Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ubingwa wa mezani kwa Morocco ni 'aibu kwa Afrika'
Hasira na mshangao vimetawala baada ya Shirikisho la Soka Afrika kuipa Morocco ubingwa wa AFCON 2025 mezani, ikibatilisha matokeo ya uwanjani, huku Senegal ikipanga kukata rufaa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
Shirikisho la soka la Senegal limesema uamuzi huo ni "aibu kwa Afrika", likisisitiza kuwa halikubaliani na hatua ya kubatilishwa kwa matokeo ya fainali hiyo iliyochezwa Januari 18 mjini Rabat. Katibu mkuu wa shirikisho hilo alitoa kauli hiyo katika mahojiano na kituo cha taifa cha Radiodiffusion Télévision Sénégalaise.
Wakati viongozi wakichukua hatua za kisheria, baadhi ya nyota wa Senegal wanaocheza Ligi Kuu England hawakusita kuonyesha hisia zao hadharani. Wachezaji akiwemo Diouf wa West Ham, Ismaila Sarr wa Crystal Palace na Habib Diarra wa Sunderland walichapisha 'emoji' za kucheka kwenye mtandao wa Instagram, wakiweka na picha zao wakishangilia ubingwa wa AFCON, hatua iliyoonekana kama kejeli kwa uamuzi wa CAF.
Kwa upande wake, shirikisho la soka la Morocco lilipokea kwa furaha uamuzi huo, likisema rufaa yao imezaa matunda na haki imetendeka baada ya kile walichodai kuwa ukiukwaji wa kanuni wakati wa fainali.
Nini kilitokea siku ya fainali?
Fainali hiyoiliyopigwa Rabat, Morocco mwezi Januari, iligubikwa na utata mkubwa baada ya wachezaji wa Senegal kususia kuendelea kucheza wakipinga maamuzi ya mwamuzi, ikiwemo penati ya dakika za mwisho kwa Morocco wakati matokeo yakiwa 0-0.
Wachezaji hao walitoka uwanjani na kusababisha mchezo kusimama kwa takribani dakika 17 huku hali ya taharuki ikitawala.
Baadaye walirejea kucheza baada ya kushawishiwa na nyota wa Senegal Sadio Mane, huku penati ya Morocco ikipanguliwa na kipa Edouard Mendy kabla ya Senegal kufunga bao la ushindi kupitia Pape Gueye katika muda wa nyongeza na kutwaa ubingwa uwanjani.
Hata hivyo, tukio la kususa ndilo lililokuja kuwa msingi wa rufaa ya Morocco na hatimaye kubadilishwa kabisa matokeo ya mchezo huo.
Uamuzi umeacha maswali mengi kuliko majibu
Uamuzi wa CAF umeibua mjadala mpana na maswali mengi kuhusu hatima ya fainali hiyo. Mchambuzi wa michezo Rob Harris wa Sky Sport amesema hatua hiyo ni ya "kushangaza sana" na haijawahi kushuhudiwa katika soka la kiwango kikubwa kama hicho. Kuna karibu maswali kumi kuhusu uamuzi huu wa CAF.
"Senegal bado wanaendelea kusherehekea ubingwa wao. Nini kitatokea kwa medali walizopewa? Watatakiwa kuzirejesha? Na je, watakubali kuzirejesha?" alihoji.
Aliongeza kuwa hata suala la kombe lenyewe linazua sintofahamu: "Itakuwaje kuhusu kombe? Liko wapi sasa, na nani anapaswa kulimiliki?"
Zaidi ya hapo, Harris aligusia athari pana zaidi, ikiwemo kwa waliobashiri (betting). "Kama uliweka dau kwa Senegal na tayari umelipwa, itakuwaje? Na wale walioweka kwa Morocco, je sasa wanadai ushindi wao?", anahoji.
Amesisitiza kuwa tukio hilo lina athari kubwa kuliko matokeo ya uwanjani pekee, akisema: "Hili ni tukio la kipekee kabisa. Fainali imechezwa, matokeo yamepatikana, medali zikatolewa, halafu baada ya siku 58 tunaambiwa yasahau yote, Morocco ndio washindi kwa mabao 3-0."
Uamuzi huo sasa unaacha doa na mjadala mkubwa katika soka la Afrika, huku wengi wakisubiri kuona hatima ya rufaa ya Senegal na iwapo uamuzi huo utabaki au kubadilishwa tena.
Taarifa hii inatokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo Skysport