Droni za Iran zilivyobadilisha nguvu ya vita katika migogoro ya kimataifa

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Ahmed Rawaba
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Katikati ya mgogoro unaoendelea kati ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran, mtaalamu wa kijeshi Akram Khareef alichapisha kitabu chake "Under the Shadow of a Witness," ambapo anaelezea asili ya ndege zisizo na rubani za Iran. Anaelezea mkakati ambao Iran imeutumia kupambana na vikwazo vya Marekani na kuwa na nguvu katika shughuli za kijeshi duniani.
Ndege zisizo na rubani za Iran zinaonekana mara kwa mara katika shughuli za Hezbollah kwenye mpaka na Israeli. Pia zinatumiwa na Wahouthi nchini Yemen. Na Septemba 2022, ulimwengu uliamka na habari za kushangaza kwamba Iran imeipa Urusi teknolojia ya ndege zisizo na rubani.
Nchi iliyo chini ya vikwazo kwa miaka 40 imewezaje kufanya yote hayo?
Vikwazo hivyo ndivyo vilivyowalazimisha viongozi wa Iran baada ya 1979 kuchunguza chaguzi zilizopo na njia zinazowezekana za kushinda vikwazo na kufanya maamuzi sahihi. Vikwazo hivyo pia viliwalazimisha kuwaamini wahandisi wao.
Shah Mohammad Reza Pahlavi alipoondoka Iran Januari 1979, aliacha jeshi ambalo lilikuwa na nguvu kubwa katika eneo hilo kwa upande wa silaha, na Jeshi la Anga la Iran lilikuwa na ndege za F-14 Tomcat, F-4 Phantom, na F-5 Tiger.
Wakati huo, jeshi la Iran lilikuwa katika nafasi ya tano duniani kwa upande wa vifaa, baada ya majeshi ya Marekani, Umoja wa Kisovieti, Uingereza, na Ufaransa. Jeshi la anga la Iran lilikuwa limeendelea zaidi kuliko Ujerumani, China, na Israeli, likiwa na ndege aina ya F-14 Tomcat, wakati huo ilikuwa miongoni mwa ndege za uwezo wa hali ya juu duniani.
Hata hivyo, uendeshaji na matengenezo yake yalitegemea mafundi na wahandisi kutoka Marekani ambao walikuwa Iran. Vipuri vilitolewa moja kwa moja na kampuni ya Marekani ya Grumman. Hivyo, jeshi la anga la Iran lilitegemea viwanda vya Marekani.
Baada ya utawala wa Shah kuanguka, viongozi wa kijeshi walikimbia nchi, waliuawa, au kufungwa. Mafundi na wahandisi wa Marekani waliondoka. Makampuni ya Marekani yalikata uhusiano na utawala mpya. Ndege ambayo Iran ilikuwa imeinunua kwa mabilioni ya dola ikawa chuma chakavu kisicho na thamani.
Uvumbuzi wa Iran

Chanzo cha picha, Dans l'ombre du Shahed
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Septemba 1980, vikosi vya Iraq vilivamia eneo la Iran. Vita vikali vilizuka kati ya nchi hizo mbili, vilivyodumu kwa miaka minane. Mbinu mbaya za mauaji na uharibifu zilitumika, ikiwa ni pamoja na silaha za kemikali. Karibu watu milioni moja waliangamia.
Vikosi vya Iraq vilipata mafanikio katika hatua za mwanzo za vita kutokana na ubora wao wa anga. Jeshi la Iraq lilinunua ndege za upelelezi kutoka Umoja wa Kisovieti na kupiga picha kutoka ndege hizo, ambazo ziliwasaidia kuona maeneo ya adui na kufuatilia mienendo yao.
Kuhusu majeshi ya Irani, yalikuwa yakipigana vita bila maono; hawakuweza kuendesha ndege za kisasa ambazo Wamarekani waliziacha, wala hawakuweza kununua teknolojia waliyohitaji ili kulinda eneo lao, kutokana na vikwazo.
Wairani walihitaji teknolojia ili kupigana vita vilivyohatarisha uhai wao. Lakini vikwazo vya kiuchumi viliwazuia kununua walichohitaji. Kwa hivyo waliamua kuvumbua teknolojia wenyewe, badala ya kuipata kutoka kwa wengine.
Kwa sababu hawakuweza kurusha ndege za upelelezi kwenye mstari wa mbele wa adui ili kuona walipo, Wairani walianza kufikiria kuhusu droni mapema 1981. Walifikiria kuweka kamera juu ya droni hizo.
Wazo lilianzia Chuo Kikuu cha Isfahan. Wanafunzi na wahandisi walifanya kazi ya kulitekeleza. Waliendelea kubuni, kutengeneza, kujaribu, na kutengeneza mifano ya awali kabla ya kuiwasilisha kwa jeshi la Walinzi wa Mapinduzi.
Vifaa rahisi, vya kizamani. Vipande vya plastiki na mbao. Baada ya miaka mingi ya kujaribu na kukosea, huku kukiwa na vikwazo na uvumilivu, vijana watatu walitengeneza droni huko Isfahan na kisha kufanya majaribio katika eneo la Khuzestan. Mmoja alikuwa rubani wa kiraia aliyejulikana kama Farshid, mwingine mwanafunzi wa fizikia aliyeitwa Saeed, na wa tatu fundi dhahabu aliyeitwa Masoud Zahedi.
Walipowasilisha mfano wa droni kwa maafisa wa kijeshi kwa mara ya kwanza, baadhi yao walidhihaki wazo hilo. Ilikuwa kama toy ya mtoto, iliyotengenezwa kwa vifaa visivyo vya kawaida. Tangi la mafuta lilikuwa mfuko wa dripu ya hospitali, na feni la nyumbani.
Droni ya kwanza

Chanzo cha picha, Dans l'ombre du Shahed
Katika msimu wa vuli 1983, kilomita 40 kutoka mstari wa mbele wa mapigano, ndege hiyo iliruka kwa mara ya kwanza juu ya wanajeshi wa Iraq. Ilirudi ikiwa na picha za maeneo ya kijeshi. Baada ya hapo amri ya kuunda droni, sasa rasmi ilitolewa.
Programu hiyo ilihama kutoka warsha ya wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Isfahan hadi makamanda wa kijeshi wa Walinzi wa Mapinduzi. Ili kupata vifaa vya kutengeneza ndege hiyo, ilibidi wakwepe vikwazo vilivyowekwa na kufikia masoko ya kimataifa.
Walinzi wa Mapinduzi walianzisha mtandao wa makampuni huko Dubai na kutumia watu huko Singapore kununua vifaa kutoka nchi kadhaa. Vifaa hivi vilisafirishwa hadi Isfahan, ambapo vilikusanywa. Kuna vifaa vilivyotengenezwa Marekani katika ndege zisizo na rubani za Shahed-136 zilizodunguliwa nchini Ukraine.
Ndege zisizo na rubani zilisaidia katika upelelezi, na vikosi vya Iran ilizitumia katika vita muhimu dhidi ya vikosi vya Iraq baada mwaka 1983. Lakini wahandisi na wanajeshi walianza kuwaza kuhusu kutengeneza ndege zisizo na rubani za kivita.
Ikiwa ndege isiyo na rubani, inaruka na kupiga picha, inaweza kushambulia na kuangamiza ikiwa itawekewa silaha. Hata hivyo, hilo lilihitaji teknolojia tofauti, ndipo Kikosi cha Raad kilitengeneza ndege zisizo na rubani za kivita zinazojulikana kama "Muhajir."
1988, Iran ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kutumia droni zenye silaha. Marekani, Uturuki, na Israeli zinajulikana kwa utengenezaji wa droni, lakini Iran ilikuwa mwanzilishi katika uwanja huu.
1988, ndege zisizo na rubani za Iran za kwanza ziliweza kuruka kwa umbali usiozidi kilomita 50. Kufikia 2026, ndege zao zisizo na rubani sasa zimeingia katika anga ya nchi kadhaa ili kushambulia.
Kwa kweli, Israeli ilikuwa ya kwanza, ikiwa ni pamoja na Marekani, kutumia droni kwa madhumuni ya kijeshi. Katika vita vya 1973 kuharibu makombora ya Misri.
Wakati wa uvamizi wa Lebanon mwaka 1982, Israeli ilitumia ndege zake zisizo na rubani za Scout na Mastiff kwa ajili ya upelelezi na kupiga makombora ya Syria katika Bonde la Bekaa.
Droni za Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Wataalamu wa Iran walifuatilia kwa karibu matukio nchini Lebanon. Washirika wao Hezbollah waliwasaidia kukusanya taarifa sahihi kuhusu ndege zisizo na rubani za Israeli. Waligundua kwamba ndege hizi zisizo na rubani hazikuwa za kisasa sana na wataalamu wao katika vyuo vikuu vya Tehran na Isfahan wana uwezo wa kuziiga.
Wachambuzi wa kijeshi wamebainisha katika ripoti nyingi kwamba mifumo ya awali ya ndege zisizo na rubani za Iran ina sifa nyingi zinazofanana na ndege zisizo na rubani za Skauti na Mastiff za Israeli. Wanasema wahandisi wa Iran walitumia mifumo ya Israeli.
Tangu miaka ya 1970, wataalamu wa silaha wanaamini silaha bora ya kombora na yenye ufanisi ni yale makombora yanayopiga katika maeneo maalumu kama yalivyoelekezwa, kuliko makombora ambayo hupiga tu popote.
Wairani waliongeza teknolojia hiyo katika silaha zao: ikiwa nchi yao haiwezi kushindana na wapinzani wake katika maendeleo ya kiteknolojia, basi lazima ishindane nao kwa idadi na gharama za kiuchumi.
Ndege isiyo na rubani, ambayo inagharimu $20,000 kutengeneza, haiwezi kushindana na kombora ambalo linagharimu dola milioni 2. Lakini ikiwa ndege zisizo na rubani 100 zitatumika, adui atalazimika kurusha makombora 100 na zaidi.
Droni ndogo za Iran hazijaundwa kwa ajili ya Mashambulizi makubwa, bali zimeundwa ili kupunguza ulinzi wa anga wa adui na kuongeza gharama. Mashambulizi ya Iran yanaweza kuendelea kwa muda mrefu zaidi kwa sababu ni ya bei nafuu mara 10 hadi 20 kuliko ulinzi wa makombora wa adui.
Hesabu inaonyesha kwamba kurusha ndege zisizo na rubani 100 kunaigharimu serikali ya Iran dola milioni 2. Hata hivyo, serikali inayodungua droni hizo hutumia dola milioni 200 kwenye makombora ili kuzuia ndege hizi.
Ndege zisizo na rubani pia zina faida nyingine: ni vigumu kwa rada kuzigundua kwa sababu zinapaa polepole na huruka chini chini. Zaidi ya hayo, kuzirusha kwa idadi kubwa kwa wakati mmoja, huifanya mifumo ya ulinzi wa anga kuzidiwa, na wakati mwingine huifanya ishindwe kuzizuia zote.














