Papa Leo kufanya ziara ya kwanza barani Afrika - Vatican

Barani Afrika, Papa Leo atazuru Algeria, Angola, Equatorial Guinea na Cameroon.

Muhtasari

Moja kwa moja

Rashid Abdallah & Asha Juma

  1. Mbuga ya Kitaifa ya Bwindi Uganda yafanya sensa ya kwanza ya sokwe

    .

    Chanzo cha picha, Elodie Freymann

    Mbuga ya Kitaifa ya Bwindi ya Uganda mwaka jana ilifanya sensa ya kwanza kabisa ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka katika mbuga hiyo na kubaini kuwa kuna sokwe 426, hesabu ambayo wataalam wanatumai itaimarisha juhudi za uhifadhi.

    Shirika la wanyama pori nchini Uganda lilifanya sensa ya sokwe kwa ushirikiano na taasisi ya Jane Goodal, iliyo na makao yake nchini Marekani mwaka uliopita na kutangaza matokeo yake wiki hii.

    Sensa hiyo ambayo ilidhamiria kufahamu idadi kamili ya sokwe katika mbuga hiyo ni hatua kubwa katika kuimarisha uhifadhi wa mbuga hiyo na Sokwe wanaoishi katika mojawapo ya mbuga inayolindwa zaidi barani Afrika.

    Afisa mkuu aliyeongoza utafiti huo amesema data hiyo sasa itasaidia kutoa muongozo wa jinsi ya kuwahifadhi sokwe hao na pia mbuga hiyo, ambayo ni moja ya misitu ya kiasili iliyosalia barani Afrika.

    Mbuga hiyo yenye ukubwa wa kilomita 320 mraba, iko kwenye orodha ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni, UNESCO na ni moja ya mbuga inayowavutia watalii wengi zaidi nchini Uganda.

    Mbunga hiyo pia ina wanyama wengine kama vile swara, nyani, ndovu, ndege, mbweha miongoni mwa wengineo.

    Soma zaidi:

  2. Tanzania yatoa tahadhari ya mafua makali, Uviko – 19 na homa ya Dengue

    .

    Wizara ya afya Tanzania imesema kuwa maambukizi ya wagonjwa wa mafua makali ya Influenza na Uviko-19 yameongezeka na kuwataka wananchi kuchukua hatua stahiki za kujikinga na maambukizi hayo.

    Taarifa hiyo iliyotolewa na mganga mkuu wa serikali Dk. Grace Magembe imetokana na kufuatilia mwenendo wa magonjwa ya mlipuko.

    "Magonjwa haya huenezwa kupitia majimaji kwenye mfumo wa nia ya hewa wa mgonjwa mwenye maambukizi na husambaa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza," taarifa hiyo ilisema.

    Wizara imesema kuwa mafua makali ya Influenza na Uviko-19 huenezwa kwa kugusa mazingira yaliyochafuliwa na majimaji yanayotoka kwa mgonjwa na kuongeza kuwa dalili zake ni homa kali, kikohozi, mafua, maumivu ya kichwa na mwili.

    "Takwimu za ufuatiliaji zinaonyesha kila mwaka kipindi cha mwezi Novemba hadi Aprili kunakuwa na ongezeko la Influenza na Uviko-19," Taarifa ilisema.

    Wizara hiyo pia imetoa tahadhari ya ugonjwa wa homa ya Dengue ambayo huongezeka kipindi hiki cha mvua za masika.

    Homa ya Dengue huenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye hupendelea kuuma nyakati za asubuhi, mchana na jioni.

    "Dalili za ugonjwa huu zinafanana na ugonjwa wa malaria", Wizara imesema.

    Wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari kujilinda na magonjwa hayo.

    Soma zaidi:

  3. Papa Leo kufanya ziara ya kwanza barani Afrika - Vatican

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Papa Leo XIV atafanya safari ya Kitume ya siku kumi kwenda Afrika na nyingine mbili barani Ulaya, Vatican ilitangaza Jumatano.

    Ziara ya kwanza itakuwa safari ya siku moja mwishoni mwa Machi hadi Monaco, ikifuatiwa na Safari ya Afrika mwezi Aprili 13-23, na hatimaye Safari ya siku sita kwenda Uhispania na katika visiwa vya Uhispania mnamo mwezi Juni.

    Barani Afrika, Papa Leo atazuru Algeria, Angola, Equatorial Guinea na Cameroon.

    Nchini Cameroon, Papa atatembelea mji mkuu Yaoundé, kitovu cha kiuchumi cha Douala, na mji wa Anglophone wa Bamenda katika eneo lenye machafuko la Kaskazini-Magharibi, ambako mzozo wa silaha umekuwa ukiendelea kwa karibu miaka kumi.

    Mpango rasmi wa shughuli za Papa wakati wa ziara yake ya mataifa manne bado haujatolewa.

    Mnamo mwezi Januari, Kardinali Fridolin Ambongo, Askofu Mkuu wa Kinshasa na Rais wa Kongamano la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar (SECAM) alidokeza mipango ya Papa Leo kuzuru Afrika mwezi Aprili.

    Alifichua hayo katika mahojiano na Vatican News, baada ya kukutana na Papa.

    "Papa anapotembelea nchi, haswa nchi zilizo katika hali mbaya kama yetu, pia ni kutoa matumaini kwa watu, haswa watu wanaoteseka," Kardinali alisema katika mahojiano ya mwezi Januari.

    Ziara ya Papa barani Afrika inafuatia safari yake ya kwanza ya nje ya Uturuki na Lebanon mwishoni mwa mwaka jana, ambapo alitoa wito wa amani na maridhiano Mashariki ya Kati.

    Mnamo mwezi Desemba, alielezea nia yake ya kutembelea bara, akitaja Algeria, mahali pa kuzaliwa kwa Mtakatifu Augustine wa Hippo, kama mahali anapoweza kufika. Papa huyo ni wa mfumo wa kidini wa Augustinian na hapo awali alitoa wito wa mazungumzo kati ya dini mbalimbali katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

    Ingawa itakuwa ni ziara ya kwanza ya Papa Leo barani Afrika tangu kushika uongozi wa Kanisa Katoliki, yeye si mgeni katika bara hilo. Akiwa Kardinali Robert Prevost, alitembelea nchi kadhaa zikiwemo Kenya na Tanzania.

    Nchi kama vile Cameroon, Angola, na Equatorial Guinea ambako Baba Mtakatifu anapanga kukaa huko, zimewahi kuwa kutembelewa na Papa.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Kiwewe cha usalama wa kombe la dunia kutokana na fedha kufungiwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maafisa wa serikali ya Marekani wameonywa kwamba kunaweza kuzuka janga la kiusalama iwapo miji itakayokuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia haitapokea fedha zilizohifadhiwa.

    Miji 11 itakayoandaa michuano hiyo haijapoka karibu dola milioni mia 9 ambazo ni sawa na pauni (£666m) zilizotengwa kufuatia kufungwa kwa sehemu ya serikali.

    Maafisa katika kikao cha Kamati ya Usalama wa ndani ya Bunge walisema kuwa kuzuiwa kwa fedha na ukosefu wa uratibu kati ya serikali za ndani na serikali kuu ni mojawapo ya sababu kuu zinazochochea kwa nini maandalizi ya usalama yamechelewa.

    Ray Martinez, afisa mkuu wa kamati ya uwenyeji wa Kombe la Dunia Miami, alisema kuwa huenda ikalazimika kufuta mipango isipokuwa waandaji wapate dola milioni 70 (paundi milioni 52) ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi.

    “Tumesalia na siku 107 kabla ya mashindano, lakini muhimu zaidi, tumebaki na takriban siku 70 kabla ya kuanza kujenga Tamasha la Mashabiki,” alisema.

    “Maamuzi haya lazima yafanyike. Bila kupokea fedha hizi, inaweza kuwa na madhara makubwa kwa upangaji na uratibu wetu.”

    Kombe la dunia linaloandaliwa kwa ushirikiano wa Canada na Mexico linaanza tarehe 11 Juni.

    Mechi ya Marekani dhidi ya Paraguay huko Los Angeles tarehe 13 Juni ndiyo mchezo wa kwanza wa mashindano ya 2026 kufanyika nchini Marekani.

    Atlanta, Boston, Dallas, Houston, Los Angeles, Kansas City, Miami, New York/New Jersey, Philadelphia, San Francisco, na Seattle ndio miji itakayokuwa wenyeji nchini Marekani.

    Shirika la dharura la Federal Emergency Management Agency (FEMA), ambalo ni sehemu ya Idara ya Usalama wa Ndani (DHS), lilianzisha mpango wa ruzuku wa Kombe la Dunia la FIFA mwezi Novemba.

    Ililenga kutoa dola milioni 625 (pauni milioni 462) kwa miji itakayokuwa wenyeji ili kushughulikia suala la usalama kulinda wachezaji, wafanyakazi, washiriki, viwanja na miundombinu muhimu katika miji yote ya mwenyeji, na kuwa imara dhidi ya mashambulizi ya kigaidi.

    Kiasi hicho kiliongezwa kwa dola milioni 250 (pauni milioni 185) mnamo mwezi Desemba ili kuimarisha uwezo wao wa kugundua, kutambua, kufuatilia, au kupunguza madhara ya mifumo ya ndege zisizo na rubani.

    Hata hivyo, tangu fedha kuzuiliwa, naibu mkuu wa polisi wa Kansas City, Joseph Mabin, alisema kwamba idara yake haina wafanyakazi wa kutosha kushugulikia mahitaji ya usalama ya jiji hilo.

    Uwanja wa Gillette huko Foxborough, Boston, umepangwa kuwa mwenyeji wa mechi saba, lakini maafisa wa mji huo wametajwa, vyanzo vya nje vikiwaambia kwamba huenda wakajiondoa katika kuwa mwenyeji wa mechi ikiwa hawatapokea fedha hizo.

    Uingereza itacheza dhidi ya Croatia huko Dallas tarehe 17 Juni, dhidi ya Ghana huko Boston tarehe 23 Juni, na dhidi ya Panama huko New York tarehe 27 Juni.

    Uskoti itacheza dhidi ya Haiti na Morocco huko Boston tarehe 14 na 19 Juni kabla ya kukabiliana na Brazil huko Miami tarehe 24 Juni.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Harry na Meghan wawasili Mashariki ya Kati kwa mazungumzo yanayoangazia wakimbizi

    .

    Chanzo cha picha, PA Media

    Mwanamfalme Harry na mkewe Meghanwamewasili Mashariki ya Kati, safari yao ya kwanza ya kimataifa pamoja katika kipindi cha miezi 18.

    Harry na Meghan watatumia siku mbili kutembelea Jordan kuangazia juhudi za kusaidia jamii zilizo katika mazingira magumu zilizoathiriwa na migogoro na kuhama makazi yao.

    Wanandoa hao, walijiondolea majukumu ya familia ya kifalme mwaka wa 2020, na wamesafiri kwenda Amman kwa mwaliko wa Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

    Ziara yao inakuja wakati wa mgogoro kwa Familia ya Kifalme kufuatia kukamatwa kwa mjomba wake Harry, Andrew Mountbatten-Windsor, kwa tuhuma za utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma.

    Mara tu baada ya kuwasili, wanandoa hao walijiunga na majadiliano yaliyoandaliwa na WHO na watu binafsi kutoka vyombo vinavyoongoza ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa na mashirika yake mengine, wawakilishi wa kidiplomasia, na wafadhili.

    Kwa siku mbili zijazo, Harry na Meghan wanatarajiwa kukutana na viongozi wa Jordan na maafisa wakuu wa huduma ya afya.

    Wanatarajiwa kushirikiana na timu za WHO, kutembelea programu za afya na afya ya akili na kukutana na wafanyakazi wa Shirika la World Central Kitchen ambao wanaratibu misaada ya chakula huko Gaza kutoka Amman.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Modi azuru Israel nchi hizo zikilenga kuimarisha uhusiano wake

    .

    Chanzo cha picha, Hindustan Times via Getty Images

    Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amezuru Israeli kwa ziara ya siku mbili, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu kuanza kwa vita vya Gaza.

    Modi anatarajiwa kuhutubia bunge la Israeli, Knesset, na kufanya mikutano na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Rais Isaac Herzog. Hakuna mkutano na viongozi wa Palestina katika ratiba yake.

    Ziara hiyo inakuja huku nchi zote mbili zikilenga kuimarisha uhusiano katika ulinzi, teknolojia na biashara - uhusiano ambao umekua kwa kiasi kikubwa tangu Modi aingie madarakani zaidi ya muongo mmoja uliopita.

    Hata hivyo, wachambuzi wanasema ziara hiyo pia itakuwa majaribio ya sera ya kigeni ya India inapojaribu kusawazisha uhusiano wake na Israeli na nchi zingine za Mashariki ya Kati.

    Mnamo mwaka 2017, Modi alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa India kutembelea Israeli. Safari hiyo ilionekana sana kama hatua muhimu katika uhusiano huo.

    Nchi hizo mbili zinashirikiana kwa karibu katika kupambana na ugaidi na masuala ya ulinzi. India pia ni miongoni mwa wanunuzi wakubwa wa silaha za Israeli.

    Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu ameita ziara ya Modi kuwa ya "kihistoria".

    "Uhusiano kati ya Israeli na India ni muungano wenye nguvu kati ya viongozi wawili wa kimataifa. Sisi ni washirika katika uvumbuzi, usalama na maono ya kimkakati ya pamoja. Kwa pamoja, tunajenga mhimili wa mataifa yaliyojitolea kwa utulivu na maendeleo," aliandika kwenye X.

    Modi pia alijibu kwa kusema kwamba India "inathamini sana urafiki wa kudumu na Israeli, uliojengwa kwa kuzingatia uaminifu, uvumbuzi na kujitolea kwa pamoja kwa amani na maendeleo".

  7. Wanawake wawili wa Uganda wakamatwa kwa madai ya kubusiana hadharani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images Europe

    Polisi wa Uganda wamewakamata wanawake wawili, wote wakiwa katika umri wa miaka 20, baada ya majirani kuripoti kuwaona wakibusiana hadharani, kitendo ambacho kimeharamishwa chini ya Sheria ya Kupinga Mapenzi ya Jinsia Moja nchini humo.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, polisi walisema wawili hao walikamatwa Jumatano tarehe 18 Februari huko Arua, kaskazini magharibi mwa Uganda.

    Mamlaka ilisema majirani waliwapiga picha kabla ya kuwaarifu polisi.

    Wanawake hao wanaendelea kuzuiliwa bila kupata uwakilishi wa kisheria, kulingana na shirika la habari la AFP.

    Sheria ya nchi hiyo inatoa adhabu kali, ikiwa ni pamoja na kifungo cha maisha jela na hukumu ya kifo kwa mahusiano ya jinsia moja kwa kile kinachoelezwa kuwa kesi za aina hii "zilizopitiliza".

    Polisi waliarifiwa na majirani waliosema wawili hao walikuwa wamejihusisha na tabia ya mapenzi ya jinsia moja, AFP inaripoti.

    "Majirani waliwasiliana na polisi wakilalamika kwamba wawili hao walikuwa wakifanya mapenzi ya jinsia moja na walionekana wakibusiana hadharani," msemaji wa polisi wa eneo hilo Josephine Angucia aliambia AFP, akiongeza kuwa majirani walitoa picha walizodai zilionyesha wawili hao wakibusiana hadharani.

    Angucia aliongeza kuwa wakazi pia waliripoti kuona makundi ya wanawake wakitembelea nyumba ya wawili hao yenye chumba kimoja cha kulala na kulala usiku kucha, jambo ambalo waliamini liliashiria mikusanyiko ya watu wa jinsia moja. Alisema kesi hiyo imefikishwa kwa waendesha mashtaka kwa ajili ya mapitio na uwezekano wa kuwasilishwa mahakamani.

    Sheria ya Uganda ya Kupinga Mapenzi ya Jinsia Moja ni miongoni mwa sheria kali zaidi duniani.

    Watu waliopatikana na hatia wanakabiliwa na kifungo cha maisha jela kwa mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja, huku wale waliopatikana na hatia ya kesi "zilizopitiliza", ikiwa ni pamoja na makosa ya kurudia kitendo hicho au vitendo vinavyowahusisha watoto au watu walio katika hatari wakikabiliwa na adhabu ya kifo.

    Sheria hiyo imeshutumiwa na serikali za Magharibi na makundi ya kutetea haki za binadamu.

    Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu Frank Mugisha alikosoa kukamatwa huko katika maoni yaliyochapishwa kwenye mtandao wa X, akisema kunaangazia mazingira hatari ambayo Waganda wa jamii ya LGBTQ+ wanakabiliana nayo.

    Alionya kwamba sheria hiyo imesababisha ulaghai, huku waathiriwa mara nyingi wakiogopa sana kushtakiwa kiasi cha kutoweza kutafuta msaada.

    Uganda ni taifa lenye wahafidhina wengi na idadi kubwa ya raia ni Wakristo.

    Imekabiliwa na uchunguzi mkali wa kimataifa tangu sheria hiyo ilipoanza kutekelezwa mnamo mwezi Mei 2023.

    Umoja wa Mataifa na serikali kadhaa za kigeni zimelaani sheria hiyo.

    Benki ya Dunia ilisitisha kwa muda mikopo kwa Uganda kabla ya kuirejesha mwaka wa 2025.

    Soma zaidi:

  8. Sierra Leone yasema wanajeshi wake wanashikiliwa nchini Guinea

    K

    Chanzo cha picha, CPJ

    Sierra Leone inaihutumu Guinea kwa kuwakamata wanajeshi wake katika mzozo wa hivi karibuni kuhusu eneo la mpakani.

    Guinea imesema wanajeshi kadhaa wenye silaha wa Sierra Leone waliingia katika eneo lake bila idhini siku ya Jumapili, na kusababisha vikosi vya kijeshi kuwakamata 16 kati yao na kukamata vifaa.

    Mzozo wa ardhi kati ya nchi hizo mbili za Afrika Magharibi ulianza tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sierra Leone vya mwaka 1991-2002 wakati Guinea ilipotuma wanajeshi kusaidia kupambana na waasi.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumanne, wizara ya habari ya Sierra Leone ilisema wanajeshi na polisi walikuwa wakijenga kituo cha mpakani na kituo kingine katika mji wa Kaliyereh uliopo mpakani siku ya Jumatatu wakati wanajeshi wa Guinea walipowasili mjini humo.

    "Serikali inashiriki kikamilifu kupitia njia za kidiplomasia na usalama ili kuthibitisha mahali walipo na kuachiliwa kwao salama na bila masharti," imesema taarifa hiyo.

    Timu imetumwa katika eneo hilo kuchunguza tukio hilo, iliongeza.

    Wizara ya ulinzi ya Guinea ilisema katika taarifa Jumanne jioni kwamba wanajeshi waliokamatwa na vitu vilivyokamatwa vimekabidhiwa kwa polisi wa mahakama ili uchunguzi uweze kufanywa.

  9. Waziri Mkuu wa Senegal apendekeza sheria kali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja

    l

    Chanzo cha picha, RAJESH JANTILAL / AFP

    Waziri Mkuu wa Senegal Ousmane Sonko amependekeza sheria ambayo inaweza kuongeza maradufu adhabu kwa watu wenye kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, na kuwafanya waadhibiwe kwa hadi miaka 10 jela.

    Pendekezo hilo lilipelekwa bungeni Jumanne baada ya kuidhinishwa na baraza la mawaziri wiki iliyopita, baada ya wimbi la kukamatwa kwa watu wanaodaiwa kuwa wapenzi wa jinsia moja.

    Akihutubia wabunge, Sonko alisema muswada huo utaadhibu kile kinachoelezwa kama "vitendo kinyume na maumbile" kwa vifungo vya gerezani kuanzia miaka mitano hadi 10, ikilinganishwa na adhabu ya sasa ya mwaka mmoja hadi mitano.

    "Ikiwa kitendo hiki kitafanywa kwa mtoto mdogo, adhabu itakuwa ya juu zaidi," alisema, akikosolewa na watetezi wa haki za binadamu.

    Mjadala kuhusu haki za LGBT umesababisha mvutano kwa muda mrefu nchini Senegal, nchi ya kihafidhina ambapo baadhi ya makundi yanasema harakati za LGBT ni uingiliaji kati wa kigeni.

    Mashirika ya kidini yamekuwa yakifanya maandamano katika miaka ya hivi karibuni yakitaka adhabu kali zaidi.

    Mapema mwezi huu, polisi waliwakamata wanaume 12 chini ya sheria zinazopinga LGBT. Vyombo vya habari vya ndani vinasema takriban watu 30 wamekamatwa kwa jumla mwezi huu.

    Wale watakaopatikana na hatia wanaweza pia kukabiliwa na faini ya hadi CFA milioni 10 (karibu $18,000; £13,000), Sonko aliongeza.

    Tarehe bado haijawekwa kwa ajili ya kura ya bunge kuhusu muswada huo, katika bunge linalodhibitiwa na chama cha Sonko cha Pastef.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Japan kupeleka makombora kwenye kisiwa karibu na Taiwan

    lonaguni kutoka ufuo wa Taiwan siku yenye mwanga

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Yonaguni kutoka ufuo wa Taiwan

    Waziri wa ulinzi wa Japani amesema anapanga kupeleka makombora kwenye kisiwa chake cha magharibi karibu na Taiwan ifikapo Machi 2031, huku mvutano wa kikanda ukiendelea.

    Ni mara ya kwanza kwa Japani kubainisha ratiba ya kupelekwa kwa kombora katika kisiwa cha Yonaguni.

    Yonaguni iko umbali wa kilomita 110 tu (maili 68) kutoka Taiwan.

    Mvutano kati ya Tokyo na Beijing umekuwa mkubwa tangu Novemba wakati Waziri Mkuu wa Japani Sanae Takaichi alipopendekeza kwamba Japani itakuwa tayari kujilinda iwapo kutakuwa na shambulio dhidi ya Taiwan.

    Wasiwasi ni kwamba shambulio lolote dhidi ya Taiwan, ambayo ni mshirika wa Marekani, linaweza kusababisha mzozo wa moja kwa moja wa kijeshi kati ya Washington na Beijing, kisha likaenea hadi kujumuisha washirika wengine wa Marekani katika eneo hilo kama vile Japani.

    Waziri wa ulinzi wa Japan Shinjiro Koizumi alitangaza ratiba ya makombora hayo siku ya Jumanne, siku moja baada ya China kuweka vikwazo vya usafirishaji nje kwa makampuni na mashirika 20 ya Japani.

    Koizumi alisema kitengo cha Yonaguni kitakuwa na makombora ya masafa ya kati yanayoweza kuzuia ndege na makombora.

    Matukio ya hivi punde yanakuja baada ya Takaichi, mhafidhina, kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge mapema mwezi huu.

    Ushindi huo ulimpa Takaichi nafasi ya kisiasa ya kuongeza nguvu katika kuimarisha uwezo wa ulinzi wa Japani.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Kansela wa Ujerumani awasili Beijing kwa ziara ya kwanza nchini China

    p

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Friedrich Merz

    Kansela wa Ujerumani amewasili nchini China huku uagizaji bidhaa kutoka China kwenda Ujerumani ulikuwa mara mbili ya bidhaa zilizosafirishwa mwaka jana kwenda Ujerumani - kulingana na takwimu za serikali kuu.

    "Tunataka ushirikiano na China ambao ni wa usawa, wa kuaminika, unaodhibitiwa na wa haki," amesema Friedrich Merz, kabla ya kuondoka kwenda Beijing.

    Kuna pengo kubwa la kibiashara linaonekana katika mazungumzo haya huku kansela akiongozana na ujumbe mkubwa wa kibiashara.

    Merz pia anatarajiwa kuishinikiza China kutumia ushawishi wake na Moscow kusaidia kukomesha vita nchini Ukraine.

    China kwa mara nyingine tena ilichukua nafasi ya kwanza kama mshirika mkubwa wa kibiashara wa Ujerumani 2025, ikichukua nafasi ya Marekani.

    Mnamo 2025, bidhaa zenye thamani ya €170.6 bilioni (£148.8bn; $200.9bn) zilitoka China hadi Ujerumani - ongezeko la 8.8% kila mwaka - huku mauzo ya nje ya Ujerumani kwenda China yakishuka kwa 9.7% hadi €81.3 bilioni .

    Uhusiano wa kibiashara na China upo zaidi katika sekta za magari, mashine na kemikali.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Mafuriko na maporomoko ya ardhi Brazil yaua watu 25

    p

    Chanzo cha picha, Bruno Stephan/Prefeitura de Juiz de Fora/Handout via Reuters

    Watu wasiopungua 25 wamefariki katika jimbo la Minas Gerais kusini-mashariki mwa Brazil baada ya mvua kubwa iliyonyesha Jumatatu jioni kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi.

    Vifo vingi viliripotiwa katika jiji la Juiz de Fora, ambapo maafisa wanasema watu 18 walifariki, huku vifo vingine saba vikiripotiwa huko Ubá.

    Shughuli za uokoaji zinaendelea, huku wafanyakazi na wakazi wakiwatafuta watu walioripotiwa kupotea baada ya nyumba na majengo kadhaa kuanguka.

    Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva alituma "rambirambi zake" kwa familia za waathiriwa na wale waliopoteza makazi yao. Pia alisema serikali imetangaza "hali ya janga" huko Juiz de Fora.

    Takriban watu 440 wameachwa bila makazi au wamelazimika kuhama makazi yao huko Juiz de Fora pekee, huku serikali ya mtaa ikitoa makazi ya muda na kuomba michango ya maji, chakula, nguo na vifaa vya usafi.

    Watoto walikuwa miongoni mwa wale waliofariki huko Juiz de Fora, lakini jiji hilo hadi sasa halijatoa taarifa yoyote rasmi kuhusu utambulisho wa waathiriwa.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Sitairuhusu Iran kuwa na silaha za nyuklia – Trump

    ll

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump ametoa hotuba yake ya kila mwaka katika majengo ya Bunge la Marekani na kusisitiza kuwa hatoiruhusu Iran kuwa na silaha za nyuklia.

    Rais wa Marekani amesema: "Kwa miongo kadhaa, imekuwa sera ya Marekani kutoruhusu Iran kupata silaha za nyuklia.”

    “Wameonywa wasijaribu kujenga upya mpango wao wa silaha, lakini wanaendelea kufuata matarajio yao mabaya ya nyuklia. Napenda tutatue tatizo hili kupitia diplomasia, lakini jambo moja ni hakika: Sitawaruhusu kupata silaha za nyuklia."

    Trump ameweka rekodi ya hotuba ndefu zaidi, akitumia karibu saa 1 na dakika 50, akiizidi rekodi ya Bill Clinton ya hotuba yake ya mwisho mwaka 2000.

    Pia unaweza kusoma:

  14. 'Iwapo Marekani itafanya makosa ya kutushambulia itapata hasara kubwa' - Mkuu wa Jeshi Iran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mkuu wa Jeshi la Iran Jenerali Mousavi

    Hapo awali tuliripoti kwamba Waziri wa Ulinzi wa Armenia Soren Papikyan alisafiri hadi Tehran na kukutana na Waziri wa Ulinzi wa Irani Aziz Nasirzadeh.

    Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi, Mkuu wa Jeshi la Iran pia alikutana naye.

    Bwana Mousavi alisema katika mkutano huo: "Sisi hatukuwa waanzilishi wa vita vyovyote, na mbinu yetu huko nyuma ilikuwa kuzuia kupanuka kwa wigo wa vita na kupunguza majeruha. Lakini hatua za Marekani zilitufanya kubadili mtazamo wetu, na wakati huu, ikiwa itafanya makosa, tutaisababishia hasara kubwa."

    Msemaji wa Ikulu ya White House Carolyn Leavitt amesema leo kuwa chaguo la kwanza la Donald Trump siku zote ni diplomasia, lakini yuko tayari kutumia nguvu ikibidi.

  15. Nigeria yakana ripoti kwamba ililipa fidia ili wanafunzi waliotekwa nyara waachiliwe huru

    p;

    Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    Maelezo ya picha, Zaidi ya wanafunzi 200 na wafanyakazi walichukuliwa na watu wenye silaha kutoka Shule ya St Mary's mwezi Novemba - wote waliachiliwa huru kufikia Krismasi

    Serikali ya Nigeria imekataa ripoti ya vyombo vya habari inayodai kwamba ililipa fidia kwa wanamgambo wa Kiislamu wa Boko Haram ili kuachiliwa huru kwa zaidi ya wanafunzi 200 na wafanyakazi waliotekwa nyara katika shule ya bweni ya Kikatoliki mwezi Novemba.

    Waziri wa Habari Mohammed Idris amesema madai hayo, yaliyotolewa na shirika la habari la AFP likinukuu vyanzo vya kijasusi, kuwa "ya uwongo na yasiyo na msingi."

    Pia amekanusha kwamba makamanda wawili wa Boko Haram waliachiliwa huru kama sehemu ya makubaliano hayo.

    Nigeria inakabiliwa na tatizo la utekaji nyara - huku wahalifu wakiwa ni pamoja na wanamgambo wa Kiislamu, wanachama wa magenge yanayojulikana kama "majambazi" na watu wanaotaka kujitenga.

    Baadhi ya wachambuzi walionukuliwa na AFP wanaamini utekaji nyara katika Shule ya St Mary huko Papiri katika jimbo la magharibi mwa Niger uliongozwa na kamanda maarufu wa wanamgambo wa Boko Haram anayejulikana kama "Sadiku."

    Ingawa Boko Haram inasalia kuwa na shughuli nyingi zaidi katika jimbo la Borno kaskazini-mashariki, ambapo kundi hilo lilianza uasi wake mwaka 2009, mitandao mingine ya uhalifu ina shughuli katika sehemu kubwa za maeneo ya kaskazini-magharibi na kaskazini-kati mwa Nigeria.

    Chanzo kimoja kilichonukuliwa na AFP kilidai fidia hiyo ilifikia takriban naira milioni 40 (karibu dola 30,000, pauni 22,000) kwa kila mateka, huku chanzo kingine kikidokeza kwamba jumla ya naira bilioni 2 (karibu dola milioni 1.5) zililipwa.

    Ripoti hiyo pia ilidai pesa hizo zilisafirishwa kwa helikopta hadi kwenye eneo la Gwoza la Boko Haram katika jimbo la Borno na kukabidhiwa kwa kamanda wa eneo hilo.

    "Madai kwamba fidia ilitolewa kwa helikopta kwa waasi, pamoja na uthibitisho wa risiti, ni hadithi ya kubuni," Idris alisema katika taarifa hiyo.

    Boko Haram walipata umaarufu mwaka 2014 kwa kuwateka nyara zaidi ya wasichana 200 wa shule kutoka kijiji cha Chibok.

    Tangu wakati huo nchi imekabiliwa na ongezeko la utekaji nyara kwa wingi, huku wachambuzi wakisema malipo ya fidia - kutoka kwa familia, wapatanishi au, katika baadhi ya matukio, mamlaka za serikali - yamesaidia kuchochea utekaji nyara."

    Pia unaweza kusoma:

  16. Mexico yawasaka wafungwa 23 waliotoroka gerezani wakati wa vurugu

    p

    Chanzo cha picha, EPA

    Polisi nchini Mexico inawasaka wafungwa kadhaa waliotoka gerezani huko Puerto Vallarta wakati wa wimbi la machafuko yaliyoanzishwa na genge la dawa za kulevya la Jalisco New Generation Cartel (CJNG) siku ya Jumapili.

    CJGN ilifanya vurugu kulipiza kisasi kwa mauaji ya kiongozi wao, Nemesio Oseguera Cervantes, anayejulikana kama "El Mencho" na vikosi vya usalama.

    Wakati wa machafuko hayo, watu wenye silaha waligonga milango ya gereza kwa gari, na kuwafungulia njia wafungwa 23 kutoroka, amesema afisa mmoja.

    Zaidi ya watu 70 - wakiwemo wanajeshi 25 - waliuawa katika operesheni ya kukamata El Mencho na vurugu zilizofuata.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Hujambo na karibu

    Nakukaribisha katika taarifa zetu za moja kwa moja, leo Jumatano tarehe 25/2/2025

Trending Now