beki Konstantinos Mavropanos, nyota wa zamani wa arsenal, kusawazisha kwa kichwa kufuatia kona ya Jarrod Bowen.
Wakati huo huo, ushindi wa Arsenal dhidi ya Everton uliwapa washinda bunduki alama muhimu tatu na kuongeza pengo kubwa kileleni mwa msimamo. Mchezaji chipukizi mwenye umri wa miaka 16, Max Dowman, aliibuka shujaa wa mechi hiyo kwa bao la kihistoria lililowapa Arsenal ushindi muhimu na kuongeza matumaini yao ya kutwaa taji.
Kwa muda mrefu, City wamekuwa wakijulikana kwa uwezo wao wa kushinda mfululizo hasa katika mechi za mwishoni mwa msimu na kuwafikia wapinzani wao kileleni. Lakini safari hii dalili zinaonyesha kuwa kazi hiyo inaweza kuwa ngumu zaidi.
Katika mechi dhidi ya West Ham, City walitawala mpira kwa muda mwingi lakini walionekana kukosa makali katika eneo la mwisho. Bao la Bernardo Silva lilionekana kuwa mwanzo wa ushindi uliotarajiwa, lakini kosa moja katika ulinzi lilitoa nafasi kwa Mavropanos kusawazisha.
Matokeo hayo yanaacha maswali mengi kuhusu uwezo wa City kama inaweza kushinda mfululizo na kuwafikia Arsenal.
Guardiola alijaribu kupunguza presha baada ya mchezo, akisema mbio za ubingwa bado hazijaisha kwa sababu timu yake haikupoteza mechi hiyo. Hata hivyo, pengo la alama tisa linaonekana kuwa kikwazo kikubwa kwa mabingwa hao wa zamani.
"Bado haijaisha, hatujafungwa, tutaendelea kupambana", anasema Guardiola
Kwa West Ham, sare dhidi ya City ilikuwa kama ushindi.
Matokeo hayo yamewaondoa kwenye eneo la kushuka daraja kwa mara ya kwanza tangu Disemba, na kuipa timu hiyo nguvu mpya katika vita vya kubaki kwenye ligi.
Mabeki wao waliokuwa imara na ujasiri kama Mavropanos uliwafanya kustahimili mashambulizi mengi ya City.
Katika mbio za kuepuka kushuka daraja, ushindi au sare kama hii mara ni muhimu sana.
Dowman aibeba Arsenal akiweka rekodi
City wakiendelea kusuasua katika mechi ya pili sasa ya ligi wakitoka sare, Arsenal wanaonekana kupata nguvu mpya kupitia kizazi kipya chenye vipaji.
Max Dowman aliingia uwanjani dakika za mwisho dhidi ya Everton na kugeuza kabisa mwelekeo wa mchezo. Baada ya kipa Jordan Pickford kwenda kwenye lango la Arsenal kutaka kufunga kona, chipukizi huyo alikimbia umbali mrefu wa uwanja, akiwapita mabeki wawili kabla ya kufunga kwa utulivu bao la pili.
Bao hilo lilizua shangwe kubwa miongoni mwa mashabiki na wachezaji wa Arsenal, huku wengi wakiliona kama tukio linaloweza kuamua hatima ya msimu wao.
Kwa klabu ambayo haijashinda taji la ligi kwa zaidi ya miongo miwili, wakati huo unaweza kuwa chanzo cha imani mpya katika mbio za ubingwa.
Kinda huo mwenye miaka 16, amevunja rekodi ya mchezaji mdogo zaidi kufunga bao katika ligi hiyo kubwa na maarufu duniani. Goli lake dhidi ya Everton amelifunga akiwa na umri wa miaka 16 na siku 73.
Kabla yake rekodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na James Vaughan, aliyoiweka mwaka 2005 alipokuwa akiichezea Everton alipofunga bao dhidi ya Crystal Palace akiwa na miaka 16 na siku 270. Nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji wenye umri mdogo zaidi inashikiliwa na James Milner wa Leeds United aliyefunga mwaka 2002 akiwa na miaka 16 na siku 356, akifuatiwa na Wayne Rooney wa Everton aliyefunga akiwa na miaka 16 na siku 360, huku nafasi ya tano ikishikiliwa na Rio Ngumoha wa Liverpool aliyefunga akiwa na miaka 16 na siku 361.
Kwa sasa, Arsenal sasa ubingwa uko mikononi mwao kama watashinda mechi 5 zijazo ikiwemo dhidi ya City, itawafanya kufikisha alama 85. City hata akishinda michezo yake yote mingine (7) ukiondoa dhidi ya Arsenal atafikisha alama 82.
Hata hivyo kwa Manchester City, bado kuna matumaini kutokana na historia yake, lakini njia ya kurudi kileleni imekuwa ngumu zaidi kuliko ilivyotarajiwa.
Chelsea imeanza kupoteza muelekeo?
Kwa upande wa Chelsea, changamoto ilionekana wazi walipokutana na Newcastle.
Chini ya kocha Liam Rosenior, Chelsea wamekuwa wakionekana kuvutia wakicheza soka la kushambulia lenye kasi. Hata hivyo, Newcastle waliwazuia kwa nidhamu kali ya ulinzi na kuwalazimisha kutafuta mbinu nyingine.
Tatizo lilikuwa wazi: wakati mpango wao wa kwanza haukufanya kazi, hakukuwa na mpango mwingine wa pili wa kuvunja ukuta wa wapinzani. Wengi wameanza kujiuliza, imeanza kupoteza muelekeo?