"Moto ulitokea angani na kuwachoma" - Waathiriwa wa vita vinavyoendelea Sudan Kusini

.
Maelezo ya picha, Mama ya watoto watano Nyawan Koang aliyekimbia vita.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Maelfu ya watu wamekuwa wakikimbia mji wa Akobo, Sudan kusini na maeneo Jirani ya jimbo la Jonglei, eneo ambalo jeshi la taifa hilo limeongeza mashambulizi yake katika jitihada za kujaribu kuudhibiti tena mji huo.

Mapigano ya hivi karibuni yamechochea Umoja wa Mataifa kuonya kuwa huenda vita vya wenyewe kwa wenyewe vikazuka tena katika taifa hilo changa.

Nyawan Koang mwenye umri wa miaka 30, na wanawe 5, walilazimika kutembea kwa siku mbili ili kufika katika Kijiji cha Duk.

Walikuwa wanakimbia kutoka Ayod, Kijiji cha wavuvi jimbo la Jonglei, baada ya vita kuzuka kati ya wanajeshi na wapinzani wao.

"Tulikuwa katikati ya makundi mawili yanayopigana. SPLA- IO na serikali." Aliiambia BBC

Majeshi ya serikali yanajaribu kuchukua udhibiti wa eneo hilo kutoka kwa makundi ambayo ni waaminifu kwa Waziri mkuu wa kwanza wa taifa hilo Riek Machar, ambaye amesimamishwa kazi kwa muda na anatumikiea kifungo cha nyumbani, baada ya kutuhumiwa kujaribu kuipindua serikali ya Rais Salva Kiir. Machar amekuwa akizuiliwa nyumbani kwake mjini Juba kwa mwaka mmoja akisubiria kufikishwa mahakamni kwa shtuma za uhaini na mauaji.

Kundi linalomuunga mkono Machar la Sudan People's Liberation Army in Opposition (SPLA-IO), wameuteka jimbo la Jonglei na majimbo mengine Jirani.

Kundi hilo likielekea kuteka mji wa Bor, katika jimbo la Jonglei, vijiji vingi vilichomwa na raia wengi kuuawa. Serikali ya taifa hilo imejibu vikali hatua hiyo kwa kuwatuma wanajeshi wengi eneo hilo kudhibiti hali.

Katika makabiliano kati ya kundi hilo na jeshi, raia wengi wa Sudan kusini waliathirika pakubwa na kushambuliwa.

Aliwapoteza wazazi wake baada ya ndehe isiyo na rubani kugonga na kulipua nyumba yao ndogo yenye paa la nyasi.

"Moto ulitoka angani na kuwachoma" Alisema.

Nyawan na familia yake ni miongoni mwa watu zaidi ya 280,000 waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano ya hivi karibuni. Maelfu ya watu walikimbilia eneo la Duk, ambapo mashirika ya misaada yanawapatia chakula, dawa na mahitaji mengine ya msingi.

Maisha ya raia wengi wa Sudan Kusini huenda yakasambaratika iwapo vita vya kisiasa vitaendelea.

Ramani ya Sudan Kusini.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mapigano kati ya vikosi vinavyomuunga mkono Rais Salva Kiir na mpinzani wake aliyekuwa makamu rais wa taifa hilo Riek Machar yalianza mwaka wa 2013, miaka miwili tu baada ya taifa hilo kujipatia uhuru.

Makubaliano ya amani ya mwaka wa 2018 yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyowaua takriban watu 400,000, lakini makubaliano hayo hayakutekelezwa kikamilifu na uhusiano kati ya wawili hao umeendelea kudorora kutokana na ukabila na mivutano ya mara kwa mara.

Haijulikani ni watu wangapi raia au wanajeshi wameuawa katika mzozo huu wa sasa. Ripoti moja ya shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa iliripoti vifo vya raia 189 Mwezi Januari.

"Raia wanateseka kutokana na ongezeko la mashambulizi, mauaji, utekaji nyara na ukatili wa kijinsia unaohusiana," alisema kiongozi wa shirika hilo Volker Türk.

Nyawan anakumbuka kuona miili kadhaa wakati akitoroka kuelekea Duk. "Lakini sijui ni upande gani ulitekeleza mauaji hayo."

Wakati vikosi vya serikali na wapiganaji wa SPLA-IO, wanaoungwa mkono na kundi jingine la silaha linaloitwa White Army, vinapigana kudhibiti maeneo tofauti, raia wasio na hatia ndio wanaumia.

"Hakuna jeshi duniani linalopigana bila raia kuathirika ," Waziri wa Habari Ateny Wek Ateny aliiambia BBC akiwa ofisini mwake mjini Juba.

Anasema jeshi lina "uwajibikaji" katika matendo yake, na anaongeza kuwa serikali yake "inajitahidi kadri iwezavyo" kuhakikisha raia hawaathiriki na vita hivyo.

Hata hivyo, baadhi ya mashambulizi dhidi ya raia yanaonekana kuwa ya makusudi.

Katika wiki ya mwisho ya mwezi Februari zaidi ya raia 20 wakiwemo wanawake na wazee waliuawa kwa kufyatuliwa silaha eneo la Ayod na wanajeshi wa serikali .

Msemaji wa jeshi,Meja Jenerali Lul Ruai Koang, aliambia BBC kwamba wanajeshi kutoka vitengo viwili na makamanda wao wanazuiliwa kufuatia uchunguzi uliofanyika na sasa wanakabiliwa na mashtaka ya kujibu katika mahakama ya kijeshi.

Katika suala la kuchochea vita Rais Kiir hakumfuta kazi Machar pekee yake bali pia mkewe Waziri wa Mambo ya Ndani Angelina Teny pamoja na viongozi wengine kadhaa wa ngazi ya juu serikalini.

Wafuasi wa Machar wanaona hatua hii kama yenye motisha za kisiasa na ukiukaji wa makubaliano ya ushirikiano wa madaraka ya Sudan Kusini.

"Tumeteseka sana"

Kama watu wengi wanaotafuta hifadhi na msaada eneo la Duk, Hoth Wan Kornyom, kiongozi wa jamii na baba wa watoto saba, amepoteza jamaa mmoja kutokana na vurugu hizo.

Ndugu yake aliuawa kwa risasi na nyumba yake kuchomwa moto. Wakati wakazi wa kijiji wa eneo la Uror walikimbia mzozo huo, baadhi ya wazazi walitengana na watoto wao na haijulikani kama wataweza kukutana tena.

.
Maelezo ya picha, Hoth Wan Kornyom anasema wazazi walitengana na watoto wao wakikimbia vita.

Neyasebit, mwenye umri wa miaka 27, ambaye pia alikimbia Uror kuelekea Duk, alisema kwamba mababu zake wawili, shemeji yake na kaka yake mdogo waliuawa katika mashambulizi ya anga. "Walikuwa tu wakiishi nyumbani," alieleza, akisisitiza kwamba hawakuwa wapiganaji.

"Tumeteseka sana. Ndiyo maana tulikimbia," aliambia BBC..

Kuibuka upya kwa vita katika jimbo la Jonglei kumeongeza mahitaji ya kibinadamu ambayo tayari yalikuwa finyu jimbo hilo. Kulingana na Shirika la Chakula Duniani (WFP), 60% ya watu milioni mbili wa Jonglei wanakabiliwa na njaa.

Kote Sudan Kusini, watu milioni 10 kati ya milioni 14 wanahitaji msaada wa chakula.

"Sudan Kusini ni mojawapo ya maeneo magumu zaidi duniani ya kusambaza misaada ya kibinadamu," alisema Adham Affandy, mkurugenzi mteule wa WFP nchini Sudan Kusini.

"Kuna vita, majanga, vita vya kikabila, uchumi kudorora pamoja na changamoto zingine."

Sudan Kusini pia ina mojawapo ya barabara duni duniani.

Wakati wa msimu wa mvua ambao unaweza kudumu hadi miezi minane kwa mwaka, takriban 80% ya maeneo tofauti nchini Sudan Kusini haiwezi kufikika, alisema Affandy.

Hii imewalazimu mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu kutumia ndege kupeleka misaada kwa maeneo yaliyoathirika, na kufanya gharama ya kusambaza misaada hiyo kuwa ghali mno.

Ila ukosefu wa usalama limesababisha mashirika mengi ya kutoa misaada kuhama nchini humo.

Tangu taifa hilo kupata uhuru mwaka wa 2011, Sudan Kusini imekuwa ikikabiliana na migogoro na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula