Kwa nini Marekani imelenga Kisiwa cha Kharg cha Iran?

Chanzo cha picha, Gallo Images/Orbital Horizon/Copernicus Sentinel Data 2024
- Author, Alys Davies
- Author, Frank Gardner
- Nafasi, BBC Security Correspondent, Riyadh
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Donald Trump amesema jeshi la Marekani limeshambulia kisiwa kidogo karibu na pwani ya Iran - makao makuu ya kituo kikubwa cha mafuta ambacho kinachukuliwa kuwa chanzo kikuu cha uchumi wa nchi hiyo.
Rais wa Marekani alisema vituo vya kijeshi vya Kisiwa cha Kharg "viliharibiwa kabisa" lakini haikulenga miundombinu yake ya mafuta.
Hata hivyo, Trump alionya kwamba atafikiria upya uamuzi wa kutolenga vituo vya mafuta kwenye kisiwa hicho iwapo Iran au wengine "watafanya chochote kuzuia" njia salama ya meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz - mojawapo ya njia muhimu zaidi za meli duniani, iliyoko kusini mwa pwani ya Iran.
Jeshi la Iran lilisema miundombinu ya mafuta na nishati inayomilikiwa na makampuni yanayoshirikiana na Marekani "itaharibiwa mara moja" iwapo miundombinu ya mafuta ya Kharg itashambuliwa.
Kwa nini Kisiwa cha Kharg ni muhimu kwa Iran?
Kisiwa cha Kharg ni eneo dogo lenye miamba lililo umbali wa maili 15 tu za baharini (kilomita 24) kutoka pwani ya Iran.
Licha ya udogo wake, ni mojawapo ya sehemu muhimu zaidi za miundombinu ya nishati ya Iran.
Marekani kushambulia kisiwa hiki kidogo lakini muhimu kaskazini mwa Ghuba ni kama kushambulia uti wa mgongo wa uchumi wa Iran.
Kisiwa hicho kidogo kaskazini mwa Ghuba ya uajemi, kilomita 25 hadi 30 kutoka pwani ya Iran, ni eneo muhimu katika sekta ya mafuta nchini humo. 90% ya mafuta kutoka Iran, husafirishwa kutoka eneo hili.
Meli kubwa sana za mafuta - zenye uwezo wa kubeba hadi galoni milioni 85 za mafuta - zinaweza kuja kwenye gati refu la kisiwa hicho kuchukua mafuta. Pwani ya kisiwa hicho iko karibu vya kutosha na maji ya kina kirefu, tofauti na pwani isiyo na kina kirefu ya bara.
Meli za mafuta kisha hurudi chini ya Ghuba na kutoka kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz, hadi China - mnunuzi mkuu wa mafuta ya Iran.
Kisiwa hicho, ambacho ni kituo cha usafirishaji wa mafuta ya Iran, hutoa chanzo kikubwa cha mapato kwa Kikosi cha Jeshi cha Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC).
Je, Marekani na Iran zimesema nini kuhusu shambulio hilo?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Siku ya Ijumaa, Trump alisema Kamandi Kuu ya Marekani "imetekeleza moja ya mashambulizi makubwa zaidi ya mabomu katika Historia ya Mashariki ya Kati na kuangamiza kabisa kila shabaha ya JESHI katika Kisiwa cha Kharg, kito cha taji la Iran".
Aliongeza kwamba, "kwa heshima", "alikuwa amechagua KUTOHARIBU Miundombinu ya Mafuta Kisiwani".
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran viliripoti kwamba hakuna uharibifu wowote uliotokea kwenye vituo vya mafuta vya kisiwa hicho. Shirika la habari la Fars lilisema mashambulizi ya Marekani yalilenga ulinzi wa anga, kambi ya wanajeshi wa majini, mnara wa kudhibiti uwanja wa ndege na eneo la kuhifadhi helikopta.
Ehsan Jahanian, naibu wa kisiasa wa gavana katika jimbo la Bushehr kusini mwa Iran, alisema "hakuna wanajeshi, wafanyikazi wa kampuni za mafuta, au wakaazi wa visiwani waliojeruhiwa katika shambulio hilo, na sekta zote zinaendelea na shughuli zao za kawaida".
Jahanian alisema mchakato wa kusafirisha mafuta kutoka Kharg "unaendelea kikamilifu", na "shughuli za makampuni yaliyo katika kisiwa hicho zinaendelea bila kukatizwa", kulingana na ripoti ya shirika la habari la Tasnim linaloshirikiana na IRGC.
Kufuatia mashambulizi hayo, jeshi la nchi hiyo lilionya kuwa miundombinu ya mafuta na nishati ya makampuni yanayoshirikiana na Marekani "itaharibiwa mara moja na kugeuzwa kuwa rundo la majivu" ikiwa vituo vyake vya nishati vitashambuliwa.
Kwa nini Marekani haikulenga vituo vya mafuta vya kisiwa hicho?
Hatua za kijeshi kuharibu miundombinu ya kisiwa hicho zitakuwa na madhara makubwa kwa Iran.
Pia kutasababisha mzozo kuongezeka.
Huenda itafanya bei ya mafuta duniani ipande zaidi na pia inaweza kusababisha Iran kulenga miundombinu zaidi ya mafuta kote Mashariki ya Kati.
Wiki mbili baada ya vita, Iran bado ina uwezo wa kurusha idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani zenye gharama nafuu na zenye milipuko mingi katika nchi jirani za Kiarabu na pia katika meli za usafirishaji.
Inawezekana, pengine, kuongeza maeneo ya kulengwa ili kujumuisha miundombinu muhimu kama vile mitambo ya kuondoa chumvi kwenye maji ambayo hutoa maji ya kunywa kwa mamilioni.
Justin Crump, mchambuzi wa kijeshi na afisa wa zamani wa Jeshi la Uingereza, alisema shambulizi hilo la bomu lilikuwa jaribio la Trump la kuizuia Iran kuzidisha mzozo huo.
"Anaonyesha kama huruma lakini huku akiongeza kuwa anaweza kuwaadhibu zaidi IRGC" kwa kulenga vituo vya mafuta, Crump, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa ushauri wa kijasusi Sibylline, aliambia kipindi cha BBC Radio 4's Today.
Trump hapo awali alisema kwamba lengo la vita hivyo lilikuwa ni watu wa Iran waweze kujitokeza na kupindua utawala wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ingawa tangu wakati huo ameelezea nia nyingine za vita hivyo, Crump alisema kulenga miundombinu ya mafuta ya kisiwa hicho ilikuwa "vigumu" kwani kungeharibu uchumi wa nchi hiyo kwa muda mrefu.
"Hilo haligusii sana juu ya mustakabali wao [ watu wa Iran]", alisema, akiongeza kwamba wakati miundombinu ya mafuta ya kisiwa hicho ilipoharibiwa wakati wa vita vya Iran-Iraq katika miaka ya 1980, ilichukua muda mrefu kujengwa upya.
Je, Marekani itajaribu kuteka kisiwa hicho?
Kumekuwa na uvumi kuhusu ikiwa vikosi vya Marekani vitajaribu wakati fulani kuchukua Kisiwa cha Kharg.
Utekaji nyara huo hautazuia tu mauzo ya mafuta ya Iran bali pia utaweza kutoa jukwaa la kutekeleza mashambulizi dhidi ya bara.
Vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti kwamba meli za majini zinazobeba hadi wanajeshi 5,000 wa majini na mabaharia sasa zinatumwa eneo la Ghuba, na kuongeza uvumi huo.
Idara ya Ulinzi ya Marekani imekataa kutoa maoni.
Kuchukua kisiwa hicho kutakatiza kabisa njia ya kiuchumi ya IRGC, na kuathiri uwezo wake wa kuendesha vita, mchambuzi wa usalama Mikey Kay, kutoka kitengo cha Usalama cha BBC, amesema.
Imefasiriwa na Asha Juma






