Mauaji ya shule Uganda: Kamatakamata yazusha maswali magumu

Chanzo cha picha, EPA
Zaidi ya watu 20 wamekamatwa Uganda wakituhumiwa kushirikiana na kundi la waasi linalolaumiwa kutekeleza mauaji katika shule moja siku ya Ijumaa.
Miongoni mwao ni mkurugenzi na mwalimu mkuu, ambao hawajaeleza chochote.
Maafisa wanasema kuna mgogoro kuhusu umiliki wa shule ambayo watu 42 waliuawa. Jeshi linasema, waasi wenye uhusiano na kundi la Dola La Kiislamu ndio wametekeleza, huku sababu nyingine za shambulio hilo zikichunguzwa.
Kundi la Allied Democratic Forces (ADF), liliundwa miaka ya 1990, lilichukua silaha dhidi ya Rais Yoweri Museveni, wakituhumu uonevu dhidi ya Waislamu. Kundi hilo kwa sasa lipo nchi jirani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kukamatwa watu kunazusha maswali magumu, ikiwa wenyeji na wale wanao wasimamia watoto hao wamehusika na kile kilichotokea. Lakini hakuna ufafanuzi wa kutosha.
Wanafunzi 37 walikuwa miongoni mwa waliuawa, jioni ya siku ya Ijumaa – washambuliaji walivamia skuli ya upili ya Lhibiriha katika mji mdogo wa Mpondwe, karibu na mpaka wa DR Congo.
Waathiriwa ambao wengi wao hukaa katika mabweni, walichomwa na kukatwa hadi kufa na wengine walipigwa risasi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baada ya shambulio hilo, kamanda wa majeshi Meja Generali Dick Olum, alisema vurugu ni njia ya ADF kuwapumbaza wanajeshi wake kutoka katika operesheni za kuwasaka ndani ya DR Congo.
Jirani katika eneo hilo ameiambia BBC, alisikia washambuliaji wakisema “Allahu Akbar,’ maana yake Mungu Mkubwa, na ‘tumefanikiwa kuvuruga utulivu wa nchi ya Museveni.’
Kulingana na taarifa ya jeshi, inashuku wapiganaji watano wa ADF walishiriki katika shambulio hilo.
ADF ambao wana mafungamano na kundi la Dola la Kiislamu, bado hawajasema ikiwa wametekeleza shambulio hilo ingawa kundi hilo limefanya mashambulio mengine ndani ya Uganda siku za nyuma.
Rais Museveni amelilaumu kundi la kigaidi la ADF kwa kilichotokea, pia amezungumza bila kufafanua kuhusu mvutano juu ya shule hiyo.
Mke wa rais, Janet Museveni, pia ni Waziri wa Elimu, amesema kuna mgogoro katika mkoa wa Kasese kati ya wale wanaotaka kuimiliki shule hiyo na shirika lisilo la kiserikali ambalo liliijenga.
Siku ya Jumamosi, alisema wakaguzi kutoka shirika hilo, walikuwepo shuleni siku moja kabla ya shambulio, na kuongezea kuwa uchunguzi mkali unaendelea.
Msemaji wa Jeshi la Uganda, Felix Kulayigye aliiambia BBC, pamoja na maafisa wa shule, watu wawili wanaotuhumiwa kuwaongoza washambuliaji kukwepa kugundulika huko Mpondwe wamekamatwa pia.













