Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kusitishwa mapigano Iran, Lebanon kutakavyosukuma mazungumzo ya Marekani na Iran
- Author, Paul Adams
- Nafasi, Diplomatic correspondent
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Wakati kuna kusitishwa kwa mapigano mapigano katika eneo la Mashariki ya Kati, swali kubwa linaibuka: je, mazingira sasa yameiva kwa mafanikio ya kihistoria katika diplomasia?
Usitishwaji huo wa kwanza ukihusisha Iran na mwingine Lebanon, hatua zote zinaelezewa kuwa "dhaifu," jambo ambalo si la kushangaza kwa makubaliano ya aina hii. Hata hivyo, kadiri mapigano yanavyopungua, hali hii inaleta mchanganyiko wa fursa kubwa pamoja na hatari zinazoweza kujitokeza.
Kwa mtazamo wa juu juu, tangazo la Alhamisi usiku la kusitisha mapigano kwa siku 10 kati ya Israel na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran linaonekana kuwa ushindi kwa Tehran.
Serikali ya Iran ilikuwa imesisitiza kuwa haiwezekani kuendeleza mazungumzo na Marekani bila kuwepo kwa usitishaji mapigano nchini Lebanon. Sasa, baada ya hatua hiyo kuchukuliwa, Iran imetangaza kuwa mlango bahari wa Hormuz "umefunguliwa kabisa."
Ingawa mazungumzo marefu ya wiki iliyopita kati ya Iran na Marekani mjini Islamabad yalionyesha kuwa maendeleo yanawezekana hata wakati mapigano yakiendelea, Iran na Pakistan zilisisitiza kuwa suala la Lebanon lazima lijumuishwe. Hilo sasa limetimia, lakini limezua hasira miongoni mwa Waisraeli wanaoishi karibu na mpaka wa kaskazini, ambao wanaamini Waziri Mkuu wao, Benjamin Netanyahu, amekubali shinikizo la Marekani badala ya kuhakikisha Hezbollah haishambuli tena Israel.
Kwa baadhi ya Waisraeli, sitisho hilo linawanufaisha Iran, kwa kuruhusu adui mkubwa wa Israel kuwa na ushawishi mkubwa juu ya mwelekeo wa matukio. Wachambuzi wengine wanasema hatua hiyo kimsingi inahalalisha uhusiano kati ya Iran na uwanja wa mapigano wa Lebanon, na kuonyesha kuwa Tehran bado ina nguvu kubwa ya kuamua kinachotokea katika eneo hilo.
Hata hivyo, kwa mtazamo mpana, pande zote zinazohusika zinaonekana kupata faida fulani. Rais wa Marekani, Donald Trump, pamoja na uongozi wa Iran, wanaweza kujipatia sifa kwa kufanikisha usitishwaji wa mapigano. Netanyahu anaweza kusema wanajeshi wa Israel bado wako kusini mwa Lebanon, huku serikali ya Lebanon sasa ikiwa kwenye mazungumzo ya moja kwa moja na Israel. Kwa upande wake, Hezbollah inasema haijashindwa na haitaweka silaha chini, angalau hadi masharti kadhaa yatimizwe, ikiwemo kuondoka kwa Israel na kurejeshwa kwa wakimbizi.
Mchambuzi Lina Khatib wa taasisi ya Chatham House anaeleza kuwa usitishwaji wa mapigano Lebabon kunafungua mlango wa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Israel na Lebanon, lakini changamoto za kufikia amani ni kubwa. Miongoni mwa masuala magumu ni mipaka, kuondolewa kwa silaha za Hezbollah na kuondoka kwa majeshi ya Israel. Ikumbukwe kuwa Israel na Lebanon zimekuwa katika hali ya vita tangu mwaka 1948 bila uhusiano rasmi wa kidiplomasia.
Khatib pia anaamini kuwa badala ya kuimarisha ushawishi wa Iran, mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Israel na Lebanon yanaweza kuanza kuiondoa Lebanon kutoka katika ushawishi wa Tehran. Hii inaashiria mabadiliko ya mizani ya nguvu katika eneo hilo, ambapo Iran inaweza kupoteza uwezo wake wa kuitumia Lebanon kama karata ya mazungumzo.
Hata hivyo, mustakabali wa eneo hilo unategemea sana mchakato mwingine wa kidiplomasia kati ya Marekani na Iran. Ajenda kuu itakuwa kupunguza kile ambacho Marekani na Israel wanaona kama tabia hatarishi ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na msaada wake kwa makundi kama Hezbollah, Hamas na Wahouthi wa Yemen.
Iran, kwa upande wake, haitakuwa tayari kuachana kirahisi na njia hizo ambazo inaona ni muhimu kwa ushawishi wake wa kikanda. Changamoto nyingine kubwa ni mpango wa nyuklia wa Iran na mustakabali wa Hormuz. Donald Trump anadai makubaliano yako karibu na hata kudai kuwa Iran imekubali kukabidhi kiasi kikubwa cha urani iliyorutubishwa, madai yaliyokanushwa vikali na Tehran.
Kwa Iran, suala la nyuklia ni nyeti sana, likilinganishwa na ardhi yake yenyewe, na imesisitiza kuwa haitakubali kuhamisha urani yake nje ya nchi. Makubaliano yoyote yatapaswa kujumuisha ahadi ya kutotengeneza silaha za nyuklia pamoja na masharti ya kusimamisha urutubishaji kwa muda fulani.
Wakati huo huo, Iran pia inapendekeza mfumo mpya wa kusimamia usafiri wa baharini katika mlango Hormuz, ikitaka kutambuliwa kwa haki yake ya kudhibiti eneo hilo kwa kushirikiana na Oman. Ingawa njia hiyo imetangazwa kuwa wazi kwa sasa, bado kuna tahadhari na mabadiliko ya njia za meli ambayo yanaweza kuathiri kasi ya kurejea kwa hali ya kawaida.
Licha ya dalili hizi chanya, bado kuna kazi kubwa mbele ya mazungumzo haya. Makubaliano ya awali ya nyuklia ya mwaka 2015 yalichukua karibu miezi 20 kufikiwa na yalihusu suala moja tu. Historia pia inaonyesha kuwa mikutano ya haraka ya Trump na viongozi kama Kim Jong Un haikuzaa matokeo makubwa ya kudumu.
Baada ya wiki kadhaa za mvutano mkali, sasa kuna dalili za mchakato wa kidiplomasia unaoanza kushika kasi, ukichochewa na sitisho la mapigano nchini Lebanon. Swali linalobaki ni kama juhudi hizi zitatosha kuzuia kurejea kwa vita. Jibu la hilo, inaonekana, bado haliko wazi hata kwa Trump mwenyewe.