Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
HPV: "Ningepoteza ulimi wangu au hata kufa"
- Author, Leigh Boobyer
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Baba wa watoto wawili karibu apoteze ulimi wake baada ya uvimbe chini ya taya yake kubainika kuwa ni saratani.
Anthony Perriam alimuona daktari baada ya kuhisi uvimbe kwa mara ya kwanza na ndani ya wiki kadhaa akagunduliwa na saratani inayohusiana na Virusi vya Papilloma vya Binadamu (HPV) kichwani na shingoni.
HPV ni kundi la virusi vinavyoathiri ngozi, na kwa kawaida havisababishi matatizo kwa watu wengi lakini kuna aina ya virusi vinaweza kusababisha saratani au vidonda vya sehemu za siri.
Anthony anasema: "Ninajiona mwenye bahati kwamba bado naweza kula na kuzungumza, lakini kama ningeiacha, ningepoteza ulimi wangu au hata kufa."
Kwa kawaida HPV haoneshi dalili zozote, kulingana na Huduma ya Afya ya Uingereza (NHS).
Lakini baadhi ya virusi vinaweza kusababisha vidonda vya sehemu za siri, au mabadiliko yasiyo ya kawaida katika seli ambazo zinaweza kukua na kuwa saratani - mara nyingi saratani ya kichwa na shingo kwa wanaume na saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake.
Chanjo inapendekezwa kwa watoto wa miaka 12 na 13 na watu walio katika hatari kubwa ya kupata HPV.
"Ukipata uvimbe, hata kama hauumi, chunguza," anasema.
"Aina hii ya saratani haizungumzwi vya kutosha, hasa miongoni mwa wanaume. Lakini kupima huokoa maisha."
Licha ya kutokuwa na dalili zozote, CT scan, biopsy na MRI zilithibitisha ugonjwa huo Machi 2023.
"Nilikuwa na mtoto wa miaka mitatu na mwingine wa miaka sita wakati huo. Wazo langu la kwanza halikuwa kuhusu mimi, lilikuwa kuhusu wao. Nilikuwa na wasiwasi sana kuhusu wao," anasema kijana huyo mwenye umri wa miaka 41 sasa.
Anthony aliondolewa uvimbe 44 shingoni mwake, na uvimbe mkubwa zaidi chini ya ulimi wake uliondolewa kwa kutumia upasuaji wa roboti.
"Waliniambia opereseheni imefanyika wakati unaofaa," anasema.
"Moja ya uvimbe ulikuwa karibu kupasuka. Kama ugeendelea zaidi, ingeweza kuenea."
Tiba
Tiba ya mionzi ilikuwa ngumu, na Anthony alipungua uzito wa kilo 22 (pauni 48.5).
"Mate yangu yote yalipotea," anasema.
"Hata kunywa ilikuwa vigumu, kwani kila kitu kiligeuka kuwa unga mdomoni mwangu."
"Nilikuwa dhaifu sana kiasi kwamba nilihitaji kiti cha magurudumu."
Anasema: "Kusukumwa kwenye kiti cha magurudumu kwenye korido na kuingia kwenye tiba ya mionzi kulianza kuathiri afya yangu ya akili.
"Lakini familia yangu ilinipa motisha ya kuvumilia na nilitaka kuishi hadi nifikishe miaka 40."
Virusi vya HPV ni nini?
Virusi vya HPV huathiri ngozi na kuna zaidi ya aina 100.
Inaweza kuambukizwa kutokana na kugusana ngozi na ngozi kwenye eneo la uzazi, kama uke, sehemu ya nyuma, mdomo, na kutumia vinyago vya ngono kwa pamoja.
Chanjo hutolewa na inafanya kazi vizuri zaidi inapotolewa kwa watoto wa miaka 12 na 13.
Hospitali ya Chuo Kikuu cha Wales inasema chanjo hiyo imepunguza viwango vya saratani ya shingo ya kizazi kwa karibu 90% kwa wanawake walio katika umri wa miaka 20 tangu ilipoanzishwa mwaka 2008.
Chanjo ya HPV inatumika duniani kote kwa miaka mingi, ni salama na yenye ufanisi, na ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa chanjo nchini Wales.
Inawasaidia wavulana na wasichana kuwa na afya njema, inazuia saratani inayohusiana na HPV na inaimarisha afya ya umma kwa ujumla."