Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tunajua nini kuhusu mapendekezo ya Pakistan ya kusitisha vita kati ya Marekani na Iran?
Pakistan imeipa Marekani na Iran pendekezo la kusitisha vita na kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, chanzo kinachofahamu mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja kimeliambia shirika la habari la Reuters siku ya Jumatatu.
Mtandao wa habari wa Axios awali uliripoti siku ya Jumapili kwamba mpango wa kusitisha mapigano wa siku 45 ulikusudiwa kuwa awamu ya kwanza ya makubaliano ya pande mbili ambayo yatafungua njia kwa mazungumzo mapana ya moja kwa moja ili kukomesha kabisa mzozo huo.
Vyanzo hivyo pia viliiambia Reuters kwamba mkuu wa jeshi la Pakistan, Asim Munir, aliwasiliana "usiku kucha" na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi.
Reuters iliripoti kwamba pendekezo la Islamabad linataka kusitishwa mapigano kuanza kutekelezwa mara moja ili kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz. Kisha kungekuwa na siku 15 hadi 20 kwa pande hizo mbili kukamilisha makubaliano kamili ya kukomesha mapigano.
Utawala wa Trump na Tehran bado hawajajibu pendekezo hili.
Maafisa wa Iran wamesema hapo awali kwamba usitishaji wowote wa mapigano unahitaji dhamana kwamba Marekani au Israel haitaishambulia Iran tena.
Hata hivyo, maafisa wa Iran pia wameelezea hamu yao ya kuona hali ilivyo katika Mlango-Bahari wa Hormuz ikibadilika, huku Tehran ikitaka udhibiti wa kudumu wa njia hiyo muhimu ya maji.
Baadhi maafisa wa Iran wamependekeza kwamba Iran ilipwe fidia kwa hasara za vita, ambayo inaweza kutozwa katika mfumo wa "ada" kwa kuzitoza meli ili kupita kwenye mlango-bahari huo.
Mazungumzo ya awali
Mazungumzo ya awali yalishindwa, huku Marekani na Iran zikikataa masharti yaliyopendekezwa au zikikataa kwamba mazungumzo yalifanyika.
Machi 24, ripoti ziliibuka kwamba mpango wenye vipengele 15 ulitumwa na Marekani kwenda Iran, huku Pakistan ikiwa ndio mpatanishi.
Televisheni ya Israel Channel 12 iliripoti kwamba mpango huo ulijumuisha matakwa kwamba Iran iharibu vituo vyake muhimu vya nyuklia, isitishe kufadhili vikundi vya kikanda vyenye silaha kama vile Hezbollah au Houthi, na kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz.
Kwa upande wa Marekani ingeondoa vikwazo dhidi ya Iran.
Tehran ilikataa mpango huo moja kwa moja— ikisema una matakwa mengi — kisha Iran ikachapisha masharti matano ili vita visimame, na masharti hayo yalichapishwa katika vyombo vya habari vya serikali ya Iran. Haya yalijumuisha fidia na dhamana kwamba Iran haitashambuliwa tena.
Kisha Machi 31, mpango wa amani wenye vipengele vitano—ulioandaliwa na Pakistan na China—ulitangazwa.
Mpango wa amani uliandaliwa baada ya waziri wa mambo ya nje wa Pakistan kusafiri hadi Beijing kutafuta msaada wa China katika juhudi za nchi hiyo za kukomesha mzozo huo.
Hayo yalijiri huku Donald Trump akisema mazungumzo yanaenda "vizuri sana," lakini Tehran wakati huo ilisema hakukuwa na mazungumzo yoyote.
Pia tulisikia kutoka kwa Trump Aprili 2, alipodai kwamba Iran imeomba Marekani isitishe mapigano. Hili lilikanushwa haraka na Iran kama "uongo usio na msingi" kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.
Nini kifuatacho?
Rais wa Marekani Donald Trump ameweka tarehe za mwisho, ameweka matakwa na kutoa vitisho. Amesema mashambulizi mapya dhidi ya Iran yatakuwa mabaya sana. Yataanza siku ya Jumanne kwa muda wa Washington, ambayo itakuwa ni Jumatano kwa Iran na Afrika Mashariki.
Ndani ya saa nne, kila daraja na kiwanda cha umeme "vitaharibiwa," Trump alisema siku ya Jumatatu.
Ili kuepuka hatima hii, kulingana na Trump, Iran inapaswa kuingia katika makubaliano "ambayo yanakubali.” Sehemu ya makubaliano hayo yanajumuisha "usafirishaji huru wa mafuta" kupitia Mlango wa Hormuz.
Saa za mwisho zinapokaribia, kumekuwa na dalili chache kwamba Iran iko tayari kukubaliana na matakwa ya Trump. Wamekataa kusitisha mapigano kwa muda na kutoa orodha yao wenyewe ya matakwa.
Hali hii inamweka rais wa Marekani katika wakati mgumu. Ikiwa hakuna makubaliano, Trump anaweza kuongeza muda tena - kwa mara ya nne katika wiki tatu zilizopita.
Lakini kurudi nyuma baada ya vitisho hivyo, vilivyojaa matusi na maonyo makali, kunaweza kupunguza kuaminika kwake huku vita vikiendelea.