"Unashirikiana na mapolisi kunishtaki kwa uhaini" Lissu amwambia shahidi aliyedai mfuasi wake

Kiongozi wa chama cha upinzani CHADEMA, Tundu Lissu ameshtakiwa kwa makosa ya uhaini.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Zaidi ya Wakenya 1,000 walijiandikisha kupigana katika vita vya Urusi na Ukraine, ripoti inasema

    .

    Chanzo cha picha, Ukraine Defence Intelligence

    Maelezo ya picha, Clinton Mogesa, 29, alifariki alipokuwa akipigania Urusi

    Jumla ya Wakenya 1,000 wamesajiliwa kupigania Urusi, kulingana na ripoti ya kijasusi ya Kenya ambayo inaeleza mtandao wa maafisa wahalifu wanaodaiwa kushirikiana na makundi ya magendo ya binadamu.

    Ripoti hiyo, iliyowasilishwa bungeni siku ya Jumatano na Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi ya Kenya (NIS), ilisema Wakenya 89 walikuwa mstari wa mbele katika vita vya Urusi na Ukraine kufikia Februari mwaka huu.

    Mkenya mmoja tayari amefariki, huku wengine kadhaa wakirejea nyumbani wakiwa wamejeruhiwa au wakiwa na wasiwasi.

    Serikali ya Kenya, ambayo hapo awali ilikadiria kuwa takriban raia wake 200 walikuwa wameajiriwa kupigania Urusi, inataka Moscow kuzuia kuandikishwa kwa raia wa Kenya katika jeshi la Urusi.

    Akiwasilisha ripoti hiyo kwa wabunge, kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung'wah, alifichua kile alichokiita mtandao "unaosumbua sana" wa maafisa wa serikali walaghai wanaodaiwa kushirikiana na makundi ya magendo ya binadamu kuwaajiri na kuwasafirisha Wakenya kupigana katika vita vya Urusi na Ukraine.

    Shirika hilo la kijasusi lilieleza kwa kina jinsi mashirika ya kuajiri yamekuwa yakishirikiana na wafanyikazi walaghai wa uwanja wa ndege wa Kenya, maafisa wa uhamiaji, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), maafisa wa kupambana na mihadarati na maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira ili kurahisisha usafiri wa waajiriwa.

    Ichung'wah alidai kuwa mashirika hayo pia yamekuwa yakishirikiana na wafanyikazi katika ubalozi wa Urusi mjini Nairobi na ubalozi wa Kenya mjini Moscow kusaidia waajiri kupata visa za Urusi.

    Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, ubalozi wa Urusi mjini Nairobi ulipuuzilia mbali madai hayo na kusema ni "hatari na ya kupotosha", ukisema kuwa wafanyakazi wake hawajawahi kuhusika na "mipango ya uhuni" au kujihusisha na usajili haramu.

  2. Polisi wa Kiislamu nchini Nigeria wawakamata Waislamu tisa kwa kutofunga Ramadhani

    .

    Chanzo cha picha, Sani Maikatanga

    Polisi wa Kiislamu katika jimbo la kaskazini la Kano nchini Nigeria wamewakamata Waislamu tisa siku ya Jumatano ambao walionekana wakila chakula katika siku ya kwanza ya mfungo wa Ramadhani mwaka huu.

    Jimbo la Kano lina idadi kubwa ya Waislamu, ambapo mfumo wa kisheria wa Kiislamu - Sharia - unafanya kazi pamoja na sheria za kawaida.

    Polisi wa Kiislamu, wanaojulikana kama Hisbah, hupekua mikahawa na masoko kila mwaka wakati wa Ramadhani ili kuhakikisha Waislamu wanafuata saa za kufunga.

    Baadhi ya vituo hukaa wazi katika maeneo ya Kano ambako Wakristo wengi wanaishi.

    Kwa Waislamu, kula ni marufuku kati ya mawio na machweo.

    Kufunga ni mojawapo ya Nguzo Tano za Uislamu, ambayo inaweka msingi wa jinsi Waislamu wanavyotakiwa kuishi maisha yao.

  3. Habari za hivi punde, Mfalme Charles asema 'sheria lazima ichukue mkondo wake' baada ya Andrew kukamatwa

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mfalme Charles na mdogo wake Andrew Mountbatten

    Tumepokea taarifa kutoka kwa Mfalme Charles kufuatia kukamatwa kwa Andrew.

    Inasema hivi: Nimejifunza kwa wasiwasi mkubwa habari kuhusu Andrew Mountbatten-Windsor na tuhuma za utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma. Kinachofuata sasa ni mchakato kamili, wa haki na ufaao ambao suala hili linachunguzwa kwa njia inayofaa na mamlaka zinazofaa. Katika hili, kama nilivyosema hapo awali, wana msaada na ushirikiano wetu kamili na wa moyo wote. Niseme wazi: sheria lazima ichukue mkondo wake. Wakati mchakato huu ukiendelea, haitakuwa sawa kwangu kutoa maoni yangu zaidi juu ya suala hili. Wakati huo huo, mimi na familia yangu tutaendelea na wajibu na huduma yetu kwenu nyote.

    Charles R.

  4. Habari za hivi punde, Mfalme na Ikulu hawakuambiwa kuhusu kukamatwa kwa Andrew

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Andrew Mountbatten

    Mfalme Charles wala kasri la Buckingham Palace hawakufahamishwa mapema kwamba Andrew Mountbatten-Windsor angekamatwa hii leo, BBC News inaelewa.

    Mfalme alitoa taarifa akijibu kukamatwa kwa kaka yake muda mfupi uliopita, ambayo unaweza kusoma kwa ukamilifu hapa

  5. Shahidi: 'Niliona Lissu akihamasisha kufanya vurugu za kuzuia uchaguzi mkuu '

    Shahidi anayefuata ni shahidi wa kificho P9 anaongozwa na wakili wa upande wa mashataka ni mkaazi wa Mbeya ana umri wa miaka ni 38

    Shahidi: Nakumbuka nikiwa nyumbani kwangu nilikuwa napitia kwenye mtandao kupitia simu yangu

    Wakili: Hiyo simu yako ilikuwa ya aina gani?

    Shahidi: Samsung 8 Pro

    Wakili: Sasa ulikuwa unaperuzi vitu gani?

    Shahidi: Nakumbuka nilikuwa naperuzi kwenye account ya Instagram

    Wakili: Hiyo instagram ni kitu gani

    Shahidi: Ni mtandao wa kijamii

    Wakili: Ambao ukoje

    Shahidi: Ni mtandao wa kijamii ambao ili uingie lazima uwe na akaunti kwenye mtandao huo na siku janja yenye uwezo wa kuingia pamoja na bando

    Wakili: Vitu gani vinapatikana huko instagram

    Shahidi: Picha na video

    Wakili: Nini kiliendelea

    Shahidi: Nilipofungua niliona video ya mheshimiwa Lissu

    Wakili: Sehemu gani?

    Shahidi: Nimesahau kidogo hiyo akaunti ambayo ilituma hiyo video

    Wakili: Nini kiliendelea baada ya kuona hiyo video ya Lissu

    Shahidi: Niliona Lissu akihamasisha kufanya vurugu za kuzuia uchaguzi mkuu

    Wakili: Hiyo video huyo mhe: Lissu alikuwa kwenye mazingira gani?

    Shahidi: Alikuwa ukumbini

    Wakili: Alikuwa katika muonekano upi?

    Shahidi: Alikuwa amevalia Fulana nyeusi na nyuma yake kulikuwa na bendera ya taifa na kulikuwa na kitambaa chenye rangi za CHADEMA

    Wakili: Unasema atavuruga kwa namna gani?

    Shahidi: Kufanya vurugu na kuzuia uchaguzi usifanye lazima kichafuke Wakili ya kuona nini kilifanyika?

    Wakili: Unakumbuka nini 4-4-2025

    Shahidi: Nilikutana na wenzangu tukaendelea kujadili juu ya video niliyoiona

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Tulikuwa tunajadili kuwa kama mhe kasema atazuia uchgauzi itakuwaje tunafanye Wakili: Wakati mnaendelea nini kiliendelea?

    Shahidi: Wakati tunaendelea kujadiliana kuna jamaa yangu ambaye simfahamu kwa jina akaniomba namba yangu ili tuendele kujadili na tuakaachana kila mtu aendeleenna shughuli zake

    Wakili: 5-4-2025 ulikuwa wapi majira ya asbh na unakumbuka

    Shahidi: Nilikuwa nyumbani nikapigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwamba ni mteja anahitaji fundi umeme nyumbani kwake, baada ya hapo nikamuambia mimi ni fundi nikamuelekeza nilipo akaomba tuonane nikamuambia sawa

    Wakili: Nini kiliendelea

    Shahidi: Nikaenda sehemu ambapo tulipanga tuonane alipofika karibu tukaonana akajitambulisha akaniambia kuwa yeye ni afisa wa polisi na akanionesha kitambulisho chake cha kazi

    Wakili: Alisema yeye anatoka wapi

    Shahidi: Alijitambulisha anatokea kituo cha polisi Mwanjelwa

    Wakili: Baada ya utambulisho

    Shahidi: Akaniambia niko chini ya ulinzi tuongozane kwenda polisi kwa kosa la uchochezi na kuzuia uchaguzi

    Wakili: Baada ta kufika kituoni

    Shahidi: Tulipofika alinikabidhi nikahojiwa baada ya muda wakaja ndugu zangu wakaniwekea dhamana nikatoka wakaniambia niwe naripoti kila jumatatu ya wiki

    Wakili: 22-4-2025 unakumbuka nini?

    Shahidi: Nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha ni polisi nahitaji kituo cha Mwanjelwa, nikaelekea kituoni nikajitambulisha wakaniita ofisini wakaniambia tumekuita ukiwa kama shahidi wa hili swala lako lililokuleta hapa

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Walinihoji wakaniandikia maelezo walipomaliza waniruhusu niondoke wakasema wakiniihitaji wataniita

    Wakili: Walikuhoji watu wangapi?

    Shahidi: Alikuwa ananihoji mmoja ila mwingine alikuwa anchangia kwa kuuliza maswali

    Wakili: Alikuhoji juu ya kitu gani?

    Shahidi: Alikuwa ananiuliza swala la kuzuia uchaguzi lilianzaje na wewe kukaa na wenzio kuongea kuhusu uchaguzi

    Wakili: Ukamwambia aje?

    Shahidi: Nilimuambia niliona clip

    Wakili: Hiyo clip ni ya nani?

    Shahidi: Ya Lissu

    Wakili amemaliza kuhoji

  6. Lissu: Waeleze majaji kama kupinga mamlaka na sheria za nchi zilizopo ni uhaini? Shahidi: Sijui

    Lissu: Swali langu la pili umesema kwamba katika moja wapo ya shughuli ulizoshiriki ni pamoja na kungamano la vijana ambalo kwa ushahidi wako halikufanyika sababu uwanjani kulitawanywa

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Waeleze majaji kama kuna sehemu imeandikwa “uwanjani kulitawanywa”

    Shahidi: Hapa ni upungufu tu wa baadhi ya maneno

    Lissu: Sio upungufu yapo au hayapo

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Asante

    Lissu: Umesema kwamba hilo kongamano kwa bahati mbaya au nzuri halikufanyika ni kweli sio kweli?

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Mfuasi wa CHADEMA kongamano lisipofanyika ni bahati nzuri? Kweli si kweli

    Shahidi: Ndiyo maana nimesema bahati mbaya au nzuri sijasema nzuri moja kwa moja

    Lissu: Ndiyo maana nimekuuliza kama wewe ni pandikizi la polisi

    Shahdi: Kama kuna maswali mengine tuendelee hilo nimeshajibu

    Lissu: Kwenye ushahidi wako umesema “siku hiyo ukiwa na simu yako” ni kweli sio kweli Shahidi: kweli

    Lissu: Waeleze majaji kama maneno “nilikuwa na simu yangu “yapo kwenye karatasi?

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Unaweza au huwezi kufuatilia mtandao wa Youtube kwa kutumia tarakilishi

    Shahidi: Mimi binafsi nimezoea kwenye simu sio tarakilishi

    Lissu: Inawezekana haiwezekani

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Waeleze majaji kama unajua kufuatilia youtube kupitia Television

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Nirudie swali langu kwenye maelezo yako kuna sehemu umeandika ulikuwa na simu siku hiyo?

    Shahidi: Hakuna

    Lissu: Umesema siku hiyo uliona video fupi ikimuonesha Mhe. Lissu akihamasisha kuzuia uchaguzi?

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Kuna mashahidi wamekuja kwenye mahakama hii wamesema hiyo video ina masaa matatu na madakika mengi tueleze kwenye karatasi yako kuna sehemu umeeleza juu ya urefu wa video hiyo

    Shahidi: Hakuna

    Lissu: Kwenye ushahidi wako umesema unafahamu Tundu Lissu kupiitia mitandao ya kijamii Shahidi: Kweli

    Lissu: Kwenye maelezo yako kuna maneno hayo?

    Shahidi: Hakuna

    Lissu: Kwenye maelezo yako umesema kuwa ukishiriki mkutano uliongozwa na mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu uliofanyika Luanda Nzovwe?

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Kwa hiyo umewahi kumuona Lissu kwenye mkutano?

    Lissu: Umesema kwenye maelezo yako kuwa baada ya kuangalia video hiyo alikufuata akakuita pembeni “njoo tuonge”?

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Kwenye maelezo yako kuna maneno “njoo tuonge”?

    Shahidi: Napitia kidogo

    Shahidi anamsomea Lissu maelezo yake

    Lissu: Kuna maneno “aliniita pembeni njoo tuongee” yapo au hayapo?

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Ukasema “niliposogea pembeni akajitambulisha kama askari polisi akaniambia twende kituoni” kweli sio kweli?

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Waeleze majaji kama maneno hayo yapo

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Badala yake kuna maneno yanasema hivi “Wakati tunaendelea kubishana kuna mtu aliyejitambulisha kama afisa polisi na akanikamata kwa kuhamasisha vurugu za kuzuia uchgauzi” kwa maelezo yako alikuja na kukumata?

    Shahidi: Sahihi

    Lissu: Kwa maelezo yako unasema ulipofika polisi alikuweka maabusu na baadaye akakupeleka kwenye chumba cha mahojiano akaniambia “kwa nini unahamasisha uasi” kweli sio kweli?

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Namsomea shahidi maana ya neno uasi kwenye kamusi kuu ya kiswahili iliyotolewa na BAKITA Uasi- Kitendo cha kuwapinga wenye mamlaka iliyopo kama vile kwenye taasisi, ofisi au chama Mtu akisema atafanya uasi ni kufanya maandamano bila kufuata taratibu waeleze majaji kama kitendo hicho cha kuvunja sheria kama ni uhaini

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Waeleze majaji kama kupinga mamlaka na sheria za nchi zilizopo ni uhaini?

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Hapa nina sheria ya uchgauzi ya 2024 na kwenye sheria hiyo hakuna kosa la kuzuia uchaguzi achilia uhaini

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Sasa naelekea kumalizana na wewe swali langu la kwanza ulipokamatwa tarehe 4-4-2025 ulipelekwa kituoni ukaandika maelezo kwa tuhuma za kupanga kufanya vurugu kuzuia uchaguzi waeleze majaji hizo tuhuma ziliishia wapi?

    Shahidi: Niliripoti mpaka nilipoambiwa nitapigiwa simu kuja kutoa ushahidi kuhusu kosa langu Lissu: Umeshtakiwa kwa kosa la kula njama ya kupiga watu mawe kwenye uchgauzi?

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Ulipanga njama na polisi ili ujifanye mwanachadema uje utoe ushahidi hapa kweli sio kweli?

    Shahidi: Sio kweli

    Lissu: Kwa nini hujapelekwa mahakamani

    Shahidi: Sijui

    Lissu: Uliripoti kwa miezi mitano polisi, je polisi wanakuambia nini?

    Shahidi: Umefika nenda

    Lissu: Waeleze majaji kama katika kipindi cha miezi mitano kama umewahi kuzungumzia tuhuma zako kula njama na kupiga watu mawe

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Kwanzia mwezi wa 5 hujawahi kuwasiliana na polisi na mpaka sasa?

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Ulifikaje Dar es salaam

    Shahidi: Nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha ni askari nikapewa wito wa kuja mahakamani Lissu: Nauli alikulipia nani?

    Shahidi: Nimejilipia mwenywe

    Lissu: Hapa Dar umefikia wapi?

    Shahidi: Gesti

    Lissu: Sitaki kujua ni gesti gani ila nani analipia?

    Shahidi: Mimi mwenyewe

    Lissu: Kwa hiyo umekuja kwa kujitolea kama raia mwema? Lissu amemaliza kuhoji

  7. Lissu: 'Nitajuaje wewe sio pandikizi la polisi'?

    Shahidi: Baadaye nikampata ndugu yangu alikuja akanidhamini..nikaambiwa kila baada ya siku 3 niende kuripoti pale kituoni

    Wakili: Elezea mnamo 17-4-2025 ulikuwa wapi majjira ya asubuhi?

    Shahidi: Nilipigiwa simu natakiwa kituo cha polisi Ilomba kuna maelezo natakiwa nikatoe zaidi Wakili: Ulipofika ukafanya nini?

    Shahidi: Niliambiwa nikifika nipige namba iliyonipigia nilipopiga nikaambiwa niingie ndani nilipoingia ndani nikamkuta askari yule yule aliyeniandika maelezo mwanzo

    Wakili: Huyo askari anaitwa nani kama unamkumbuka?

    Shahidi: Namkumbuka kwa jina moja anaitwa Amani

    Wakili: Wewe na amani pale kituoni mlifanya nini?

    Shahidi: Baada ya kukutana akanihoji maswali nilipomaliza nikasaini akaniambia niendelee na utaratibu wa kuripoti tena kila baada ya siku 3

    Wakili: Kwa shahidi huyu ni hayo tu

    Wakati wa Lissu kumuuliza shahidi maswali

    Lissu: Shahidi unanisikia?

    Shahidi: Nakusikia

    Lissu: Hapo ulipo unaweza kuniona?

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Kwa taarifa yako hata mimi siwezi kukuona kwa hiyo hatuonani

    Lissu: Naomba ueleze mfuasi wa CHADEMA anakuwa na kitambulisho gani?

    Shahidi: Mfuasi wa CHADEMA anakuwa hana kitambulisho sababu anakuwa sio mwananchama

    Lissu: Anakuwa hana kitambulisho

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Mimi mwenyekiti wa CHADEMA au kiongozi wa CHADEMA aliyepo hapa atajuaje wewe ni mfuasi?

    Shahidi: Atajua

    Lissu: Hakuna namna ya kujua wewe ni mfuasi wa CHADEMA kweli sio kweli?

    Shahidi: Hakuna lakini mimi ni mfuasi wa CHADEMA

    Lissu: Eleza kama wafuasi wa CHADEMA wanaorodheshwa mahali fulani?

    Shahid: Binafsi sijajua wanaorodheshwa wapi

    Lissu: Kwa hiyo hujaorodheshwa si ndiyo?

    Shahidi: Sahihi

    Lissu: Eleza kama wafuasi wa CHADEMA kuna mahali wanaweza kujitambulisha ili wajulikane Shahidi: Wafuasi wa CHADEMA hakuna sehemu wanajitambulisha

    Lissu: Hapo ulipo kwenye hicho kisanduku na mimi hapa kizimbani waeleze majaji kama naweza kuelewa kama ni mwana CCM au ni polisi?

    Shahidi: Mimi binafsi sijui kama wewe utaelewa

    Lissu: Umesema hunioni na mimi sikuoni na hakuna orodha ya wafuasi wa CHADEMA hakuna sehemu umeenda kujitambulisha nitajuaje kama wewe ni mfuasi?

    Shahidi: Sijui utajuaje

    Lissu: Nitajuaje wewe sio pandikizi la polisi?

    Shahidi: Sijajua neno utajuaje

    Lissu: Sababu sikuoni nitajuaje kama wewe sio pandikizi la polisi

    Shahidi: Itabidi uiambie Mahakama tukufu ikuambie

    Lissu: Majaji hawajaniambia chochote mimi nazungumza na wewe nijibu swali langu nitajuaje wewe sio pandikizi la polisi?

    Shahidi: Mimi sijui kwa kweli

    Lissu: Ukisema hujui ndiyo jibu sahihi kabisa

    Lissu: Mfuasi wa CHADEMA a…

    Lissu anamsomea shahidi maelezo yake ya 17-4-2025 kisha atamuonesha maeneo anayotaka kumhoji

    Lissu: Kwenye ushahidi wako leo umeieleza mahakama kwamba wewe ni mfuasi wa CHADEMA tangu 2021 kweli si kweli?

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Wasomee majaji kwenye kielelzo chako D12 pale unaposema “Mimi pia ni…” mpaka nitakapokuambia uache

    Shahidi: Mimi pia ni mfuasi wa chama hicho

    Lissu: Naomba nipate kielelzo D12 (Maelezo aliyoandika shahidi polisi) anapatiwa

    Lissu: Hiyo sehemu niliyomuambia asome imeandikwa “Mimi pia ni mwanachama/ shabiki wa cham cha CHADEMA” kwa hiyo shahidi ulitaka kuficha ukweli mahakamani

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Mbona husemi ilvyoandikwa

    Shahidi: Mimi nikijitambulisha kama mfuasi wa CHADEMA sijui askari alipitiwa na nani

    Lissu: Ya askari tumuachie askari

  8. Shahidi: Nilikaa chini baadae wakaniambia nitoe viatu, mkanda na wakaniambia nikae maaabusu

    Shahidi ni PW13 shahidi wakificho ana umri wa miaka 35 dini yake ni muislam

    Wakili anamuongoza shahidi PW13

    Wakili: Shahidi unajishughulisha na kazi gani?

    Shahidi: Mimi ni dereva bodaboda

    Wakili: Unafanyia wapi?

    Shahidi: Katika Halmashauri ya jiji la Mbeya

    Wakili: Una muda gani kwenye shughuli hizi?

    Shahidi: Nina mwaka wa 8-9 tangu nimeanza shughuli hizi za bodaboda

    Wakili: Ieleze mahakama hii wewe ni mfuasi wa chama gani?

    Shahidi: Mimi ni mfuasi wa chama cha demokrasi na maendeleo CHADEMA

    Wakili: Umekuwa mfuasi wa chama hicho toka lini?

    Shahidi: Kwa kumbukumbu zangu nimekuwa toka mwaka 2021

    Wakili: Elezea kama ulikumbuka ulishiriki matukio gani ya CHADEMA

    Shahidi: Maandamano ya kutoka Mbalizi mpaka Kabwe 2024 kingine ni kumpokea Mhe. Mbowe 2024, kungamano liloandaliwa na vijana na lilikitakiwa kufanyika viwanja vya shule Luanda Nzovwe lakini bahati mbaya halikufanyika likizuiliwa na serikali

    Wakili: Ilikuwa mwaka gani?

    Shahidi: Nimesahau kidogo

    Wakili: Nani alikuwa kiongiozi wa kongamano hili?

    Shahidi: Hatukufanikiwa kufanya kongamano hili pale viwanjani tulitawanywa.

    Wakili: Unakumbuka tarehe 4-4-2025 unakumbuka nini?

    Shahidi: Nlikiwa kwenye kijiwe changu nikiwa na simu yangu napita pita mitandaoni nikaona video fupi ya hotuba ya mhe. Tundu Lissu akipinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu 2025

    Wakili: Hiyo hotuba uliona katika mtandao gani?

    Shahidi: Youtube

    Wakili: Nani alikuwa anahutubia hotuba hiyo uliyoiona?

    Shahidi: Mhe: Tundu Lissu

    Wakili: Wewe binafsi unamfahamuje Tundu Lissu

    Shahidi: Mimi binafsi nimemfahamu kupitia mitandao ya kijamii na baada ya kuwa mfuasi wa chama hicho mwaka 2021

    Wakili: Eleza Mhe, Lissu ni nani?

    Shahidi: Mhe. Lissu kwa sasa ni mwenyekiti wangu wa CHADEMA

    Wakili: Baada ya kusikia video hizo ulifanyaje

    Shahid: Baada ya kufungua hizo video na kuridhika na anachozungumza nikajaribu kuongea na wenzangu kuwashawishi ili kushirikiana nao kile anachokitaka mwenyekiti tuungane tuwe kitu kimoja

    Wakili: Endelea

    Shahidi: Tuwe kitu kimoja Kupambana na kuzuia uchaguzi 2025

    Wakili: Ulikuwa unashawishi kwa namna gani?

    Shahidi: Watu wanaokwenda kupiga kura kufanya fujo, ikiwemo na kupiga mawe

    Wakili: Huo ushawishi ulikuwa unafanyika wapi?

    Shahidi: Katika kijiwe changu ninachopakia pikipiki

    Wakili: Nini kilitokea?

    Shahidi: Baada ya kuendelea na mivutano ya hapa na pale kuna walioridhika na maelezo yangu na ambao hawakuridhika sisi tukaendelea na mambo yetu baadaye akatokea mtu mmoja akanifuata na kuniambia njoo tuongee niliposogea pembeni

    Shahidi: Niliposogea pembeni na kujitambulisha alijitambulisha yeye ni afisa polisi akaniambia nahitajika kwenda kituoni kuna mahojiano baina ya mimi na yeye

    Wakili: Ulipofika kituoni mambo yalikuwaje?

    Shahidi: Nilikaa chini baadae wakaniambia nitoe viatu, mkanda na wakaniambia nikae maaabusu (lockup)

    Wakili: Baada ya kuweka mahabusu

    Shahidi: Nikachukuliwa nakupelekwa kwenye chumba wakawa wananihoji kuwa pale nilikuwa nafanya nini na kwa nini nilikuwa nahamasisha kufanya uhasi

    Wakili: Uhasi kuhusu nini?

    Shahidi: Kwa nini mnahamasisha uhasi kwenda kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025

    Wakili: Baada ya mahojiano nini kilifuatiwa?

    Shahidi: Waliniambia nitafute mtu wa kujidhamini ili niweze kutoka pale na kuendelea na taratibu zingine Wakili:Ikawaje

  9. Lissu: Matendo gani niliyofanya ili kushtakiwa kwa uhaini ?

    Lissu: Kwa hiyo kwenye sheria ya kanuni za adhabu kwa mujibu wako kuna kosa la kuzuia uchaguzi

    Shahidi: Lipo hilo kosa

    Lissu: Naomna ueleze baada ya kumpeleka huyu P9 kituoni unasema uliendelea na shughuli zako naomba uwaeleze majaji kama unafahamu huyu P9 hakupelekwa mahakamani?

    Shahidi: Sifahamhamu

    Lissu: Utashangaa nikukuambia hakupelekwa mahakamani

    Shahidi: Siwezi kujua

    Lissu: Utashangaa kwamba hakushtakiwa kwenye kosa alilofanya badala yake amekuwa shahidi na wa kesi hii?

    Shahidi: Hilo sifahamu

    Lissu: Unafahamu kama kulikuwa na mapatano kati ya polisi wa mbeya na P9 aishtakiwe aje kutoa ushahidi kwenye kesi yangu?

    Shahidi: Hilo sifahamu

    Lissu: Unafahamu nashtakiwa kwa kosa gani?

    Shahidi: Najuanu unashtakiwa kwa uhaini

    Lissu: Matendo gani niliyofanya kustakiwa kwa uhaini

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Kwa hiyo umekuja hapa bila kujua?

    Shahidi: Kuna matamko yako ya mitandaoni

    Lissu: Mimi nina maelfu ya hotuba zangu mitandaoni

    Shahidi: Niliona mitandaoni ukihamasisha uchgauzi wa mwaka huu sijui utakuwaje

    Lissu: Umewasilisha mahakami hiyo video

    Shahidi: Sijawasilisha Lissu: Sina maswali zaidi

  10. Habari za hivi punde, Mdogo wa Mfalme Charles wa Uingereza Andrew Mountbatten akamatwa

    .

    Chanzo cha picha, BAV MEDIA

    Andrew Mountbatten Windsor, mwanamfalme wa zamani wa Uingereza na mdogo wa Mfalme Charles, amekamatwa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma huku polisi wakichunguza madai kwamba alishiriki habari za siri na Jeffrey Epstein aliyepatikana na hatia ya uhalifu wa kingono.

    Sasa tumeona taarifa kutoka kwa polisi wa Thames Valley, ambayo inasema:

    "Kama sehemu ya uchunguzi, leo (19/2) tumemkamata mtu wa miaka sitini kutoka Norfolk kwa tuhuma za utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma na wanaendelea na upekuzi kwenye makao yake huko Berkshire na Norfolk.

    "Mwanamume huyo bado yuko chini ya ulinzi wa polisi kwa wakati huu.

    "Hatutamtaja mtu aliyekamatwa, kulingana na mwongozo wa kitaifa. Tafadhali kumbuka pia kwamba kesi hii sasa iko hai kwa hivyo tahadhari inapaswa kuchukuliwa kwa uchapishaji wowote ili kuepuka kudharau mahakama."

    Mkuu Msaidizi Konstebo Oliver Wright alisema: “Baada ya tathmini ya kina, sasa tumefungua uchunguzi kuhusu madai haya ya utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma.

    “Ni muhimu kulinda uadilifu na madhumuni ya uchunguzi wetu tunaposhirikiana na washirika wetu kuchunguza kosa hili linalodaiwa.

    "Tunaelewa maslahi makubwa ya umma katika kesi hii, na tutatoa taarifa kwa wakati unaofaa."

    "Andrew Mountbatten Windsor amekana makosa yanayohusiana na Faili za Epstein"

    .

    Chanzo cha picha, BAVMEDIA

  11. Lissu: 'Nikikuambia kwa mujibu wa sheria za Tanzania hakuna kosa la uchaguzi mkuu utasemaje'?

    Lissu: Waeleze majaji kwenye maelezo yako umetaja jina la OCS wa Mwanjerwa?

    Shahidi: kwenye maelezo yangu halipo

    Lissu: Kwenye maelezo yako umeeleza sehemu yoyote huyu mtuhumiwa P9 amefanya makosa yake?

    Shahidi: Kwenye maelezo sijataja

    Lissu: Sasa bwana vijiwe namsomea shahidi maana ya neno kijiwe kwa mujibu wa kamusi kuu ya Kiswahili iliyotolewa na BAKITA Vijiwe mahali ambapo vijana hususani wasio na kazi hukaa …sasa swali langu jiji la Mbeya lina vijiwe vingapi?

    Shahidi: Hapo sifahamu

    Lissu: Umetaja katika vijiwe vya Mbeya ameenda vijiwe gani na gani?

    Shahidi: Sijataja

    Lissu: Eleza kama umetaja tarehe ambayo huyu P9 amefanya hayo makosa?

    Shahidi: Tarehe 5

    Lissu: Hapana tarehe 5 ulikwenda kumkamata

    Shahidi: Ni tarehe hiyo hiyo

    Lissu: kwenye maelezo yako kuna sehemu umataja tarehe 5 alifanya kosa?

    Shahidi anasoma maelezo yake

    Lissu: Kwa akili yako wewe askari polisi hicho ulichosema kinaeleza alifanya makosa tarehe ngapi? Kinaonyesha alifanya makosa lini?

    Shahidi: Haioneshi

    Lissu: Waeleze majaji kama kwenye maelezo yako umeelza huyu P9 alikuwa anapanga njama na nani?

    Shahidi: Humu haijaeleza

    Lissu: Eleza kama kwa ufahamu wako kuna kosa katika sheria za nchi la kuzuilia uchaguzi mkuu usifanyike?

    Shahidi: Nafahamu kosa lipo?

    Lissu: Kwa mujibu wa sheria gani? Shahidi: Hapo kwenye sheria

    Lissu: Nikikuambia kwa mujibu wa sheria za Tanzania hakuna kosa la uchaguzi mkuu utasemaje? Shahidi: Kosa lipo

    Lissu: Naomba nimuoneshe shahidi sheria ya Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2024 imesainiwa na mama…hamna mahali popote ambapo imetengeneza kosa la kuzuia uchgauzi mkuu

    Shahidi: Hilo mimi sifahamu

    Lissu: Na kwenye sheria kuu ya jinai hakuna kosa lolote la kuzuia uchaguzi mkuu

    Shahidi: Hilo kosa lipo

    Lissu: Naomba shahidi atuoneshe hilo kosa kwenye penal code - Shahidi anapewa penal code

    Shahidi: Hii ni ya Kingereza

  12. Lissu: Hayo maneno “anahamasisha na kuchochea uchaguzi mkuu usifanyike” umeyasoma hapo

    Lissu: Waeleze majaji kama ungependa maelezo yako hayo yawe kilelezo mahakamani

    Shahidi: Kwa jinsi ukivyoniuliza…

    Lissu: Hata sijaanza kuuliza nataka maelezo yako yaingie huko tukimaliza tutaendelea

    Shahidi: Sawa Upande wa mashtaka umekubari maelezo yapokelewe kama kielelezo

    Lissu: Naomba shahidi apewe kielelezo (D11)…Sasa shahidi hicho ni kielelezo mahakamani na swali langu la kwanza katika ushahidi wako leo umesema wewe ni askari polisi wa kituo cha central mbeya mjini kweli sio kweli?

    Shahidi: Kweli

    Lissu: Angalia maelezo yako waeleze majaji uwaambie kuna sejemu yooyote umesema unafanya kazi Mbeya Central polisi?

    Shahidi: Hapa hakuna

    Lissu: Asante…Swali langu la pili linahusu matukio ya 5-4-2025 ambapo ukesema ukiwa kituo cha Polisi Mwanjerwa uliitwa na mkuu wa kituo ukaambiwa umtafute P9 kwa kosa ulilosema anahamasisha uchgauzi mkuu wa 2025 usifanyike kwenye vijiwe mbalimbali kweli si kweli?

    Shahidi: Ni kweli

    Lissu: Sasa naomba unagalie kwenye kielelzo D11 pale inaposema “Nakumbuka mnamo tarehe 5-4-2025 nikiwa kazini” usome mpaka mwisho wa sentesi hiyo alafu ueleze kama kuna maneno yoyote kwamba huyu P9 alikuwa ana hamasisha uchaguzi usifanyike kwenye vijiwe mbalimbali?

    Shahidi: Yapo

    Lissu: Naomba usome kwa sauti

    Shahidi: Anasoma maelezo

    Lissu: Hayo maneno “anahamasisha na kuchoche uchaguzi mkuu usifanyike” umeyasoma hapo

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Kwenye ushahidi wako umesema hivi “Baada ya kujitambulisha kwamba wewe ni askari polisi” kwa maelezo yako ukesema “kwakua alikuwa mtu muelewa tuliongozana kituo cha Polisi” angalia kama hayo maneno yapo kwenye maelezo yako

    Shahid: Haya maneno hayapo

    Lissu: Safi….Naomba ueleze nani aliyerekodi hayo maelezo yako?

    Shahidi: Haya maelezo niliandika mimi mwenyewe

    Lissu: Eleza kama ni kweli au si kweli kwamba mtu anayeandika maelezo hua anapewa onyo aseme ukweli mtupu

    Shahidi: Rudia swali

    Lissu: Wakati wa kuandika maelezo kwenye hiyo karatasi huwa kuna mahali kuna onyo? Shahidi: Hakuna

    Lissu: Hakuna neno nitasema kweli tu na nikisema ukweli nishtakiwe

    Shahidi: Hayo maneno unajiambia wewe mwenyewe?

    Lissu: Unaifahamu PGO?

    Shahidi: Nafahamu

    Lissu: Unafahamu kwamba kwa mujibu wa PGO anayeandika maelezo anatakiwa kusimamiwa na polisi anayefanya kazi hiyo kwa mujibu wa PGO

    Shahidi: Sifahamu

    Lissu: Naomba apewe PGO…

    Shahidi: Hii PGO ni ya kingereza

    Lissu: Kwa hiyo huwezi kujibu kwakua hujui Kingereza?

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Swali langu ni hili kwa mujibu wa PGO hakuna ruhusa ya kujiandikia maelezo yako wewe mwenyewe ni kweli sio kweli?

    Shahidi: Hapo sijui

    Lissu: Angalie kielelezo D11 kule mwishoni umeeleza kwamba “Mimi Koplo Vincet nathibitisha kuandika melezo yangu kwa usahihi kwa kifungu cha 10 3C” hayo maneno yapo?

    Shahidi: Hayapo

    Lissu: Naona kielelezo chake kumbe kuna mambo mengi humu….angalia ukurasa wa mwisho wa maelezo yako ueleze majaji kama kwenye hiyo sheria kuna hicho kifungu 10 3C?

    Shahidi: Haya maelezo wakati naandika mwaka 2025 kilikuwepo

    Lissu: Kilikuwepo?

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Asante….waeleze majaji kama kuna mtu yoyote aliyeshuhudia ukiandika haya maelezo? Shahidi: Niliandika mimi mwenyewe

    Lissu: Umeeleza kwamba uliambiwa na OSC wa kituo cha Mwanjerwa umkakamate P9 kwa sababu ana hamasisha na kuchochea kwenye vijiwe uchaguzi 2025 usifanyike…wakati una mkamata alikuwa na kosa gani?

    Shahidi: Kwa muda huo alikuwa hachochei alikuwa anapanga njama

  13. Tundu Lissu: Naskia wewe ni 'Homeboy' wangu

    Maswali kutoa kwa Lissu kwenda kwa Shahidi ndio yameanza sasa

    Lissu: Shahidi umesema unaitwa detective Koplo Vicent?

    Shahidi: Hapana mimi naitwa H937 Detective Koplo Vicent

    Lissu: Kwa hiyo ukienda kwa baba yako na mama yako unasema unaitwa H937…..

    Shahidi: Hapana

    Lissu: Unaitwa nani?

    Shahidi: Koplo Vicent Kipii

    Lissu: Nasikia wewe ni Homeboy wangu

    Shahidi: Ndiyo mimi ni homeboy wako

    Lissu: Basi kwakua wewe ni homeboy wangu nitaomba ujibu maswali yangu….Koplo Vicent Kipii uliandika maelezo yako 17-4-2025?

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Ukipewa maelezo yako utayatambua

    Shahidi: Ndiyo

    Lissu: Naomba shahidi apewe maelezo yake

    Lissu: Waelezo majaji kama hayo maelezo ni ya kwako

    Shahidi: Ni sahihi haya ni maelezo yangu

    Lissu: Nataka kuhoji sifa au uaminifu wake naomba nimsomee maelezo yake kisha nitamueleza maeneo ninayotofautiana naye alafu akabithi mahakamani kama kielelezo (Lissu anamsomea maelezo shahidi)

  14. ‘‘Nimekuja kukukamata kwa kosa la uchochezi…’’, Shahidi P9 alivyokamatwa

    Wakili: Baada ya kupewa maelekezo hayo?

    Shahidi: Mkuu wa kituo alinipatia namba yake ya simu ya P9 mkuu wa kituo alipata namba toka kwa msiri wake

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Kwakua nilikuwa nimeshapata mawasiliano yake na nikafanya uchunguzi wangu nikagundua ni fundi umeme ikabidi nitumie mbinu ya kujifanya mteja nataka huduma yake nyumbani kwangu

    Wakili: Nini kiliendelea?

    Shahidi: Niliwasiliana naye kirafiki tu kama mteja na tukakubaliana tukutane maeneo ya Kabwe

    Wakili: Baada ya hapo?

    Shahidi: Baada ya hapo alikuwa amefika pale Kabwe na kwakua mimi nilikuwa kituo cha Mwanjerwa pale karibu, kweli nikakutana naye

    Wakili: Niki kiliendelea baada ya kukutana naye?

    Shahidi: Nilipokutana naye pale nilimuambia mimi sina shida ya fundi umeme nikajitambulisha kama askari polisi nikampatia kitambulisho pale pale

    Wakili: Baada ya hapo?

    Shahidi: Nikamueleze kuwa nimekuja kukukamata kwa kosa la uchochezi na kuhamasisha vurugu za kuzuia uchaguzi wa 2025

    Wakili: Mwisho wake?

    Shahidi: Bahati nzuri alikuwa ni mtu muelewa nikamuambia yupo chini ya ulinzi basi nilivyoona sio mtu mwenye vurugu niliongozana naye mpaka kituo cha Mwanjerwa nikamkabithi kwa mkuu wa kituo

    Wakili: Baada ya kumkabithi ulielekea wapi?

    Shahidi: Baada ya hapo niliendelea na mambo yangu mengine

    Wakili wa mashataka amemaliza kumuongoza shahidi

  15. Mashahidi wa kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu waendelea kutoa ushahidi

    .

    Chanzo cha picha, MWANANCHI

    Karibu katika matangazo yetu mubashara kukufahamisha muendelezo wa kusikilizwa kwa kesi ya kiongozi wa chama cha upinzani CHADEMA, Tundu Lissu ambaye ameshtakiwa kwa makosa ya uhaini.

    Shahidi wa leo ni wa 12 kutoa ushahidi wake.

    Jaji: Shahidi unaitwa nani?

    Shahidi: H937 Detective Coplo Vicent umri miaka 36 dini mkristo

    Wakili: Umesema unaitwa nani?

    Shahidi: H937 Detective Coplo Vicent

    Wakili: Unaishi wapi?

    Shahidi: Mbeya

    Wakili: Sehemu gani?

    Shahidi: Mbeya Mjini

    Wakili: Unafanya kazi gani?

    Shahidi: Mimi ni askari polisi

    Wakili: Hivyo kazi unafanyia wapi?

    Shahidi: Central wilaya ya Mbeya

    Wakili: Tangu lini?

    Shahidi: Nipo Central tangu mwaka 2012

    Wakili: Kwa ujumla katika jeshi la polisi wewe umejiunga mwaka gani?

    Shahidi: Nimejiunga mwaka 2011

    Wakili: Mafunzo ulipatia wapi

    Shahidi: CCP Moshi

    Wakili: Ulihitimisha lini mafunzo yako

    Shahidi: 30/3/2012

    Wakili: Baada ya kuhitimu?

    Shahidi: Nilipangiwa mkoa wa Mbeya

    Wakili: Majukumu yako ya kila siku hapo kituoni ni yapi?

    Shahidi: Kupeleleza kesi, kukamata na kutoa ushahidi mahakamani

    Wakili: Katika kitengo cha upelelezi una miaka mingapi?

    Shahidi: Katika kitengo cha upelelezi nina miaka 6

    Wakili: Kabla ya hapo ulikuwa wapi?

    Shahidi: Kabla ya hapo nilikuwa general duty

    Wakili: Ieleze mahakama mnano 5/4/2025 majira ya asubuhi ulikuwa wapi?

    Shahidi: Nilikuwa kwenye kituo cha polisi nakagua na kuendelea na majukumu yangu

    Wakili: Kwa wakati huo unakumbuka nini?

    Shahidi: Nikiendelea na shughuli zangu niliitwa na mkuu wa kituo na kunipa maelekezo ya kumkata P9

    Wakili: Alikuwa anatuhumiwa na nini mpaka wewe uende kumkamata

    Shahidi: Ana hamasisha, anachochea uchaguzi wa mwakan2025 usifanyike. Kwa hivyo, nilipewa maelekezo ya kumkamata

  16. José María Balcázar achaguliwa kuwa rais wa nane wa Peru ndani ya muongo mmoja

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bunge la Peru Jumatano jioni lilimchagua mbunge José María Balcázar kuwa rais wa nane wa nchi hiyo katika kipindi cha muongo mmoja, akichukua nafasi ya kiongozi mwingine wa mpito ambaye aliondolewa madarakani siku iliyopita kwa madai ya ufisadi miezi minne tu tangu alipochukua uongozi.

    Balcázar, jaji wa zamani mwenye umri wa miaka 83 anayewakilisha chama cha mrengo wa kushoto cha Perú Libre, aliwashinda wagombea wengine watatu kwa wingi wa kura kati ya wabunge 130.

    Urais unaozunguka nchini Peru unaonyesha mgogoro wa kisiasa unaochochewa na ukosefu wa wingi wa wabunge kwa viongozi. Wabunge mara nyingi wametumia tafsiri pana ya kifungu cha katiba kuhusu "ukosefu wa maadili" kuwaondoa marais walio madarakani.

    Balcázar, jaji mstaafu mwenye uzoefu wa karibu miaka 30 katika mahakama, aliapishwa muda mfupi baada ya zoezi la kupiga kura lililoendeshwa na kiongozi wa Bunge, Fernando Rospigliosi.

    Soma zaidi:

  17. Uingereza kutoa wito wa uwajibikaji kwa ukatili unaofanyika Sudan

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Uingereza intarajiwa kutoa wito wa uwajibikaji dhidi ya ukatili unaotekelezwa nchini Sudan katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo hii Alhamisi.

    Uingereza imechukua kiti cha urais wa kila mwezi wa shirika hilo la kimataifa, na waziri wa mambo ya nje wa (Uingereza) Yvette Cooper atakuwa atatumia fursa ya uongozi kwa kipindi hiki ili kuweka kipaumbele kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa takriban miaka mitatu.

    Waziri wa mambo ya nje, Yvette Cooper anatarajiwa kushinikiza kuafikiwa kwa suluhu la kibinadamu na kuangazia unyanyasaji wa kingono, ambao Umoja wa Mataifa unasema unatumika kama silaha ya kivita.

    Jeshi na upinzani, vikosi vya Rapid Support Forces, wanatuhumiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia, lakini wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wanasema wapiganaji wa RSF hasa wanatekeleza ubakaji kwa kiwango kikubwa sana.

    Yvette Cooper anaiita vita dhidi ya miili ya wanawake na amejitolea pauni milioni 20 kusaidia manusura.

    Atakuwa mwenyekiti wa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushinikiza upatikanaji wa suluhu katika mgogoro huo kibinadamu nchini Sudan.

    Pande zote mbili zinazozozana wanapewa silaha za hali ya juu zaidi na mataifa ya nje.

    Soma zaidi:

  18. Rais wa zamani wa Korea Kusini akabiliwa na hukumu ya kifo katika kesi ya uasi

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Mahakama ya Korea Kusini imeanza kusikiliza kesi ya Rais wa zamani Yoon Suk Yeol ikiwa ana hatia ya kupanga uasi kuhusu azma yake ya kuweka sheria ya kijeshi mnamo Desemba 2024, katika kesi ambayo inaweza kumfanya Yoon ahukumiwa kifo.

    Hukumu hiyo, ambayo itafuatiliwa kwa karibu katika nchi iliyogawanyika sana, ndiyo yenye athari kubwa zaidi kwa kiongozi aliyeondolewa madarakani, ambaye jaribio lake la kuweka sheria ya kijeshi lilisababisha mgogoro wa kisiasa wa kitaifa na kujaribu ustahimilivu wa taasisi za kidemokrasia za Korea Kusini.

    Waendesha mashtaka walitaka Yoon apewe adhabu ya kifo mnamo mwezi Januari, wakisema "sheria yake ya kijeshi isiyo ya kikatiba na isiyo halali ilidhoofisha utendaji wa Bunge la Kitaifa na Tume ya Uchaguzi ... kwa kweli iliharibu utaratibu wa kikatiba wa kidemokrasia huria."

    Mnamo mwezi Januari, Yoon alifungwa jela miaka mitano kwa kuzuia kukamatwa kwake na kughushi nyaraka.

    Kuanzisha uasi kuna adhabu kali zaidi ya kifo au kifungo cha maisha chini ya sheria ya Korea Kusini.

    Korea Kusini ilitoa hukumu ya kifo mara ya mwisho mwaka 2016, lakini haijamnyonga mtu yeyote tangu mwaka 1997.

    Soma zaidi:

  19. Wachimbaji madini wadhaniwa kufa kwa uvujaji wa kaboni-monoksidi Nigeria

    .

    Wachimbaji madini wasiopungua 33 wamefariki dunia kutokana na uvujaji wa kaboni-monoksidi unaoshukiwa kutokea kwenye mgodi wa madini ya risasi na zinki katika jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria, walioshuhudia wameiambia BBC.

    Inaaminika kuwa mkasa huo ulitokea kabla tu ya jua kuchomoza katika eneo lililo nje ya mji wa Wase linaloendeshwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Solid Unity Nigeria Ltd.

    Gesi yenye sumu inaaminika kukusanyika chini ya ardhi katika handaki zisizo na hewa nzuri, na kusababisha wafanyakazi kuanguka kabla tu ya mwisho wa zamu yao ya usiku.

    Waligunduliwa na wale waliokuwa wakiripoti kazini asubuhi - wachimbaji wengine zaidi ya 20 waliokolewa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.

    Pia unaweza kusoma:

  20. Israel inaendeleza 'hatua za taratibu' kunyakua Ukingo wa Magharibi, UN

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba mipango ya Israel ya kuimarisha udhibiti wa sehemu za Ukingo wa Magharibi ni sawia na kutwaa eneo hilo kimabavu.

    Rosemary DiCarlo alikuwa akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la umoja huo.

    "Tunashuhudia hatua kwa hatua unyakuzi wa eneo la Ukingo wa Magharibi, kama hatua za Israel za upande mmoja zinavyozidi kubadilisha mazingira," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rosemary DiCarlo aliuambia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu suala la Palestina.

    "Zikitekelezwa, hatua hizi zitajumuisha upanuzi hatari wa mamlaka ya kiraia ya Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, ikiwa ni pamoja na katika maeneo nyeti kama Hebron.

    "Hatua hizo zinaweza kusababisha upanuzi wa makazi kwa kuondoa vikwazo vya ukiritimba na kurahisisha ununuzi wa ardhi na vibali vya ujenzi."

    Hatua zilizoidhinishwa hivi majuzi zimepangwa kuongeza udhibiti wa Israel katika sehemu za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambako mamlaka ya ndani ya Palestina inajitawala.

    Waziri wa mambo ya nje wa Israel Gideon Saar ameelezea Umoja wa Mataifa kuwa umeathirika na chuki dhidi ya Israel.

    Pia unaweza kusoma:

Trending Now