Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu kuendelea kesho
Kesi ya uhaini dhidi ya Kiongozi wa Upinzani nchini Tanzania imesikilizwa leo jijini Dar es Salamaa.
Muhtasari
- Obama afafanua kauli yake kuhusu 'majanabi' baada ya kusema 'ni kweli wapo’
- Kenya yaagiza uchunguzi kuhusu raia wa Urusi ambaye amekuwa akiwarekodi kisiri wanawake wa Kenya
- Iran iko tayari kuruhusu ukaguzi katika vituo vyake vya nyuklia
- Wanajeshi wa Nigeria wazuia mashambulizi ya wanamgambo wa Kiislamu
- Kimbunga chauwa watu 59 Madagascar
- Mshukiwa wa mauaji ya Bondi Beach afikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza
- Kesi ya Tundu Lissu yaahirishwa hadi kesho
- Tundu Lissu aanza kumuhoji Shahidi P8
- Mgomo wa usafiri wa anga wavuruga safari za ndege Kenya
- Tundu Lissu amemeliza kumhoji shahidi wa kificho P2
- Lissu amuuliza shahidi 'tutajuaje kama wewe sio chawa wa Mama'
- Lissu aomba kumuhoji shahidi juu ya maneno aliyosema yapo sahihi
- Jaji aruhusu Lissu aanze kuuliza maswali kwa shahidi
- Kesi ya Tundu Lissu inaendelea: Shahidi P2 aanza kuhojiwa
- Lissu tayari afikishwa mahakamani
- Waziri wa zamani wa nishati wa Ukraine akamatwa akijaribu kuondoka nchini humo
- Donald Trump awataka Hamas kuweka chini silaha
- Wito wa utatuzi wa migogoro watolewa katika kilele cha mkutano wa AU, Addis Ababa
- Washukiwa wa utekaji nyara eneo la Benue, Nigeria wakamatwa
- Netanyahu asema makubaliano ya Marekani na Iran lazima yajumuishe kuharibu miundombinu ya nyuklia
Moja kwa moja
Asha Juma & Rashid Abdallah
Jeshi la Wanamaji la Iran lafanya mazoezi baharini
Idara ya Mahusiano ya Umma ya Jeshi la Wanamaji la Iran (IRGC} imetangaza kufanyika kwa mazoezi katika eneo la Mlango wa Hormuz, ikisema lengo ni kuchunguza utayari wa vitengo vya Jeshi la Wanamaji la IRGC kukabiliana na vitisho vinavyoweza kutokea vya kijeshi.
Shirika la habari la IRNA, likinukuu idara ya mahusiano ya umma ya IRGC, liliripoti kwamba mazoezi hayo yalifanyika chini ya kauli mbiu ya "Udhibiti wa Mlango wa Hormuz."
Kulingana na ripoti hiyo, malengo ya mazoezi hayo hili ni pamoja na "kuchunguza utayari wa vitengo vya Jeshi la Wanamaji la IRGC, kukagua mipango ya usalama ya IRGC na hatua za kijeshi dhidi ya kukabiliana na vitisho vya usalama na kijeshi katika eneo la Mlango wa Hormuz."
Mazoezi hayo yanafanyika usiku wa kuamkia duru mpya ya mazungumzo kati ya Tehran na Washington, na huku meli ya kubeba ndege za kijeshi ya Gerald R. Ford ya jeshi la Wanamaji la Marekani, ikielekea Mashariki ya Kati kujiunga na meli ya kubeba ndege za kivita ya Abraham Lincoln na kikosi chake kazi.
Ligi Kuu England itasimamisha mechi kuruhusu wachezaji Waislamu kufungua swaumu
Ligi Kuu England na Ligi ya Soka ya Uingereza zitaanza tena taratibu zao Ramadhani kwa mechi kusimama kwa muda mfupi ili kuwapa nafasi wachezaji Waislamu kufungua.
Ramadhani inaanza wiki hii na itadumu kwa mwezi mmoja. Wakati wa Ramadhani Waislamu hujizuia kula na kunywa kuanzia alfajiri hadi machweo ya jua.
Kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, manahodha wa klabu pamoja na maafisa wa mechi watakubaliana muda wa kupumzika katika mchezo ili kuwaruhusu wachezaji Waislamu au maafisa wa mechi kupata iftari.
Timu na maafisa wa mechi watajadiliana mapema kama kuna uhitaji wa kusimamisha mchezo.
Mchezo hautasimama wakati mechi ikiendelea, lakini utasimama wakati wa kupiga mpira wa adhabu, baada ya goli, au mpira wa kurusha.
Mwaka 2021, makubaliano yaliwekwa ili kuwaruhusu wachezaji Waislamu kupata iftari wakati wa mechi za Ligi Kuu.
Mapumziko haya ya kwanza yalifanyika katika mchezo kati ya Leicester City na Crystal Palace Aprili 2021. Mechi hiyo ilisitishwa wakati wa mpira wa adhabu kuruhusu Wesley Fofana wa Leicester na Cheikhou Kouyate wa Palace kufungua swaumu.
Mojawapo ya nguzo tano za Uislamu ni kwamba wakati wa Ramadhani, Waislamu hufunga wakati wa mchana.
Wachezaji Waislamu katika Ligi Kuu ni pamoja na Mohamed Salah, William Saliba, Rayan Ait-Nouri na Amad Diallo miongoni mwa wengine.
Mwaka 2022, mchezaji wa zamani wa Liverpool Sadio Mane alifichua kwamba klabu hiyo ilibadilisha ratiba zao za mazoezi ili kuwasaidia wachezaji Waislamu wakati wa mwezi wa Ramadhani.
Obama afafanua kauli yake kuhusu 'majanabi' baada ya kusema 'ni kweli wapo’
Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amefafanua kwamba uwezekano wa dunia kutembelewa na viumbe hai (majanabi) ni "mdogo" baada ya maoni aliyotoa kuhusu viumbe vya nje ya dunia kuzusha mjadala mtandaoni.
"Wapo lakini sijawaona," alimwambia mtangazaji wa Marekani Brian Tyler Cohen wakati wa mahojiano ya mtandaoni yaliyochapishwa Jumamosi.
"Hawahifadhiwi katika Eneo la 51. Hakuna kituo cha chini ya ardhi wanakohifadhiwa, labda iwe wanajificha wasionekane na rais wa Marekani," aliongeza.
Lakini Obama amefafanua kauli yake kwa kusema: "Kitakwimu, ulimwengu ni mkubwa sana kiasi kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa maisha huko nje. Lakini umbali kati ya mifumo ya jua ni mkubwa sana kiasi kwamba nafasi ya kumetembelewa na viumbe vya kigeni ni ndogo, na sikuona ushahidi wowote wakati wa urais wangu kwamba viumbe vya nje ya sayari vimewasiliana!"
Obama, alihudumu kama rais wa Marekani kati ya 2009 na 2017, hapo awali alisema kuhusu majanabi na UFO - akimwambia mtangazaji wa televisheni James Corden mwaka 2021 kwamba alipoingia madarakani aliuliza kama kuna maabara "ambapo tunahifadhi vielelezo juu ya viumbe wa kigeni na chombo cha anga za juu cha kigeni."
"Walifanya utafiti na jibu lilikuwa hapana," alisema.
Pia unaweza kusoma:
Kenya yaagiza uchunguzi kuhusu raia wa Urusi ambaye amekuwa akiwarekodi kisiri wanawake wa Kenya
Serikali imeagiza vyombo vya usalama na uchunguzi kuchunguza haraka tukio ambalo raia wa Urusi anadaiwa kurekodi kwa siri na kusambaza picha za wanawake wa Kenya bila idhini yao.
Katika taarifa, Waziri wa jinsia Hanna Cheptumo alikashifu kisa hicho akielezea kama aina ya unyanyasaji wa kijinsia unaowezeshwa na teknolojia ambao unatishia usalama wa wanawake na wasichana.
Kama Serikali, tunaona ukiukaji kama huo sio tu kitendo cha uhalifu lakini pia vitisho kwa mfumo wa jamii yetu, ambayo msingi wake ni heshima, utu na ulinzi wa watu walio hatarini," Cheptumo alisema.
Waziri huyo alisema Serikali itachukua hatua kali huku mashirika husika yakiagizwa kufuatilia suala hilo mara moja, ikiwa ni pamoja na ushirikiano na mamlaka za kimataifa kutokana na hali yake ya kuvuka mpaka.
"Mtu yeyote atakayepatikana na hatia atakabiliwa na nguvu kamili ya sheria za Kenya chini ya Kanuni ya Adhabu, Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandaoni, na sheria zote muhimu zinazolinda wanawake na watoto," alisema.
Aidha amewataka wananchi kujiepusha na kushiriki au kusambaza maudhui, akionya kuwa kufanya hivyo kunaendeleza unyanyasaji na kunaweza kuvutia dhima ya uhalifu.
Wakati huohuo Msemaji wa serikali Isaac Mwaura amelilaani vitendo vya mwanamume huyo, akimshutumu kwa kuwadhulumu wanawake na kukiuka faragha yao kwa kurekodi majibizano yao na kushiriki picha mtandaoni bila ridhaa.
"Ninamlaani mwanamume wa Urusi kwa kuwadhulumu wanawake wetu," Mwaura alisema. "Hata hivyo, kama Waafrika, lazima pia tujifunze kujipenda wenyewe. Wanawake wetu hawapaswi kutambua kwamba kila mtu ambaye ni mzungu ni tajiri moja kwa moja."
Katika muda wa saa 24 zilizopita, mwanamume mwenye asili ya Kirusi, aliyejulikana tu kama Yaytseslav, amekuwa akivuma kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii.
Hii inafuatia ufichuzi kuwa amekuwa akirekodi kwa siri matukio ya faragha na wanawake wengi barani Afrika na kushiriki video hizo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Vitendo vyake vilidhihirika hivi majuzi baada ya kutoa msururu wa video zilizowashirikisha wanawake wa Ghana, jambo ambalo lilipelekea uchunguzi zaidi.
Uchunguzi wa kina ulibaini kuwa Yaytseslav ameripotiwa kushiriki video za wanawake kutoka Kenya, Afrika Kusini, Ghana, na nchi nyingine nyingi za Afrika.
Iran iko tayari kuruhusu ukaguzi katika vituo vyake vya nyuklia
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Kitaifa la Iran, Ali Larijan amesema Tehran itaruhusu ziara katika vituo vya chini ya ardhi na chini ya milimani ili kuthibitisha kwamba mpango wake wa nyuklia ni kwa ajili ya amani.
Katika mahojiano na Al Jazeera, Larijani amesema "ili kushughulikia wasiwasi wa wengine, ni lazima tukubali kanuni za Shirika la Kimataifa la Nishati ya Nyuklia (IAEA). Tulipokubali mkataba wa NPT, pia tulikubali mfumo wa ufuatiliaji wa Shirika hilo. Ukaguzi unaweza kubadilishwa; kila mwezi au hata kila siku, ili kubaini shughuli yoyote ya kutiliwa shaka."
Katibu wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Iran amesema: "Hata kama teknolojia hiyo iko chini ya ardhi au mlimani, hakuna tatizo; Shirika linaweza kuifuatilia na tunaruhusu ufuatiliaji huu."
Alisisitiza kwamba "suala la makombora halina uhusiano wowote na mazungumzo na halitajadiliwa katika mazungumzo haya."
Kwa upande mwingine rais wa Marekani, Donald Trump amesema masafa ya makombora ya Iran ni mojawapo ya masharti yake ya kufanya mazungumzo na Iran.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu pia ameonya jana kwamba katika makubaliano yoyote na Iran, kuacha kurutubisha urani hakutatosha bali miundombinu yote ya nyuklia lazima ivunjwe.
Pia alisisitiza kwamba makubaliano yoyote na Iran lazima yajumuishe suala la makombora ya balestiki.
Pia unaweza kusoma:
Wanajeshi wa Nigeria wazuia mashambulizi ya wanamgambo wa Kiislamu
Wanajeshi wa Nigeria wamezuia mashambulizi ya wanamgambo wa Kiislamu katika kambi mbili za kijeshi katika jimbo la Borno, na kusababisha idadi isiyojulikana ya wanajeshi kuuawa, limesema jeshi Jumatatu.
Borno, kitovu cha uasi wa makundi ya Kiislamu kwa miaka 17 nchini Nigeria, imeshuhudia wapiganaji wa Boko Haram na Islamic State West Africa Province (ISWAP) wakizidisha mashambulizi dhidi ya wanajeshi na raia.
Mashambulizi yaliyoratibiwa ya wikendi yalilenga Pulka, karibu na mpaka wa Cameroon, na Mandaragirau kusini mwa Borno.
Msemaji wa jeshi Sani Uba amesema ISWAP ilianzisha shambulio kwa kutumia malori na pikipiki huko Mandaragirau, lakini wanajeshi walizuia shambulio.
Baadhi ya wanajeshi na wanachama wa Kikosi cha Pamoja cha Raia waliuawa vitani, na waliojeruhiwa walisafirishwa kwa ndege kwa matibabu, Uba alisema, bila kutoa maelezo zaidi.
Katika shambulio la pili, wapiganaji wa Boko Haram na ISWAP walijitosa katika eneo la wanajeshi huko Pulka Jumamosi jioni, wakivunja mzingiro na kuharibu malazi na baadhi ya vifaa.
Wanajeshi walipambana, na kwa msaada wa vikosi vingine, waliwarudisha nyuma wanamgambo, amesema Uba.
Jeshi lilisema hakuna wanajeshi waliojeruhiwa katika shambulio la Pulka, ingawa taarifa za kijasusi za kuaminika zinaonyesha kuwa waasi walipata hasara kubwa, ikiwa ni pamoja na kifo cha kamanda mkuu Abou Aisha kutokana na jeraha la risasi shingoni.
Uba alisema shughuli za ufuatiliaji zilifichua njia za damu, makaburi yasiyo na kina kirefu na vifaa vilivyoachwa.
Pia unaweza kusoma:
Kimbunga chauwa watu 59 Madagascar
Watu 59 wamefariki wakati Kimbunga Gezani kilipopiga Madagaska wiki iliyopita, ofisi ya usimamizi wa maafa imesema siku ya Jumatatu, wakati ikitathmini athari za dhoruba ya pili kupiga taifa hilo la kisiwa cha Bahari ya Hindi mwaka huu.
Kimbunga hicho kilisababisha watu 16,428 kupoteza makazi yao, huku watu 15 wakiwa hawajulikani walipo, 804 walijeruhiwa na 423,986 waliorodheshwa kama walioathiriwa na janga hilo, imesema Ofisi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Hatari na Maafa (BNGRC).
Gezani kilipiga nchi nzima siku 10 tu baada ya Kimbunga cha Tropical Fytia kuua watu 14 na zaidi ya watu zaidi ya 31,000 kukimbia makazi yao, kulingana na ofisi ya masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.
Katika kilele chake, kimbunga Gezani kilivuma kwa upepo wa kasi ya kilomita 185 (maili 115) kwa saa, huku upepo ukipanda hadi karibu kilomita 270 kwa saa - wenye nguvu ya kutosha kurarua mabati ya chuma kutoka kwenye paa na kung'oa miti mikubwa.
Kimbunga hicho kilielekea magharibi kupitia Mto Msumbiji, na kusababisha upepo mkali na mawimbi ya hadi mita 10 kusini mwa Msumbiji, imesema mamlaka ya nchi hiyo.
Pia unaweza kusoma:
Mshukiwa wa mauaji ya Bondi Beach afikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza
Mshukiwa wa mauaji ya Bondi Beach, Naveed Akram, amefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza siku ya Jumatatu, miezi miwili baada ya yeye na baba yake kushukiwa kutekeleza shambulio la risasi nchini Australia.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 24 alifikishwa mahakamani huko Sydney na anakabiliwa na mashtaka 59 yanayohusiana na ufyatuaji risasi huko Bondi Beach, ikiwa ni pamoja na mashtaka 15 ya mauaji na moja ya kufanya shambulio la kigaidi.
Inadaiwa Naveed na baba yake, Sajid, walifanya shambulio katika sherehe ya Hanukkah katika ufuo maarufu Desemba 14, na kuwaua watu 15 na kuwajeruhi zaidi ya 40.
Sajid, mwenye umri wa miaka 50, alipigwa risasi na kuuawa na polisi katika eneo la tukio, huku Naveed akijeruhiwa vibaya na baadaye kupelekwa hospitalini kisha gerezani.
Jumatatu ilikuwa mara ya kwanza Akram kuonekana na kuzungumza tangu kukamatwa kwake.
Akram anatarajiwa kufikishwa mahakamani mwezi Aprili.
Pia unaweza kusoma:
Kesi ya Tundu Lissu yaahirishwa hadi kesho
Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Tundu Lissu imeahirishwa hadi kesho saa nne asubuhi.
Kuahirishwa huko kumetokana na kushindwa kuwasili kwa shahidi wa tatu.
Tundu Lissu aanza kumuhoji Shahidi P8
Lissu: Shahidi unanisikia?
Shahidi: Ndiyo nakusikia
Lissu: Maelezo uliyoandika polisi 22-04-2025 unaweza kuyatambua wakikuonesha
Shahidi: Hilo sio jukumi langu ni jukumu la mawakili
Lissu: Hayo maelezo uliyotoa polisi tarehe 22-04-2025 utayatambua?
Shahidi: Ndiyo maana nasema hilo ni jukumu la mawakili
Jaji: Elewa swali la mshatakiwa, utayatambua maelezo?
Shahidi: Kuyatambua nitayatambua kwakua mimi ndiyo niliyeyatoa
Lissu: Naomba shahidi aonyeshwe maelezo yake ya tarehe 22-04-2025
Shahidi anaepelekewa maelezo kwenye chumba chake cha siri
Lissu: Umeyatapata?
Shahidi: Bila shaka
Lissu: unayatambua maelezo hayo na yana sahihi yako?
Shahidi: Bila shaka
Lissu: Naomba kusoma maelezo yako baada ya hapo nitamueleza maeneo ninapopingana naye kisha awasilishe kama kielelezo mahakamani.
Lissu: Waeleze majaji kama maelezo (aliyosoma Lissu) yapo sahihi na maelezo yako?
Shahidi: Bila shaka
Lissu: Bila shaka nini?
Shahidi: Yapo sahihi
Lissu: Waeleze majaji kama ungependa maelezo yako yawasilishwe kama sehemu ya ushahidi
Shahidi: Ndiyo
Lissu: Swali langu la kwamza likatokana na ushahidi uliotoa, unasema tarehe 25 ulikuwa na simu ya Oppos F1s simu janja ni kweli sio kweli?
Shahidi: Ni kweli
Lissu: Naomba uwaaeleze majaji katika maelezo yako kuna sehemu ulisema ulikuwa na simu?
Shahidi: Kwenye maelezo haya hakuna sehemu nilisema nina simu
Lissu: Waelezo majaji katika maelezo kama kuna sehemu ulisema ulikuwa na simu janja aina ya Oppo 1FS
Shahidi: Hapana hakuna
Lissu: Waeleze majaji kama kuna sehemu ulisema ulikuwa na bando ama MB
Shahidi: Hakuna
Lissu: Asante
Lissu: Waeleze majaji kama kwenye maelezo yako kuna sehemu ulisema ulikuwa na bando
Shahidi: Hakuna
Lissu: Waeleze majaji kama siku hiyo ya tarehe 4-4-2025 uliona video yoyote kwenye Facebook au Youtube na ulionyesha kwenye maelezo yako
Shahidi: Kwenye maelezo sikuandika
Lissu: Unasema uliingia kwenye account ya Jambo TV na ukiona Tundu Lissu akisema tutafanya uasi
Shahidi: Ndiyo
Lissu: Naomba uwaeleze majaji kwenye maelezo yako kama kuna sehemu ulisema hivyo
Shahidi: Kwenye maelezo yangu hakuna hayo
Lissu: Unasema ulivyokamatwa na kupekelekwa kwa RCO ulikabidhiwa kwa afande Rashid kuandika maelezo yako ni kweli sio kweli?
Shahidi: Ni kweli
Lissu: Elezea majaji kulingana na maelezo yako kama kuna sehemu yoyote ulieleza juu ya wewe kuchukuliwa maelezo yako na Rashidi
Shahhidi; Hakuna sehemu kama hiyo
Lissu: Waeleze majaji kama kwenye maelezo yako kuna sehemu ulihojiwa kwa nini unahamasisha vijana kufanya uasi
Shahidi: Hayapo
Lissu: Umesema ulipohojiwa kwa nini unahamasisha vijana kufanya uasi dhidi ya serikali kwa kuunga mkono NRNE
Shahidi: Ndiyo
Lissu: Waeleze majaji ni wapi kwenye maelezo yako ulisema juu ya kuhojiwa kwako
Shahidi: Hayapo
Lissu: Umesema ulipelekwa kwenye ofisi RCO kuhojiwa ukiwekwa mahabusu
Shahidi: Ndiyo
Lissu: Waeleze majaji kama kuna sehemu yoyote kwenye maelezo yako ulisema juu ya kuwekwa mahabusu
Shahidi: Hakuna
Lissu: Umesema uliporipoti 22-04-2025 ulikabidhiwa kwa afande mwingine anaitwa Michael
Shahidi: Kweli
Lissu: Kwa mujibu wa maelezo yako waeleze majaji ni wapi ulieleza kuwa ukichukuliwa na kupelekwa afande Michael
Shahidi: Hakuna
Lissu: Nitakuwa nakosea nikisema ulishindwa kusema mambo haya kwa polisi kwakua haya umuhimu kwa polisi kuyajua?
Shahidi: Utakuwa unakosea
Lissu: Umeileza mahakama ni kwa nini ulishimdwa kuwaeleza polisi leo hapa mahakamani
Shahidi: Sikusema lakini naweza kutoa sababu
Lissu: Muda wa kutoa sababu umepita
Lissu: Unafahamu maana ya neno kukinukisha kwa kiswahili?
Shahidi: Kukinukisha ni kiswahili hivyo naelewa
Lissu: Kukinukisha inatokana na kunuka au kunukia. Je, una fahamu maana ya kukinukisha?
Shahidi: Si…
Lissu: Ulikamatwa kwa kosa la kufanya vurugu hiyo kesi ipo wapi?
Shahidi: Nilipokamatwa sikujua kama nitaachiwa mimi kijana mdogo nina malengo yangu na nilisema ukweli wangu kama unavyojua ukweli humuweka mtu huru na hata ningekataa serikali ingenikamata
Lissu: Sina maswali ziada
Watu waangua kicheko baada ya shahidi kuishukuru serikali kwa kumfutia kesi
Shahidi P8 amemaliza kuhojiwa.
Kesi ya Tundu Lissu inaendelea: Shahidi P8 aanza kuhojiwa
Shahidi P8 anapandishwa kizimbani naye anaanza kwa kujitambulisha kuwa ana miaka 26 na dini yake ni Mkristo.
Wakili: Nikumbushe tarehe 8 April unakumbuka nini?
Shahidi: Nakumbuka nikiwa katika shughuli zangu za kuhamasisha vijana maeneo ya Njoro Pespi
Wakili: Ulisema nini kwa vijana una hamasisha?
Shahidi: No reform no election
Wakili: Nini kikatokea?
Shahdi: Nilishangaa tu ghafla nimekamatwa na vijana wenzangu walikimbia
Wakili: Baada ya kukamatwa nini kilitokea?
Shahidi: Nilipelekwa ofisi za RCO Moshi
Wakili: Nini kilitokea hapo kwa RCO?
Shahidi: Nilifikishwa kwa Afande anaitwa Rashidi kuandika maelezo
Wakili: Nini kikaendelea baada ya kufika kwa RCO?
Shahidi: Niliulizwa maswali kwakua nilikuwa naogopa nilisema ukweli wote
Wakili: Uliulizwa maswali gani?
Shahidi: Kwanza alinuuliza ninapoishia pia akaniuliza kwa nini nahamaasisha vijana kufanya uasi
Wakili: Kwa Afande Rashid ni ukweli upi ulisema?
Shahidi: Kwamba nahamasisha vijana kufanya uasi dhidi ya serikali na kuunga mkono kauli ya mwenyekiti wa Chama
Wakili: Baada ya kueleza hayo?
Shahidi: Kulikuwa na kituo cha polisi ambapo nilipelekwa huko na kukaa mahabusu kwa saa kadhaa majira saa 11 jioni niliachiwa kwa dhamana
Wakili: Dhamana ilikutaka ufanye nini?
Shahidi: Nilijidhamini mwenyewe na kuambiwa kila Jumatatu nije kuripoti polisi kuanzia Jumatatu ya tarehe 14-4-2025 nikapangiwa kuripoti tena tarehe 21 kwakua ilikuwa Pasaka nikaambiwa nifike 22-4-2025
Wakili: 22-04-2025 ikawaje?
Shahidi: Nilifika ofisini saa 2 asubuh nikaripoti na nikafuatwa na Afande mmoja kupelekwa ofisini kwa Afande Michael
Wakili: Ofisini kwa Afande Michael nini kiliendelea?
Shahidi: Alinichukua maelezo kama nikivyoeleza hapo awali
Wakili: Ni hayo tu kwa upande wangu.
Mgomo wa usafiri wa anga wavuruga safari za ndege Kenya
Usumbufu umeripotiwa katika viwanja vya ndege kote Kenya baada ya wafanyakazi wa usafiri wa anga kuanza mgomo kufuatia mzozo kuhusu mishahara na mazingira ya kazi.
Shirika la ndege la kitaifa ambalo husimamia viwanja vya ndege nchini humo limesema uwanja wa ndege mkuu wa Kenya katika mji mkuu, Nairobi, unakabiliwa na ndege kuchelewa kuondoka na kutua siku ya Jumatatu kutokana na mgomo huo.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya imetoa taarifa Jumatatu ikiarifu umma kuhusu athari za mgomo huo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kati ya wafanyakazi wa usafiri wa anga na mamlaka ya usafiri wa anga.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta ni mojawapo ya vituo vya usafiri vyenye shughuli nyingi barani Afrika, ukihudumia mamilioni ya abiria kila mwaka.
Shirika la ndege la Kenya Airways, shirika la ndege la kitaifa la nchi hiyo, pia limesema linakabiliwa na changamoto za uendeshaji zinazoathiri safari za ndege kuondoka na kuwasili.
Mzozo wa wafanyakazi kati ya chama cha wafanyakazi wa usafiri wa anga na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya unatokana na malalamiko ya wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na kushindwa kuhitimishwa kwa makubaliano kati yao, wasiwasi wa mishahara, na masuala yanayohusiana na mazingira ya kazi.
Maafisa wa chama hicho wanasema mgomo utaendelea hadi mazungumzo yenye maana yatakapofanyika na madai yao kushughulikiwa.
Wiki iliyopita, muungano huo ulitoa notisi ya mgomo wa siku saba, na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya iliwasiliana na mahakama katika jaribio la kuzuia hatua hiyo.
Pia unaweza kusoma:
Tundu Lissu amemeliza kumhoji shahidi wa kificho P2
Lissu: Umeleza mahakama kwamba uliona video ya mkutano wangu na wanahabari tarehe 4-4-2025 ni kweli sio kweli?
Shahidi: Kweli
Lissu: umewaonyesha majaji video hiyo iliyoiona?
Shahidi: Hapana
Lissu: Umewasilisha video hiyo kama kielelezo mahakamani
Shahidi: Sijui
Lissu: Majaji watajuaje kama kweli ulitazama video hiyo?
Shahidi: Waende kwenye mtandao wa Youtube wataiona
Lissu: Kwa hiyo majaji watafute bando…sasa unasema ulikamtwa na polisi ni kweli sio kweli?
Shahidi: Ni kweli
Lissu: Waelekeze majaji kwa ufahamu wako kwenda kusikiliza maelekezo ya viongozi wa chama, kwa nini mwenyekiti amekamtwa na mkutano kuzuiliwa ni kosa kisheria?
Shahidi: Sijui sheria
Lissu: Ni kweli kwamba mkutano uliozuiliwa ulitolewa taarifa kamili kwa polisi?
Shahidi: Sifahamu
Lissu: Umeeleza kuwa ulikamatwa na kupelekwa kituo cha polisi kwa kosa la kochochea ni kweli sio kweli?
Shahidi: Ni kweli
Lissu: Ulipokwenda mfaranyaki kusikiliza maelekezo ya viongozi wa chama ulienda kuchochea au kufanya vurugu?
Shahidi: Sijui
Lissu:Ulikamatwa bila kosa?
Shahidi: Sijui
Lissu: Baada ya kukamatwa ulifunguliwa kesi ya uchochezi mahakamani?
Shahidi: Hapana
Lissu: Kwa hiyo hawa polisi walikukamata bure na kukupa kesi ya uchochezi uli uwe shahidi kwenye kesi ya mwenyekiti?
Shahidi: Sijui
Lissu: Ilikuwaje kesi yako ya uchochezi kuisha na wewe ukazaliwa kuwa shahidi?
Shahidi: Sijui
Lissu: Ieleze mahakama kama uliwasiliana na polisi juu ya kesi kabla ya hapo?
Shahidi: Sikufanya mawasiliano
Lissu: Kuna mahala popote ulipoandika maelekezo kuhusu kesi hii tangu mwaka jana mpaka mwaka huu?
Shahidi: Hapana
Lissu: Kuna taarifa yoyote umepeleka polisi tangu tarehe 24-4 mwaka jana mpaka ulipoletwa vito wa kufika kwenye kesi hii?
Shahidi: Hapana
Lissu: Kuna kiongozi wa CHADEMA yoyote aliyekutishia kukuuwa?
Shahidi: Hapana
Lissu: Kuna mwanachama amekutishia kukuuwa?
Shahidi: Hapana
Lissu: Kuna mwanachama au kiongozi yoyote alikutishia kukudhulumu kutokana na kesi hii?
Shahidi: Hapana isipokuwa vitisho kwenye mitandao ya kijamii
Lissu: Uliripoti polisi unaweza kuwataja?
Shahidi: Hapana na siwajui
Lissu: Nataka uangalie hayo maelezo yako hasa kielelezo D6 nataka kuuliza kuhusu siku ya April 7, 2025 majira ya saa 7 mchana waeleze majaji kama ulikuwa na mwandishi yoyote wa jambo TV?
Shahidi: Sikua naye
Lissu: Waeleze majaji kama siku hiyo wewe na mwandishi wa Jambo TV mlienda makao makuu ya upelelezi Dodoma na kukutana na afisa upelelezi Andrew Chunu?
Shahidi: Sio kweli
Lissu: Kuna mtu anaitwa Adrew Chunu anasema kuwa wewe pamoja na P mlikutana na chunu kwenye makao makuu ya upelelezi Dodoma na kushuhudia makabidhiano ya memory card kati ya P na inspector Chunu
Shahidi: Sio kweli
Lissu: Hivyo ndivyo wanavyosema polisi kwenye makaratasi yao hivyo ni kweli ulikuwa dodoma makao makuu ya upelelezi?
Shahidi: sikuwa Dodoma
Lissu: Waeleze majaji kama katika hotuba yangu nilisema watu wakafanye fujo
Shahidi: Sikusema
Lissu: Waeleze majaji kama kusema “tutazuia uchaguzi ni kosa la jinai kwa sheria za nchi hii”
Shahidi: Sijui sheria
Lissu: Unasema kwamba uliaminishwa na maneno yangu ya kwenye hotuba Je, ni kosa kisheria
Shahidi: Sijui!
Lissu: Sina mswali zaidi
Tundu Lissu amemeliza kumhoji shahidi wa kificho P2
Lissu amuuliza shahidi 'tutajuaje kama wewe sio chawa wa Mama'
Lissu: Naomba shahidi apewe kielelezo D6
Lissu: Umepata kielelezo shahidi?
Shahidi: Ndiyo nimepata
Lissu: Unasema tarehe 22-04-2025 ulipelekwa kituo cha polisi cha Central kuchukuliwa maelezo hayo ni kweli sio kweli?
Shahidi: Ni kweli
Lissu: Sasa naomba uwaeleze majaji mahali popote ulipozungumzia tarehe 22-04-2025
Shahidi: Sikuzungumzia lakini nilisaini
Lissu: Kwa hiyo shahidi katika karatasi hii, sehemu ya kuwa ulipelekwa kituo cha Central na ukachukuliwa maelezo tarehe 22-04-2025 yapo?
Shahidi: Hapana lakini ni maelekezo ya siku moja
Lissu: Katika maelezo yako kuna sehemu umetaja kituo kikuu cha polisi Songea?
Shahidi: Sijakitaja
Lissu: Shahidi kwenye ushahidi wako uliulizwa unamfahamu vipi huyu Lissu, ukasema unamfamu kwa sababu ni mwanasiasa maarufu na anafahamika na watu wengi?
Shahidi: Ndiyo
Lissu: Katika maelezo yako Je, kuna sehemu umesema hayo?
Shahidi: Hakuna ila mimi ni mfuasi wako
Lissu: Taratibu kaka tutafika kwenye ufuasi wako, turudi tarehe 4 kwenye maelezo yako, unasema uliona kwenye mtandao wa kijamii, mweyekiti akifanya mkutano na waandishi wa habari siku hiyo, hayo maelezo yapo kwenye maelezo yako?
Shahidi: Hapana hayapo
Lissu: Umeieleza mahakama kwamba kwenye video ulioona kwenye mtandao wa kijamii, inasema kuwa mwenyekiti ametuelekeza kuwa hakutakuwa na uchaguzi. Sasa naomba uangalie maelekezo yako na uwaeleze majaji kama maelezo hayo yapo?
Shahidi: Ndiyo yapo
Lissu: Kwa uelewa wako maneno “wanaotaka kugombea udiwani, ubunge na uraisi wasahau” yapo? Wafuasi wangu wanakuwa na akili unaanza kunipa wasiwasi.
Shahidi: Hayapo
Lissu: Umesema kwenye maelezo yako kuwa wewe ni mfuasi wa CHADEMA, Je, kuna alama mtu anawekwa kichwani ili kujulikana kama ni mfuasi wa CHADEMA?
Shahidi: Sijui
Lissu: Una kadi ya CHADEMA?
Shahidi: Hapana
Lissu: Sasa kama huna kadi na huna chapa usoni majaji watajuaje kama wewe ni mfuasi wa chadema?
Shahidi: Sijui kwa utaalamu wangu
Lissu: Unakitambulisho chochote cha kuthibitisha ufuasi wako wa CHADEMA?
Shahidi: Sina
Lissu: Sasa tutajuaje kama wewe sio chawa wa Mama… shahidi umesema umechangia michango mbalimbali ya chama?
Shahidi: Ndiyo
Lissu: Umesema ulilipa pesa kwenye mitandao, Je, siku hizi pesa za uwanachama zinalipwa kwa mitandao?
Shahidi: Sijui
Lissu: Una risiti?
Shahidi: Sina nilitoa kwa imani kwakua anayechangisha ni kiongozi
Lissu: Tutajuaje kama ulilipa elfu 10 ya uwanachama…Je, tutajuaje kama ulilipia?
Shahidi: Siwezi kujua
Soma zaidi:
Lissu aomba kumuhoji shahidi juu ya maneno aliyosema yapo sahihi
Lissu: Naomba unieleze kama niliyosoma yapo sahihi kwa mujibu wa karatasi uliyonayo?
Shahidi: Yapo sahihi
Lissu: Nataka nikuhoji juu ya maneno uliyosema yapo sahihi kwa kujibu wa maelezo yako unasema tarehe 4-4-2025, ukiwa unapitia mitandao ya kijamii ukiona mkutano wa Lissu na waandishi wa habari
Shahidi: Ndiyo ni sahihi
Lissu: Unasema uliona video yangu ikisema “hakuna mwanachama wa CHADEMA atagombea nafasi ya ubunge au urais…” Je, hiyo ni sahihi
Shahidi: Ndiyo ni sahihi
Lissu: Sehemu ya tatu ni juu ya ulipoulizwa kama unamfahamu Mheshimiwa Tundu Lissu na wewe ni mfuasi wake toka akiwa bungeni ni sahihi?
Shahidi: Ni sahihi
Lissu: Sasa nataka uwaeleze majaji kama unataka hayo maelezo yako yawasilishwe mahakamani
Shahidi: Sawa yawasilishe
Jaji aruhusu Lissu aanze kuuliza maswali kwa shahidi
Lissu: Shahidi unanisikia sawa sawa?
Shahidi: Hapana sikusikii
Lissu: Na kelele zote hizi unisikii?
Shahidi: Nakusikia
Lissu: Swali langu la kwanza waelezee majaji kama uliandika maelezo polisi
Shahidi: Nilichukuliwa maelezo polisi
Lissu: Ndiyo haya maeleo ya tarehe 22/04/2025 uliyasaini maelezo hayo?
Shahidi: Ndiyo nilisaini
Lissu: Je ukioneshwa maelezo hayo utayatambua?
Shahidi: Ndiyo
Lissu: Naomba shahidi aonyeshwe maelezo ya tarehe 22/04/2025.
Lissu: Naomba nikusome maelezo uliyoyasaini polisi baada ya hapo nitauliza maswali
"Umesema watazuia uchaguzi Je, unajua ni namna gani watazuia uchaguzi?", Wakili auliza
Upande wa mashataka: Nini kiliendelea huko mjini?
Shahidi: Nilipofika pale niliona viongozi wa kitaifa wa chama wakiita waandishi wazungumze nao lakini wakaingia polisi na kutuweka chini ya ulinzi. Katika purukushani nikajikuta nimekamatwa na kupelekwa kituo cha polisi karibu na ofisi ya mkuu wa mkoa Ruvuma.
Upande wa Mashataka: Nini kiliendelea kituoni?
Shahidi: Niliwekwa maabusu na baadaye nikahojiwa na polisi juu ya tuhuma nilizokutwa nazo
Wakili: Nini kiliendelea?
Shahidi: Baada ya kuchukuliwa maelezo niliachiliwa kwa dhamana nikaambiwa niripoti kila jumatatu kituoni.
Wakili: Nini kiliendelea?
Shahidi: Nilianza kuripoti pale polisi lakini siku ya Jumatatu iliyofuata nilipangiwa kuja siku nyingine maana ilikiwa siku ya Pasaka.
Wakili: Umekuwa ukimtaja Tundu Lissu kama mwenyekiti wa chama, Je, unamfahamu vipi ukiwa Songea?
Shahidi: Ni mwanasiasa na nimekuwa nikimfahamu kwenye mitandao ya kijamii na harakati za chama pale alipotangaza kugombea uwenyekiti ndipo nilipoanza kuwa mfuasi wake.
Wakili: Katika maelezo yako umesema watazuia uchaguzi je unajua kwa namna gani watazuia uchaguzi?
Shahidi: Nilikiwa sijui
Soma zaidi:
Kesi ya Tundu Lissu inaendelea: Shahidi P2 aanza kuhojiwa
Shahidi P2 anaanza kuhojiwa na upande wa mashtaka na kuanza kujitambulisha kuwa anatokea Songea, Ruvuma na ni mfuasi wa CHADEMA toka mwaka 2021.
Anasema huwa anashiriki kwenye mikutano mbalimbali ya chama akiwa kama mwanachama wa CHADEMA.
Tarehe 4.4.2025 alikuwa kwenye manispaa ya Songea akifanya shughuli zake za kawaida na wakati anapitia mitandao ya kijamii alikutana na video za kisiasa kuhusiana na mkutano wa Lissu jijini Dar es salaam.
Shahidi: Katika maelekezo hayo alisisitiza uchaguzi usifanyike kama njia ya kuleta mageuzi. Baada ya video hiyo nilipata kujua namna jambo hilo litatekelezwa na nikanza kutafuta viongozi ili kupata uelewa zaidi.
Upande wa mashtaka: Nini kikaendelea?
Shahidi: Nikamtafuta mwenyekiti wa vijana CHADEMA Songea Esau Chiza kujua nini kitaendelea.
Upande wa Mashataka: Baada ya kumtafuta nini kiliendelea?
Shahidi: Tarehe 7-4-2025 nilitoa mchango wa shilingi 10,000 kwa ajili ya ziara ya Mheshimiwa Lissu kwenye mkoa wetu wa Ruvuma.
Upande wa mashataka: Nini kiliaendelea?
Shahidi: Tarehe 9 Aprili nikiwa kwenye shughuli zangu ndiyo nikaona kwenye taarifa ya habari Mheshimiwa mwenyekiti Lissu alikamatwa lakini ilipofika tarehe 10, nilijianda kwenda kwenye mkutano ilikupata ufafanuzi nilipofika nilikutana na magari ya polisi.
Upande wa Mashataka: Baada ya kuona hivyo ukafanya nini?
Shahidi: Nilifika kwenye ofisi za CHADEMA mjini Songea nikawasiliana na wanachama wengine nikaambiwa makamu mwenyekiti atazungumza na wanachama kutoa ufafanuzi kwa nini mkutano haukufanyika na kwa nini mwenyekiti alikamatwa.
Upande wa Mashataka: Huyo Makamu mwenyekiti ni nani?
Shahidi: Makamu Mwenyekiti ni John Heche.
Soma zaidi:
Lissu tayari afikishwa mahakamani
Karibu katika matangazo ya moja kwa moja tukikujuza kesi ya Tundu Lissu inavyoendelea mahakamani na Bosha Nyanje, Mimi ni Asha Juma.
Kesi ya kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu inarejelewa leo Jumatatu kufuatia kuahirishwa kwake siku ya Ijumaa.
Baadhi ya wafuasi wa CHADEMA walijitokeza kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu.
Tayari Lissu amefikishwa kizimbani na sasa kinachosubiriwa ni kuanza kwa kesi upande wa mashtaka, wanampadisha na shahidi.
Shahidi atakayesikilizwa leo ni shahidi P2 ambaye ni shahidi wa kificho na ataanza kwa kujitambulisha kuwa ana miaka 38 na dini yake ni mkristo.
Soma zaidi: