Jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi ECOWAS imeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ilivyo nchini Venezuela na kutoa wito wa kujizuia na kuheshimu sheria za kimataifa.
Katika taarifa iliyotolewa jijini Abuja, Nigeria, ECOWAS inatambua haki ya mataifa kupambana na uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi na biashara ya dawa za kulevya lakini imeonya kwamba juhudi hizo "lazima zifanyike kulingana na kanuni zilizowekwa za sheria za kimataifa."
Kambi hiyo imeikumbusha jumuiya ya kimataifa kuhusu wajibu wake wa kuheshimu uhuru na mipaka ya chini katika Kifungu cha 2(4) cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
ECOWAS imesema "inaunga mkono kikamilifu msimamo wa Umoja wa Afrika," na kuhimiza mazungumzo jumuishi miongoni mwa Wavenezuela kama njia ya kutatua mgogoro huo.
ECOWAS imetoa kauli hii kufuatia mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na kukamatwa kwa Rais Nicolás Maduro.
Umoja wa Afrika umeonyesha "wasiwasi mkubwa" kuhusu matukio hayo, ukisisitiza kwamba hali hiyo inatishia amani na usalama wa kimataifa.
Umoja wa bara la Afrika, "umesisitiza umuhimu wa mazungumzo, utatuzi wa migogoro kwa amani, na heshima kwa mifumo ya kikatiba na kitaasisi, katika roho ya ujirani mwema, ushirikiano, na kuishi kwa amani miongoni mwa mataifa."
Umoja wa Afrika umesema changamoto za ndani za Venezuela "zinaweza kushughulikiwa kupitia mazungumzo ya kisiasa miongoni mwa Wavenezuela wenyewe."
Afrika Kusini imehimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha mkutano haraka, ikielezea mashambulizi ya Marekani na kumkamata Maduro kama "uvamizi wa kijeshi."
Wizara ya Mahusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya nchi hiyo imesema vitendo vya Marekani ni ukiukaji dhahiri wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambao unazitaka nchi zote wanachama kujiepusha na matumizi ya nguvu dhidi ya uhuru wa eneo au uhuru wa kisiasa wa taifa lolote.
Jirani wa Afrika Kusini, Namibia pia amelaani vitendo vya Marekani, akielezea kukamatwa kwa Maduro na mkewe kama ukiukaji wa uhuru wa Venezuela.
Wizara ya Mahusiano na Biashara ya Kimataifa ya Namibia imesisitiza kwamba uadilifu wa eneo na uhuru wa kisiasa wa mataifa yote lazima uheshimiwe kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Venezuela, taifa la Amerika Kusini linakabiliwa na miaka mingi ya kutokuwa na utulivu wa kisiasa, ugumu wa kiuchumi, na shinikizo la kimataifa, na kuacha mgawanyiko mkubwa kuhusu njia bora ya kutatua mgogoro huo.