Mambo manne yanayoweza kutokea katika mzozo wa Marekani na Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Saeed Jaafari
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Inaaminika kuwa Marekani iko kwenye duru ya pili ya mazungumzo ya kusitisha mapigano na Iran, huku ujumbe kutoka Pakistan ukiwasili katika mji mkuu wa Iran, Tehran.
Usitishaji mapigano, ambao umedumu kwa wiki mbili, bado upo baada ya zaidi ya saa 20 za mazungumzo kati ya Marekani na Iran yaliyoandaliwa na Pakistan ambayo yalimalizika Jumapili bila maendeleo yoyote.
Baada ya kushindwa mazungumzo ya awali, Rais Donald Trump alitangaza kile alichokiita mkakati mpya dhidi ya Iran, wa kuzuia meli za Iran kuingia na kutoka katika bandari zake kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya maji kwa biashara ya mafuta ya kimataifa.
Kurudi Vitani

Chanzo cha picha, Getty Images
Aprili 8, Iran na Marekani zilikubaliana kusitisha mapigano kwa wiki mbili baada ya majuma kadhaa ya mapigano.
Tofauti katika tafsiri ya vifungu vya makubaliano ya kusitisha mapigano, zimewafanya baadhi ya waangalizi kuona makubaliano hayo ni njia ya kusitisha tu vita kwa muda na sio makubaliano endelevu ya kuacha kabisa kupigana.
"Nafasi ya kufikia makubaliano ilikuwa haipo tangu mwanzo mzozo ulipoanza," anasema Behnam Ben Taleblu, mtafiti katika Taasisi ya fikra tunduizi ya Foundation for Defense of Democracies, yenye makao yake makuu Washingto
Wakati huo huo, kauli zinazokinzana kutoka kwa maafisa wa pande zote mbili zimezidisha hali hiyo kuwa mbaya.
Ingawa maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu wanazungumzia ukiukwaji wa mara kwa mara wa mpango wa kusitisha mapigano, Marekani na Israeli hazitoi maelezo mengi kuhusu ahadi zao.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tofauti hii katika mazungumzo imeongeza kutoaminiana na kutilia shaka uimara wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Ikiwa juhudi za kurudi kwenye meza ya mazungumzo hazitaleta matokeo chanya, usitishwaji huu wa mapigano utakuwa tu ni njia ya kupumzika, kuruhusu pande hizo kupona, kujipanga upya, kutathmini upya nafasi zao, na kujiandaa kwa awamu inayofuata ya vita.
Marekani inaweza kuanza kushambulia miundombinu muhimu kama vile mitambo ya umeme, madaraja, au vifaa vya nishati na Iran itajibu mashambulizi haya.
Wakati huo huo, Israel, inaweza kutumia mbinu ya mauaji ya watu mashuhuri.
Hamid Reza Azizi, mtafiti juu ya mahusiano ya kimataifa, anasema: "Israel inaweza kutekeleza mauaji ya watu binafsi na watu mashuhuri wa Iran, wakiwemo wale waliohusika katika mazungumzo hayo."
Anasema "sera iliyotangazwa ya Donald Trump ya kuziba Mlango-Bahari wa Hormuz inaongeza hatari ya makabiliano, hata kama pande hizo hazikusudii."
Kurudi vitani kutaleta athari za kiuchumi na kusababisha mzozo mpana wa kikanda na shinikizo la kiuchumi duniani, kufanya hali iwe ngumu zaidi.
Mashambulizi ya Wastani

Chanzo cha picha, Getty Images
Jengine linaloweza kutokea ni kurudi kwenye aina ya mapambano ambayo yanaweza kuelezewa kama "mapambano yasiyo makali".
Hii ina maana kwamba mzozo unaweza usifikie kiwango cha vita kamili, na pande zote zinaweza kuchukua hatua za kijeshi, ambazo zinaweza kujumuisha kuendelea na mashambulizi machache dhidi ya miundombinu, malengo ya kijeshi, au hata njia za usambazaji.
Kuongezeka kwa shughuli za makundi yanayounga mkono Irani nchini Iraq au Bahari ya Shamu, kunaweza kupanua wigo wa kijiografia wa mzozo huo.
Hamid Reza Azizi anasema, "Pande zote mbili zinataka kutumia mbinu zao za kutoa shinikizo ili kuushawishi upande mwingine bila kuingia katika vita kamili."
Anasema: "Ikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano yatavunjika, kwa upande wa Iran ina uwezekano wa kuchukua hatua kupitia vikosi vyake vya washirika, haswa nchini Yemen."
Muendelezo wa diplomasia

Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya kushindwa kwa mazungumzo nchini Pakistani, bado haiwezekani kuhitimisha kwamba diplomasia haiwezekani au mapatano hayawezekani.
Pakistan, ikiwa nchi mwenyeji wa mazungumzo haya, huenda ikaendelea na juhudi zake katika siku zijazo za kuhimiza Tehran na Washington kufikia makubaliano.
Wakati huo huo, baadhi ya wapatanishi wa muda mrefu, kama vile Qatar, Oman, na hata Saudi Arabia na Misri, wanaweza kuanza kufanya kazi kujaribu kuzuia kuongezeka kwa mgogoro huo.
Hata hivyo, jambo muhimu ni kwamba maendeleo yoyote katika mazungumzo yao, yanategemea kupunguza mapengo kati ya pande hizo mbili.
Pendekezo la Marekani lenye vipengele 15 na pendekezo la Iran la vipengele 10 linaonyesha kwamba pande zote mbili bado zinatoa kipaumble kufanya mazungumzo kwa kuzingatia misimamo yao badala ya kutafuta yale wanayokubaliana.
Kwa hivyo, ingawa duru mpya ya mazungumzo inawezekana, kutarajia makubaliano ya haraka na makubwa ni jambo gumu kwa sasa.
Kuendelea kwa Vizuizi

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani alitangaza kwamba jeshi la majini la nchi yake linakusudia kuweka kizuizi cha majini dhidi ya Iran, kuzuia meli za kiraia au meli za mafuta kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Pia alitishia kuzuia meli zozote zinazolipa ada ya usafiri kwa Iran katika maji ya kimataifa ili kuvuka mlangobahari huo, mkakati unaoonekana kulenga kuizuia Iran kupata mapato ya mafuta, kuunyonga uchumi wake, na wakati huo huo kuiathiri China, mshindani muhimu zaidi wa Marekani, ambaye ndiye mnunuzi mkuu wa mafuta ya Iran.
Behnam Ben Taleblu, kutoka Taasisi ya Ulinzi wa Demokrasia, anasema "kuziba bandari za Jamhuri ya Kiislamu kunaweza kuwa na ufanisi mkubwa, ikiwa rasilimali za kutosha zitatengwa kwa ajili ya ujasusi, ufuatiliaji na upelelezi."
Anaongeza: "Matokeo halisi ya hatua hiyo itakuwa ni kuinyima serikali ya Iran uwezo wake wa kuuza nje bidhaa yake kuu."
Lakini wachambuzi wengine wanasema kuna gharama kubwa kwa Marekani kutekeleza mpango huo, na kuviweka vikosi vyake vya kijeshi karibu na Iran na kutavifanya iwe katika hatari zaidi ya kushambuliwa.
Zaidi ya hayo, ili mpango huo uwe na ufanisi, vikosi vya majini vitalazimika kuendelea kuwepo karibu na mipaka ya Iran kwa muda mrefu, jambo ambalo lina gharama sana.
Kuendelea na sera kama hiyo kunaweza pia kusababisha bei ya juu ya mafuta na nishati duniani, huku uwezekano mkubwa wa Wahouthi kuingilia kati kuvuruga Mlango-Bab al-Mandab, na kuongeza bei ya mafuta zaidi.
Bila shaka inaonekana kwamba Iran na Marekani zimeingia katika awamu ambayo vita na mazungumzo yanaendelea kwa wakati mmoja, huku pande zote mbili zikiendelea kutegemea jeshi huku njia za kidiplomasia zikiwa wazi kwa kiasi fulani.















