Kisa nadra cha mwanamke aliyepata ujauzito wa wanaume wawili kwa wakati mmoja

Muda wa kusoma: Dakika 4

Mwaka wa 2018,mwanamke mmoja alitembelea maabara moja katika chuo kikuu cha Colombia, ili kupima vinasaba vya vijana wake wawili mapacha.

Maabara hiyo ilifanya vipimo vya kawaida hadi kurudia tena, ila majibu yalikuwa yakushangaza. Mapacha hao walikuwa na mama mmoja na baba tofauti.

Hali hii ni ya kipekee, kisayansi inaitwa "heteropaternal superfecundation."

Visa kama hivi ishirini vimeripotiwa kote duniani na matokeo kuchapishwa katika majarida ya kisayansi.

Ingawa wanasayansi wa chuo hicho walisema walijua inaweza kutokea ila hawakuwa wameshuhudia kitaalam.

Jinsi walivyogundua

Ili kujua baba wa mtoto, wanasayansi kutoka taasisi ya vinasaba katika chuo kikuu cha Colombia walitumia teknlojia iitwayo 'microsatellite markers.'

Hii inahusisha kuchambua vipande vidogo sana vya vinasaba vya DNA kutoka kwa mtoto, mama na mtu anayedaiwa kuwa baba, kisha kuvilinganisha.

"Tunakusanya vinasaba kutoka kwa kila mtu, tunachunguza kati ya maeneo 15 hadi 22 yanayoitwa microsatellites, na kuyalinganisha moja baada ya nyingine," alisema Profesa William Usaquén, mkurugenzi wa maabara hiyo, katika mahojiano na BBC Mundo.

Baada ya kukusanya sampuli za damu,wanasayansi hufanya mchakato wa kikemia ili kutenganisha DNA na vipengele vingine.

Vinasaba hivyo huwekwa kwa mashine spesheli.

Kioevu kinachopatikana huchanganywa na rangi maalum zinazong'aa ili kuashiria maeneo 15 hadi 22 ya microsatellites yanayochunguzwa.

Kisha vinasaba hivyo hupitishwa kwenye mashine nyingine inayosoma microsatellites katika kila sampuli na kuzigeuza kuwa mfuatano wa namba, mchakato unaojulikana kama electrophoresis.

Kwa kutumia mfuatano huo wa namba, watafiti huamua uwezekano wa mwanaume aliyepimwa kuwa baba wa mtoto.

Nusu ya muundo wa kijenetiki wa mtoto unapolingana na wa mama na nusu nyingine kulingana na wa baba, basi baba wa mtoto huthibitishwa.

Matokeo ya kipekee

Katika kesi ya mapacha hao, wanasayansi walichambua maeneo 17 ya microsatellites katika DNA ya mama, watoto hao wawili na mwanaume anayedaiwa kuwa baba mzazi.

Matokeo hayo yalionyesha DNA ya mwanaume huyo ililingana na ya mtoto mmoja kati ya mapacha hao

"Nimekuwa mkurugenzi wa maabara hii kwa miaka 26, na hii ni kesi ya kwanza kabisa kuiona na hadi sasa ndiyo ya kipekee," anasema Usaquén.

"Tulikuwa tumesikia kutoka kwa ripoti nyingine kuwa kesi kama hizi hutokea, lakini kwa kiwango cha chini sana duniani," anaongeza Andrea Casas, mtaalamu wa jenetiki na mtafiti katika Taasisi ya Jenetiki ya Chuo Kikuu cha Colombia.

Baada ya matokeo hayo timu hiyo ya wanasayansi ilirudia vipimo hivyo, ili kuondoa makosa yoyote ambayo huenda yalitokea wakati wa kuchanganya sampuli. Ila baada ya vipimo kadhaa, matokeo yalibakia yale yale.

kwanini hali hii ni nadra sana?

Makala ya mwaka 2014, iliyochapishwa na wanasayansi katika maabara moja huko Baltimore, nchini Marekani, iliripoti kuwa kati ya hifadhidata ya vipimo 39,000 vya kugundua baba ya watoto, ni visa vitatu tu vya 'superfecundation' ya watoto kuwa na baba tofauti vilivyobainika.

Usaquén anaeleza kwa nini tukio hili la kibiolojia hutokea kwa nadra sana

"Kwanza, mwanamke lazima awe na wapenzi wawili alioshiriki nao mapenzi. Pili, lazima afanye mapenzi na wanaume wote wawili ndani ya kipindi kifupi sana. Zaidi ya hayo, lazima kuwe na 'polyovulation"

Polyovulation ni utolewaji wa mayai mawili au zaidi katika mzunguko mmoja wa hedhi.

"Na mwisho, mayai yote lazima yatungishwe," anaongeza Usaquén.

Mapacha wenye baba tofauti hawawezi kamwe kuwa mapacha wanaofanana kwa sababu mapacha wanaofanana hutokana na yai moja lililorutubishwa na mbegu moja ya kiume.

Maisha ya faragha

Katika hali nyingi ambapo mwanamke anatoa mayai zaidi ya moja, kama yai moja tu litatungishwa, lile lingine au mengine hufa haraka baada ya muda mfupi.

Hii pia ndiyo sababu nyingine kwa nini 'superfecundation' ya watoto kuwa na baba tofauti ni nadra sana kwasababu yai la pili lazima litungishwe kabla halijafa.

Kulingana na Maktaba ya Kitaifa ya Tiba ya Marekani, yai huishi kwa chini ya saa 24 baada ya kutolewa.

Hata hivyo, Andrea Casas anaeleza kuwa mayai si lazima yatoke kwa wakati mmoja.

"Wakati mwingine ovari moja hutoa yai, na siku mbili au tatu baadaye ovari nyingine hutoa yai jingine," anasema.

Hii huongeza uwezekano wa utungisho kutokea kwa nyakati tofauti.

Sababu nyingine inayofanya visa hivi viwe nadra ni kwamba watu wengi hawafanyi vipimo vya kujua baba ya mtoto ni nani.

Watafiti kutoka taasisi hiyo wanapendekeza kuwa jambo hili linaweza kuwa la kawaida zaidi siku za usoni "kutokana na upatikanaji wa mbinu za kisasa kuongezeka kwa umaarufu wa vipimo vya vinasaba."

Wanasayansi wengi hutaka kujua maisha ya mwanamke ili kujua nini huchochea hatua hii lakini maadili ya utafiti yanawazuia kuuliza kuhusu maisha binafsi ya wanaopimwa.

"Vipimo vya vinasaba hufanywa kila wakati kwa heshima kubwa,uadilifu na faragha ya wahusika,"anasema Usaquén

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula