Ramadhani 2026: Nchi zilizoanza kufunga leo na zinazoanza kesho

Muda wa kusoma: Dakika 4

Mamilioni ya Waislamu duniani wanaanza mfungo mtukufu wa mwezi wa Ramadhani, kipindi muhimu katika kalenda ya Kiislamu ambacho ni moja ya nguzo tano za Uislamu. Kwa waumini wa dini hiyo, Ramadhani si tu kujizuia kula na kunywa, bali ni safari ya kiroho inayolenga kujenga uchamungu (Taqwa), nidhamu binafsi na huruma kwa wasiojiweza.

Mfungo huu huanza mara tu mwezi mwandamo wa Ramadhani unapoonekana. Katika Uislamu, kuandama kwa mwezi ndiko kunakoashiria kuingia kwa mwezi mpya, na hivyo kutangazwa rasmi kuanza kwa ibada ya swaumu. Uamuzi huo hufanywa na mamlaka za kidini au serikali kulingana na ushahidi wa kuonekana kwa mwezi au kwa kutumia hesabu za kielimu za anga.

Hata hivyo, kila mwaka hushuhudiwa tofauti ya siku ya kuanza kwa Ramadhani baina ya baadhi ya nchi za Kiislamu. Wakati wengine hutangaza kuanza kwa saumu siku moja, wengine huanza siku inayofuata. Tofauti hiyo mara nyingi huzua mjadala miongoni mwa waumini kuhusu sababu za mgawanyiko huo.

Mwaka huu pia hali hiyo imejitokeza. Baadhi ya nchi zimetangaza kuuona mwezi na kuanza kufunga leo, huku nyingine zikisubiri kukamilika kwa siku 30 za Shaaban au uthibitisho wa muandamo wa mwezi katika anga zao kabla ya kuanza kesho.

Katika hali zote, lengo hubaki lilelile: Kuingia katika mwezi wa ibada, toba na mshikamano wa kijamii unaowaunganisha Waislamu kote duniani.

Nchi zilizoanza kufunga leo na zitakazoanza kesho

Baadhi ya mataifa ya Kiislamu yametangaza rasmi kuanza kwa Ramadhani leo Februari 18 baada ya kuthibitisha kuonekana kwa mwezi jana jioni. Miongoni mwa nchi hizo ni Saudi Arabia, United Arab Emirates, Qatar, Bahrain, Kuwait na Yemen.

Nchi nyingine zilizothibitisha kuanza kwa mfungo leo ni Iraq, Lebanon, Sudan na Somalia. Katika mataifa hayo, Jumatano imetangazwa kuwa siku ya kwanza ya Ramadhani 1447 Hijria.

Kwa upande mwingine, baadhi ya nchi zimetangaza kuwa mwezi haukuonekana katika maeneo yao, hivyo kuamua kukamilisha siku 30 za mwezi wa Shaaban na kuanza kufunga kesho. Miongoni mwa nchi hizo ni Syria, Turkey, Egypt na Jordan.

Nchi nyingine zitakazoanza kesho ni Libya, Algeria, Singapore na Indonesia. Aidha, Oman ilikuwa tayari imetangaza mapema kuwa saumu ingeanza Alhamisi.

Nchi nyingi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania ambapo Baraza la Kuu la Waislam (BAKWATA) hutangaza kuonekana kwa mwezi, Kenya, Uganda na zingine zinatarajiwa kuanza kesho mwezi wa Ramadhan.

Kwa nini kuna tofauti ya siku ya kuanza Ramadhani?

Tofauti ya kuanza kwa Ramadhani hutokana na mbinu zinazotumika kuthibitisha kuingia kwa mwezi mpya. Baadhi ya nchi hutegemea ushuhuda wa kuonekana kwa mwezi kwa macho (ru'yah), ambapo kamati maalum hupokea taarifa za waangalizi wa mwezi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Nchi nyingine hutumia hesabu za kitaalamu za unajimu (hisab) kubaini kuzaliwa kwa mwezi mpya, hata kama haujaonekana kwa macho kutokana na hali ya hewa au sababu za kijiografia. Tofauti katika misimamo ya kifiqhi kuhusu ipi njia sahihi zaidi pia huchangia utofauti huu.

Kijiografia, dunia ina tofauti za muda na maeneo ya anga. Mwezi unaweza kuonekana katika eneo moja la Mashariki ya Kati lakini usionekane Afrika Kaskazini au Asia ya Kusini Mashariki kwa siku hiyo hiyo. Hali ya hewa kama mawingu mazito nayo inaweza kuzuia kuonekana kwa mwezi.

Hali hii si ya kuanza tu kwa Ramadhani, bali hata mwisho wake wakati wa kutangaza Sikukuu ya Eid. Hivyo, tofauti ya siku moja au mbili imekuwa jambo la kawaida katika ulimwengu wa Kiislamu, ingawa kwa wengi lengo la ibada hubaki kuwa moja.

Ramadhani ni nini na masharti ya kufunga ni yapi?

Kufunga katika mwezi wa Ramadhani ni ibada ya kujizuia kula, kunywa na kufanya mahusiano ya kindoa kwa makusudi kuanzia alfajiri hadi kuzama kwa jua. Ibada hii huanza kwa kuweka nia moyoni, bila ulazima wa kuitamka kwa sauti.

Ni wajibu kwa kila Mwislamu aliyebalehe, mwenye akili timamu na asiye na udhuru wa kiafya au wa kisheria. Wagonjwa sugu, wajawazito, wanaonyonyesha au wasafiri wanaweza kupewa ruhusa ya kutofunga endapo kufunga kutaleta madhara kwao, lakini hulazimika kulipa Qada au kutoa fidia pale inapohitajika.

Katika historia ya Kiislamu, Ramadhani ni mwezi ambao Qurani Tukufu ilianza kuteremshwa. Ndani yake mna Laylatul Qadr, usiku unaoelezwa kuwa na thamani kuliko miezi elfu, jambo linaloongeza uzito wa kiroho wa mwezi huu.

Mbali na faida za kiroho, wataalamu wanasema kufunga kunaweza kusaidia mwili kuimarika, kupunguza mafuta yasiyotakiwa na kuchangia afya ya moyo. Hata hivyo, lengo kuu la saumu hubaki kuwa ni kujenga Taqwa, nidhamu na kumkaribia Mwenyezi Mungu kupitia ibada na matendo mema.