Araghchi hayupo Pakistan kuzungumzia nyuklia - Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, hana “jukumu lolote linalohusiana na mazungumzo ya nyuklia” katika ziara yake nchini Pakistan, kwa mujibu wa mkuu wa kamati ya usalama wa taifa ya Iran.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tehran jana usiku, Ebrahim Azizi alisema waziri huyo yuko Islamabad “kwa ajili ya mazungumzo ya mahusiano ya pande mbili pekee.”
Azizi ambaye pia ni kamanda wa zamani wa Jeshi la walinzi wa mapinduzi ya kiislamu (IRGC) alisema masuala ya shughuli za nyuklia “yanabaki kuwa moja ya mipaka mikuu ambayo Iran haiwezi kuvuka.”
Kwa upande mwingine, Marekani imeitaka Iran kusitisha mpango wake wa nyuklia, ikisisitiza kuwa hilo linapaswa kuwa sehemu ya makubaliano yoyote ya mwisho ya amani.



