Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi vikosi maalum vya jeshi la Marekani hufanya oparesheni ya uokoaji wakati wa vita
Ripoti zinasema kuwa rubani wote wawili wa ndege ya Marekani aina ya US F-15 iliyodunguliwa na Iran wameokolewa, hii ikiwa moja wapo ya misheni ya kipekee ya uokoaji kufanywa na jeshi la Marekani katika historia yake ya miongo kadhaa ya vita.
Kwa mujibu shirika la habari la CBS, rubani wa pili pia aliokolewa kupitia mojawapo ya oparesheni ngumu zaidi.
Oparesheni ya uokoaji
Nchini Marekani, vikosi maalum vya anga hupewa mafunzo ya kufanya oparasheni kama hizi za kipekee za uokoaji wa wanajeshi wanaojipata katika hali tata au kama tukio hili ambapo ndege za kijeshi zinaangushwa na adui.
Ikilinganishwa na oparesheni ambazo hufanyika kutoa misaada kwa binadamu au kuwaokoa watu waliokwama katika maeneo tofauti, oparesheni ya kijeshi hufanyika katika maeneo ambayo kuna mzozo na mapigano.
Kama ilivyotokea nchini Iran, baadhi ya oparesheni hizo hutokea katika ardhi ya adui.
Oparesheni ya utafutaji na uokoaji hufanywa na ndege aina ya helikopta, ikiwa imeambatana na ndege zingine za kuiongezea mafuta na kutekeleza mashambulizi wakati wanashika doria angani huku wakiendeleza oparesheni yao.
Kamanda mmoja wa zamani wa kikosi maalum cha uokoaji aliiambia shirika la habari la CBS kuwa oparesheni hiyo ya uokoaji kama ile iliyotokea Iran huhusisha angalau wanajeshi 24 wakichunguza eneo la tukio kutumia helikopta za black hawk.
Aliongezea kuwa kikosi hicho huwa tayari kuruka nje ya ndege ikiwa itabidi, ili kumtafuta mmoja wao aliyetoweka.
Kulingana na CBS, iwapo mwanajeshi aliyepotea atapatikana, atapewa matibabu hitajika, na kuondolewa katika ardhi ya adui na kuhamishwa hadi eneo salama.
Kamanda huyo wa zamani anasema "hicho ndicho hasa wanachofundishwa kufanya kote duniani. Wanaitwa Swiss Army Knife of the Air Force."
Video iliyochapishwa kutoka Iran siku ya Ijumaa inaonyesha helikopta za kijeshi za Marekani, pamoja na angalau ndege moja ya kujaza mafuta angani zikiendeleza operesheni katika jimbo la Khuzestan.
Muda ni jambo la muhimu sana katika operesheni hizi, kwani vikosi vya Iran vina uwezekano pia wa kuwa vinatafuta mtu au watu hao wa Marekani kwa wakati huohuo.
Jonathan Hackett, aliyewahi kuwa mtaalamu wa operesheni maalum wa Kikosi cha Wanamaji cha Marekani, aliiambia BBC kwamba timu za uokoaji mwanzoni zingetafuta dalili zozote za kuonyesha wanajeshi hao wangali hai.
Alisema:
"Wao huanza utafutaji katika eneo ambalo mtu huyo alionekana mara ya mwisho, kisha kupanua eneo la utafutaji kwa mduara huo, wakizingatia kasi ya mtu huyo kusonga katika hali tofauti, na katika maeneo hayo yenye mazingira magumu."
Jonathan Hackett aliongeza kuwa aina hii ya operesheni huenda ikawa ni "operesheni isiyo ya kawaida ya uokoaji," na lazima ifanywe kwa msaada wa vikosi vya eneo hilo. Hii ina maana kwamba makundi ya wenyeji wa eneo hilo huenda tayari wamewasiliana mapema na jeshi la Marekani ili kuratibu mipango ya dharura na kusaidia katika uokoaji.
Alisema kuwa kusini magharibi mwa Iran ni makazi ya watu wa jamii ya Lor, jamii ndogo ambayo "kihistoria imekuwa ikipinga serikali ya sasa" na huenda ikawa tayari kusaidia wageni kupata njia salama ya kupita.
Historia ya uokoaji
Operesheni za utafutaji na uokoaji wakati wa mapigano ina historia ndefu, ikianzia wakati wa vita vya kwanza vya dunia, ambapo marubani walikuwa wakitua kwa dharura bila mipango rasmi ili kuwaokoa wenzao walioanguka nchini Ufaransa.
Timu ya uokoaji ya Jeshi la Marekani ilianzishwa mwaka 1943, wakati wanajeshi wawili wa kutoa matibabu ya dharura walitua eneo la Burma, linalojulikana sasa ka Myanmar, ili kuwasaidia wanajeshi waliokuwa wamejeruhiwa.
Kulingana na gazeti la Smithsonian Air and Space Magazine, uokoaji wa kwanza kwa kutumia helikopta ulifanyika mwaka mmoja baadaye, wakati luteni wa Marekani alipowaokoa wanajeshi wanne nchini Japan. Tukio hili pia liliandikisha historia ya matumizi ya kwanza ya helikopta katika mstari wa mbele wa vita.
Vitengo rasmi vya utafutaji na uokoaji vilianzishwa nchini Marekani baada ya kumalizika kwa vita vya kwanza vya dunia, lakini mfumo wake wa kisasa ulianza wakati wa vita nchini Vietnam.
Katika operesheni moja maarufu, iliyojulikana kama Operation Beit 21, ndege kadhaa ziliharibiwa na wanajeshi kadhaa wa Marekani waliuawa, katika jaribio la kumuokoa rubani mmoja aliyekuwa ameanguka eneo la vita kaskazini mwa Vietnam
Vita vya Vietnam vilishuhudia operesheni za utafutaji na uokoaji wa wanajeshi kwa kiwango kikubwa na kwa ugumu zaidi.
Uzoefu wa kipindi hicho uliisaidia jeshi la Marekani kuboresha na kuweka taratibu ambazo zimekuwa msingi wa operesheni za kisasa za uokoaji.
Vikosi vya uokoaji vya jeshi la anga ya Marekani
Ingawa kila tawi la jeshi la Marekani lina uwezo wa kufanya operesheni za utafutaji na uokoaji wakati wa vita kwa kiwango fulani, Jeshi la Anga la Marekani ndilo lenye jukumu kuu la kuwatafuta na kuwaokoa wanajeshi.
Kazi hii hufanywa hasa na vikosi vinavyojulikana kama Pararescue Jumpers, kikosi ambacho ni sehemu ya vikosi vya operesheni maalum vya jeshi la Marekani.
Kikosi hicho huhudumu kwa kauli isemayo "hakuna kikosi kitakachobaki kwenye eneo la vita."
Wanajeshi hawa wamefunzwa kuwa wapiganaji na waokoaji kwa wakati mmoja na hupitia moja ya mchakato wa mafunzo magumu zaidi katika jeshi lote la Marekani.
Mafunzo haya yanajumuisha mafunzo ya kukimbia hatari, na kuwaokoa raia.
Mafunzo hayo huchukuwa takriban miaka miwili, na hujumuisha kuruka kwa parachuti, kuogelea, kukabiliana na bomu za chini ya maji, kuishi katika hali ngumu, kuhepa hatari na kuwaokoa raia.
Wao pia hufunzwa kutoa matibabu ya dharura, kuwaokoa waliojeruhiwa vibaya na kutumia silaha.
Operesheni za hivi karibuni za uokoaji zilizotekelezwa na wanajeshi wa Marekani
Vikosi vya utafutaji na uokoaji vilitumwa kwa wingi wakati wa vita nchini Iraq na Afghanistan, na kutekeleza maelfu ya operesheni ya kuwaokoa wanajeshi wa Marekani na washirika waliokuwa wamejeruhiwa au waliokuwa wanahitaji kuondolewa maeneo hatari.
Mwaka wa 2005, timu za uokoaji za Jeshi la Anga zilihusika katika kumuokoa mwanajeshi wa Vikosi Maalumu wa US Marine Corps, aliyekuwa amejeruhiwa na kujificha katika kijiji kimoja nchini Afghanistan, baada ya kikosi chake kushambuliwa na wanajeshi watatu kuuliwa, tukio ambalo baadaye lilitafsiriwa kuwa filamu iitwayo Lone Survivor.
Operesheni za kuokoa marubani wa Marekani waliopotea au kuanguka zimekuwa chache katika miongo ya hivi karibuni.
Mwaka wa 1999, rubani wa ndege ya kivita ya F-117 stealth, aliyepigwa risasi akiwa katika anga za Serbia alipatikana na kuokolewa.
Katika tukio lililopata umaarufu mkubwa nchini Bosnia mwaka wa 1995, rubani wa Marekani Scott O'Grady, aliokolewa katika operesheni ya pamoja ya utafutaji na uokoaji kati ya Jeshi la Anga la Marekani na US Marine Corps, baada ya ndege yake ya kivita kupigwa risasi, aliweza kunusurika na kupatikana siku sita baadaye.