Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani, Israel na Falme za Kiarbu zinataka nini kutoka Iran?
Watu wengi, ingawa si kila mtu, wanataka vita hivi viishe haraka iwezekanavyo. Lakini kwa masharti gani? Hapo ndipo misimamo inapotofautiana. Tuanze na Marekani:
Marekani
Malengo ya vita ya Rais Donald Trump yamekuwa hayaeleweki, yakionekana kuyumbayumba kati ya kupunguza uwezo wa mpango wa nyuklia wa Iran, hadi kusalimu amri kwa taifa hilo na kukubali matakwa yote ya Marekani na Israel, na kuanguka kabisa kwa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu.
Hadi sasa, Iran haijasalimu amri wala kuanguka. Lakini jeshi lake limedhoofishwa sana na siku 16 za mabomu.
Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran huko Geneva mwezi Februari, yaliyosimamiwa na Oman, yalikuwa yakipiga hatua katika jambo la nyuklia.
Wa-Oman wanasema Iran ilikuwa tayari kufanya makubaliano makubwa ambayo yalitoa uhakikisho mkubwa kwamba Tehran haitafuti silaha za nyuklia.
Kile ambacho Iran haikuwa tayari kujadili ni kupunguza au kufuta mpango wake wa makombora ya masafa marefu wala usaidizi wake kwa makundi inayoyaunga mkono katika eneo hilo, kama vile Houthi huko Yemen au Hezbollah huko Lebanon.
Kile inachotaka Washington, na washirika wake wengi, vita hivi viishe kwa kuanguka kwa utawala wa Ayatollah, na kuwepo kwa serikali ya mpya, iliyochaguliwa kidemokrasia ambayo haitoi tena tishio kwa watu wake au majirani zake. Lakini kufikia Jumatatu, hilo halionyeshi dalili zozote za kutokea.
Ikiwa hilo haliwezekani, matokeo mengine bora zaidi kwa Marekani juu ya vita hivi, yatakuwa kama Jamhuri ya Kiislamu iliyoharibiwa vibaya itabadilisha tabia yake, kuacha kuwatendea vibaya raia wake na kukomesha uungaji mkono wake kwa wanamgambo wenye msimamo mkali katika eneo hilo.
Hili pia linaonekana kuwa gumu baada ya Iran kumchagua kiongozi wake mkuu mpya, mtu ambaye ana uwezekano mkubwa wa kuikera Washington, naye ni Mojtaba Khamenei, mwana wa marehemu, Ayatollah Ali Khamenei.
Kwa kupanda kwa bei ya mafuta duniani, kuzuiwa kwa kiasi fulani kwa Mlango-Bahari wa Hormuz na kuongezeka kwa wasiwasi nyumbani ambapo Marekani inaingizwa katika mzozo mwingine wa gharama kubwa wa Mashariki ya Kati, kutakuwa na shinikizo kubwa kwa Rais Trump kumaliza vita hivi.
Lakini itakuwa vigumu kwake kusema ameshinda ikiwa utawala wa Tehran utasalia madarakani, bila kutetereka.
Iran
Iran inataka vita visimame haraka iwezekanavyo lakini sio kwa masharti yoyote ya Washington. Inajua kwamba inaweza kupambana zaidi na Trump katika vita hivi, kutokana na jiografia yake.
Iran ina ufuo mrefu zaidi kuliko nchi yoyote ya Ghuba na ina uwezo wa kuzuia usafirishaji wa meli - kwa muda usiojulikana katika Mlango- Bahari wa Hormuz - meli ambazo katika nyakati za kawaida hubeba takriban 20% ya mafuta yote duniani.
Wito wa rais wa Marekani kwa nchi nyingine kusaidia kukabiliana na matokeo ya vita alivyoanzisha na Israel unakumbwa na upinzani. Uingereza, Ulaya na nchi zingine zina wasiwasi wa kuziweka meli zao za majini katika hatari, zikisindikiza meli za kibiashara kupitia Mlango-Bahari, wakati hazikuunga mkono vita hivi hapo awali.
Kimsingi, Iran inasema vita lazima vimalizike kwa dhamana kwamba haitashambuliwa tena na pia inataka fidia ya vita kwa uharibifu wa mabilioni ya dola uliosababishwa na mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel.
Iran inajua haitapata chochote kati ya hayo. Lakini uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Kikosi chake cha Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) wanataka tu kunusurika katika mzozo huu ili waweze kutangaza ushindi kwa watu wao na ulimwengu.
Israel
Kati ya mataifa matatu yanayopigana - Marekani, Iran na Israel - Waisraeli wanaonekana hawana haraka katika kumaliza vita hivi. Wanataka kuona akiba kubwa ya makombora ya Iran ikiharibiwa, pamoja na maghala ya kuhifadhia silaha, vituo vya kamandi kuu, maeneo ya rada na kambi za IRGC.
Bila shaka, haya yote yanaweza kujengwa baada ya vita kumaliza, kwa hivyo Israel inataka Iran ielewe kwamba kuna gharama kubwa katika kufanya hivyo, yaani Jeshi la Anga la Israel lina uwezo wa kurudi na kuwapiga mabomu tena katika miezi michache ijayo.
Israel inaona makombora ya Iran na mpango wake wa nyuklia kuwa tishio.
Kwa ujumla, serikali ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu inaona vitisho hivi kama kitu ambacho Israel haiwezi kuishi nacho.
Mataifa ya Kiarabu
Mataifa ya Kiarabu ya Ghuba - Saudi Arabia, UAE, Qatar, Bahrain, Kuwait na Oman - yalidhani yanaweza kuishi kwa amani na Jamhuri ya Kiislamu.
Wamekasirika kwamba licha ya kukataa kuunga mkono vita hivi dhidi ya Iran, bado wamekuwa wakikabiliwa na mashambulizi ya karibu kila siku kutoka ndege zisizo na rubani na makombora ya Iran.
Katika saa chache za kwanza za Jumatatu hii pekee, wizara ya ulinzi ya Saudi Arabia iliripoti kuwa imedungua zaidi ya makombora 60 yaliyolenga eneo lake.
"Mstari mwekundu umevukwa," afisa mmoja wa Ghuba aliniambia. "Hakuna kuaminiana tena kati yetu na Tehran na hatuwezi kuwa na uhusiano wa kawaida nao baada ya hili."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah