Mataifa ya Afrika yanavyohaha kunusuru raia wao kupigana vita

Muda wa kusoma: Dakika 4

Mataifa kadhaa ya Afrika yanaendelea kukumbwa na changamoto kubwa ya kuwazuia au kuwaokoa raia wao wanaoripotiwa kujiunga na jeshi la Urusi kupigana katika vita vya Ukraine, huku serikali zikijaribu kuweka sawa uhusiano wao wa kidiplomasia na Moscow.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, anatarajiwa kufanya ziara nchini Urusi wiki hii katika jitihada za kushughulikia suala la Wakenya wanaoripotiwa kujiunga na jeshi la Urusi.

Serikali ya Kenya inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa familia za baadhi ya waliokwenda vitani, ambazo zinataka hatua zichukuliwe ili kuwarudisha nyumbani. Hata hivyo, Nairobi inaonekana kuchukua mkondo wa tahadhari ili kuepuka mvutano wa moja kwa moja na Moscow.

Mudavadi amesema Kenya haitaki raia wake kujiunga na jeshi la kigeni kupigana vita vya Ukraine.

"Tunataka Wakenya wasiajiriwe kabisa katika jeshi hilo," alisema Mudavadi akizungumza kabla ya safari yake.

Aliongeza kuwa serikali inalazimika kushughulikia suala hilo kwa uangalifu kwa kuwa Urusi ni taifa lenye nguvu kubwa duniani na lina uhusiano wa muda mrefu na Kenya.

Waafrika vitani

Ripoti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa Waafrika wengi wamejiunga na vikosi vya Urusi, mara nyingi wakiahidiwa kazi za kiraia zenye mishahara mikubwa kupitia mawakala au kampuni za watu wa kati. Hali hiyo imezua wasiwasi katika nchi kadhaa za bara hilo, ikiwemo Ghana na Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa Ukraine, zaidi ya Waafrika 1,700 wanapigana upande wa Urusi katika vita vinavyoendelea. Hata hivyo wachambuzi wanaamini idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko inayoripotiwa rasmi.

Ripoti ya Idara ya Ujasusi ya Kenya inasema zaidi ya Wakenya 1,000 wanaweza kuwa wamejiunga na vikosi vya Urusi, ingawa serikali haijathibitisha idadi kamili.

Mwezi Februari, Ghana ilisema zaidi ya raia wake 50 wamefariki katika vita hivyo baada ya "kushawishiwa" kujiunga kwenye vita. Waziri wa mambo ya nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, alisema huenda idadi halisi ikawa kubwa zaidi.

Kwa upande wake, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi, Maria Zakharova, alithibitisha Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov atakutana na Mudavadi kujadili maendeleo ya uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Moscow na Nairobi.

Uchunguzi Afrika Kusini

Nchini Afrika Kusini, maafisa wanasema uchunguzi unaendelea kubaini mazingira yaliyowafanya baadhi ya raia wake kwenda kupigana vitani. Mkurugenzi mkuu wa idara ya mambo ya nje ya nchi hiyo, Zane Dangor, amesema uchunguzi huo pia utaangalia iwapo kundi la mamluki la Urusi linalojulikana kama Wagner Group lilihusika katika kuajiri Waafrika hao.

Shirika la utafiti la Inpact lenye makao yake Geneva limesema limehakiki orodha ya raia 1,417 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika waliodaiwa kujiunga na vikosi vya Urusi. Ripoti yake inaonyesha kuwa Cameroon, Misri na Ghana ni miongoni mwa nchi zilizo na idadi kubwa ya walioajiriwa.

Mtafiti wa Inpact, Lou Osborn, amesema huenda takwimu hizo ni sehemu ndogo tu ya tatizo.

"Tunaamini tunaanza tu kugundua ukubwa halisi wa tatizo hili," alisema.

Waziri wa Ghana Ablakwa amesema mataifa ya Afrika yanapaswa kushughulikia suala hilo kwa pamoja.

"Ikiwa Waafrika wanavutwa kuingia katika vita vya kigeni kupitia udanganyifu au unyonyaji, basi Afrika inapaswa kujibu kwa pamoja," alisema.

Hata hivyo mchambuzi wa International Crisis Group, Pier Pigou, anaamini kuwa suala hilo huenda lisiharibu sana uhusiano kati ya Urusi na nchi nyingi za Afrika isipokuwa kama litazua hasira kubwa ya kisiasa ndani ya mataifa hayo.

Je, tutashuhudia Waafrika kwenye vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati?

Kadri taarifa za kuajiriwa kwa Waafrika kupigana katika vita vya nje zinavyozidi kuibuka, wachambuzi wanaonya kuwa hali hiyo inaweza kuongezeka katika migogoro mingine ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na ile ya Mashariki ya Kati. Marekani ikishirikiana na Israel inakabiliana na Iran ambayo inaelekeza mashambulizi pia katika mataifa mengine ya Mashariki ya Kati.

Baadhi ya wataalamu wanasema ukosefu wa ajira, umaskini na ahadi za mishahara mikubwa kutoka kwa mawakala wa ajira wa nje vinaweza kuwafanya vijana wengi barani Afrika kuwa rahisi kushawishiwa kujiunga na mapigano katika maeneo yenye migogoro.

Wakati huo huo, serikali za Afrika zinakabiliwa na kazi ngumu ya kulinda raia wao dhidi ya udanganyifu huo huku zikidumisha uhusiano wa kidiplomasia na mataifa yenye ushawishi mkubwa duniani.

Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa bila hatua za pamoja za kikanda na kimataifa kudhibiti mitandao ya ajira kwa wapiganaji wa kigeni, kuna uwezekano kwamba Waafrika zaidi wataendelea kuonekana katika migogoro ya nje ya bara lao, hali inayoweza kuibua maswali mapya kuhusu usalama, ajira na mustakabali wa vijana barani Afrika.