Baada ya Rostam Aziz kununua NMG: je uhuru wa habari upo shakani?

    • Author, Wycliffe Muia
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Baada ya tajiri wa Tanzania, Rostam Aziz, kununua hisa nyingi za Kampuni ya Nation Media Group – kampuni kubwa zaidi ya vyombo vya habari Afrika Mashariki, wanasiasa, waandishi na wachambuzi wameonyesha wasiwasi wao kuhusu uhuru wa waandishi wa habari na uhuru wa habari kw aujumla katika kanda hiyo.

Kila siku, mamilioni ya Wakenya, Watanzania, Waganda na Wanyarwanda hutegemea magazeti, vituo vya televisheni, redio na mitandao ya kidijitali iliyo chini ya NMG kupata habari za kuaminika.

Magazeti kama Daily Nation, Mwananchi na Daily Monitor yamejijengea sifa ya kutoa habari huru, hasa katika nchi ambazo waandishi wanakabiliwa na shinikizo la kisiasa.

Kwa ujumla nchini Tanzania, inamiliki Mwananchi Communications Limited, inayochapisha magazeti ya The Citizen, Mwananchi na Mwanaspoti.

Uganda, inamiliki Monitor Publications Limited, inayochapisha gazeti la Daily Monitor. Nchini Kenya, NMG inachapisha magazeti kadhaa yakiwemo Daily Nation, Business Daily, The EastAfrican na Taifa Leo, pamoja na kuendesha vituo vya televisheni na redio kama NTV Kenya, NTV Uganda, KFM na Nation FM.

Kupitia magazeti, televisheni, redio na majukwaa ya kidijitali, NMG imekua kuwa moja ya kampuni kubwa zaidi za vyombo vya habari binafsi katika eneo la Afrika Mashariki.

Lakini sasa NMG amekuja mmiliki mpya mwenye hisa nyingi, mfanyabiashara na bilionea, Rostam Aziz.

Rostam Aziz, aliyewahi kutajwa na Forbes kama tajiri namba moja Tanzania mwaka 2013, alitangaza kwamba kampuni yake ya Taarifa Ltd, imenunua 54% ya hisa za NMG. Makubaliano haya bado yanahitaji pia idhini ya Mamkala za udhibiti wa vyombo vya habari katika nchi husika.

Rostam Aziz alikuwa Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ana uhusiano mkubwa na viongozi wa kisiasa kanda nzima, jambo ambalo limeibua hofu kuwa anaweza kuingilia maamuzi ya kiuhariri katika kampuni hiyo ya NMG.

Hata hivyo, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Nairobi, tajiri huyo mwenye umri wa 65 alisisitiza na kuunga mkono "uhandishi wa kuaminika na ulio huru" na kuongeza kuwa ushirikiano huu utaendelea kulinda ubora wa kiuhariri na heshima ya taasisi.

NMG, iliyoanzishwa mwaka 1959 na Aga Khan, imejijengea sifa ya kudumisha uhuru wa kiuhariri hata katika nyakati zenye ghasia za kisiasa katika ukanda huo wa Afrika mashariki. Uamuzi wa Aga Khan Fund for Economic Development (Akfed) kuuza kampuni hiyo ulijitokeza baada ya mapitio ya uwekezaji wake na kuamua kuzingatia sekta nyingine.

Wanasiasa na waandishi kama Churchill Otieno, rais wa sasa wa Africa Editors Forum, wamesema mabadiliko ya umiliki yameibua maswali makubwa: "Suala kubwa si nani ananunua, bali ni namna ya kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari baada ya mabadiliko haya," aliandika kwenye mtandao wa LinkedIn.

Hata kama Aziz ameahidi kudumisha uhuru wa kiuhariri, uhusiano wake na viongozi wa kisiasa, ikiwemo Rais wa Kenya William Ruto, au chama tawala cha CCM huko Tanzania, unaleta hofu kwamba vyombo vya NMG vinaweza kushawishiwa kisiasa.

Aziz amekuwa karibu na Rais Ruto kupitia uwekezaji mkubwa katika nishati, ikiwa ni pamoja na kufungua kampuni ya gesi (Taifa Gas plant) huko Mombasa mwaka 2023.

Kwa kuwa Ruto anataka kuchaguliwa tena kuwa rais mwaka ujao, Wakenya wengi watafuatilia kwa makini kuona kama Daily Nation au vyombo vingine vya NMG vitambeba kisiasa.

"Yeye ni mtu aliyejijengea sifa, anajulikana sana na ana nguvu kubwa," alisema Asha Abinallah, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya teknolojia na vyombo vya habari Tech and Media Convergency iliyoko Tanzania, akizungumza na BBC.

Aliongeza kuwa kuna uwezekano kwamba vyombo vya NMG vinaweza kuungana na sera za serikali za Kenya na Tanzania sasa baada ya Aziz kuinunua na kuwa mmiliki mkubwa.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari, tajiri huyo alikanusha mashaka hayo kwa nguvu, akisisitiza kuwa ununuzi wa NMG ni uwekezaji wa kibiashara tu na wa kimkakati unaolenga kuendeleza uboreshaji wa vyombo vya habari.

Alisema Ruto si kiongozi wa kwanza wa Kenya aliyekuwa karibu naye, na alitaja urafiki wake pia na Rais wa zamani Uhuru Kenyatta, pamoja na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, aliyefariki Oktoba iliyopita.

"Ninaamini katika mahusiano. Hayo ni mahusiano binafsi, hayahusiani na masuala ya kibiashara," alisema Aziz.

"Nina uhusiano wa karibu na viongozi wa Zambia, nina uhusiano wa karibu na viongozi wa Uganda na nina uhusiano wa karibu na viongozi kanda nzima."

Aziz pia anachukuliwa kwa ukubwa kuwa na uhusiano wa karibu na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa zamani Jakaya Kikwete, wote kutoka chama cha CCM ambacho yeye aliwahi kuwa Mbunge.

Wachambuzi wanasema kuwa uhusiano wa aina hii umeisaidia biashara zake kukua katika nchi za Afrika Mashariki.

Rostam Aziz alizaliwa mwaka 1960 magharibi mwa Tanzania katika familia iliyohamia huko kutoka eneo la sasa la Iran zaidi ya karne moja iliyopita. Alisoma Sekondari nchini Tanzania kabla ya kuendelea na masomo ya uchumi katika Chuo kikuu nchini Uingereza. Baada ya kumaliza, alirudi Tanzania na kuanza kujipatia kipato kupitia biashara, kisha kupanua himaya yake ya biashara kwenye sekta za mawasiliano, madini na nishati.

Ingawa NMG inakabiliwa na changamoto za kibiashara kutokana na kupungua kwa mapato ya magazeti na mabadiliko ya kidijitali, Aziz si mgeni kwenye sekta ya habari. Katika miaka ya 1990, alishirikiana na wadau wwengine kuanzisha Mwananchi Communications, ambayo ilikuwa inachapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, kabla ya kampuni hiyo kununuliwa na NMG. Mwaka 2006, alinunua kampuni nyingine ya vyombo vya habari, Habari Corporation, iliyofungwa mwaka 2020 kutokana na changamoto za kibiashara.

Aziz ameahidi kudumisha uhuru wa kiuhariri wa NMG huku akiwekeza kuhakikisha kampuni inafanikiwa. Wakati baadhi ya wachambuzi wanafuatilia kuona kama ataweza kutimiza ahadi hiyo, wawekezaji wa hisa wameonyesha imani: hisa za NMG zilipanda kwa 28.3% ndani ya siku mbili, zikifikia kiwango cha juu zaidi katika miaka miwili iliyopita. Aziz pia ameahidi kuongeza uwekezaji katika mifumo ya kidijitali ya NMG ili kukidhi mabadiliko ya matumizi ya habari.

Keith Mwau, mtaalamu wa uchumi, alisema: "Kwa kampuni iliyokabiliwa na kupungua kwa mapato na wimbi la ukuaji wa kidijitali, ahadi hii ya uwekezaji ina uzito mkubwa."