Makadirio mabaya ya Donald Trump kuhusu vita vya Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Gazeti la The Independent linasema kuwa "makadirio mabaya ya Trump kuhusu Iran yameanza kuonekana."
Uchambuzi huo unasema kuwa wiki mbili baada ya Trump kuanzisha vita nchini Iran, ni wazi kwamba makadirio yake siyo sahihi.
Hakutilia maanani kuwa kuishambulia Iran kwa mabomu kutaongeza bei ya mafuta na gesi nchini Marekani. Gazeti hilo pia linasema Trump alionywa kuhusu Iran kufunga mlango wa bahari wa Hormuz, ila alipuuzilia mbali mawaidha hayo.
Aidha Trump hakutilia maanani kuwa kupanda kwa bei ya mafuta duniani, kutaiongezea Urusi mapato na kuisaidia kuimarika kiuchumi na katika vita dhidi ya Ukraine.
Siku kumi na nne baada ya kuishambulia Iran, sababu ya Marekani kuendelea na vita hivyo haiko wazi tena. Gazeti hilo linasema msimamo wa Trump "umeanza kuyumbayumba" na sasa anataka mataifa mengine kutuma meli za kijeshi eneo hilo, hii ikionyesha kubadilika kwa msimamo wake wa awali aliosema kuwa hahitaji msaada kutoka Uingereza, "Uingereza wanataka kujiunga na vita hivi kama tayari tumeshinda, hatuhitaji msaada wao" alisema Trump.
Gazeti hilo pia linasema kuwa "kama kungekuwa na udhibitisho wowote kuwa Iran ina silaha za nyuklia, basi Israel wangekuwa na haki ya kujilinda dhidi ya hatari hiyo. Ila hakuna udhibitisho kuwa Iran ilikuwa inakaribia kumiliki silaha za nyuklia hata baada ya Marekani na Israel kuvamia handaki za Iran mwezi Juni mwaka uliopita."
Trump alianzisha vita hivyo akifikiria kuwa utawala wa Iran umedhoofika, lakini hata baada ya mashambulizi yake, hilo halijakuwa dhahiri. Gazeti hilo la The Independent lionaongezea kuwa "Utawala wa Iran unaonekana kuwa imara kuliko alivyodhania Trump" "hatari ya kumshambulia kiongozi mkuu Ali Khamenei tayari limepita na sasa nafasi yake imechukuliwa na mwanawe" ambaye anasemekana kuwa na msimamo mkali zaidi.
Gazeti hilo linachambua kuwa licha ya makadirio mabaya ya Trump, bado anataka Ukraine ipate amani ila sasa anaiimarisha kiuchumi Urusi, bado anataka amani Mashariki ya Kati, huku Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akimshauri vibaya kuwa wakiishambulia Iran kwa mabomu kadhaa utawala wake utaporomoka ila sasa ameanzisha "vita visivyokwisha"
Mafunzo kutoka Lebanon

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tukiangazia gazeti la Ufaransa la Le Monde, "Makadirio mabaya ya Israel nchini Lebanon" gazeti hilo linashtumu mashambulio ya Israel nchini Lebanon, kwa kile wanakisema ni kundi la Hezbollah kuiunga mkono Iran.
Gazeti hilo limeandika kuwa Waziri wa ulinzi wa Israel, Isreal Katz alitangaza tarehe 13, kuwa "serikali ya Lebanon italipa gharama kubwa ya uharibifu wa miundo mbinu ya serikali hiyo inayotumiwa na Hezbollah, iwapo kundi hilo halitasalimisha silaha mara moja"
Gazeti hilo linasema tishio hilo ni "kukosa kuona mbali" kwani hakuna sababu yoyote ya kuanzisha oparesheni hiyo katikati ya vita vingine vinavyoendelea na tayari vimewauwa zaidi ya watu 700 "siyo sahihi".
Gazeti hilo linachambua kuwa baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon mwaka wa 1990, Hezbollah ndilo kundi pekee lililoruhusiwa kubaki na silaha zao. Hezbollah walisema kusalia kwao na silaha ni kutokana kujikinga dhidi ya Israel, ambayo ilikuwa imedhibiti eneo la kusini mwa Lebanon.
Hezbollah ambayo inafadhiliwa na Iran, baada ya Israel kujiondoa rasmi mwaka wa 2000 na kuliipa kundi hilo umaarufu.
Ila umaarufu wa kundi hilo ulipungua baada ya kushiriki katika mauaji ya Waziri mkuu wa taifa hilo Rafik Hariri mwaka wa 2005, vita na Israel mwaka wa 2006 ambao vilisababisha uharibifu mkubwa katika taifa hilo na mamlaka za Beirut kushindwa kudhibiti kundi hilo.
Gazeti hilo linasema kuwa "licha ya Hezbollah kudhoofishwa baada ya shambulio la Isral mwaka wa 2014, na kusababisha watu wengi kukimbia makazi yao, inaonyesha jinsi imekuwa vigumu kuilazimisha Hezbollah kujisalimisha"
Gazeti hilo linasema kwamba kumaliza hadhi ya Hezbollah kama 'dola ndani ya dola' ni jambo muhimu sana, lakini njia pekee ya kufanikisha hili ni kwa kuimarisha taasisi za Lebanon.
Gazeti hilo la Le Monde inaitaka Marekani "kujifunza kutokana na masomo ya historia na isiunge mkono Israel tena katika mtazamo wake kuhusu Lebanon."
Kuishambulia Lebanon kwa mabomu tena kutadhoofisha mamlaka yake, ambazo bado hazina uwezo wa kuidhibiti Hezbollah. Kuanzisha eneo la usalama la Israel ndani ya ardhi ya Lebanon kutafufua kauli za upinzani, ambazo wanamgambo walizitumia baada ya kujiondoa mwaka wa 2000, na muda unakwisha ili kuepuka kurudia makosa ya zamani," kulingana na Le Monde.
Wasiwasi kuhusu Kombe la Dunia
Tunamalizia uchambuzi wetu na gazeti la Marekani la USA Today katika taarifa inayosema "Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha wa Marekani (ICE) unaelezea wasiwasi kuhusu michezo ya Kombe la Dunia" ambayo mwenyeji wake ni Canada, Mexico na Marekani kutoka mwezi Juni hadi Julai.
Mwandishi wa taarifa hiyo anasema, michuano ya kombe la dunia, litawavutia mamilioni ya watu kote duniani, ila mafanikio yake yatatokana na usalama na mikakati ya usafiri.
Gazeti hilo linaelezea kuwa wasiwasi huu unatokana na kwamba Idara ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha ya Marekani (ICE) itakuwa sehemu muhimu ya mfumo wa jumla wa usalama wa Kombe la Dunia," kulingana na kauli ya Todd Lyons, kaimu mkurugenzi wa ICE.
Pia kumekuwa na ongezeko la wito wa kususia mashindano hayo kwa sababu za kiusalama, huku makundi ya mashabiki, ikiwemo Football Supporters Europe, yakielezea wasiwasi kuhusu "kufanya vikosi vya polisi kuwa vya kijeshi" nchini Marekani.Timu moja ya Ujerumani imeghairi ziara yake ya Marekani, na mijadala kuhusu kususia mashindano hayo inaendelea katika majukwaa ya mashabiki mtandaoni.
Aidha gazeti hilo pia linasema "mashabiki kutoka Amerika Kusini, Afrika na Mashariki ya Kati wanajiuliza ikiwa visa halali pekee inatosha. Na je, makosa madogo tu katika nyaraka yanaweza kusababisha mtu kuzuiliwa?"
Uchambzi huo unamalizia kwa kusema ni muhimu kwa Marekani kuweka vitu wazi kuhusu usalama na maelezo kuhusu kupata visa ya kuingia nchini humo, na tiketi ya kushiriki katika michezo hiyo.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliuala











