Rais Donald Trump amemkosoa Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer kwa mara ya pili wiki hii, akisema "inasikitisha kuona" uhusiano wa kipekee ukiharibika baada ya Uingereza kusita kutoa msaada kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran.
Starmer amesema Uingereza haikushiriki katika shambulizi dhidi ya Iran lililofanywa na Marekani na Israeli kwa sababu hatua yoyote ya kijeshi ya Uingereza lazima iwe na "mpango unaofaa uliotathminiwa vyema" na hakuamini katika "kupinduliwa kwa serikali kupitia nguvu ya nje".
Lakini tangu wakati huo ameruhusu Marekani kutumia kambi za Uingereza kuanzisha kile alichokiita mashambulizi kidogo ya kujilinda ili kudhoofisha uwezo wa Iran, ambayo imewashambulia washirika wa Marekani katika eneo hilo kwa ndege zisizo na rubani na makombora.
Siku ya Jumatatu, kambi ya Uingereza huko Cyprus ilishambuliwa na ndege isiyo na rubani ambayo maafisa wa Cyprus walisema huenda ilirushwa na kundi la Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran.
Trump alisema hakuhitaji msaada wa Uingereza kuishambulia Iran lakini akaongeza kuwa kusuasua huko kumeikatisha tamaa.
"Inasikitisha sana kuona kwamba uhusiano huu si kama ulivyokuwa," Trump aliambia gazeti la Sun katika mahojiano yaliyochapishwa Jumanne.
Aliambia Telegraph siku ya Jumatatu kwamba Starmer alionekana kuwa na "wasiwasi kuhusu uhalali" wa mashambulizi dhidi ya Iran, alipoanza kufikiria iwapo ataruhusu kambi muhimu ya kijeshi ya Uingereza, Diego Garcia, itumike.
Akizungumza na gazeti la Sun, Trump alisema kwamba hajawahi kufikiria kuwa angeiona Uingereza ikiwa mshirika wa kusuasua, na badala yake alizisifu Ufaransa na Ujerumani.
"Huu ulikuwa uhusiano imara zaidi kuliko wote," alisema. "Na sasa tuna uhusiano imara sana na nchi zingine barani Ulaya."
"Ufaransa imekuwa bora. Wote wamekuwa wazuri. Uingereza imekuwa tofauti sana na nchi zingine."
Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zote zilitoa taarifa ya pamoja kujibu mashambulizi ya Iran siku ya Jumamosi, zikisema kwamba zilikuwa na mawasiliano ya karibu na Marekani, Israel na washirika wake katika eneo hilo, na zikatoa wito wa kuanza tena kwa mazungumzo.
Starmer amekosolewa kutoka pande zote za nyumbani kwa uamuzi huo, huku wapinzani upande wa kushoto wakimtaka alaani kitendo hicho cha kijeshi na upande wa kulia, viongozi wa upinzani Kemi Badenoch na Nigel Farage wakimshambulia Starmer kwa kushindwa kumuunga mkono mshirika mkuu wa usalama na ujasusi wa Uingereza.