Jeshi la Israel limeanzisha wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya Iran
Jeshi la Israel linasema limeanzisha wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya ‘miundombinu ya serikali’ ya Iran.
Muhtasari
- Muhtasari wa vita vya Mashariki ya Kati ndani ya wiki moja
- Polisi yathibitisha shambulio na utekaji nyara katika jimbo la Borno Nigeria
- Daktari afanya upasuaji kwa kutumia roboti kwa mgonjwa aliye umbali wa maili 1,500
- Trump asema ni 'kupoteza muda' kutuma wanajeshi wa ardhini wa Marekani nchini Iran
- Kocha wa Morocco ajiuzulu huku Kombe la Dunia likikaribia
- Wanajeshi wa mpakani wa Pakistan na Afghanistan washambuliana, huku raia 100,000 wakikimbia makwao
- Iran haina intaneti kwa siku sita sasa - Netblocks
- Tajiri wa Hong Kong Jimmy Lai hatakata rufaa dhidi ya hukumu ya miaka 20 jela
- Wanne wakamatwa Uingereza kwa tuhuma za kuisaidia idara ya ujasusi ya Iran
- Wakaazi wa Tehran wasimulia 'milipuko ya mara kwa mara' inavyowakosesha usingizi
- Air Tanzania kuwarejesha nyumba Watanzania waliokwama Dubai
- China na Iran zinajadiliana kuhusu njia salama kwa meli za mafuta- ripoti
- Marekani na Venezuela zakubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia baada ya Maduro kukamatwa
- Ukraine yaishutumu Hungary kwa kuwateka raia wake saba
- Hezbollah yawataka raia wa Israel kuondoka karibu na mpaka wa Lebanon
- Marekani yazamisha zaidi ya meli 30 za Iran
- Marekani yasema 'kiwango cha mashambulizi dhidi ya Iran kitaongezeka' huku Israel ikishambulia Beirut na Tehran
Moja kwa moja
Ambia Hirsi & Rashid Abdallah
Indonesia kupiga marufuku mitandao ya kijamii kwa watoto chini ya miaka 16

Chanzo cha picha, Getty Images
Indonesia inasema itapiga marufuku mitandao ya kijamii na majukwaa mengine maarufu ya mtandaoni kwa watoto walio chini ya miaka 16, katika vikwazo vinavyolenga kuwalinda vijana kutokana na unyanyasaji mtandaoni.
Meutya Hafid, waziri wa mawasiliano na masuala ya kidijitali nchini, alitangaza kwamba akaunti za watoto walio chini ya umri wa miaka 16 kwenye majukwaa "yenye hatari kubwa" zitazimwa kuanzia tarehe 28 Machi.
"Hii itaanza na majukwaa kama vile YouTube, TikTok, Facebook, Instagram, Threads, X, Bigo Live, na Roblox," amesema Hafid,
Bado hakuna majibu ya haraka kutoka kwa mitandao itakayo athirika.
Turmp ataka Iran ijisalimishe bila masharti

Chanzo cha picha, White house
Rais wa Marekani Donald Trump anasema "hakutakuwa na makubaliano na Iran isipokuwa ijisalimisha bila masharti.
Akiandika kwenye jukwaa lake la mitandao ya kijamii la Truth Social, Trump amesema: "Baada ya kujisalimisha, kutakuwa na na uteuzi wa kiongozi mkuu ambaye anakubalika.
Trump amesema, "sisi, na washirika wetu wengi, tutafanya kazi bila kuchoka kuirudisha Iran kutoka ukingoni mwa uharibifu, na kuifanya iwe kubwa kiuchumi, bora, na imara zaidi kuliko hapo awali."
Muhtasari wa vita vya Mashariki ya Kati ndani ya wiki moja

Mashariki ya Kati imetumbukia katika mgogoro, kufuatia mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yakilenga miundombinu ya makombora ya nchi hiyo, maeneo ya kijeshi na uongozi. Tehran, kujibu, imeanzisha mashambulizi katika eneo lote, ikiwa ni pamoja na Israel.
Huu ni muhtasari wa mambo yalivyo baada ya wiki moja baada ya vita.
Siku ya Jumamosi: Israeli ilianzisha mashambulizi dhidi ya Iran. Ndani ya saa moja, Rais wa Marekani Donald Trump alithibitisha kuhusika kwa nchi yake kupitia video ya dakika nane iliyochapishwa kwenye mtandao wa Kijamii wa Truth Social. Kufikia Jumamosi jioni, Trump alithibitisha kwamba mashambulizi hayo yamemuua Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei na maafisa wengine kadhaa wakuu.
Siku ya Jumapili: Iran ilianzisha mashambulizi makubwa ya kulipiza kisasi dhidi ya Israeli na washirika wa Marekani katika Ghuba. Mashambulizi haya yalilenga UAE, Kuwait, Bahrain, Qatar na Oman.
Siku ya Jumatatu: Operesheni ya Israel ilipanuka hadi Lebanon, huku Jeshi la Ulinzi la Israel likisema linailenga Hezbollah, kundi linaloungwa mkono na Iran. Gharama ya kiuchumi ya vita pia ilionekana wazi siku hiyo, huku bei ya mafuta ikipanda na hisa za ndege zikishuka.
Siku ya Jumanne: ripoti ziliibuka kuhusu kiwango cha uharibifu ndani ya Iran, huku mwandishi mmoja wa habari ndani ya nchi hiyo akisema "kila sehemu" ya mji mkuu, Tehran, imeathiriwa.
Siku ya Jumatano: Mzozo huo - ambao kwa kiasi kikubwa unatumia anga - ulienea hadi baharini, huku Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth akitangaza kwamba Marekani imezamisha "meli ya kivita ya Iran" katika Bahari ya Hindi.
Siku ya Alhamisi: Mzozo huo uliongezeka tena, huku wizara ya mambo ya nje ya Azerbaijan ikisema ndege mbili zisizo na rubani za Iran zilishambulia nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege.
Leo Ijumaa: Wakazi wa Tehran wanasema mashambulizi ya Israel na Marekani yanaendelea hadi sasa - huku Marekani ikisema mashambulizi yataongezeka kuzidi.
Polisi yathibitisha shambulio na utekaji nyara katika jimbo la Borno Nigeria

Chanzo cha picha, AP
Polisi wa Nigeria wameithibitishia BBC kwamba watu kadhaa kutoka jamii ya Ngoshe katika jimbo la Borno, Nigeria wameuawa na wengine kutekwa nyara na wanaume wenye silaha.
Msemaji wa polisi katika Jimbo la Borno, Nahum Daso Kenneth, ameimbia BBC siku ya Ijumaa kwamba shambulio hilo lilitokea Jumatano usiku lakini akasema bado hawezi kuthibitisha idadi ya watu walioathirika.
Amesema, "operesheni ya utafutaji na uokoaji inaendelea.”
Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kwamba wanamgambo wamewateka nyara zaidi ya wanawake na watoto 100 wakati wa shambulio hilo.
Ripoti zinasema washambuliaji hao pia walilenga kambi ya kijeshi iliyo karibu na kambi ya watu waliokimbia makazi yao katika eneo hilo, na kuwaua wanajeshi kadhaa na raia, wakiwemo mkuu wa kijiji hicho na baadhi ya wazee.
Umaru Yakubu Kirawa, mwandishi wa habari wa eneo hilo huko Borno, ameiambia BBC wakazi wamethibitisha watu wengi wameuawa na mamia wametekwa nyara.
Ngoshe ni jamii yenye Waislamu wengi, na inaripotiwa kwamba shambulio hilo lilitokea usiku huku watu wengi wakifungua mfungo wao wa Ramadhani.
Kwa miaka mingi, Jimbo la Borno limekuwa kitovu cha uasi wa Kiislamu nchini Nigeria, huku kukiwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa Boko Haram na wapiganaji wa Kiislamu wa kundi la Dola la Kiislamu Afrika Magharibi (Iswap).
Boko Haram ilipata umaarufu duniani mwaka 2014 baada ya kuwateka nyara zaidi ya wasichana 200 wa shule kutoka Chibok katika jimbo hilo.
Pia unaweza kusoma:
Daktari afanya upasuaji kwa kutumia roboti kwa mgonjwa aliye umbali wa maili 1,500

Chanzo cha picha, PA
Daktari bingwa wa upasuaji huko London anasema amefanya upasuaji wa kwanza wa roboti wa masafa marefu nchini Uingereza kwa mgonjwa aliyeko umbali wa maili 1,500 (kilomita 2,400) huko Gibraltar.
Daktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo Profesa Prokar Dasgupta amesema alijihisi "kama yupo karibu na mgonjwa" alipokuwa akifanya operesheni ya tezi dume kwa Paul Buxton.
Mgonjwa huyo wa saratani, mwenye umri wa miaka 62, anasema "halikuwa jambo la kawaida" kushiriki "sehemu ya historia ya matibabu."
Inatumainiwa kwamba upasuaji kwa kutumia roboti utaweza kuwaepushia wagonjwa wa siku zijazo na "gharama kubwa na usumbufu" wa kusafiri kwa matibabu, na kusaidia kutoa huduma bora za afya kwa watu walio katika maeneo ya mbali zaidi.
Madaktari bingwa wa upasuaji wa Uingereza wameshiriki kwa mafanikio makubwa ya upasuaji wa kutumia njia ya mtandao, ikiwa ni pamoja na upasuaji wa kutumia roboti katika umbali wa maili 4,000.
Buxton anasema anajisikia vizuri sana" kufuatia upasuaji huo wa tarehe 11 Februari.
Operesheni hiyo ilifanywa kutoka The London Clinic kwa kutumia roboti iliyo na kamera ya 3D HD na mikono minne, yote ikidhibitiwa kupitia rimoti ambayo inapeleka mawasiliano chini ya sekunde 0.06.
Rimoti hiyo nchini Uingereza iliunganishwa na roboti huko Gibraltar kupitia kebo za nyuzinyuzi, kwa kutumia mfumo wa 5G.
Timu ya madaktari huko Gibraltar ilibaki ikiwa tayari ikiwa roboti ingeshindwa, lakini roboti hiyo ilifanya mchakato wote.
Operesheni hiyo ilitumia Mfumo wa Roboti wa Toumai, kwa ushirikiano kati ya Kliniki ya London na Mamlaka ya Afya ya Gibraltar.
Hili ni jaribio la kwanza kati ya majaribio mawili, la pili lilihusisha mwanaume mwenye umri wa miaka 52 tarehe 4 Machi, pia huko Gibraltar.
Dasgupta atafanya upasuaji kama huo tena tarehe 14 Machi, ambao utarushwa moja kwa moja kwa madaktari bingwa 20,000 wa upasuaji wa mfumo wa mkojo duniani katika mkutano wa Chama cha Ulaya cha Mfumo wa Mkojo.
Huduma ya Kitaifa ya Matibabu ya Uingereza (NHS) inatoa kipaumbele upasuaji unaosaidiwa na roboti, ikilenga kufanya operesheni 500,000 zinazotumia roboti kila mwaka ifikapo mwaka 2035.
Pia unaweza kusoma:
Trump asema ni 'kupoteza muda' kutuma wanajeshi wa ardhini wa Marekani nchini Iran

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Marekani Donald Trump ameiambia NBC News, kwamba itakuwa ni "kupoteza muda" kwa sasa kutuma wanajeshi wa Marekani nchini Iran, na si jambo analofikiria kwa sasa.
"Ni kupoteza muda. Wamepoteza kila kitu. Wamepoteza jeshi lao la wanamaji. Wamepoteza kila kitu," alisema Trump siku ya Alhamisi.
Aliongeza kuwa kauli ya awali ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi kwa NBC kwamba Iran iko tayari ikiwa kutakuwa na uvamizi wa ardhini wa Marekani au Israel ni "matamshi yasiyo na maana.”.
Trump pia amesema anataka "kusafisha" muundo wa sasa wa uongozi wa Iran.
"Tunataka wawe na kiongozi mzuri. Tuna watu ambao nadhani wangefanya kazi nzuri," amesema, bila kumtaja mtu yeyote.
Kocha wa Morocco ajiuzulu huku Kombe la Dunia likikaribia

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Aliyekuwa Kocha wa Morocco Walid Regragui Kocha wa Morocco Walid Regragui amejiuzulu nafasi yake siku ya Alhamisi, ikiwa imebaki miezi mitatu tu kabla ya fainali za Kombe la Dunia huku akisema timu hiyo inahitaji mwongozo mpya.
Uamuzi huo ulikuwa unatarajiwa kwa wiki kadhaa lakini umethibitishwa katika mkutano na waandishi wa habari usiku ambapo Regragui alisema timu hiyo "inataji maono mapya na nguvu tofauti."
"Uamuzi wangu wa kuondoka ni kwa ajili ya timu," amesema Regragui, ambaye aliipeleka Morocco kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia huko Qatar 2022 na pia alikuwa kocha mwezi Januari walipopoteza katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Senegenal.
Mohamed Ouahbi atachukua nafasi yake, rais wa Shirikisho la Soka la Morocco, Fouzi Lekjaa, alisema katika mkutano huo huo na waandishi wa habari. Ouahbi mzaliwa wa Ubelgiji alikuwa meneja wakati Morocco iliposhinda Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 20 nchini Chile mwaka jana.
Regragui mwenye umri wa miaka 50 alikosolewa na mashabiki licha ya rekodi nzuri ya ushindi mara 36 katika mechi 49, sare nane na kupoteza mara tano pekee tangu alipochukua nafasi hiyo Septemba 2022.
Regragui alitaka kujiuzulu baada ya Morocco kupoteza fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Senegal mwezi Januari, lakini alishawishika kuahirisha uamuzi wake hadi Morocco itakapoamua mrithi.
Morocco itacheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa baadaye mwezi huu huku ikijiandaa kwa Kombe la Dunia, litakaloanza Juni. Watacheza dhidi ya Ecuador jijini Madrid Machi 27 na Paraguay jijini Lens, Ufaransa siku nne baadaye.
Katika Kombe la Dunia, Morocco itashiriki Kundi C pamoja na Brazil, Scotland na Haiti.
Pia unaweza kusoma:
Wanajeshi wa mpakani wa Pakistan na Afghanistan washambuliana, huku raia 100,000 wakikimbia makwao

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Watoto wa Afghanistan waliokimbia makazi yao, pamoja na familia zao, kufuatia mapigano kati ya vikosi vya Pakistan na Afghanistan, wamekaa nje ya hema lao la muda huko Lal Pur katika jimbo la Nangarhar mashariki, Afghanistan Wanajeshi wa Pakistan na Afghanistan wamefyatuliana risasi katika maeneo kadhaa siku ya Ijumaa huku Umoja wa Mataifa ukisema mzozo wao wa wiki moja umelazimisha watu zaidi ya 100,000 kuhama makazi yao.
Mataifa hayo ya Asia Kusini hayaonyeshi dalili zozote za kuacha mapigano ambayo ni mabaya zaidi kuwahi kutokea kwa miaka mingi, na kuongeza hali tete katika eneo hilo ambalo pia linakumbwa na mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran - taifa linalopakana na Afghanistan na Pakistan.
Mapigano yamejumuisha mashambulizi ya anga ya Pakistani kwenye vituo vya serikali ya Taliban, kama vile kambi ya anga ya Bagram kaskazini mwa mji mkuu wa Afghanistan Kabul.
Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan imesema vikosi vya Taliban vilishambulia vituo vya kijeshi vya Pakistani kando ya mpaka wa kilomita 2,600 (maili 1,600), na kuharibu vituo vingi na kuangusha ndege isiyo na rubani.
Vyanzo vya usalama vya Pakistani vimesema wamefanya operesheni za ardhini na angani dhidi ya maeneo ya kijeshi ikiwemo Kandahar, kitovu cha Taliban na mahali ambapo uongozi wake mkuu upo, na kuharibu vituo kadhaa vya mpaka wa Afghanistan.
Watu kadhaa walikusanyika Kabul siku ya Ijumaa kupinga mashambulizi ya Pakistan katika eneo la Afghanistan, wakiimba kuilaani Pakistan, kwa mujibu wa Shirika la habari la Bakhter.
Watu wanaoishi katika miji ya mpakani wameiambia Reuters kwamba wanajeshi huanza kurusha makombora mengi baada ya jua kutua, huku familia zikikaa kitako kwa ajili ya kufungua mfungo wao katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
"Hali nchini Afghanistan na Pakistani bado ni tete huku kukiwa na migogoro inayoendelea mpakani," limesema shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, na kuongeza kuwa takriban watu 115,000 nchini Afghanistan na 3,000 nchini Pakistani wamekimbia makwao.
Pia unaweza kusoma:
Iran haina intaneti kwa siku sita sasa - Netblocks

Chanzo cha picha, Reuters
Iran imekosa intaneti kwa siku sita kamili, linasema kundi huru la ufuatiliaji wa intaneti la NetBlocks.
Kundi hilo linasema nchi hiyo inapata intaneti kwa 1% katika saa 144.
Kuzimwa kwa intaneti ni mojawapo ya mambo yanayofanya iwe vigumu kwa mashirika ya habari ya kimataifa kuripoti kuhusu kinachoendelea ndani ya Iran.
Iran pia ilikata huduma za intaneti wakati wa maandamano ya kupinga serikali mapema mwaka huu.
Tajiri wa Hong Kong Jimmy Lai hatakata rufaa dhidi ya hukumu ya miaka 20 jela

Chanzo cha picha, AFP kupitia Getty Images
Maelezo ya picha, Jimmy Lai, kama anavyoonekana katika picha iliyopigwa muda mfupi kabla ya kukamatwa kwake mwaka 2020 Tajiri wa Hong Kong anayeunga mkono demokrasia Jimmy Lai, ambaye yuko gerezani, hakata rufaa dhidi ya hukumu yake chini ya sheria tata ya usalama wa taifa ya jiji hilo.
Watu kutoka timu yake ya wanasheria wa kimataifa wameiambia BBC kuwa wenzao wa ndani wamepewa maagizo "yaliyo wazi" kutoka kwa Lai ya kutokata rufaa. Hawakusema ni kwa nini, na wamekataa kutoa maoni zaidi.
Lai na watu wengine walihukumiwa kwa kula njama ya kuchapisha maudhui ya uchochezi na kula njama ya kushirikiana na raia wa kigeni - mashtaka ambayo ameyakanusha – na amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela mwezi uliopita.
Tajiri huyo pia alikutwa na hatia ya ulaghai, ambayo ilibatilishwa mwezi uliopita katika rufaa iliyofanikiwa.
Kesi kuhusu usalama wa taifa dhidi ya Lai ilitokana na mkutano alioufanya na makamu wa rais wa Marekani Mike Pence na waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo wakati wa maandamano ya kuunga mkono demokrasia mwaka 2019.
Lai amesisitiza kwamba hajawahi kutumia kujuana kwake na raia wa kigeni ili kubadilisha sera za kigeni za Hong Kong, na mkutano huo ulijadili tu hali ilivyokuwa Hong Kong wakati huo.
Kifungo chake cha miaka 20 ni adhabu kali zaidi kutolewa chini ya sheria ya usalama wa taifa, ambayo China iliiweka baada ya maandamano ya 2019.
Lai, raia wa Uingereza, ndiye mtu maarufu zaidi kati ya mamia waliokamatwa chini ya sheria hiyo. Ni mkosoaji wa China, na mara nyingi alitumia gazeti lake, Apple Daily, kama chombo cha ukosoaji.
Mkuu wa Hong Kong, John Lee, amepongeza hukumu hiyo, akisema "matendo maovu ya Lai yalipita kiasi" na gazeti lake limewashawishi vijana wengi wa Hong Kong kushiriki katika maandamano hayo.
Lakini makundi ya haki za binadamu na mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk wamelaani hukumu hiyo, huku Turk akisema hukumu hiyo inapaswa "kufutwa mara moja kwa kuwa haiendani na sheria za kimataifa."
Mwanawe Lai, Sebastien, amesema ni "hukumu ya kifo" kwa baba yake mwenye umri wa miaka 78 ambaye amekuwa gerezani tangu 2020.
Wanafamilia wa Jimmy Lai wanasema afya yake imezorota kiasi kwamba kucha zake wakati mwingine hutoka na meno yake kuoza.
Hong Kong imekanusha vikali madai yote ya hali mbaya ya maisha gerezani na kusema yuko katika hali nzuri ya afya.
Wakosoaji wanasema sheria ya usalama wa taifa iliyowekwa na Beijing imetumika katika ukandamizaji na imesababisha hali ya hofu.
Beijing na Hong Kong zinasema sheria hii n muhimu ili kudumisha utulivu na zinakana kwamba imedhoofisha uhuru wa jiji.
Pia unaweza kusoma:
Wanne wakamatwa Uingereza kwa tuhuma za kuisaidia idara ya ujasusi ya Iran

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Watu wanne wamekamatwa kama sehemu ya uchunguzi wa kupambana na ugaidi unaohusishwa na Iran, wamesema Polisi wa Jiji la London.
Polisi walimkamata raia mmoja wa Iran na watatu wa Uingereza na Iran kwa tuhuma za kusaidia huduma ya ujasusi ya nchi ya kigeni.
Ukamataji huo unahusiana na ufatiliaji unaoshukiwa kufanyika katika maeneo na watu binafsi wanaohusishwa na jamii za Kiyahudi jijini London, wamesema polisi.
Kamanda Helen Flanagan, mkuu wa Idara ya Kupambana na Ugaidi ya London, amesema kukamatwa kwa watu hao ni sehemu ya "uchunguzi wa muda mrefu na sehemu ya kazi yetu inayoendelea ya kuvuruga shughuli ovu pale tunaposhuku."
Aliongeza: "Tunaelewa kuwa umma unaweza kuwa na wasiwasi, haswa jamii ya Wayahudi, na kama kawaida, ningewaomba waendelee kuwa macho na ikiwa wataona au kusikia chochote kinachowahusu, basi wawasiliane nasi."
Akizungumza na ITV's Good Morning Britain muda mfupi baada ya habari kusambaa kuhusu kukamatwa kwa watu hao, Naibu Waziri Mkuu David Lammy alisema: "Iran ndiyo mfadhili mkuu wa ugaidi duniani kote na kwa bahati mbaya, hilo linaathiri pia jamii yetu."
Mwanaume wa miaka 40 na mwanaume wa miaka 55 walikamatwa huko Barnet, mwanaume wa miaka 52 huko Watford na mwanaume wa miaka 22 huko Harrow.
Wanaume hao wanne walikamatwa chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa, ambayo ilianzishwa mwaka 2023 ili kuboresha sheria za upelelezi wa kukabiliana na ujasusi, na kupambana na uingiliaji kati wa kigeni.
Wanaume wengine sita wenye umri wa miaka 29, 39, 42, 49 na wawili wenye umri wa miaka 20, walikamatwa huko Harrow kwa tuhuma za kumsaidia mtuhumiwa.
Wanaume wote 10 wamekamatwa.
Pia unaweza kusoma:
Wakaazi wa Tehran waelezea 'milipuko ya mara kwa mara' inavyowakosesha usingizi

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
"Nyumba ilitikisika kwa dakika tano mfululizo. Jana usiku hali ilikuwa mbaya sana," anasema mwanamume aliye na umri wa miaka 30 na mkaazi wa Tehran alipoulizwa na mwandishi wa BBC hali ilivyo huko.
Anasema hali jana ilikuwa mbaya sana. Nilishindwa kulala kutokana na "milipuko ya mara kwa mara."
Mpaka sasa ni vigumu kuwasiliana na watu walio ndani ya Iran huku baada ya mtandao wa mawasiliano kukumbwa na hitilafu nchini humo. Hata hivyo baadhi ya watu wameweza kuunganishwa kwa muda mfupi.
BBC haifichui utambulisho wa wale wanaozungumza na waandishi wake, ili kulinda usalama wao.
"Niliamka baada ya kusikia milipuko saa kumi na moja asubuhi na sijaweza kulala tangu wakati huo," ana sema mwanamke mmoja katika mji mkuu huo. "
Hali ilikuwa mbaya sana. Walikuwa wakishambulia sana kiasi kwamba madirisha yote yalikuwa yakitikisika," mwanamke mwingine anasema.
Pia unaweza kusoma:
Air Tanzania kuwarejesha nyumba Watanzania waliokwama Dubai

Chanzo cha picha, Air Tanzania
Shirika la ndege la Tanzania, Air Tanzania limetangaza mpango wa kuwarejesha nyumbani raia wa nchi hiyo walioathiriwa na hatua ya kusitishwa kwa safari za ndege kufuatia mgogoro uliozuka eneo la Mashariki ya Kati baada ya Marekani na Israel kuishambulia Iran na kumuua Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei Jumamosi iliyopita.
Katika taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Machi 6, Air Tanzania imesema ndege hiyo maalum itasafiri kutoka Dar es Salam kuelekea Dubai na kurejea Dar es Salaam siku ya Jumapili.
Imesisitiza ndege hiyo sio ya kibiashara na kuongeza kwamba itawapatia kipaumbele wasafiri ambao walikuwa wamekata tiketi kabla ya safari kusitishwa.
Mashirika ya ndege ya kimataifa yalikiahirisha safari za kuelekea Mashariki ya Kati tangu Iran ilipoanza kulipiza kisasi hatua ya Marekani na Israel dhidi yake kwa kushambulia kambi za jeshi la Marekani zilizo katika mataifa ya Kiarabu katika eneo hilo.
Ndege zinazoingia na kutoka katika viwanja vya ndege vya Tel Aviv, Dubai, Doha na vituo vingine vya kimataifa katika eneo hilo zimesitishwa.
Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza inawashauri raia wa Uingereza dhidi ya safari zote za kwenda Bahrain, Kuwait, Qatar na Falme za Kiarabu (UAE).
Wale ambao tayari wapo katika maeneo hayo wameshauriwa kuwa makini.
Iran imefanya mashambulizi katika mataifa ya Ghuba kama sehemu ya kulipiza kisasi mashambulizi ya Marekani na Israel yaliyoanza mapema Jumamosi.
Usafiri wa mbali umeathiriwa zaidi, huku Heathrow ikiwaomba wasafiri kuthibitisha safari zao na mashirika yao ya ndege.
Maelezo zaidi:
China na Iran zinajadiliana kuhusu njia salama kwa meli za mafuta- ripoti

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mlango wa Bahari wa Hormuz China inajadiliana na Iran kuziruhusu meli zinazosafirisha mafuta ghafi na gesi ya Qatar kupitia mlango wa Bahari wa Hormuz, Reuters imeripoti Alhamisi, ikinukuu vyanzo ambavyo haikutaja
Mgogoro kati ya Marekani na Israel na Iran ambao sasa umeingia siku ya saba umeathiri mamia ya meli zilizotia nanga karimu na kivuko hicho ambacho ni njia kuu ya usafiri duniani na kusababisha bei ya mafuta kupanda.
Reuters na Bloomberg zilinukuu data ya kufuatilia meli iliyoonyesha meli ya mafuta inayodai kuwa ya Kichina ilipitia mkondo huo siku ya Alhamisi, ingawa BBC haijaweza kuthibitisha mienendo yake.
China ni mnunuzi mkubwa wa mafuta ya Iran na imelaani mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya nchi hiyo.
Maelezo zaidi:
Marekani na Venezuela yarejesha uhusiano wa kidiplomasia baada ya Maduro kukamatwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodriguez na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Marekani Doug Burgum walikubaliana kufanya kazi pamoja kuendeleza shughuli ya uchimbaji madini nchini Venezuela wiki hii. Marekani na Venezuela zimekubaliana kurejelea tena uhusiano wa kidiplomasia na kibalozi.
Taarifa zinasema pande hizo mbili zitafanya juhudi za pamoja ili kukuza utulivu, kuunga mkono ufufuaji wa uchumi na kuendeleza maridhiano ya kisiasa.
Wakati uhusiano wao wa kidiplomasia umekuwa ukiimarika tangu jeshi la Marekani lilipomkamata Rais wa Venezuela Nicolás Maduro mwezi Januari katika shambulio la kushtukiza, kutangazwa kwa uhusiano rasmi wa nchi hizo mbili kunaashiria hatua kubwa.
Rais Donald Trump aliamuru wanajeshi kumkamata Maduro na mkewe, na kuwafikisha katika mahakama ya Manhattan kujibu mashtaka ya kutumia silaha na dawa za kulevya, madai ambayo wanayakanusha.
Ubalozi wa Marekani mjini Caracas, uliofungwa mwaka 2019, tayari umefunguliwa tena, na Washington imemteua mwanadiplomasia mpya nchini Venezuela.
Hapo jana (Alhamisi) serikali ya Venezuela ilisema iko tayari kuendeleza "hatua mpya ya mazungumzo yenye tija, kwa msingi wa kuheshimiana".
Ilisema uhusiano huo lazima uwe na "manufaa ya kijamii na kiuchumi kwa watu wa Venezuela".
Vyanzo vya habari viliiambia BBC kwamba wafanyakazi zaidi wa kidiplomasia kutoka ubalozi wa Marekani huko Bogotá, Colombia, wanatarajiwa kupelekwa mjini Caracas hivi karibuni.
Hatua hiyo itarahisisha zaidi maafisa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na kutoa huduma za kibalozi.
Soma pia:
Ukraine yaishutumu Hungary kwa kuwateka raia wake saba

Chanzo cha picha, Re
Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andrii Sybiha Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine ameishutumu Hungary kwa kuwashikilia mateka wafanyakazi saba wa benki ya serikali ya Ukraine huko Budapest.
Andrii Sybiha amechapisha kwenye mtandao wa X, kuwa Waukraine hao walikuwa safarini kupitia Hungary kwa gari wakibeba fedha kutoka Austria kwenda Ukraine, wakati walipokamatwa.
Amesema hadi sasa haijulikani mahali walipo wala sababu za kukamatwa kwao hazijulikani, na kuishutumu Hungary kwa kuiba fedha na ugaidi unaofanywa na serikali.
Hungary - ambayo ina uhusiano wa karibu na Urusi - bado haijatoa tamko lolote.
Hapo awali, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alimkosoa Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban kwa kuzuia msaada wa Ulaya kwa Kyiv.
Orban ameishutumu Kyiv kwa kuweka "kizuizi cha mafuta" kwa Hungary na kuchelewesha makusudi kufunguliwa tena kwa bomba la Druzhba.
Maelezo zaidi:
Hezbollah yawataka raia wa Israel kuondoka karibu na mpaka wa Lebanon

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Israel imefanya mashambulizi zaidi ya 1,000 ya anga dhidi ya Lebanon katika muda wa siku mbili zilizopita Kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran linawataka raia wa Israel wanaoishi miji iliyo umbali wa kilomita 5 kutoka mpaka wa Lebanon kuondoka.
Onyo hilo limewekwa katika ujumbe kwenye chaneli yake ya Telegraph kwa Kiebrania mapema Ijumaa, kulingana na shisrika la habari la Reuters.
"Uvamizi wako wa kijeshi dhidi ya mamlaka ya Lebanon na raia wake, uharibifu wa miundombinu ya kiraia na kampeni ya kuwafukuza raia hautapita bila kupingwa," Hezbollah ilisema.
Jeshi la Ulinzi la Israel, IDF, lilianza wimbi la mashambulizi dhidhi ya Lebanon ya Alhamisi jioni, baada ya kuwaambia watu waondoke maeneo ya kusini mwa mji mkuu wa Beirut, ambayo ni ngome ya Hezbollah.
Muda mfupi uliopita, IDF pia ilisema imeanza "wimbi kubwa la mashambulizi dhidi ya miundombinu ya utawala wa kigaidi wa Iran mjini Tehran".
Maelezo zaidi:
Marekani yazamisha zaidi ya meli 30 za kivita za Iran

Chanzo cha picha, White House
Kamanda wa Kamandi Kuu ya Marekani, Admiral Brad Cooper, anasema kuwa Marekani imezamisha zaidi ya meli 30 za Iran kufikia sasa.
Aliongeza, "Katika saa chache tu zilizopita, tuliishambulia meli ya kubeba ndege zisizo na rubani ya Iran ambayo ukubwa wake ni sawa na ile iliyobeba ndege za kivita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Sasa inawaka moto."
Cooper amesema kuwa Marekani imeshambulia kwa mabomu takriban maeneo 200 nchini Iran katika muda wa saa 72 zilizopita.
Huku hayo yakijiri afisa wa Ikulu ya White House ameithibitishia BBC kwamba maafisa wa utawala wa Trump wanapanga kukutana na wasimamizi wa ulinzi wa Marekani leo Ijumaa, kujadili utengenezaji wa silaha.
Mkutano huo utafanyika katika Ikulu ya White House na utahudhuriwa na kampuni kama vile Lockheed Martin & RTX, kampuni mama ya Raytheon, shirika la habari la Reuters liliripoti hapo awali.
Majadiliano yanatarajiwa kujumuisha kuongeza kasi ya utengenezaji wa silaha, huku Pentagon ikiwa mbioni kujaza tena hifadhi yake silaha ya baada ya shambulio dhidi ya Iran kulingana na Reuters.
Katika mkutano na waandishi wa habari muda mfupi uliopita, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth alisema Marekani ina silaha nyingi na inaweza kuendeleza operesheni yake dhidi ya Iran hadi itakapofikia lengo lake.
Pia unaweza kusoma:
Marekani yasema 'kiwango cha mashambulizi dhidi ya Iran kitaongezeka' huku Israel ikishambulia Beirut na Tehran

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa wa Marekani Donald Trump na Waziri wake wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth wameikosoa hatua ya Uingereza kwa kukataa vituo vyake vya kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati kutumiwa kuishambulia Iran.
Trump hapo awali aliangazia kile kinachoendelea nchini Iran katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House.
Kwa upande wake Hegseth alisema kwa "bahati mbaya "Uingereza ilikataa ombi letu "kutoka siku ya kwanza".
"Lakini tulifikia lengo letu. Tulifika huko, na hiyo sasa ni sehemu ya mpango ambao tunatumia kufanya mashambulizi ya angani...Ni vikosi zaidi vya wapiganaji, ni uwezo zaidi, ni uwezo wa kujilinda zaidi, na ni mashasmbulizi ya mara kwa mara," alisema.
"Kiwango mashabulizi dhidi ya Iran na Tehran kinakaribia kuongezeka kwa kasi," alisema.
Hegseth pia alisema Marekani na Israel zinawalenga wale waliokuwa wakiwakandamiza waandamanaji nchini Iran.
"Kadiri unavyofanya hivyo zaidi, kuharibu nia na uwezo wao, ndivyo unavyotengeneza fursa kwa watu kusimama kwa ujasiri," Hegseth alisema.
Melezo zaidi:
