Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tunachokijua kuhusu ndege ya "Doomsday" yenye kustahimili mashambulizi ya nyuklia
"Doomsday Plane" ni ndege aina ya Boeing E-4B iliyoundwa kuwa kituo cha kutoa amri na maelekezo wakati wa dharura kama mashambulizi ya nyuklia na majanga mengine makubwa nchini Marekani.
Ndege hii ilianza kutumika mwaka wa 1974 wakati wa kilele cha vita baridi, ili kutoa maelekezo iwapo hali itakuwa mbaya nchini Marekani na vituo vya kuendesha vita ardhini kuharibiwa.
Ndege hii iliundwa kutumika wakati wa vita, na huwa kituo cha kutoa amri na maelekezo angani na Rais wa Marekani, waziri wa ulinzi na wakuu wa majeshi wakati wa vita ili kuhakikisha wanadhibiti mawasiliano na vyombo vingine vya serikali.
Ndege ya "Doomsday" inaweza kupaa kwa siku saba mfululizo, na ina uwezo mkubwa kushinda ndege zingine za kivita.
Kikosi cha Doomsday
Marekani ina kikosi cha ndege nne za E-4B ambazo hufanya safari za anga mara kwa mara mwaka mzima ili kuhakikisha utayari wake wa kijeshi endapo kuna dharura.
Jeshi la anga la Marekani, kwa sasa linafanya kazi ya kujenga upya na kurekebisha ndege tano za Boeing 747-8, ambazo awali zilikuwa zikitumika na shirika la ndege la Korean air, ili zichukue nafasi ya E-4B.
Ndege hizi zitakuwa na vifaa vya kujikinga dhidi ya mnunurisho,sumaku umeme, antena za mawasiliano, tarakilishi, mifumo ya kijeshi na uwezo wa kuongeza mafuta angani. Ndege hizo tano zitagharimu takriban dola bilioni 13.
Ndege ya Doomsday ina sifa zinazofanya iwe bora kupaa angani wakati wa majanga, kwani ina uwezo wa kipekee wa kustahimili mashambulizi ya nyuklia, mashambulizi ya kimtandao na sumaku umeme huku ikiwa na uwezo wa kurusha makombora.
Ndege hii pia ina uwezo mkubwa wa mawasiliano, kwani ina setilaiti 67 zinazoweza kutumika kuwasiliana na mtu yeyote mahali popote, pamoja na kuwa na kinga za joto na nyuklia.
Ndege hii huendeshwa kwa injini nne, ikiwa na uwezo wa kuongezwa mafuta angani.
Marekani iliboresha ndege yake ya Boeing E-4A Doomsday Plane, ambayo ilitumika hadi mwishoni mwa mwaka wa 1974, na kuibadilisha kuwa E-4B.
Jeshi la anga la Marekani ilipokea ndege yake ya kwanza aina ya E-4B mwaka wa 1980 kisha ndege zote za kikosi cha Doomsday zikaboreshwa kuwa mfululizo wa B.
Ndege hii hutoa mawasiliano kwa vituo vya amri katika sekta mbalimbali baada ya majanga kama vile kimbunga na tetemeko la ardhi. Ndege hii ya kijeshi imeboreshwa kutoka kwa ndege ya kiraia ya Boeing 747-200.
Kituo hiki pia hutumika hutoa maagizo ya dharura wakati wa vita na kuratibu kazi za mamlaka za kiraia hadi hali za kawaida zirejelewe.
Sifa za ndege ya "Doomsday"
- Ndege ya "Doomsday" inaweza kupaa bila kutua kwa siku saba mfululizo.
- Wale walio ndani ya ndege hiyo wanaweza kuwasiliana na wale walio ardhini mahali popote duniani wakati ndege hiyo ipo angani.
- Uwezo wake unazidi ndege za kivita za jeshi la anga la Marekani
- Ndege hiyo inaweza kustahimili mashambulizi ya nyuklia, vimondo, nyota zinazoanguka, na mashambulizi mengine ya angani.
- Injini yake inafanya kazi masaa 24 kwa siku, siku 365 kwa mwaka, ikimaanisha haipumziki na iko tayari kupaa wakati wowote iwapo dharura itatokea.
- Ndege hii inagharimu takriban dola za Marekani milioni 223.
- Nchi nyingine kando na Marekani inayomiliki ndege kama hii ni Urusi.
- Rubani mkuu wa ndege hiyo anaweza kuona mahali walipo rais wa Marekani, makamu wa rais, waziri wa ulinzi, waziri wa mambo ya nje, na mwanasheria mkuu kupitia skrini zilizoko ndani ya ndege hiyo.
- Vikosi vya majini vilivyojificha ndani ya bahari vinaweza kupokea maagizo ya kijeshi kutoka kwa ndege hiyo.
- Ndege ya "Doomsday" ni tofauti na "Air Force One," ambayo hutumika kwa ziara za kawaida za Rais wa Marekani.
Matumizi ya ndege ya "Doomsday"
Ndege hii husafirisha Rais wa Marekani, waziri wa ulinzi, na wakuu wa majeshi wakati wa vita.
Uwezo wa kipekee wa ndege hiyo ilipata umaarufu wakati wa muhula wa kwanza wa utawala wa rais Trump, baada ya kuwa na majibizano na rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.
Ndege hiyo ilionekana ikielekea Washington mwezi Juni mwaka uliopita na Januari mwaka huu.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula