Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuiangamiza Iran "ndani ya usiku mmoja" ikiwa itashindwa kufikia makubaliano kabla ya tarehe ya mwisho aliyoiweka kwa Tehran kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji duniani.
Tarehe ya mwisho ya Trump ya kufikiwa kwa "makubaliano" - ambayo yanajumuisha usafirishaji huru wa mafuta kupitia Ghuba - imewekwa saa 20:00, saa za Washington DC siku ya Jumanne (00:00 GMT Jumatano).
Akizungumza katika Ikulu ya White House, Trump alisema kwamba anaamini viongozi "wenye busara" nchini Iran walikuwa wakijadiliana kwa "nia njema", lakini matokeo yake yamesalia kuwa yasio na uhakika.
Iran imekataa mapendekezo ya kusitisha mapigano kwa muda, badala yake imetoa wito wa kukomeshwa kabisa kwa vita na kuondolewa kwa vikwazo.
Mkutano wa Trump na waandishi wa habari uliofanyika pamoja na Jenerali Dan Caine, mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi na waziri wa ulinzi Pete Hegseth umefanyika siku chache baada ya vikosi vya Marekani kuwapata marubani wawili wa ndege ya kivita ya F-15 iliyodunguliwa kusini mwa Iran.
Ingawa sehemu kubwa ya matamshi ya Trump yaliangazia kile alichokielezea kama uokoaji wa "kishujaa" wa marubani, alirudia tena onyo lake kwamba Marekani inaweza kuanzisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati na usafiri ya Iran ikiwa Mlango-Bahari wa Hormuz hautafunguliwa tena kufikia tarehe ya ukomo ya Jumanne.
"Nchi nzima inaweza kuangamizwa kwa usiku mmoja - na usiku huo unaweza kuwa kesho usiku," alisema Jumatatu, akimaanisha leo usiku.
Mara tu tarehe ya mwisho itakapopita, Trump aliongeza, Iran itarudishwa ksiku za "Enzi ya Mawe".
"Hawatakuwa na madaraja," alisema. "Hawatakuwa na viwanda vya umeme."
Licha ya Iran kukataa matakwa ya Marekani hapo awali, Trump aliendelea kuonyesha matumaini kwamba Iran ilikuwa ikijadiliana kwa nia njema baada ya safu ya mfululizo za uongozi wa Iran kuuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel.
Maendeleo yenye tija katika mazungumzo yoyote hayawezekani kufanyika bila kusitisha mapigano kwanza, kulingana na afisa wa kikanda anayefahamu majadiliano hayo.
Afisa huyo - ambaye aliomba kutotajwa jina kutokana na jinsi mazungumzo yalivyo nyeti - alisema kwamba majadiliano yalikuwa magumu kwa sababu ya changamoto ya mawasiliano kutoka kwa maafisa wa Iran kutokana na hatua ya kuminywa kwa intaneti.
"Ili kufikisha ujumbe kwa Iran, kupata jibu kwa wakati unaofaa ni jambo lisilowezekana," afisa huyo alisema. "Wastani wa muda wa kutoa majibu umekuwa siku moja hivi."
Pakistani, Uturuki na Misri zote zinahusika katika juhudi za upatanishi.