Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mpango wa kufuta uchaguzi wa urais unawaweka Wazimbabwe katika mvutano mkubwa
Kuna hofu inayoongezeka ndani ya makundi ya upinzani nchini Zimbabwe kwamba chama tawala cha ZANU-PF kinajaribu tena kujiongezea mamlaka, huku kikiendeleza marekebisho ya katiba yanayolenga kuipa bunge,badala ya wapiga kura, haki ya kumchagua rais, na pia kuongeza muda wa urais kutoka miaka mitano hadi saba.
"Kupindua katiba huku ni mapinduzi, mapinduzi ya polepole yanayotokea Zimbabwe," mwanasiasa mkongwe wa upinzani na waziri wa zamani wa fedha Tendai Biti aliiambia BBC.
Hata hivyo, ZANU-PF, ambayo imekuwa madarakani tangu uhuru mwaka 1980, imejitetea vikali kuhusu mabadiliko hayo yaliyopendekezwa.
"Hakuna kinachotuzuia kubadilika, kwenda kwenye mfumo mwingine ambao ni wa gharama ndogo," alisema msemaji wa chama hicho Patrick Chinamasa.
Mitazamo hiyo tofauti inaonesha mgawanyiko mkubwa uliosababishwa na muswada huo wa mabadiliko ya katiba, ukigawanya wafuasi wa ZANU-PF na wa upinzani.
Hili lilidhihirika wakati wa vikao vya hadhara vya bunge vilivyofanyika hivi karibuni, vilivyowapa wananchi nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko hayo ambayo yangeleta:
- Uchaguzi wa urais, unaofanyika tangu 1990, kufutwa
- Muda wa urais na ubunge kuongezwa kutoka miaka mitano hadi saba
- Uchaguzi wa ubunge wa 2028 kuahirishwa hadi 2030
- Rais Emmerson Mnangagwa, ambaye muhula wake wa pili na wa mwisho unatarajiwa kuisha 2028, kubaki madarakani hadi 2030
- Bunge jipya kumchagua rais ajaye
"Ninaunga mkono muswada huu kikamilifu," alisema mwanamke mmoja katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa michezo mjini Harare wiki iliyopita.
Maelfu ya watu walijaza ukumbi huo, ambapo kila mzungumzaji aliyepanda jukwaani alitoa wito kwa Mnangagwa aendelee kubaki madarakani baada ya 2028.
Emmerson Mnangagwa aliingia madarakani mwaka 2017 baada ya kumuondoa kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe kwa msaada wa jeshi, na baadaye akashinda uchaguzi uliozua utata mwaka 2018 na 2023.
"Kikomo cha urais lazima kiongezwe kutoka miaka mitano hadi saba, na wabunge tunaowachagua lazima waruhusiwe kumchagua rais," alisema mwananchi mmoja katika mkutano wa hadhara.
Wakati kipaza sauti kilipohamishiwa upande ambako wakosoaji wakuu wa muswada huo walikuwa wameketi, kulitokea hali zilizofanana na vurugu na vitisho ambavyo mara nyingi vimeharibu siasa za Zimbabwe, ikiwa ni pamoja na kusukumana, kugombana, na kupigana, pamoja na kunyang'anywa simu za mkononi na waandishi wa habari kuamriwa kufuta video za vurugu hizo.
Mwanachama mkongwe wa upinzani na mwanasheria Fadzayi Mahere aliiambia BBC kwamba wafuasi wa ZANU-PF walisababisha "vurugu" ili kuwazuia wakosoaji kuonesha kupinga muswada huo.
Patrick Chinamasa alikanusha kwamba wafuasi wa chama tawala ndio waliohusika na vurugu hizo.
"Ni sababu gani sisi kama ZANU-PF kuwa na vurugu wakati umma uko upande wetu? Upinzani haukubali kwamba mtazamo wao unashindwa kupata uungwaji mkono," aliiambia BBC.
Lakini upinzani unasema Zimbabwe inaona wimbi jipya la ukandamizaji. Kabla ya vikao hivyo, makundi ya upinzani yanasema polisi walipiga marufuku zaidi ya mikutano yao kumi na miwili.
Kiongozi wa Chama cha National Constitutional Assembly, Lovemore Madhuku, alisema alipigwa na watu waliovaa barakoa mwezi uliopita huku polisi wakitazama.
Tendai Biti, ambaye anaongoza kundi la Constitution Defenders Forum, yuko nje kwa dhamana baada ya kushtakiwa kwa kufanya mkutano wa hadhara bila ruhusa rasmi.
"Tuna historia ya ukandamizaji nchini Zimbabwe," Biti aliiambia BBC.
Bunge linatarajiwa kupitisha muswada huo katika wiki zijazo, katika kile kinachoonekana kuwa kilele cha kampeni iliyoanza mwaka 2024, ikiwa na kauli mbiu "2030, yeye (Mnangagwa) bado atakuwa kiongozi."
Kampeni hiyo imekabiliwa na wapinzani wakali ndani ya ZANU-PF, lakini mkosoaji wake mkuu, Blessed Geza, anayejulikana pia kama "Bombshell", alifariki dunia mapema mwaka huu.
Kwa wafuasi wa rais huyo mwenye umri wa miaka 83, mabadiliko hayo ya kisiasa yataimarisha demokrasia kwa kumaliza kile wanachokiita kampeni za uchaguzi zenye sumu ambazo mara nyingi husababisha vurugu na matokeo kupingwa.
"Kama unavyojua, uchaguzi wowote wa rais, si Zimbabwe pekee, vurugu huhusishwa na kura za wananchi," alisema Patrick Chinamasa akiutetea muswada huo.
Lakini kwa wakosoaji, muswada huo ni hatua ya kurudisha "urais wa kifalme" waliopigania kuumaliza wakati wa utawala wa Mugabe wa miaka 37.
Katiba mpya iliyopitishwa mwaka 2013 nchini Zimbabwe iliweka kikomo cha mihula miwili ya urais, na pia ikasema kuwa jaribio lolote la kuongeza muda wa urais lazima liidhinishwe na wananchi kupitia kura ya maoni na muhimu zaidi, kwamba rais aliye madarakani hawezi kunufaika na ongezeko lolote la muda bila idhini ya wananchi katika kura ya pili ya maoni.
Kwa watu kama Tendai Biti, muswada huu unafuta mafanikio hayo yaliyopatikana kwa taabu, na unaweza kupingwa mahakamani kwa sababu, kwa maoni yao, unakiuka sharti la katiba la kufanya kura ya maoni kabla ya kuongeza muda wa urais.
Hata hivyo, ZANU-PF ina uhakika kuwa inafuata katiba, ikisema hakuna haja ya kura ya maoni kwa kuwa, kwa mtazamo wao, kikomo cha mihula miwili bado kipo, mabadiliko ni kwamba sasa kila muhula utakuwa miaka saba badala ya mitano.
Lakini wakosoaji wanahofu kuwa ZANU-PF, inayoongozwa na Emmerson Mnangagwa, inaweza kuwa inasogea kwa hila kuondoa kabisa mipaka ya mihula ya urais.
"Ikiwa wanaweza kufanya hivi kwa miaka miwili, ni nini kinachowazuia kufanya hivyo kwa miaka 20?" Biti alisema.
Patrick Chinamasa alikana madai kwamba muswada huo unaashiria "mabadiliko makubwa" katika namna ZANU-PF itakavyoongoza Zimbabwe.
"Ni kwamba kwa wakati huu tunataka kuendeleza utulivu wa kisiasa. Tunataka kuendeleza maendeleo ya kiuchumi yanayoendelea tangu mheshimiwa alipoingia madarakani mwaka 2018," alisema.
"Wakati muda wake utakapokwisha tutachagua viongozi wengine."
Kwa upinzani, Zimbabwe inarejea katika historia yake ya giza.
"Wanafanya kosa lilelile ambalo Mugabe alifanya, la kufunga kabisa nafasi za demokrasia," Biti alisema.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi