Jinsi droni za kawaida tu zinavyowapa Islamic State nguvu mpya Afrika Magharibi

Ndege isiyo na rubani ya quadcopter ikielea kwenye jua.

Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images

    • Author, Makuochi Okafor
    • Nafasi, BBC Africa
    • Akiripoti kutoka, Lagos
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Makundi yenye itikadi kali za kidini yanazidi kufanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika eneo la Afrika Magharibi, na hivyo kuzusha hofu kwamba yanaimerisha uwezo wa kuendesha "vita kutoka angani".

Shirika linaloongoza kufuatilia ghasia, Acled, limerekodi takriban mashambulizi 69 ya ndege zisizo na rubani kutoka kwa washirika wa al-Qaeda nchini Burkina Faso na Mali tangu 2023, wakati washirika wawili wa Islamic State (IS) wamefanya mashambulizi takriban 20 – mengi yakiwa nchini Nigeria, ambayo imekuwa ikipambana na vikundi vingi vya waasi kwa karibu miaka 25.

Shambulio la hivi punde zaidi la ndege zisizo na rubani lilitokea katika jimbo la kaskazini-mashariki la Borno nchini Nigeria tarehe 29 Januari, wakati wanajihadi walipofanya mashambulizi ya pande mbili - na ndege nyingi zisizo na rubani na wapiganaji wa ardhini - kwenye kambi ya kijeshi.

Jeshi lilisema wanajeshi wake tisa waliuawa katika shambulio la Islamic State la Jimbo la Afrika Magharibi (Iswap) - lililotambuliwa na Acled kama mshirika "muhimu" wa IS katika "vita vya ndege zisizo na rubani".

Wanajihadi hao walikuwa wakifanya mashambulizi kwa kutumia "ndege za kibiashara, ambazo gharama yake ni ya chini [zisizo na rubani]" ambazo "zilitengenezwa kwa vilipuzi", huku pia wakizitumia kufanya uchunguzi katika kujiandaa kwa mashambulizi ya ardhini, mchambuzi mkuu wa Afrika Ladd Serwat aliiambia BBC.

Licha ya ukweli kwamba serikali ya Nigeria inadhibiti uagizaji wa ndege za kibiashara na zile zisizo na rubani, na kukataza matumizi yake bila kibali rasmi, wanajihadi waliweza kuzipata kupitia mitandao yao ya magendo katika mipaka ya kanda hiyo, alisema mtafiti mkuu mwenye makao yake nchini Nigeria katika taasisi ya Utawala Bora Afrika, Malik Samuel.

"Kuongezeka kwa matumizi ya ndege zisizo na rubani zenye silaha na makundi yenye itikadi kali katika eneo la Sahel na Ziwa Chad inatia wasiwasi sana, na inaashiria mabadiliko makubwa," mchambuzi wa masuala ya usalama Audu Bulama Bukarti aliiambia BBC.

"Ndege zisizo na rubani hupunguza gharama ya kufanya mashambulizi, kuruhusu wanamgambo kukusanya taarifa za kijasusi wakikabiliwa na kiwango kidogo cha hatari na kuwezesha mashambulizi kwenye maeneo ya kijeshi ambayo hapo awali yalikuwa magumu kufikiwa," aliongeza.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kulingana na Serwat, kundi la Iswap limefanya mashambulizi 10 ya ndege zisizo na rubani tangu 2024 kaskazini-mashariki mwa Nigeria na pia kaskazini mwa Cameroon, kusini mwa Niger, na kusini mwa Chad - nchi zote hizo zikiathiriwa na uasi unaoendelea nchini Nigeria.

Idadi kama hiyo ya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yalifanywa na mshirika mwingine wa IS, Kundi la Islamic State la Jimbo la Sahel (ISSP), huko Afrika Magharibi, data ya Acled inaonyesha.

Katika shambulizi lake la hivi karibuni, kundi la ISSP lilifanya shambulizi kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa katika mji mkuu wa Niger, Niamey, na kambi za kijeshi zilizo karibu pia mnamo tarehe 29 Januari, huku wizara ya ulinzi ikisema kuwa wanajeshi wanne walijeruhiwa na 20 kati ya washambuliaji waliuawa.

Serwat alisema kuwa wakati baadhi ya ripoti zinadai ISSP ilitumia mota na RPG, wengine walisema kuwa wanamgambo hao walifanya shambulizi la ndege zisizo na rubani.

"Ikiwa ndege isiyo na rubani ilitumiwa, hii inawakilisha mara ya kwanza kundi la ISSP kutumia ndege isiyo na rubani yenye vilipuzi nchini Niger," aliongeza.

Kundi la kijihadi ambalo limetumia ndege zisizo na rubani zaidi ni Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) lenye uhusiano na al-Qaeda. Acled inasema imefanya mashambulizi 69 nchini Mali na Burkina Faso, na moja kuvuka mpaka wa Togo.

JNIM fighters, in camouflage, train at an undisclosed location

Chanzo cha picha, Al-Zallaqa

Maelezo ya picha, JNIM inachukuliwa kuwa kundi lenye nguvu zaidi la wanajihadi katika eneo la Afrika Magharibi

"Mpango wa ndege zisizo na rubani wa JNIM umeendelezwa kwa kasi na kuenea katika mitandao iliyounganishwa nchini Mali na Burkina," mchambuzi mkuu wa Acled Afrika Magharibi Héni Nsaibia alisema.

'Military Africa', ambayo ni chanzo cha tasnia ya ulinzi mtandaoni, kiliripoti kuwa Februari mwaka jana, JNIM pia ilitumia ndege zisizo na rubani zinazojulikana kama 'first-person view' (FPV) - rubani ana uwezo wa kuona moja kwa moja kutoka kwenye ndege – na kudondosha vifaa vya vilipuzi vilivyotengenezwa kwa chupa za plastiki, kwenye maeneo ya kijeshi katika mji wa Djibo nchini Burkina Faso.

"Hii iliashiria ongezeko kubwa, kwani ndege zisizo na rubani za FPV - ndogo, nyepesi, na zinazotumiwa mara nyingi nchini Ukraine - zinawezesha ulengaji sahihi," Military Africa iliripoti.

Samuel alisema vikundi vya jihadi vilishawishiwa na kufunzwa na wapiganaji wa kigeni kila mara kutumia mbinu mpya - kuanzia kutengeneza mabomu ya barabarani na mikanda ya kujitoa mhanga, na sasa wamejifunza kutumia ndege zisizo na rubani zilizodhamiriwa kuwa za matumizi ya kawaida tu na kuzibadilisha kuwa silaha.

Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yanaweza kupunguza majeruhi miongoni mwa wanajihadi, huku ikipata "ufanisi" zaidi katika kufikia maeneo lengwa, Samuel alisema.

Mchambuzi wa Acled Nsaibia aliiambia BBC kuwa ingawa mashambulizi mengi ya ndege zisizo na rubani za JNIM nchini Mali na Burkina Faso yalilenga wanajeshi na wanamgambo wanaounga mkono serikali, baadhi pia yamewakumba raia, ikiwa ni pamoja na masoko katika jamii zinazodhaniwa kuwa zinashirikiana na vikosi vya serikali.

Kuhusu Iswap, ilijulikana kuwa ilifanya shambulizi moja tu la ndege isiyo na rubani ambayo iliua raia - mnamo Juni 2025, wafugaji wawili waliuawa na mmoja kujeruhiwa kaskazini mwa Cameroon, Nsaibia alisema.

Katika ripoti ya mwaka jana, mtafiti katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama yenye makao yake makuu nchini Afrika Kusini, Taiwo Adebayo, aliandika kwamba ili kukabiliana na tishio hilo, majeshi ya Afrika Magharibi yalihitaji kufanya "mashambulizi ya mapema" ili kuharibu maeneo ya kuunganisha vipuri na kurusha ndege zisizo na rubani, na kupata teknolojia ya juu zaidi ya kukabiliana na droni hizo, ikiwa ni pamoja na mifumo ya ulinzi wa anga.

Vinginevyo, alionya, wanajihadi wanaweza kuongeza uwezo wao wa vita vya ndege zisizo na rubani na kufanya "mashambulizi yenye athari kubwa" ambayo inaweza kuzidisha ukosefu wa uthabiti katika eneo la Afrika Magharibi.

Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Ambia Hirsi