Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Washirika wa Iran waliosalia ni kina nani?
Mashariki ya kati iko katika hatari ya vita vikubwa vya kikanda baada ya Israel na Marekani kuishambulia Iran siku ya Jumamosi. Iran ilijibu shambulio hilo kwa kulenga kambi za kijeshi za Marekani zilizoko eneo la Mashariki ya Kati.
Jordan,Qatar,Kuwait,Falme za Kiarabu,Bahrain,Saudi Arabia na Israel, zililengwa na makombora ya Iran, na kuleta hofu ya vita vikubwa kuzuka.
Mataifa haya yote ni washirika wakaribu wa Marekani, na hawana uhusiano dhabiti na jirani yao Iran ambayo imekuwa ikikataa kwa muda mrefu ushawishi wa Marekani, huku Israel ikiwa na ushawishi mkubwa mashariki ya kati.
Makundi kama Hamas ya Gaza,Hezbollah nchini Lebanon,wahouthi nchini Yemen na makundi mengine nchini Syria na Iraq, ambazo zinatajwa kuwa makundi ya kigaidi, yamekuwa yakiilenga Israel kwa muda mrefu.
Tehran pia imejitafutia marafiki wenye mtazamo sawa na wao wa kupinga ushawishi wa Marekani, kama Rais wa Urusi Vladimir Putin, aliyekuwa rais wa Syria Bashar al-Assad na aliyekuwa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro.
Ila muungano wa ushirikiano wa viongozi hawa umefifia katika siku za hivi karibuni, baada ya baadhi ya viongozi hao kuondolewa madarakani.
Maduro anatumukia kifungo nchini Marekani huku Bashar al-Assad yuko mafichoni baada ya serikali yake kupinduliwa.
Hezbollah, ambayo kwa muda mrefu imekuwa mojawapo ya maadui wakubwa zaidi wa Israel, imepungua kwa ukubwa kufuatia mfululizo wa mashambulio ya Israeli dhidi ya uongozi wake, wakati Hamas nayo imeonekana kuwa dhaifu zaidi baada ya vita vyake na Israel huko Gaza.
Tunachunguza nani ambao wamekuwa washirika wa jadi wa Iran katika eneo hilo na ni yupi bado anabaki mwaminifu kwa Tehran.
Syria, rafiki ambaye Iran ilipoteza
Syria ilikuwa mshirika wa karibu wa Iran kupitia Bashar al-Assad, ambaye walimtumia kupata ushawishi katika mataifa ya kiarabu. Ila urafiki huo ulififia baada ya Assad kuondolewa madarakani mwaka wa 2024.
Kiongozi wa sasa wa Syria, Ahmed al-Sharaa ambaye ni muislamu wa kisunni,amejitoa katika muungano huo wa kuipinga Marekani, na kuanza kushirikiana na Trump, na hata kuzuru ikulu ya White House.
Hezbollah, kundi la wanamgambo nchini Lebanon ambalo limekuwa mojawapo ya washirika wakubwa wa Iran, imefifia baada mfumo wa kutumiwa misaada kupitia Iraq na Syria kuharibika.
Wahouthi nchini Yemen
Kundi la wanamgambo wa kihouthi ni mojawapo ya washirika wakuu wa Iran mashariki ya kati, kundi hili limepata umaarufu tangu kudhoofika kwa Hezbollah nchini Lebanon.
Kundi la kihouthi ambalo ni la Shia linadhibiti 30% ya Yemen, na limeshutumiwa katika utawala wake wa kukandamiza watu na kukiuka haki za kibanadamu.
Kundi hilo lilianzishwa mwaka wa 1990, na wanachama wake ni wa Zaidi, jamii ndogo ya waislamu wa Shia nchini Yemen, ambao wanapatikana kaskazini mwa taifa hilo ambalo lina watu million 33.
Mashambulizi ambayo kundi hili imetekeleza dhidi ya Israel na Marekani yameongezeka tangu vita vya Gaza kuzuka tarehe 7 mwezi Oktoba 2023.
Mara kwa mara, kundi hili pia hurusha makombora na ndege zisizo na rubani ambazo hufanikiwa kufika Israel, ingawa nyingi hudunguliwa na Israel.
Mwaka wa 2025, Marekani ililenga vituo zaidi ya elfu moja vya wahouthi nchini Yemen, katika juhudi za kutaka kuliangamiza kundi hilo, ambalo lilikuwa limeanza kuharibu biashara ya meli.
Hezbollah
Kundi la Kishia la Hezbollah nchini Lebanon, hadi kufikia mwaka wa 2024, walikuwa washirika wakubwa wa Iran.
Hezbollah ilianzishwa mwaka wa 1982, kama kundi la kuipinga Israel, lakini imeimarisha nguvu zake, na walikuwa na zaidi ya wapiganaji elfu thelathini nchini Lebanon.
Kwa miongo kadhaa, Hezbollah imekuwa ikipokea ufadhili na mafunzo kutoka kwa utawala wa Iran, ambao walikuwa wakiitumia kuishambulia Israel.
Ila ujio wa vita vya Gaza ilivuruga kila kitu eneo hilo.
Wakati Hamas iliishambulia Israel mwaka wa 2023, Israel ilijibu vikali kwa kurusha mabomu eneo la Gaza, huku Hezbollah ikianzisha mashambulizi mengine karibu na mpaka wa Israel na Lebanon.
Israel ilijibu na mashambulizi makali na kumuua kiongozi wa kundi hilo Hassan Nasrallah pamoja na maelfu ya wapiganaji wa kundi hilo.
Kudhoofika kwa Hezbollah kulichangia kuondolewa kwa Bashar al-Assad, na kuiacha Tehran upweke.
Ila Hezbollah bado ina nguvu ya kuishabulia Israel.
Makundi ya wanamgambo wa kishia wa Iraq
Chini ya muungano huu kuna makundi tofauti ya uasi ya kishiia zenye uhusiano thabiti na Iran, ambayo inazifadhili na kuzipa silaha.
Makundi haya ambayo pia yanajulikana kama nguvu za uhamasishaji wa umma (PMF), muungano huu wa makundi ya uasi linaloshirikiana na jeshi la Iraq, linafanya kazi kwa uhuru na, baadhi yao hupokea amri moja kwa moja kutoka kwa kiongozi mkuu wa Iran, Ali Khamenei.
Hivi karibuni pia wameanza kujulikana kama "upinzani wa kiislamu wa Iraq", na wamefanya mashambulio ya droni kaskazini mwa Israel.
Siku ya Jumamosi baadhi ya wapiganaji wa kundi hili waliuawa katika mlipuko uliotokea eneo la Jurf al Sakhar,kusini mwa Baghdad, msemaji wa kundi hilo aliliambia shirika la habari la Reuters.
Mmoja wa viongozi wa kundi hilo, Kataib Hezbollah, hizi majuzi aliwaambia wapiganaji wa kundi hilo kujiandaa kwa "vita virefu" iwapo Iran itashambuliwa na Marekani.
Hamas
Kundi hili la Kipalestina ambalo limekuwa likipokea ufadhili na mafunzo kutoka Iran kwa miongo kadhaa, limedhoofishwa na vita vya Gaza ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka miwili.
Ingawa kundi hilo bado linaudhibiti wa eneo la Gaza, uwezo wake wa kutekeleza mashambulizi kwa kiwango kikubwa umelamazwa.
Israel imewauwa viongozi wake wengi wa kijeshi na kisiasa, ikiwemo Ismael Haniya ambaye aliuawa katika shambulio lililotekelezwa na Israel mjini Tehran mwaka wa 2024.
Sehemu nyingine ya dunia
Iran imeimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na kijeshi na Urusi katika miaka ya hivi karibuni, ikipokea silaha na teknolojia kutoka Urusi wakati pia inajaribu kuepuka vikwazo vya kimataifa.
Moscow ilikosoa vikali mashambulizi ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran siku ya Jumamosi, ikisema nchi hizo mbili "zimeingiza Mashariki ya Kati kwenye mzozo ambao haujadhibitiwa."
Aidha, Kremlin pia inataka kuendeleza uhusiano wake na mataifa mengine muhimu katika eneo hilo kama Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, na Israel.
Ukaribu kati ya Urusi na Marekani kufuatia kurudi kwa Trump madarakani unaweza kuwa sababu nyingine Moscow inajizuia jinsi inavyoweza kujibu kushambuliwa kwa Iran.
China pia ilidai kusitishwa mara moja kwa vita na kutaka uhuru wa Iran kuheshimiwa.
Beijing imekuwa mshirika mkuu wa kibiashara wa Tehran.
Mnamo 2025, China ilinunua 80% ya mafuta ya Iran, ambayo imeekewa vikwazo na Marekani.
Licha ya ushirikiano huo, Beijing inamaslahi yake ya kimataifa ambayo inaizuia kujihusisha na vita hivyo moja kwa moja.
Iran pia iko na ukaribu na Korea Kaskazini, uhusiano ambao ulianza miaka ya 1980 wakati wa vita vya Iraq na Iran.
Iran pia imedumisha uhusiano wake na Venezuela kuanzia miaka ya 2000 baada ya Caracas na Tehran kutia saini mikataba tofauti ya kibiashara.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula