'Sampuli ya kipekee sana ya kibaiolojia': Siri iliyojificha katika damu ya hedhi

Muda wa kusoma: Dakika 9

Kama wanawake wengi wanaopata hedhi, Emma Backlund alipendelea kutofikiria sana kuhusu damu anayopoteza kila mwezi. Lakini mwaka 2023, kampuni ya teknolojia ya kibaolojia NextGen Jane ilipomuomba damu ya hedhi yake kwa ajili ya utafiti, Backlund alikubali kwa urahisi.

Alihifadhi tamponi nane kutoka kwenye mzunguko mmoja wa hedhi na kuzituma kwa posta kwenda maabara ya kampuni hiyo huko Oakland.

Ingawa lilikuwa ombi lisilo la kawaida, halikuwa gumu sana kwake kulifanya, hasa kama lingeweza kusaidia wasichana wa baadaye kuepuka maumivu makali aliyopitia alipokuwa akikua.

"Nikiwa na miaka 11 nilipopata hedhi yangu ya kwanza, nilidhani nakufa," anasema Backlund, mwanafunzi wa shahada ya uzamili mwenye miaka 27 kutoka Minnesota nchini Marekani.

"Nakumbuka nikimwambia mama yangu ninahitaji kwenda hospitali. Na karibu kila hedhi niliyopata tangu wakati huo ilikuwa hivyo. Nilikuwa natapika kila mwezi. Nilikuwa nakosa shughuli za kijamii na hata shule. Ilikuwa ni maumivu ya kuchoma, kuchoma sana tumboni, na maumivu makali sana."

Ilichukua miaka 13 kwa Backlund kugundua kuwa alikuwa na ugonjwa unaoitwa Endometriosis, ambao ni ugonjwa sugu unaosababisha tishu zinazofanana na zile za ndani ya mfuko wa uzazi kukua nje ya mfuko huo.

Endometriosis husababisha watu milioni 190 duniani, takribani asilimia 10 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa, kuteseka na hedhi nzito, maumivu makali ya nyonga, matatizo ya kibofu au utumbo, na hata utasa.

Mbaya zaidi ni kwamba mara nyingi huchukua kati ya miaka 5 hadi 12 kupata utambuzi sahihi wa ugonjwa huu, kama ilivyokuwa kwa Backlund.

Ili kuthibitisha ugonjwa huu, mara nyingi daktari hutumia upasuaji mdogo unaoitwa laparoscopy, ambapo kamera ndogo huingizwa ndani ya eneo la nyonga, anasema Ridhi Tariyal, mwanzilishi mwenza na mkurugenzi mkuu wa NextGen Jane.

Ndiyo sababu Tariyal na viongozi wengine wa kampuni bunifu wanafanya kazi ya kutengeneza kipimo bora cha uchunguzi, kipimo kitakachokuwa cha haraka, cha bei nafuu, na kisichohitaji upasuaji. Pia kinaweza kufichua mambo mengi zaidi kuhusu afya ya mwanamke kuliko tu kugundua endometriosis.

Siri, wanaamini, iko kwenye damu ya hedhi.

Thamani kubwa sana kwa utafiti

Madaktari wamekuwa wakichunguza sampuli za mkojo tangu nyakati za kale za Babyloni na Sumerian , takribani miaka 6,000 iliyopita. Baadaye, sampuli za kinyesi na damu inayochukuliwa kwenye mishipa (venous blood) zilianza pia kutumika katika uchunguzi wa kitabibu, karibu karne moja au mbili zilizopita.

Lakini damu ya hedhi haijawahi kupewa umakini mkubwa katika tiba. Hata hivyo, ni majimaji yenye muundo mgumu: takribani nusu yake ni damu ya kawaida, na sehemu iliyobaki ina protini, homoni, bakteria, tishu za endometriamu, pamoja na seli zinazotoka kwenye uke, mlango wa kizazi, mirija ya uzazi, ovari, na maeneo mengine.

"Unapata aina za seli na alama nyingine za kibiolojia ambazo huwezi kuzipata kwenye damu ya kawaida, mate, au aina nyingine za sampuli," anasema Ridhi Tariyal. "Kimsingi ni kama uchunguzi wa tishu (biopsy) wa asili unaokupa taarifa kuhusu viungo vya uzazi."

Kampuni yake, NextGen Jane, hutuma tamponi za pamba zilizoundwa maalum kwa washiriki wa kujitolea kama Emma Backlund. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2014, kampuni hiyo imechambua zaidi ya sampuli 2,000 za damu ya hedhi kutoka kwa zaidi ya wanawake 330.

"Unaweza kutumia damu ya hedhi kutafuta karibu hali yoyote ya kiafya inayohusiana na mfuko wa uzazi na zipo nyingi," anasema Christine Metz, mwanabiolojia wa uzazi katika Feinstein Institutes for Medical Research ya Northwell Health nchini Marekani.

Zaidi ya muongo mmoja uliopita, Metz alianza kuchunguza damu ya hedhi ili kutambua alama za kibiolojia (biomarkers) za ugonjwa wa Endometriosis. Lakini sasa pia ana shauku ya kuona kama majimaji hayo yanaweza kutoa dalili za magonjwa mengine, kama vile Endometrial cancer, Adenomyosis, hali ambapo utando wa ndani wa mfuko wa uzazi hukua ndani ya ukuta wa mfuko wa uzazi na Endometritis, ambayo ni uvimbe au uvimbe wa muda mrefu wa utando wa mfuko wa uzazi.

"Majimaji ya hedhi yana thamani kubwa sana katika kuelewa afya ya mfuko wa uzazi, jambo ambalo hatuna njia nyingine rahisi ya kulifikia," anasema Metz. "Ni sampuli ya kibaolojia iliyo ya kipekee sana."

Kwa mfano, utafiti mmoja uligundua protini 385 ambazo hupatikana tu katika damu ya hedhi.

Mbali na kupatikana kila mwezi, faida nyingine kubwa ya damu ya hedhi ni kwamba inatoa picha pana zaidi ya afya ya mfuko wa uzazi ikilinganishwa na kipande kidogo cha tishu kinachochukuliwa wakati wa kipimo kinachoitwa endometrial biopsy.

"Mfuko wa uzazi una ukubwa takribani wa tunda la zabibu kubwa (grapefruit), hivyo kwa biopsy ya endometriamu hupati tathmini ya sehemu yote," anasema Metz, ambaye huwapa washiriki wa utafiti wake vikombe vya hedhi (menstrual cups) kukusanya sampuli. "Lakini majimaji ya hedhi yanawakilisha utando wote wa endometriamu unaomwagika."

Utafutaji wa alama maalum za kibaolojia

Kwa sababu damu ya hedhi imekuwa ikipuuzwa kwa muda mrefu katika utafiti wa kisayansi, bado haijulikani wazi kama ugonjwa wa Endometriosis una alama maalum za kibaolojia (biomarkers) zinazoweza kutegemewa kwa kipimo cha uchunguzi.

Hata hivyo, Christine Metz pamoja na mshirika wake wa utafiti, mtaalamu wa jenetiki Peter Gregersen, wamechunguza zaidi ya wanawake 3,700, na matokeo ya awali yanaonesha matumaini.

"Kuna tofauti nyingi," anasema Metz. Kwa mfano, wanawake walio na endometriosis waliothibitishwa kuwa nayo huwa na idadi ndogo sana ya seli za kinga zinazoitwa uterine natural killer cells.

Seli hizi ni sehemu ya mfumo wa kinga na zina jukumu muhimu katika ujauzito wa mapema, kama vile:

Kusaidia kiinitete kujipandikiza kwenye mfuko wa uzazi,

Kusaidia ukuaji wa kondo la nyuma (placenta), na kulinda dhidi ya maambukizi.

"Zinahusiana sana na uwezo wa kupata ujauzito, hivyo kuwa na chache sana si jambo zuri," anasema Metz.

Timu yake pia iligundua tofauti muhimu katika seli zinazoitwa stromal fibroblast, ambazo husaidia kurekebisha na kujenga upya utando wa mfuko wa uzazi baada ya kila hedhi.

Waligundua kwamba wakati endometriosis ipo:

seli hizi huonesha ishara nyingi zaidi za uvimbe (inflammatory markers),

na huwa hazina uwezo mkubwa wa kusababisha mabadiliko yanayosaidia kuandaa mfuko wa uzazi kwa ujauzito.

Tatizo hili pia limehusishwa na magonjwa mengine kama:

Polycystic Ovary Syndrome (PCOS),

na kuharibika kwa mimba mara kwa mara (recurrent miscarriages).

Maabara ya Christine Metz pia iligundua kuwa uonyeshaji wa baadhi ya jeni hubadilika kwa wagonjwa wenye Endometriosis.

Kwa pamoja, tofauti hizi ndizo ambazo madaktari wanaweza kuzitafuta wakati wa kutumia kipimo mbadala kisichohitaji upasuaji cha kugundua endometriosis kupitia uchambuzi wa damu ya hedhi.

Metz ana matumaini ya kuomba idhini ya Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani ili kuanzisha kifaa cha kujipima nyumbani (at-home diagnostic kit) ifikapo mwaka 2027.

Kwa upande mwingine, watafiti wa NextGen Jane wanatoa na kuchambua messenger RNA (mRNA) kutoka kwenye damu ya hedhi ili kutafuta alama maalum za ugonjwa wa endometriosis (biomarkers).

Hadi sasa, wamegundua alama kadhaa wanazoamini zinaweza kutofautisha kwa uhakika wanawake wenye endometriosis na wale walio na afya nzuri, hasa kwa wanawake wanaokabiliwa na matatizo ya utasa.

Utafiti mwingine unaofanyika nchini Marekani unaohusisha mamia ya wanawake wenye endometriosis unaendelea sasa ili kuthibitisha matokeo hayo, anasema Ridhi Tariyal.

Mnamo Mei 2025, NextGen Jane ilipokea ruzuku ya dola milioni 2.2 za Marekani (£1.62 milioni) ili kufadhili uthibitishaji wa kitabibu (clinical validation) wa kipimo cha hedhi cha kugundua endometriosis kwa wagonjwa wenye matatizo ya uzazi.

Siyo afya ya uzazi tu

Lakini damu ya hedhi inaweza kuwa muhimu zaidi kuliko kugundua tu ugonjwa wa Endometriosis. Kwa mfano, utafiti wa NextGen Jane umeonesha pia uhusiano kati ya afya ya mfuko wa uzazi na kuzeeka kwa mwili.

"Bado ni data za awali," anasema Ridhi Tariyal, lakini kuna "mwelekeo unaoonekana wazi" kati ya kupungua kwa homoni ya estrogen mwilini, mbayo mara nyingi huhusishwa na mchakato wa kuzeeka na mabadiliko yanayotokea katika hedhi.

Uchunguzi wao pia unaonesha kuwa siku zijazo damu ya hedhi inaweza kusaidia kugundua magonjwa ya mfumo wa kinga, kama vile:

Hypothyroidism (tezi ya thyroid kuzalisha homoni chache sana)

Hyperthyroidism (tezi ya thyroid kuzalisha homoni nyingi kupita kiasi)

Katika hali hizi, tezi ya thyroid hutengeneza homoni muhimu zinazodhibiti metabolism ya mwili, hasa thyroxine (T4) na triiodothyronine (T3).

"Inatokea pia kwamba watu wengi wenye endometriosis mara nyingi huwa na ugonjwa fulani wa autoimmune," anasema Tariyal.

Kwa sababu mwili hubadilika kutoka hali ya uvimbe kwenda kupona kwa jeraha bila makovu wakati wa mzunguko wa hedhi, kuchunguza damu ya hedhi kunaweza kutoa mfumo mpya wa kisayansi wa kujifunza magonjwa ya uchochezi na ya mfumo wa kinga, kama vile:

Rheumatoid arthritis

Lupus

Multiple sclerosis.

Damu ya hedhi pia imeonekana kuwa na manufaa katika kugundua ugonjwa wa kisukari. Katika tafiti zilizofanywa mwaka 2021 na 2024, watafiti kutoka kampuni ya kuanzisha teknolojia ya afya ya Qvin iliyoko California waligundua kwamba kiwango cha wastani cha sukari katika damu ya hedhi kinaonesha kwa usahihi kiwango cha sukari katika damu ya mwili kwa ujumla.

Matokeo haya yalisababisha kutengenezwa kwa kipimo cha kwanza na cha pekee kilichoidhinishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani mwaka 2024 cha kupima sukari kwa kutumia damu ya hedhi. Kipimo hicho ni taulo la kike maalum wanaloita Q-Pad.

Taulo hilo lina kipande kinachoweza kutolewa ili kukusanya damu, ambacho mtumiaji hukituma kwa maabara za Qvin kwa ajili ya uchambuzi.

Kampuni hiyo pia ilionesha, katika utafiti wa mwaka 2022 uliofanyika nchini Thailand, kwamba sampuli zilizokusanywa kwa kutumia pedi yao maalum zilikuwa bora zaidi katika kugundua aina hatari za virusi vya Human papilloma (HPV) ambavyo vinaweza kuongeza hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi, ikilinganishwa na kipimo cha kawaida cha Pap smear.

Jaribio kubwa zaidi la kuthibitisha matokeo haya linaendelea sasa nchini Marekani.

Kuanzia mwaka huu, utafiti huo pia utaangalia kama Q-Pad inaweza kutumika kupima magonjwa ya zinaa, kama vile: Chlamydia na kisonono, anasema Mads Lillelund, mmoja wa wakurugenzi wakuu wa Qvin.

Baadaye, Lillelund anatarajia pia kuchunguza viashiria vingine vya afya, kama vile:

homoni za thyroid,homoni za uzazi, viashiria vya uvimbe na hata kingamwili (antibodies) zinazoonesha mwitikio wa kinga dhidi ya virusi vya SARS-CoV-2.

Vivyo hivyo, kampuni ya kuanzisha teknolojia ya afya ya theblood yenye makao yake Berlin kwa sasa inathibitisha kifaa cha kupima kinachoweza kusaidia kutabiri:

Endometriosis, kuingia mapema kwenye ukomo wa hedhi (early menopause), Polycystic Ovary Syndrome (PCOS) na matatizo ya uzazi.

Mabadiliko ya mtazamamo kuhusu hedhi

Licha ya maendeleo haya, mambo mengi kuhusu damu ya hedhi bado hayajafahamika kikamilifu. Moja ya maswali makubwa, watafiti wengi wanakubaliana, ni kwamba bado hatujatambua vipengele vyote vilivyomo ndani yake na jinsi vinavyoweza kubadilika haraka wakati wa hedhi.

Utafiti katika eneo hili bado uko katika hatua za mwanzo, hasa kwa sababu ya unyanyapaa wa kitamaduni unaozunguka mada ya hedhi.

"Sote tumekuzwa tukiamini kuwa ni jambo la aibu hata kulizungumzia," anasema Christine Metz.

Changamoto nyingine ni upendeleo wa kihistoria katika tafiti za kitabibu, ambazo mara nyingi zilihusisha zaidi wanaume kuliko wanawake, pamoja na ukosefu wa fedha za kutosha kwa tafiti za afya ya wanawake.

Duniani kote, tafiti kuhusu afya ya wanawake zilipokea asilimia 5 tu ya fedha za utafiti na maendeleo mwaka 2020.

"Ugunduzi mwingi wa dawa umefanywa zaidi kwa wanaume, labda wanaume weupe, huku kukiwa na utofauti mdogo wa kijinsia au kikabila," anasema Mads Lillelund. "Kwa kweli, fedha nyingi zaidi zimetumika kutafiti upara wa wanaume kuliko ugonjwa wa Endometriosis."

Wanawake wengi, akiwemo Emma Backlund, wanaoishi na maumivu ya kila siku ya endometriosis na matatizo mengine ya mfuko wa uzazi, wanasema utafiti wa aina hii ulichukua muda mrefu sana kuanza.

Kukua akiwa na hedhi zenye maumivu makali huku akijiuliza nini kilikuwa kibaya "kulimfanya ajisikie mpweke na kutengwa sana," anasema Backlund.

Lakini kama watafiti wa damu ya hedhi watafanikiwa kutengeneza kipimo cha uchunguzi kisichohitaji upasuaji, ana matumaini kwamba kizazi kijacho cha wasichana kitapata matibabu mapema zaidi, na hivyo kuepuka maumivu ya mwili na msongo wa kihisia aliopitia alipokuwa akikua.