Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Upinzani wasema jeshi linaendeleza 'mapigano ya kikatili' Sudan Kusini

Serikali ya Sudan Kusini imesema dhamira yake ni kuchukua tena maeneo yote yaliyo chini ya upinzani.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya leo. Kwaheri.

  2. Safari za ndege kuelekea kaskazini mwa Ethiopia zasitishwa - kunani?

    Safari za ndege za abiria kati ya mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, na miji katika eneo la kaskazini mwa Tigray zimefutwa kutokana na hofu ya kurejea kwa migogoro, huku kukiwa na ripoti za mapigano katika eneo moja.

    Shirika la Ndege la Ethiopia, ambalo huwa na safari katika maeneo yote nchini, liliwatumia abiria ujumbe mfupi kuhusu kufutwa kwa safari hizo likitaja "hali zisizotarajiwa".

    Siyo shirika la ndege wala serikali hakuna aliyetoa maoni zaidi.

    Mwandishi wa BBC katika jiji kuu la Tigray la Mekelle alithibitisha habari hizo kutoka kwa wafanyakazi wa uwanja wa ndege ambao walikuwa wameambiwa wasiende kazini.

    Utekelezaji wa mkataba wa amani wa 2022 wa kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kikatili huko Tigray umekuwa ukiendelea kudorora huku mvutano ukiongezeka juu ya eneo lenye mgogoro kabla ya uchaguzi wa mwezi Juni.

    Kuna ripoti za mapigano kati ya jeshi la shirikisho na wapiganaji wa Tigray huko Mai Degusha, eneo linalozozaniwa la wilaya ya Tselemti magharibi mwa Tigray.

    Vyanzo pia vinaripoti harakati mpya za kijeshi kusini mwa Tigray, na kuibua wasiwasi kuhusu mzozo mpya.

    Soma zaidi:

  3. Nicki Minaj ajitangaza kuwa “shabiki namba moja” wa Trump

    Nyota wa muziki wa kufoka foka aliye na asili ya Trinidad na Marekani, Nicki Minaj, amejitangaza kuwa “shabiki namba moja” wa Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumatano, huku pia akionyesha viza ya Trump iitwayo “gold card”, ambayo huwapa wahamiaji, haki ya kuishi Marekani na njia ya kupata uraia wa nchi hiyo.

    Rais Donald Trump, alimwalika msanii huyo kupanda jukwaani mjini Washington DC baada ya Minaj kutangaza kuunga mkono mpango unaojulikana kama “Trump Accounts”, unaotoa misaada kwa ajili ya watoto.

    Hapo awali alikuwa mkosoaji wa sera kali za Trump kuhusu uhamiaji, na Minaj — ambaye amesema aliwasili Marekani akiwa mtoto pamoja na wazazi wake — alianza kuusifu uongozi wake katika miaka ya hivi karibuni.

    Tukio hilo linajiri huku kukiwa na maandamano kufuatia maafisa wa Idara ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE) kuhusika katika matukio ya kuwapiga risasi na kuwaua raia wa Marekani.

    Mpango wa gold card wa Trump ulizinduliwa mwezi Desemba kama njia ya haraka kwa wahamiaji matajiri kama Minaj kupata uraia wa Marekani.

    Waombaji hulipa dola milioni moja za Marekani pamoja na ada ya uchakataji ya dola 15,000, ili kupata haki ya kuishi nchini Marekani.

    Mpango huo umekosolewa kwa kuanzishwa wakati Rais Trump anaongeza masharti makali dhidi ya wahamiaji wasio na vibali.

    Minaj, ambaye ameukaribisha mpango huo, anaripotiwa kueleza katika chapisho la Facebook mwaka 2018 kwamba “aliingia nchini humo kama mhamiaji haramu akiwa na umri wa miaka mitano,” wakati huo akikosoa sera ya serikali kama yenye kutenganisha familia.

    ‘Kadi ya dhahabu’ ya Minaj inampa haki isiyo na kikomo ya kuishi Marekani, lakini bado si raia wa nchi hiyo kwa mujibu wa makubaliano hayo.

    Trump alitania kuwa ataacha kucha zake zikue ndefu ili kumuiga rapa huyo, kisha akashikana naye mkono wakati mzungumzaji mwingine akipanda jukwaani.

    Wasanii wengine wa muziki nchini Marekani wamekuwa wakimkosoa zaidi rais na sera zake za uhamiaji.

    Bruce Springsteen alitoa wimbo unaopinga ICE siku ya Jumatano uitwao Streets of Minneapolis, mji ambako Alex Pretti na Renee Nicole Good waliuawa hivi karibuni katika matukio mawili tofauti.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Urusi yaonya matumizi ya nguvu dhidi ya Iran

    Urusi imesema siku ya Alhamisi kwamba bado kuna fursa ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani na kuonya kwamba matumizi yoyote ya nguvu dhidi ya Tehran yatakuwa na athari mbaya na kusababisha machafuko kote Mashariki ya Kati.

    Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alikuwa akitoa maoni siku moja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuihimiza Iran kuja kwenye meza ya mazungumzo na kufanya makubaliano kuhusu silaha za nyuklia la sivyo inaweza kushambuliwa na Marekani.

    "Tunaendelea kutoa wito kwa pande zote kujizuia na kuachana na matumizi yoyote ya nguvu kutatua masuala yanayowakabili. Ni wazi kwamba uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo bado upo... Lazima tuzingatie zaidi mifumo ya mazungumzo," Peskov aliwaambia waandishi wa habari.

    "Vitendo vyovyote vya nguvu vinaweza tu kusababisha machafuko katika eneo hilo na kusababisha athari mbaya sana katika suala la kuvuruga mfumo wa usalama katika eneo lote."

    Urusi imeimarisha uhusiano wa karibu na Iran tangu kuanza kwa vita vyake nchini Ukraine na kusaini mkataba wa ushirikiano wa kimkakati wa miaka 20 na Jamhuri ya Kiislamu mnamo Januari 2025.

    Soma zaidi:

  5. Upinzani wasema jeshi linaendeleza 'mapigano ya kikatili' Sudan Kusini

    Upinzani nchini Sudan Kusini, SPLM-IO, umesema umejipata na kile ilichoeleza kuwa ni mapigano ya kikatili yanayoendelezwa na wanajeshi wa serikali katika Jimbo la Jonglei mashariki mwa nchi hiyo, na kuonya matokeo yake kuwa yanaweza kusababisha makabiliano siku zijazo.

    Msemaji wa SPLM-IO, Pal Mai Deng, aliambia BBC siku ya Alhamisi kwamba wanajeshi wa serikali wanafanya mashambulizi, huku kukiwa na mapigano makali katika eneo la Yuai, mji mkuu wa kaunti ya Uror.

    Deng alisema, "Tumekuwa katika makabiliano ya kikatili ya kijeshi nao tangu jana. Wanafanya mashambulizi."

    Alisema mapigano ya sasa yanaweza kuwa na umuhimu mkubwa.

    "Maamuzi yatafanywa kulingana na hatima ya makabiliano ya kijeshi yanayoendelea. Itakuwa ni mapigano ya mwisho yatakayoamua hatma ya makabiliano yajayo," Deng alisema.

    Jeshi la Sudan Kusini, hata hivyo, limepuuza mapendekezo kwamba mapigano hayo yanaashiria wakati muhimu.

    Msemaji wa jeshi, Meja Jenerali Lul Ruai Koang amesema operesheni za serikali zilikuwa zikiendelea. "Huu sio mwisho. Bado tuko na dhamira yetu ni kuchukua tena maeneo yote yaliyo chini ya upinzani," Koang aliiambia

    Kwa mujibu wa jeshi, wametwaa vijiji kadhaa kutoka kwa vikosi vya upinzani huku likiendelea na mashambulizi ya kurejesha miji ya kimkakati iliyotekwa na wapiganaji hivi karibuni.

    Wakati huo huo, Koang anasema raia walionaswa katika mapigano hayo waliwekwa sehemu yenye ulinzi na kupewa chakula, ikiwa ni pamoja na unga wa mahindi na mafuta ya kupikia.

    Mashirika ya kiraia yameonya kuwa mzozo huo unazidisha hali kuwa mbaya zaidi kwa raia.

    Soma zaidi:

  6. Maafisa wa mpakani waliohusika katika mauaji ya Pretti wapewa likizo

    Ulinzi wa Forodha na Mipaka wa Marekani (CBP) unasema maafisa wawili waliohusika katika shambulio la risasi la raia wa Marekani huko Minneapolis wameamriwa kwenda likizo.

    Mauaji ya Alex Pretti, muuguzi wa wagonjwa mahututi mwenye umri wa miaka 37, siku ya Jumamosi yalisababisha maandamano mapya katika jimbo la Minnesota, malalamiko ya umma kote Marekani na wito kutoka kwa wabunge wa pande zote mbili wa kumwondoa kazini katibu wa Idara ya Usalama wa Nchi (DHS).

    Kulingana na ripoti ya awali ya DHS iliyotumwa kwa Bunge, maafisa wawili walimfyatulia Pretti risasi wakati wa mapigano. Taarifa rasmi za awali zilidai Pretti alionyesha bunduki yake.

    Haijulikani ni lini maafisa hao waliamriwa kwenda likizo, au watakaa nje ya kazi kwa muda gani.

    CBP iliambia BBC siku ya Jumanne kwamba imewaondoa maafisa hao kazini kwa kufuata itifaki ya kawaida. Kwa kawaida maafisa wa kutekeleza sheria wa shirikisho wanaohusika katika ufyatuaji risasi huenda likizo wakati tukio hilo linachunguzwa.

    Maafisa wa Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha (ICE) aliyempiga risasi raia mwingine wa Marekani, Renee Good, mwenye umri wa miaka 37, huko Minneapolis mnamo Januari 7 pia alipewa likizo akisubiri uchunguzi.

    Soma zaidi:

  7. Habari za hivi punde, Milio ya risasi na milipuko yasikika karibu na uwanja wa ndege wa Niger

    Milio ya risasi na milipuko mikubwa imesikika nchini Niger karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa nje ya mji mkuu, Niamey.

    Simulizi nyingi za mashahidi na video zilionyesha mifumo ya ulinzi wa anga ikionekana ikishambulia makombora yasiyotambulika mapema Alhamisi.

    Hali baadaye ilitulia, ripoti zinasema, huku afisa mmoja akiripotiwa kusema hali sasa ilikuwa imedhibitiwa, bila kufafanua zaidi.

    Haijulikani ni nini kilisababisha milipuko hiyo, au kama kulikuwa na majeruhi wowote. Hakujakuwa na taarifa rasmi kutoka kwa serikali ya kijeshi.

    Milio ya risasi na milipuko ilianza muda mfupi baada ya saa sita usiku, kulingana na wakazi wa kitongoji kilicho karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani, shirika la habari la AFP linaripoti. Walisema utulivu ulirejea baada ya saa mbili.

    Uwanja wa ndege una kituo cha jeshi la anga na uko takriban kilomita 10 (maili sita) kutoka ikulu ya rais.

    Niger inaongozwa na Abdourahamane Tiani ambaye alichukua madaraka katika mapinduzi ya 2023 yaliyomuondoa madarakani rais mteule wa kiraia wa nchi hiyo.

    Kama majirani zake Burkina Faso na Mali, nchi hiyo imekuwa ikipambana na makundi ya jihadi ambayo yamefanya mashambulizi mabaya kote katika eneo hilo.

    Pia ni mzalishaji mkuu wa madini ya urani.

    Soma zaidi:

  8. Kocha wa Senegal apigwa marufuku baada ya vurugu za fainali ya AFCON

    Kocha wa Senegal, Pape Thiaw, amefungiwa michezo mitano baada ya matukio ya vurugu wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2025 dhidi ya Morocco mwezi huu.

    Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) lilimtoza Thiaw faini ya $100,000 (£72,000), likisema amepatikana na makosa ya kuonyesha "tabia zisizofaa wakati wa mchezo" na "kushusha hadhi ya mchezo".

    Fainali iliyofanyika tarehe 18 Januari mjini Rabat, ambayo Senegal ilishinda kwa bao 1-0, iligeuka kuwa vurugu wakati wachezaji wa Senegal walipoondoka uwanjani baada ya Morocco kupewa penalti ya dakika za mwisho.

    Thiaw, akiwa bado amekasirishwa na uamuzi wa mwamuzi muda mfupi kabla ya kumpiga faulo nahodha wa Morocco Achraf Hakimi kabla ya Ismaila Sarr kuingia kwa kichwa, aliwaamuru wachezaji wake waondoke uwanjani.

    Mechi hiyo ilicheleweshwa kwa takriban dakika 17 kabla ya mshambuliaji wa Senegal Sadio Mane kuwashawishi wachezaji wenzake kurudi uwanjani.

    Penalti ya Brahim Diaz iliokolewa na kipa wa Senegal Edouard Mendy, na mwamuzi Jean-Jacques Ndala kisha akapuliza filimbi mara moja kumaliza mchezo.

    Pape Gueye alifunga bao la ushindi katika dakika ya nne ya muda wa ziada na kuifungia Senegal ushindi wa pili wa Afcon katika miaka mitano.

    Washambuliaji wa Senegal Iliman Ndiaye na Sarr walipigwa marufuku ya mechi mbili kwa "tabia isiyofaa kimichezo dhidi ya mwamuzi", huku Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) likipigwa faini ya jumla ya $615,000 (£444,000).

    Mshambuliaji wa Morocco Ismael Saibari alipewa marufuku ya mechi tatu na kutozwa faini ya $100,000 (£72,000), huku mlinzi Hakimi akipewa marufuku ya mechi mbili, huku mchezo mmoja ukisimamishwa kwa miezi 12.

    Ombi la shirikisho la soka la Morocco (FRMF) la kutaka matokeo ya mechi hiyo yabatilishwe baada ya wachezaji wa Senegal kuondoka uwanjani lilitupiliwa mbali na kamati ya nidhamu ya Caf.

    Marufuku ya Thiaw na wachezaji hao wanne yanahusiana na mechi za Caf pekee na hayataathiri maandalizi ya Kombe la Dunia nchini Marekani, Canada na Mexico.

    Soma zaidi:

  9. CAF yaipiga faini ya dola 200,000 Morocco kwa kutaka 'kuiba' taulo la Senegal

    Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeorodhesha adhabu walizotoa kwa Morocco na Senegal kufuatia vurugu iliyoshuhudiwa wakati wa fainali ya AFCON 2026.

    Mashabiki wengi wa mpira walikuwa na hamu ya kujua hatua zipi zitashukuliwa na shirikisho hilo huku kila upande ukiamini mwenzake alikosea na anafaa kupata adhabu kali zaidi.

    CAF limempiga marufuku kocha wa Senegal, Pape Thiaw, michezo mitano na kumtoza faini ya $100,000 kutokana na mwenendo usio wa kispoti baada ya kuwaambia wachezaji wake waondoke uwanjani wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa dhidi ya Morocco.

    CAF pia ililazimisha shirikisho la soka la Senegal kulipa faini ya $615,000 kutokana na mwenendo wa timu na mashabiki wake, huku wachezaji Iliman Ndiaye na Ismaila Sarr wakifutwa michezo miwili ya CAF kwa mwenendo wa kutojali taratibu dhidi ya refa.

    Hata hivyo, ombi la Morocco la kubatilisha matokeo ya mechi baada ya wachezaji wa Senegal kuondoka uwanjani, jambo lililosababisha kucheleweshwa kwa dakika 14, lilitupiliwa mbali na Kamati ya Nidhamu ya CAF.

    Wenyeji Morocco pia walitakiwa kulipa faini jumla ya $315,000 kutokana na mwenendo wa wavulana wa mipira (ball boys) wakati wa mechi, mwenendo wa wachezaji na wafanyakazi wao katika eneo la VAR, pamoja na matumizi ya mwangaza leza na mashabiki.

    Kapteni wa Morocco, Achraf Hakimi (michezo miwili ya CAF, mojawapo ikisimamishwa kwa mwaka mmoja) na Ismael Saibari (michezo mitatu ya CAF), walifutwa kwa mwenendo usio wa kispoti baada ya kujaribu kuondoa taulo ya kipa wa Senegal, Edouard Mendy, wakati mvua inanyesha Rabat.

    Kocha wa Senegal, Thiaw, aliwaamuru wachezaji wake waondoke uwanjani mwishoni mwa mechi baada ya goli lao kubatilishwa, na dakika chache baadaye Morocco walipatiwa penati, ambayo hatimaye Brahim Diaz aliipoteza.

    Soma Pia:

  10. Kiongozi wa waasi wa Congo asema mkataba wa madini muhimu na Marekani ni batili kisheria

    Kiongozi wa muungano wa waasi wa Congo unaojumuisha kundi la M23, Corneille Nangaa, amesema kuwa mkataba kati ya Kinshasa na Washington kuhusu madini muhimu katika mkoa unaokumbwa na vita ni batili kisheria, wenye mapungufu makubwa, na hali yake inatia shaka kuhusu utekelezaji wake.

    Nangaa, anayesimamia Alliance Fleuve Congo (AFC), alikuwa akirejelea makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati yaliyosainiwa Washington Desemba 4, ambayo yangewezesha Marekani kupata ufikiaji mkubwa wa madini muhimu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ubadilishanaji wa uwekezaji na ushirikiano wa usalama.

    Katika mahojiano na Reuters mjini Goma Jumatatu, Nangaa alisema kuwa mpango huo una upungufu wa uwazi na mapungufu ya kisheria, akirejelea kile alichokiita “ukosefu wa uwazi katika mazungumzo” na “mapungufu ya taratibu, hasa ukiukwaji wa Katiba na sheria.”

    Ukosoaji wa Nangaa unaibua maswali zaidi kuhusu uwezekano wa uwekezaji wa Marekani mashariki mwa Congo, mkoa uliokumbwa na vita, mwaka mmoja baada ya M23 kuchukua Goma, mji mkubwa zaidi wa mkoa, katika shambulio la ghafla.

    Sehemu kubwa ya madini muhimu mashariki mwa Congo, ikiwa ni pamoja na coltan, ziko katika maeneo ambayo sasa yanashikiliwa na M23, ambayo imechukua eneo kuu la migodi kama Rubaya katika Kivu Kaskazini.

    Nangaa alisema kuwa maeneo ya migodi yaliyotolewa kwa Washington yanaweza baadaye kuwa chanzo cha migongano, kwa sababu tayari yanaweza kuwa yametolewa kwa washirika wengine.

    “Wamarekani wanaweza kuwa wamesaini mkataba huo, lakini wanapaswa kujua kuwa walisaini na utawala usio halali, na pia uliyo na ufisadi,” alisema.

    Kwa upande mwingine, Ikulu ya Congo ilikanusha shutuma za Nangaa, ikisema ushirikiano huo “uko ndani ya mamlaka ya kikatiba” ya rais na serikali waliochaguliwa.

    Ikulu ilisema hofu kuhusu migongano na wamiliki wa mikataba ya awali ni “makadirio tu”, na kwamba ushirikiano wowote utafuata mikataba halali na kanuni za madini za Congo.

    Serikali ya Congo imesema kuwa ushirikiano huu utawasilishwa kwa wabunge kwa ajili ya idhini mwezi Machi.

    “Tuna wingi thabiti bungeni, hivyo tunaamini tutapata idhini ya bunge,” alisema Makamu wa Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi wa Taifa, Daniel Mukoko Samba, kwa Reuters huko Davos wiki iliyopita.

    Soma Pia:

  11. Uzalishaji wa bangi kwa matumizi ya tiba waruhusiwa nchini Brazil

    Anvisa (Wakala wa Taifa wa Udhibiti wa Afya wa Brazil) imeruhusu rasmi, siku ya Jumatano (Januari 28), kilimo cha mmea wa Cannabis sativa nchini Brazil kwa matumizi ya tiba na utafiti wa kisayansi.

    Uamuzi huo umetokana na maelekezo ya Mahakama ya Juu ya Haki (STJ), ambayo mwezi Novemba 2024 ilithibitisha uhalali wa uzalishaji wa bangi kwa madhumuni ya tiba na/au dawa pekee, kama sehemu ya kulinda haki ya afya.

    Kwa matumizi ya tiba, wakurugenzi wa Anvisa wameidhinisha kwa kauli moja kilimo cha katani ya viwandani (industrial hemp), aina maalumu ya Cannabis sativa yenye kiwango cha tetrahydrokannabinoli (THC) kisichozidi asilimia 0.3.

    THC ndiyo kiungo kikuu cha mmea kinachosababisha athari za kisaikolojia.

    Aina hii ya bangi haisababishi kulevya, lakini ina kiwango kikubwa cha cannabidiol (CBD), ambayo inathaminiwa kwa uwezo wake wa tiba katika kusaidia wagonjwa wenye wasiwasi (anxiety), maumivu sugu, kifafa, matatizo ya usingizi, pamoja na magonjwa mengine ya mfumo wa neva.

    Kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa, uzalishaji utakuwa na mipaka kulingana na mahitaji ya dawa, na kampuni zitawajibika kutoa taarifa na sababu za kiasi kinachozalishwa, ikiwemo ukubwa wa ardhi (hekta) itakayotumika kwa kilimo.

    Kilimo hicho hakijaruhusiwa kwa umma kwa ujumla, bali kinaruhusiwa kwa kampuni na mashirika maalumu pekee, na hatua hii haijumuishi matumizi ya burudani ya bangi.

    Soma pia:

  12. China yawanyonga wanachama 11 wa genge la ulaghai la Myanmar

    China imewanyonga wanachama 11 wa familia maarufu iliyokuwa ikiendesha vituo vya ulaghai nchini Myanmar, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.

    Mahakama ya mkoa wa Zhejiang iliwahukumu wanachama wa familia ya Ming mwezi Septemba mwaka jana kwa makosa mazito yaliyohusisha mauaji, kuwazuia watu kinyume cha sheria, ulaghai, pamoja na kuendesha nyumba za kamari haramu.

    Familia ya Ming ilikuwa miongoni mwa koo kadhaa zilizotawala mji wa Laukkaing, uliopo karibu na mpaka wa China.

    Chini ya utawala wao, mji huo uliokuwa maskini na usiotambulika uligeuzwa kuwa kitovu cha kasinon, nyumba za starehe za ngono na uhalifu wa kifedha.

    Milki yao ya ulaghai iliporomoka mwaka 2023 baada ya wanachama wake kukamatwa na kukabidhiwa kwa China na makundi ya kijeshi ya kikabila yaliyokuwa yameuteka mji wa Laukkaing katika muktadha wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea Myanmar.

    Kwa miaka mingi, mitandao ya ulaghai nchini Myanmar imewanasa maelfu ya raia wa China, na pia bara la Afrika halijasazwa, ambao ni miongoni mwa mamia ya maelfu ya watu waliotekwa au kusafirishwa kwa nguvu hadi katika kambi hizo, ambako walilazimishwa kuwalaghai watu wa nchi za nje.

    Mwaka jana, mitandao ya kijamii nchini China ilitikiswa na habari za muigizaji mdogo aliyesafiri kwenda Thailand kwa kazi ya uigizaji lakini baadaye akalazimishwa kupelekwa katika kituo cha ulaghai Myanmar.

    Visa kama hivi vilizidisha hasira ya umma nchini China, huku Beijing kwa muda mrefu ikiishinikiza serikali ya kijeshi ya Myanmar kudhibiti magenge ya ulaghai.

    Kwa mujibu wa Mahakama Kuu ya China, shughuli za ulaghai na kamari za genge la Ming zilipata zaidi ya yuan bilioni 10 (sawa na dola bilioni 1.4 za Marekani) kati ya mwaka 2015 na 2023.

    Mahakama hiyo ilitupilia mbali rufaa zao mwezi Novemba. Mahakama ilisema uhalifu wa genge hilo ulisababisha vifo vya raia 14 wa China na kujeruhi watu wengine wengi.

    Soma Pia:

  13. Nyota wa Bollywood Arijit Singh atangaza kustaafu uimbaji katika filamu akiwa na miaka 38

    Mashabiki wa mwimbaji maarufu wa India, Arijit Singh, wameonyesha huzuni na heshima zao baada ya kutangaza kuwa hataimba tena nyimbo za filamu (playback singing), hatua inayofunga ukurasa muhimu katika muziki wa Bollywood wa kisasa.

    Baadhi ya mashabiki wamesema sauti yake ilikuwa “sauti ya huzuni na furaha zetu”, huku wengine wakisema ilikuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya watu wengi.

    Katika sinema ya India, playback singing ni pale mwimbaji anaporekodi wimbo studio na waigizaji wanauigiza kwa kusawazisha midomo kwenye filamu.

    Arijit Singh amekuwa mmoja wa waimbaji wakuu katika mtindo huu, hasa kwa nyimbo za mapenzi na nyimbo zilizopendwa sana.

    Singh, mwenye umri wa miaka 38, alitangaza uamuzi wake kupitia Instagram siku ya Jumanne, akisema: “Ninaacha hapa. Ilikuwa safari nzuri.”

    Tangu hapo, mitandao ya kijamii imejaa ujumbe wa mashabiki wakikumbuka jinsi nyimbo zake zilivyokuwa sehemu ya utamaduni wa India.

    Hakueleza sababu ya kuacha kuimba kwa filamu, lakini taarifa zinasema atakamilisha miradi aliyokuwa ameanza, na ataendelea kutunga na kuimba muziki wake binafsi, nje ya filamu za kibiashara.

    Hatua hii imewashangaza wengi kwa sababu imetokea wakati bado yuko kilele cha mafanikio.

    Hivi karibuni, aliimba mbele ya umati mkubwa uliojaa katika Wembley Arena, London, jambo linalofikiwa na waimbaji wachache wa India.

    Licha ya umaarufu wake, Arijit Singh amejulikana kwa kuepuka maisha ya umaarufu kupita kiasi.

    Hatoi mahojiano mara kwa mara, hapendi matangazo makubwa, na huonekana hadharani kwa mavazi ya kawaida.

    Aliwahi kusema: “Nachukia kuwa mtu maarufu.”

    Mwaka 2013, aliimba wimbo “Tum Hi Ho” katika filamu Aashiqui 2, wimbo uliobadilisha mwelekeo wa muziki wa mapenzi Bollywood kwa kuleta hisia za ndani na unyenyekevu.

    Wimbo huo ulipendwa sana kote India, ukachezwa redioni, harusi na vipindi vya televisheni.

    Baadaye, Singh alisema alihisi kero kusikia sauti yake kila mahali, na akaanza kupunguza idadi ya nyimbo alizokuwa akiimba.

    Licha ya yote, wengi wanaamini kuwa sauti ya Arijit Singh itaendelea kuishi na kuathiri muziki wa India kwa muda mrefu ujao.

    Soma Pia:

  14. Wademocrat wapendekeza masharti magumu ili kudhibiti vitendo vya ICE

    Wademocrat katika Baraza la Seneti wametoa orodha ya matwakwa yanayokusudia kudhibiti vitendo vya maafisa wa uhamiaji wanaohusika na msako dhidi ya wahamiaji haramu ICE, matakwa ambayo maseneta hao wanasema sharti yafungamanishwe na mswada wa fedha kwa ajili ya wizara ya usalama wa ndani.

    Miongoni mwa matakwa hayo ni kuwapiga marufuku maafisa hao wa ICE kuvaa barakoa na doria kali za kushtukiza na badala yake wahitaji waranti, hati ya upekuzi, wa kumkamata mtu kutoka kwa Jaji.

    Kiongozi wa wademocrat kwenye seneti Chuck Schumer amesema matakwa yao sharti yazingatiwe akisema

    ''Tunataka barakoa zivuliwe na Kamera wanazovaa mwilini ziwashwe,maafisa wa uhamiaji wanapaswa kukatazwa kuvaa barakoa, lazima kamera zao ziwashwe na walazimike kubeba vitambulisho vinavyostahili.Hakuna tena maafisa wasiojulikana,hakuna tena operesheni za kisirisiri na iwapo warepublican watapinga,ni kwamba wanachagua vurugu badala ya kuwepo utaratibu,hivyo ndivyo ilivyo''

    Unaweza Kusoma Pia:

  15. Je, unafahamu uwezo wa Jeshi la Iran Revolutionary Guard ?

    IRGC (Islamic Revolutionary Guard Corps) ni jeshi maalumu la Iran lililoanzishwa mwaka 1979 baada ya Mapinduzi ya Kiislamu.

    Kazi yake ni nini?

    • Kulinda utawala wa Kiislamu wa Iran.

    • Kumtii moja kwa moja Kiongozi Mkuu wa Iran, si serikali ya kawaida.

    • Kudhibiti usalama wa ndani na nje ya nchi.

    IRGC hufanya nini?

    • Ina jeshi lake, anga, majini na idara ya ujasusi

    • Inaendesha operesheni nje ya Iran kupitia kikosi chake kinachoitwa Quds Force

    • Inahusishwa na kusaidia makundi yenye silaha katika nchi kama Syria, Iraq, Lebanon na Yemen

    • Ina ushawishi mkubwa katika siasa na uchumi wa Iran.

    Kwa nini inapingwa?

    Nchi za Magharibi zinaishutumu IRGC kwa:

    • Kusaidia ugaidi

    • Kukandamiza haki za binadamu

    • Kuchochea migogoro katika Mashariki ya Kati.

    Kwa sababu hizo:

    • Marekani tayari imeliorodhesha IRGC kama kundi la kigaidi.

    • Umoja wa Ulaya unajadili kufanya uamuzi huo huo.

    Utawala wa rais Donald Trump umedai kwamba wapiganaji wa Quds pia wanatumiwa na Iran kama njia mojawapo ya kuwasaidia magaidi katika eneo la mshariki yakati-ikiwemo kundi la Hezbollah nchini Lebanon pamoja na kundi la Palestina Islamic Jihad -kwa kuwapatia fedha , mafunzo, silaha na vifaa.

    Wapiganaji wa Quds pia wametuhumiwa na Marekani kwa kupanga njama kutekeleza mashambulio ya kigiaidi , moja kwa moja ama kupitia washirika wake katika mabara matano kati ya saba.

    Wapiganaji wa Quds walidai kuhusika katika njama ya kumuua balozi wa Saudia nchini Marekani kwa kulipua mgahawa mjini Georgetown.

    Na mwaka uliopita , mahakama nchini Ujerumani ilimuhukumu mwanachama wa wapiganaji wa Quds kwa kumpeleleza kiongozi wa kundi la Ujerumani na Isra na watu wakaribu.

    Unaweza pia Kusoma:

  16. Umoja wa Ulaya wafikia makubaliano kuitangaza IRGC kuwa kundi la kigaidi

    Umoja wa Ulaya umefikia makubaliano ya kuitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) kuwa kundi la kigaidi.

    Baada ya Uhispania na Ufaransa kuunga mkono hatua hiyo, pamoja na utayari wa Italia na Ujerumani ambazo hapo awali zilikuwa zimeunga mkono wazo hilo ndani ya Umoja wa Ulaya, inaonekana kuwa wabunge wa Bunge la Ulaya wamekubaliana kuidhinisha uamuzi huo.

    Siku ya Jumatano, Januari 28, Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola, aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: “Wiki hii, Ulaya ina fursa na wajibu wa kihistoria wa kulitangaza rasmi Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la utawala wa Iran kuwa kundi la kigaidi.”

    Kabla ya kauli hiyo, mbunge wa Bunge la Ulaya, Hannah Neumann, alikuwa ametangaza kukubali kwa Uhispania na akaandika kwenye mtandao wa X:

    “Sasa kinachobaki ni Ufaransa.” Baadaye, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa alitangaza kuwa Paris inaunga mkono uamuzi huo.

    Inatarajiwa kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya watapiga kura leo, Alhamisi, Januari 29, kuhusu kuweka vikwazo vipya dhidi ya watu wanaokiuka haki za binadamu na kampuni 10 zinazohusishwa na utengenezaji wa ndege zisizo na rubani (drones) za Iran.

    Awali wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia alisema angependekeza IRGC iongezwe katika orodha ya makundi ya kigaidi ya Umoja wa Ulaya.

    Kufuatia kauli hiyo, Iran ilimwita balozi wa Italia mjini Tehran kwenda Wizara ya Mambo ya Nje kulalamikia hatua hiyo.

  17. Ndege yaanguka Colombia, watu wote 15 waliokuwemo wafariki dunia

    Ndege ya abiria imeanguka kaskazini mwa Colombia, na kuwaua watu wote 15 waliokuwemo, shirika la ndege la serikali la nchi hiyo, Satena, limethibitisha.

    Katika taarifa, shirika hilo lilisema ndege yake aina ya Beechcraft 1900'', ilipata ajali mbaya,” lakini halikutoa maelezo zaidi.

    Mabaki ya ndege hiyo sasa yamepatikana katika eneo la milima.

    Orodha rasmi ya abiria inajumuisha mbunge Diógenes Quintero Amaya na Carlos Salcedo, mgombea katika uchaguzi ujao wa bunge.

    Awali, Satena ilisema mawasiliano na ndege hiyo yalikatika dakika 11 kabla ya muda uliopangwa wa kutua katika mji wa Ocaña, karibu na mpaka wa Venezuela, saa 12:05 kwa saa za eneo (17:05 GMT) siku ya Jumatano.

    Kwa mujibu wa shirika la ndege, Safari ya NSE 8849 iliondoka katika mji wa Cúcuta, takribani kilomita 100 (maili 62) kaskazini-mashariki mwa Ocaña, ikiwa imebeba abiria 13 na wahudumu wawili wa ndege.

    Operesheni ya utafutaji miili imeanzishwa katika eneo la milima, na namba ya simu ya dharura imewekwa kwa ajili ya ndugu wa waliokuwemo ndani ya ndege.

    Akizungumza na chombo cha habari cha ndani, Semana, gavana wa Norte de Santander, William Villamizar, alisema miili saba imepatikana.

    Taarifa ya kuthibitisha kifo cha Quintero imeshirikiwa kupitia ukurasa wake wa Facebook, ikimuelezea kama “mtu ambaye katika maisha yake yote aliwahudumia wale waliokuwa na uhitaji mkubwa zaidi.”

    Quintero alikuwa akishikilia kiti kimoja kati ya viti 16 katika bunge la Colombia vilivyotengwa kuwakilisha waathirika wa mgogoro kati ya jeshi la waasi wa Kimaaandiko ya Marx, Vikosi vya Mapinduzi vya Silaha vya Colombia (FARC), na serikali ya Colombia.

    Soma pia:

  18. Iran yasema itajibu mapigo hadi Tel Aviv iwapo Marekani itathubutu kuishambulia

    Iran imetangaza kuwa imejumuisha mji wa Tel Aviv katika orodha ya maeneo itakayoshambulia iwapo itashambuliwa na Marekani au washirika wake, ikionya kuwa itajibu kwa haraka, kwa shambulilo lisilo na kifani. Kauli hiyo imekuja wakati mvutano kati ya Tehran, Washington na Israel ukiendelea kuongezeka.

    Onyo hilo limetolewa na mshauri mkuu wa kiongozi wa juu wa Iran, Ali Shamkhani, ambaye alisema kuwa shambulio lolote la kijeshi la Marekani litachukuliwa kama tangazo la vita. Alisisitiza kuwa dhana ya “shambulio dogo” haipo na kwamba Iran italenga mshambuliaji ambaye ni Marekani pamoja na mji wa Tel Aviv.

    Jeshi la Iran na walinzi wa mapinduzi pia wamesema wako tayari kwa hali zote za kivita. Msemaji wa walinzi wa mapinduzi, Ali Mohammad Naeini, alionya kuwa uzoefu wa vita vya awali umeonyesha kushindwa kijeshi dhidi ya Iran, akisisitiza kuwa majeshi ya Iran ndiyo yataamua mwisho wa mapambano.

    Wakati huo huo, Marekani imeongeza kwa kiasi kikubwa uwepo wake wa kijeshi Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na kupeleka meli kubwa ya kivita ikiongozwa na manowari ya kubeba ndege ya Abraham Lincoln. Hatua hiyo imechochea hofu ya uwezekano wa shambulio la mapema kutoka Washington.

    Rais Donald Trump ameionya Iran kwamba "muda unakwisha" wa kujadili makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia kufuatia ongezeko la vikosi vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Ghuba.

    Kwa upande wmignien Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema serikali ya Iran iko dhaifu kuliko wakati mwingine wowote na huenda ikakabiliwa na maandamano mapya ya wananchi, huku akibainisha kuwa haijulikani ni nani atachukua nafasi ya Kiongozi wa juu iwapo angeondolewa madarakani.

    Kwa upande wake, Iran imekanusha madai ya udhaifu wa ndani, ikieleza kuwa maandamano ya hivi karibuni ni njama za kigeni. Serikali ya Tehran imesisitiza kuwa itatetea mamlaka, uhuru na mfumo wake kwa nguvu zote endapo itakabiliwa na shambulio lolote la kijeshi.

  19. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya habari za moja kwa moja leo Alhamisi Januari 29, 2025

Trending Now