Tamasha la Wireless lafutwa baada ya Kanye West kunyimwa kuingia Uingereza
Chanzo cha picha, Reuters
Waandaaji wa Tamasha la Wireless wamesema kuwa tamasha la mwaka huu limefutwa. Hii ni kwa sababu serikali ya Uingereza imemzuia YE (Kanye West) kuingia nchini.
Kwa sababu ya uamuzi huo, tamasha haliwezi kufanyika. Watu wote walionunua tiketi watarudishiwa pesa zao zote.
Waandaaji pia walieleza kwamba kabla ya kumualika YE, walizungumza na makundi mbalimbali yaliyohusika na tukio hilo, na wakati huo hakuna aliyetoa malalamiko yoyote.
Walisisitiza kuwa chuki dhidi ya Wayahudi ni mbaya na inaumiza, na wanaelewa kwamba suala hili limeathiri watu binafsi kwa kiasi kikubwa.
Uamuzi wa kumualika ulianza kukosolewa kutokana na kauli zake za zamani za chuki dhidi ya Wayahudi, ikiwa ni pamoja na kuupa wimbo jina la “Heil Hitler” na kujitangaza kuwa yeye ni Mnazi.
YE amesema kuwa kusema tu samahani haitoshi, lakini bado ana matumaini ya kupata nafasi ya kuzungumza na jamii ya Wayahudi nchini Uingereza siku zijazo.
Trump aonya 'kuuangamiza mfumo mzima' wa Iran leo iwapo haitafikia makubaliano
Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Marekani Donald Trump amechapisha kwenye mtandao wa Truth, akionya: "Mfumo mzima utaangamizwa usiku wa leo, na hautarejeshwa tena".
Anaendelea: "Sitaki hilo litokee, lakini huenda likatokea.
Hata hivyo, sasa kwa kuwa tuna mabadiliko kamili ya Utawala, ambapo akili tofauti, nadhifu, na zisizo na msimamo mkali zinatawala, labda jambo la ajabu la kimapinduzi linaweza kutokea, NANI ANAJUA?
"Tutabaini usiku wa leo, moja ya nyakati muhimu zaidi katika historia ndefu na ngumu ya Dunia. Miaka 47 ya ulafi, ufisadi, na kifo, hatimaye itaisha. Mungu awabariki Watu Wakuu wa Iran!"
Rapa wa zamani wa Migos, Offset, amepigwa risasi nje ya kasino huko Florida, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Marekani.
Mtu huyo mwenye umri wa miaka 34, ambaye jina lake halisi ni Kiari Kendrell Cephus, yuko "imara" na "anafuatiliwa kwa karibu" hospitalini, msemaji aliiambia Variety.
Idara ya Polisi ya Seminole imeiambia BBC Newsbeat kwamba tukio hilo lilitokea Jumatatu jioni na kwamba watu wawili wamekamatwa kuhusiana na ufyatuaji risasi huo. BBC Newsbeat imewasiliana na wawakilishi wa Offset ili kupata maoni yao.
Polisi walisema tukio lilitokea "katika eneo la valet" baada ya saa 13:00 Jumatatu, nje ya Seminole Hard Rock Hollywood" na "kusababisha majeraha yasiyotishia maisha".
Jeshi hilo pia lilisema "uchunguzi unaendelea". Offset anajulikana zaidi kwa kuwa sehemu ya wanamuziki watatu wa hip-hop Migos pamoja na Quavo na Takeoff.
Alifunga ndoa na mwimbaji na rapa wa Marekani Cardi B mnamo 2017 na wanandoa hao wana watoto watatu.
Raia wa Chad waliotekwa na Boko Haram bado wanashikiliwa mateka
Chanzo cha picha, Getty Images
Ripoti zinasema sita kati ya raia saba wa Chad waliotekwa nyara katika eneo la Ziwa Chad na wapiganaji kutoka kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Boko Haram, bado wako kifungoni.
Utekaji nyara huo ulifanyika mapema wiki iliyopita katika eneo la N’Guigmi-Daboua, la mpaka wa mbali unaounganisha Niger, Chad na Nigeria.
Licha ya uwepo wa vikosi vya kikanda na kimataifa, eneo hilo bado liko katika hatari kubwa ya kushambuliwa na vikundi vyenye silaha.
Vyanzo vinasema mmoja wa mateka tayari ameuawa. Watekaji nyara sasa wanadai fidia kubwa kwa ajili ya kuachiliwa kwa mateka sita waliobaki.
Miongoni mwa waliotekwa nyara ni daktari kijana wa Chad ambaye tukio lake limevutia umakini mkubwa. Inasemekana alikuwa akikamilisha mafunzo maalum ya upasuaji wa watoto katika mji mkuu wa Niger, Niamey, na alikuwa akisafiri kwenda nyumbani kuhudhuria mazishi ya baba yake wakati gari lake lilipokamatwa.
Wanamgambo hao wanadai faranga milioni 500 (karibu dola milioni moja za Marekani) kwa ajili ya kuachiliwa kwake pekee.
Kwa mateka wengine watano, kundi hilo linasemekana kuomba faranga za CFA milioni 50 kila mmoja. Kiasi kinachohusika ni zaidi ya uwezo wa familia nyingi katika eneo hilo na kinasisitiza jukumu linaloongezeka la utekaji nyara kwa ajili ya fidia katika kufadhili vikundi vya wanamgambo vinavyofanya kazi karibu na Ziwa Chad.
Familia za waathiriwa zinasema hawajawasiliana na maafisa nchini Chad au Niger. Wasiwasi wao umeongezeka kutokana na video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ambazo zinaonekana kuonesha mateka wakiomba msaada na kuthibitisha kwamba mmoja wa wenzao ameuawa.
Ukweli wa picha hizo haujathibitishwa kwa uhuru na BBC.
Chama cha Madaktari cha Chad, pamoja na familia ya daktari aliyetekwa nyara, kimeanzisha juhudi za kuchangisha fedha katika jaribio la kupata kuachiliwa kwa mateka hao. Utekaji nyara huo unaangazia ukosefu wa usalama unaoendelea katika bonde la Ziwa Chad, ambalo linabaki kuwa mojawapo ya maeneo yenye vurugu zaidi duniani yanayohusiana na shughuli za jihadi.
Habari za hivi punde, Watu watatu wauawa karibu na ubalozi mdogo wa Israel mjini Istanbul -Ripoti
Watu watatu wameripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi karibu na ubalozi mdogo wa Israel mjini Istanbul, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uturuki.
Maafisa wawili wa polisi wanasemekana kujeruhiwa, kwa mujibu wa shirika la utangazaji la serikali ya Uturuki.
Haijathibitishwa rasmi ni wangapi wamejeruhiwa katika tukio hilo.
Huku hayo yakijiri Jeshi la Israel linasema kuwa Iran imerusha makombora zaidi kuelekea nchini humo.
Taarifa ya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF, inasema kuwa mifumo ya ulinzi wa anga kwa sasa inafanya shughuli ya kuzuia makombora hayo.
Katika taarifa nyingine IDF imewashauri raia wa nchi hiyo kuondoka katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ulinzi baada ya kuambiwa hapo awali kujificha katika maeneo hayo.
Ethiopia yamkamata mshukiwa mkuu wa genge la ulanguzi wa binadamu
Chanzo cha picha, Jason Florio-MOAS
Polisi nchini Ethiopia wanamzuilia mshukiwa wa biashara haramu ya binadamu anayetuhumiwa kuhusika na vifo vya zaidi ya watu 100 na unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake zaidi ya 50.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Idara ya polisi nchini Ethiopia inasema mshukiwa mkuu, anayejulikana kama Yetbarek Dawit, pia Kibrom, alikamatwa pamoja na wenzake tisa katika mji wa Shire, kaskazini mwa Ethiopia.
Anadaiwa kuwasafirisha zaidi ya watu 3,000 kwa njia zisizo halali.
Kulingana na uchunguzi huo, kundi hilo limekuwa likiwateka vijana tangu 2018 kutoka Ethiopia, Sudan, Eritrea, Djibouti, Kenya, na Somalia, kuwasafirisha hadi Libya.
Polisi waliripoti kwamba wahalifu hao walikuwa wakiendesha vitui vitano vya kuwazuiliwa watu nchini Libya, ambapo waathiriwa walishikiliwa mateka na kudhulumiwa vibayai.
Kundi hilo linaaminika kujipatia zaidi ya dola milioni 19 kupitia vitendo hivi vya uhalifu.
Inasemekana kuwa waathiriwa walilazimika kuwasiliana na familia zao kutuma pesa.
Wale ambao hawakuweza kulipa fidia walipewa chakula mara moja tu kwa siku na kuteswa kwa kupigwa na nyaya za umeme, kufungwa minyororo mikononi na miguuni mwao, na kuchomwa kwa kumiminiwa mwilini plastiki iliyoyeyushwa.
Uchunguzi wa polisi ulithibitisha kuwa wa weni wathiriwa wengi alipoteza maisha, wengine walijeruhiwa vibaya kimwili, na wanawake walifanyiwa ukatili wa kijinsia, uliowababishia madhara makubwa ya kimwili na kisaikolojia.
Polisi pia walisema kwamba wamekusanya ushuhuda kutoka kwa waathiriwa zaidi ya 100 na familia zao wanaoishi Ethiopia, Libya, Uswizi, Uholanzi, Uingereza, na Canada.
Israel yaonya Wairani kutosafiri kwa treni huku Trump akitishia 'kushambulia' miundombinu
Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images
Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) lawaonya watu nchini Iran wasipande treni leo.
Katika chapisho lililoshirikiwa kwenye akaunti ya kijeshi ya mitandao ya kijamii ya Farsi, inawaambia watu nchini Iran "kwa ajili ya usalama wenu" "mujiepushe kutumia usafiri wa treni" kote nchini "hadi saa 21:00 kwa saa za Iran".
Inaongeza kwamba "uwepo wenu kwenye treni na karibu na njia za reli kuna hatarisha maisha yenu".
Hii inakuja huku Rais wa Marekani Donald Trump akitishia kushambulia maeneo ya miundombinu ya raia kote Iran, ikiwa utawala utakataa kuruhusu kupita kwa uhuru katika njia ya Mlango-Bahari wa Hormuz ifikapo saa 20:00 EDT Jumanne (01:00 BST Jumatano).
Katika taarifa mpya zilizotolewa usiku kucha, jeshi la Israeli pia lilisema limekamilisha wimbi la mashambulizi ya angani yanayolenga "miundombinu mjini Tehran" inayohusiana na utawala huo, na kuwaua watu waliosema ni wanachama wa Hezbollah.
Kando na hilo, jeshi pia lilisema limezuia makombora yaliyorushwa kuelekea Israeli na Iran.
Watu kumi wauawa katika mapigano kati ya Hamas na wanamgambo Gaza
Chanzo cha picha, Reuters
Vyanzo vya ndani vinasema kuwa takriban Wapalestina 10 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israeli na mapigano kati ya Hamas na wanamgambo wa Palestina wanaoungwa mkono na Israeli katikati mwa Gaza.
Inasemekana mashambulizi hayo yaliwalenga maafisa wa usalama wa Hamas ambao walikuwa wamepambana na wanamgambo wa mashariki mwa kambi ya wakimbizi ya Maghazi. Haijulikani ni wangapi kati yao walikufa katika mashambulizi hayo au katika mapigano ya ardhini.
Msemaji wa hospitali ya al-Aqsa huko Deir al-Balah alisema walipokea miili ya watu 10 kutoka eneo la tukio. Watu wengine kadhaa walijeruhiwa na wengine walikuwa katika hali mbaya, waliongeza.
Hakukuwa na taarifa yoyote ya haraka kutoka kwa jeshi la Israel au Hamas.
Mashahidi walisema wanamgambo wanaoungwa mkono na Israeli waliweka kituo cha ukaguzi mashariki mwa Maghazi, ambapo walishambuliwa na maafisa wa usalama wa Hamas, na kusababisha mapigano.
Mashahidi hao waliongeza kuwa ndege zisizo na rubani za Israeli ziliingilia kati kuwasaidia wanamgambo, zikifanya mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa Hamas katika maeneo matatu.
Israel na Hamas wameshutumuana kwa kukiuka mara kwa mara makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo walikubaliana karibu miezi sita iliyopita.
Takriban Wapalestina 723 wameuawa huko Gaza katika mashambulizi ya Israeli tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoongozwa na Hamas.
Jeshi la Israel limesema wanajeshi wake watano wameuawa katika mashambulizi ya makundi ya Wapalestina katika kipindi hicho hicho.
Artemis II: Wanaanga waliokwenda kwenye Mwezi waanza kurejea Duniani
Chanzo cha picha, NASA
Artemis II: Wanaanga waliokwenda kwenye Mwezi waanza kurejea Duniani
Wanaanga wanne wameanza safari ya kurudi Duniani kwa chombo Artemis II baada ya kufanikiwa kufika kwenye Mwezi na kushuhudia matukio ya kipekee.
Imekuwa siku ya kihistoria kwa wanaanga hao waliotumia chombo Artemis II, ambao sasa wanarejea Duniani baada ya kukamilisha safari ya kwenda kwenye mwezi.
Haya ndiyo yaliyotokea katika saa chache zilizopita:
Karibu saa 19:00 BST, waliokuwa kwenye chombo Artemis II wamevunja rekodi ya kufika umbali mrefu zaidi binadamu kuwahi kusafiri kutoka Duniani - rekodi ya awali ya maili 248,655 (400,171km) kutoka Duniani iliwekwa na walisafiri na chombo Apollo 13 mnamo 1970.
Chombo cha anga cha Orion kilipita nyuma ya Mwezi, na kupoteza mawasiliano na NASA wakiwa wanarudi Duniani - hitilafu hiyo ilitarajiwa na ilidumu kwa takriban dakika 40.
"Houston, Uadilifu, angalia mawasiliano," yalikuwa maneno ya kwanza kutoka kwa mtaalamu wa misheni hiyo Christina Koch wakati walipoanza kuwasiliana tena, ambaye pia alisema "ilikuwa jambo bora kuanza kupata mawasiliano ya Dunia tena"
Wakati wakipaa nyuma ya Mwezi, chombo cha angani cha Orion pia kilifikia umbali wake wa juu zaidi kutoka Duniani - rekodi mpya ya umbali mrefu zaidi mwanadamu kuwa kusafiri kutoka sayari yetu ya nyumbani.
Rekodi mpya imewekwa kwa kufikia maili 252,756 (kilomita 406,771)
Kilichofuata kwa waliokuwemo kwenye chombo hicho ilikuwa kushuhudia kupatwa kabisa kwa jua, kulikodumu kama saa moja - wanaanga walitumia muda huo kupiga picha na kuwaambia timu ya sayansi huko Houston kile walichoweza kuona, kwa kutilia maanani kwamba hakuwa na "maneno ya kutosha" kuelezea walichokiona "tajriba ya kipekee".
"Najua uchunguzi huu hautakuwa na thamani yoyote ya kisayansi lakini ninafurahi sana kwamba tulianzisha safari hii Aprili 1, kwa sababu wanadamu labda hawajaendele kiasi cha haja kuona kile tunachokiona," alisema Victor Glover, rubani wa chomboArtemis II.
Kamanda Reid Wiseman pia alitoa maoni yake: "Ni kitu ambacho hakielezeki. Haijalishi tutatazama tunacho kiona kwa muda gani, akili zetu hazichanganui picha hii tunayoiona. Ni ya kuvutia sana, isiyo ya kawaida... hakuna cha kuelezea, nitahitaji kubuni maneno mapya, hakika hakuna maneno ya kuelezea tunachokiona nje ya dirisha hili."
Wanaanga hao wanne walipoanza kutuma data zao zote Duniani kwa kipindi cha saa saba zilizopita wakati wanafanya uchunguzi wao, pia walipokea simu kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump.
Wachezaji saba wa Eritrea waingia mitini baada ya mechi ya kimataifa
Chanzo cha picha, ENFF
Wachezaji saba kutoka kikosi cha mpira wa miguu cha Eritrea waliopata ushindi wa kihistoria huko Eswatini wiki iliyopita hawajarudi nyumbani, chanzo cha karibu na timu hiyo kimeiambia BBC.
Huku baadhi ya wachezaji wenzao wakirejea, inasemekana wote saba walitoroka.
Kumekuwa na visa kadhaa ambapo Waeritrea wanaoshiriki katika michezo mbalimbali hawarudi nyumbani baada ya mechi za kimataifa katika miaka ya hivi karibuni.
Makundi ya haki za binadamu yameelezea serikali ya Asmara kama ya ukandamizaji mkubwa - dai ambalo mamlaka inakataa. Licha ya idadi ndogo ya watu, mamia ya maelfu ya Waeritrea wametafuta hifadhi nje ya nchi.
Habari za wachezaji hao kutoroka zitakuwa pigo kwa timu hiyo, ambayo, baada ya ushindi wake wa 2-1 dhidi ya Eswatini na ushindi wa jumla wa 4-1, ilikuwa ikisherehekea kurudi katika hatua za makundi za kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 19.
Ni wachezaji 10 pekee kati ya 24 waliokuwa na makao yao nchini Eritrea na ni wachezaji watatu tu kati ya hao, akiwemo nahodha wa timu hiyo Ablelom Teklezghi, ambao sasa wamerejea, vyanzo kutoka Asmara viliiambia BBC Tigrinya.
Ingawa haijulikani wazi wachezaji waliopotea wamekwenda wapi, ripoti zinasema baadhi yao wameonekana Afrika Kusini.
Waliotoroka ni pamoja na kipa Kubrom Solomon na winga mkongwe Medhanie Redie.
Vyombo vya habari vya serikali ya Eritrea vimekuwa kimya sana kuhusu kurejea kwa timu hiyo iliyoshinda, jambo ambalo kwa kawaida lingeambatana na shamrashamra za kuwakaribisha nyumbani.
Vyanzo vinasema maandalizi yalifanywa kwa ajili ya mapokezi lakini yalifutwa kufuatia habari za kutoweka kwa wachezaji hao.
Kanye West anachunguzwa iwapo anastahili kuingia Uingereza
Chanzo cha picha, PA Media
Serikali inapitia upya iwapo Kanye West anapaswa kuruhusiwa kuingia Uingereza baada ya kuzua ghadhabu ilipotangazwa kuwa ndiye atakayeongoza tamasha la London ambalo rapa huyo alikuwa amepangiwa na kusababisha ukosoaji juu ya matamshi yake ya awali ya chuki dhidi ya Wayahudi.
Nyota huyo, ambaye sasa anajulikana kama Ye, alitoa wimbo unaoitwa Heil Hitler na kuuza fulana za swastika mwaka jana. Baadaye aliomba msamaha na kutupia kidole cha lawana ugonjwa alionao wa hisia zinazobadilika-badilika.
Waliokuwa wasimamizi wa tamasha hilo wamejiondoa, na wakosoaji wanatoa wito kwa waandaaji wake kumuondoa kwenye tamasha hilo na viza yake ya kuingia Uingereza ifutiliwe mbali.
Mawaziri wana mamlaka ya kuwapiga marufuku raia wa kigeni kuingia au kuondoka Uingereza ikiwa uwepo wao hautachukuliwa kuwa "wenye manufaa kwa umma".
Rapa huyo tayari amepigwa marufuku kuingia Australia, ambayo ilifuta viza yake baada ya kutoa wimbo wa Heil Hitler mwezi Mei mwaka jana.
DR Congo yakubali kuwachukua wahamiaji kutoka Marekani
Chanzo cha picha, Getty Images
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imekubali kuwapokea wahamiaji waliohamishwa kutoka Marekani ambao wenyewe si WaCongo chini ya makubaliano yanayoanza kutekelezwa mwezi huu, maafisa walisema.
Wizara ya Mawasiliano ilisema mfumo wa mapokezi wa muda umeanzishwa, huku vituo vya kuwahudumia wanaowasili vikitambuliwa katika mji mkuu, Kinshasa.
"Msaada wa vifaa na kiufundi" utatolewa na Marekani, taarifa hiyo ilisema Jumapili, ikiongeza kuwa serikali ya Congo haitagharamia chochote kuhusiana na suala la kifedha kutekeleza mpango huo.
Serikali haikusema ni wahamiaji wangapi watakaowakubali.
Marekani tayari imewatuma wahamiaji katika nchi zingine kadhaa barani Afrika kama sehemu ya msako wao dhidi ya uhamiaji.
Huku kukiwa na wasiwasi kwamba wahamiaji wanaweza kurejeshwa katika nchi zao za asili - ambapo baadhi wanaogopa mateso - maafisa wa Congo walisema hakuna uhamisho kama huo unaopangwa.
Uamuzi wa kuwapokea wahamiaji kutoka nchi nyingine - yaani wale ambao hawatoki katika taifa linalowatuma wala kuwapokea - unaendana na dhamira ya DR Congo kwa utu wa binadamu, mshikamano wa kimataifa na kulinda haki za wahamiaji, taarifa hiyo ilisema.
Mamlaka ya Congo pia ilisema kwamba mpango huo si "mfumo wa kudumu wa kuhama au utoaji wa sera za uhamiaji kwa watu wengine".
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kwamba ingawa haikutoa maoni yoyote kuhusu "mawasiliano ya kidiplomasia na serikali zingine," serikali bado "imeshikilia msimamo wake" katika "ahadi yake ya kukomesha uhamiaji haramu na kuimarisha usalama wa mpaka wa Marekani".
Trump atishia kuiangamiza Iran ndani ya 'usiku mmoja'
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuiangamiza Iran "ndani ya usiku mmoja" ikiwa itashindwa kufikia makubaliano kabla ya tarehe ya mwisho aliyoiweka kwa Tehran kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji duniani.
Tarehe ya mwisho ya Trump ya kufikiwa kwa "makubaliano" - ambayo yanajumuisha usafirishaji huru wa mafuta kupitia Ghuba - imewekwa saa 20:00, saa za Washington DC siku ya Jumanne (00:00 GMT Jumatano).
Akizungumza katika Ikulu ya White House, Trump alisema kwamba anaamini viongozi "wenye busara" nchini Iran walikuwa wakijadiliana kwa "nia njema", lakini matokeo yake yamesalia kuwa yasio na uhakika.
Iran imekataa mapendekezo ya kusitisha mapigano kwa muda, badala yake imetoa wito wa kukomeshwa kabisa kwa vita na kuondolewa kwa vikwazo.
Mkutano wa Trump na waandishi wa habari uliofanyika pamoja na Jenerali Dan Caine, mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi na waziri wa ulinzi Pete Hegseth umefanyika siku chache baada ya vikosi vya Marekani kuwapata marubani wawili wa ndege ya kivita ya F-15 iliyodunguliwa kusini mwa Iran.
Ingawa sehemu kubwa ya matamshi ya Trump yaliangazia kile alichokielezea kama uokoaji wa "kishujaa" wa marubani, alirudia tena onyo lake kwamba Marekani inaweza kuanzisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati na usafiri ya Iran ikiwa Mlango-Bahari wa Hormuz hautafunguliwa tena kufikia tarehe ya ukomo ya Jumanne.
"Nchi nzima inaweza kuangamizwa kwa usiku mmoja - na usiku huo unaweza kuwa kesho usiku," alisema Jumatatu, akimaanisha leo usiku.
Mara tu tarehe ya mwisho itakapopita, Trump aliongeza, Iran itarudishwa ksiku za "Enzi ya Mawe".
"Hawatakuwa na madaraja," alisema. "Hawatakuwa na viwanda vya umeme."
Licha ya Iran kukataa matakwa ya Marekani hapo awali, Trump aliendelea kuonyesha matumaini kwamba Iran ilikuwa ikijadiliana kwa nia njema baada ya safu ya mfululizo za uongozi wa Iran kuuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel.
"Tutajua tu," alisema.
Maendeleo yenye tija katika mazungumzo yoyote hayawezekani kufanyika bila kusitisha mapigano kwanza, kulingana na afisa wa kikanda anayefahamu majadiliano hayo.
Afisa huyo - ambaye aliomba kutotajwa jina kutokana na jinsi mazungumzo yalivyo nyeti - alisema kwamba majadiliano yalikuwa magumu kwa sababu ya changamoto ya mawasiliano kutoka kwa maafisa wa Iran kutokana na hatua ya kuminywa kwa intaneti.
"Ili kufikisha ujumbe kwa Iran, kupata jibu kwa wakati unaofaa ni jambo lisilowezekana," afisa huyo alisema. "Wastani wa muda wa kutoa majibu umekuwa siku moja hivi."
Pakistani, Uturuki na Misri zote zinahusika katika juhudi za upatanishi.