Maafisa wa serikali ya Marekani wameonywa kwamba kunaweza kuzuka janga la kiusalama iwapo miji itakayokuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia haitapokea fedha zilizohifadhiwa.
Miji 11 itakayoandaa michuano hiyo haijapoka karibu dola milioni mia 9 ambazo ni sawa na pauni (£666m) zilizotengwa kufuatia kufungwa kwa sehemu ya serikali.
Maafisa katika kikao cha Kamati ya Usalama wa ndani ya Bunge walisema kuwa kuzuiwa kwa fedha na ukosefu wa uratibu kati ya serikali za ndani na serikali kuu ni mojawapo ya sababu kuu zinazochochea kwa nini maandalizi ya usalama yamechelewa.
Ray Martinez, afisa mkuu wa kamati ya uwenyeji wa Kombe la Dunia Miami, alisema kuwa huenda ikalazimika kufuta mipango isipokuwa waandaji wapate dola milioni 70 (paundi milioni 52) ifikapo mwishoni mwa mwezi Machi.
“Tumesalia na siku 107 kabla ya mashindano, lakini muhimu zaidi, tumebaki na takriban siku 70 kabla ya kuanza kujenga Tamasha la Mashabiki,” alisema.
“Maamuzi haya lazima yafanyike. Bila kupokea fedha hizi, inaweza kuwa na madhara makubwa kwa upangaji na uratibu wetu.”
Kombe la dunia linaloandaliwa kwa ushirikiano wa Canada na Mexico linaanza tarehe 11 Juni.
Mechi ya Marekani dhidi ya Paraguay huko Los Angeles tarehe 13 Juni ndiyo mchezo wa kwanza wa mashindano ya 2026 kufanyika nchini Marekani.
Atlanta, Boston, Dallas, Houston, Los Angeles, Kansas City, Miami, New York/New Jersey, Philadelphia, San Francisco, na Seattle ndio miji itakayokuwa wenyeji nchini Marekani.
Shirika la dharura la Federal Emergency Management Agency (FEMA), ambalo ni sehemu ya Idara ya Usalama wa Ndani (DHS), lilianzisha mpango wa ruzuku wa Kombe la Dunia la FIFA mwezi Novemba.
Ililenga kutoa dola milioni 625 (pauni milioni 462) kwa miji itakayokuwa wenyeji ili kushughulikia suala la usalama kulinda wachezaji, wafanyakazi, washiriki, viwanja na miundombinu muhimu katika miji yote ya mwenyeji, na kuwa imara dhidi ya mashambulizi ya kigaidi.
Kiasi hicho kiliongezwa kwa dola milioni 250 (pauni milioni 185) mnamo mwezi Desemba ili kuimarisha uwezo wao wa kugundua, kutambua, kufuatilia, au kupunguza madhara ya mifumo ya ndege zisizo na rubani.
Hata hivyo, tangu fedha kuzuiliwa, naibu mkuu wa polisi wa Kansas City, Joseph Mabin, alisema kwamba idara yake haina wafanyakazi wa kutosha kushugulikia mahitaji ya usalama ya jiji hilo.
Uwanja wa Gillette huko Foxborough, Boston, umepangwa kuwa mwenyeji wa mechi saba, lakini maafisa wa mji huo wametajwa, vyanzo vya nje vikiwaambia kwamba huenda wakajiondoa katika kuwa mwenyeji wa mechi ikiwa hawatapokea fedha hizo.
Uingereza itacheza dhidi ya Croatia huko Dallas tarehe 17 Juni, dhidi ya Ghana huko Boston tarehe 23 Juni, na dhidi ya Panama huko New York tarehe 27 Juni.
Uskoti itacheza dhidi ya Haiti na Morocco huko Boston tarehe 14 na 19 Juni kabla ya kukabiliana na Brazil huko Miami tarehe 24 Juni.