Balozi wa Iran nchini Uingereza asema Iran itajilinda dhidi ya uchokozi

Kuli hiyo inakuja wakati huu rais wa Iran akiomba radhi na kuahidi kutoshambulia mataifa Jirani,balozi huyo amesema sera ya nchi yake ni kujilinda.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Rais Ruto atuma vikosi vya dharura kufuatia mafuriko yaliyoua watu 25 Nairobi

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Kenya William Ruto ameagiza kupelekwa mara moja kwa kikosi cha dharura kutoka taasisi mbalimbali kusaidia juhudi za uokoaji kufuatia mafuriko ya ghafla yaliyosababisha vifo kadhaa katika jiji kuu la Nairobi.

    Mamlaka zinasema watu 25 wamefariki dunia baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

    Mapema Jumamosi, wahudumu wa misaada walionekana wakitoa miili ya watu kutoka kwenye maji katika sehemu tofauti za Nairobi baada ya mvua hizo kubwa.

    Mafuriko yalizoa makumi ya magari, baadhi ya nyumba na pia kuathiri safari za ndege katika uwanja mkubwa wa ndege wa Afrika Mashariki, Jomo Kenyatta.

    Shirika la ndege la Kenya Airways lilitangaza kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba baadhi ya safari za ndege zililazimika kubadilisha uelekeo wa safari kutoka Nairobi kwenda mji wa pwani wa Mombasa kutokana na mvua hizo.

    Kwa mujibu wa shirika la msalaba mwekundu la Kenya, mbali na Nairobi, mafuriko pia yameripotiwa katika kaunti ya Kisumu baada ya mto kufurika na kuvunja kingo zake.

    Jumla ya kaya 381 zimeathirika, huku nyumba na mashamba yakifunikwa na maji.

    Wakati huo huo, Idara ya hali ya hewa ya Kenya imetabiri kuwa mvua kubwa zitaendelea kunyesha mwishoni mwa wiki hii.

    Ripoti ya mwaka 2024 kutoka taasisi ya kimataifa inayofuatilia mabadiliko ya tabia nchi imebaini kuwa ongezeko la joto duniani linachangia kiwango cha mvua kuwa kikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, hali inayosababisha mafuriko wakati wa msimu wa mvua kuwa mara mbili zaidi ya hapo awali.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Waandamanaji wanaopinga vita nchini Iran wakusanyika nje ya ubalozi wa Marekani jijini London

    xcv

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelfu ya waandamanaji wanaopinga vita nchini Iran wameelekea kwenye ubalozi wa Marekani huko London. Wengi wao wanapiga kelele huku wameshikilia mabango yanayomkashifu Rais Donald Trump.

    Waandaaji wanasema kwamba maandamano haya sio kuunga mkono serikali ya Iran, bali ni wito wa kumaliza kile wanachokiita “vitendo visivyo halali, visivyo na msingi na wala haki.” Wanasema kwamba Uingereza haipaswi kufuata upuuzi wa viongozi wa Marekani, na kwamba hakuna msingi wowote wa kushambulia ili kuleta mabadiliko ya serikali.

    Hayo yanajiri wakati huu rais wa Marekani Donald Trump akisema kuwa Marekani inaendelea kufanya vizuri katika operesheni zake dhidi ya Iran.

    Katika hotuba yake, alisema majeshi ya Marekani yamefanikiwa kuharibu meli 42 za kijeshi za Iran ndani ya siku tatu.

    Trump alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na nguvu na uwezo mkubwa wa majeshi ya Marekani.

    Katika hotuba hiyo, Trump pia alizungumzia askari wa Marekani waliopoteza maisha katika mapigano hayo.

    Alisema mara tu baada ya hotuba hiyo angeenda kukutana na familia za wanajeshi hao waliofia vitani, ili kutoa rambirambi na heshima kwa mchango wao kwa taifa.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Balozi wa Iran nchini Uingereza asema Iran itajilinda dhidi ya uchokozi

    XCV

    Chanzo cha picha, Reuters

    Balozi wa Iran nchini Uingereza Seyed Ali Mousavi ameiambia BBC kwamba Itaendelea kujilinda dhidi ya Marekani na Israel ikiwa zitaendeleza uchokozi.

    Katika mahojiano maalum na BBC balozi Mousavi aliulizwa iwapo Iran itakomesha mashambulizi yake dhidi ya kambi za kijeshi katika maeneo mengine ya mashariki ya kati.

    Amesema kuna utayari kutoka upande wa Iran kutoshambulia majirani zake.

    Kuli hiyo inakuja wakati huu rais wa Iran akiomba radhi na kuahidi kutoshambulia mataifa Jirani,balozi huyo amesema sera ya nchi yake ni kujilinda.

    Aidha anaongeza: "inategemea na hatua za Wamarekani na mamlaka ya Israeli. Ikiwa uchokozi ... utaendelea bila shaka tutajilinda. Na ikiwa wanataka kutumia vituo hivi vya kijeshi, ingawa hatutaki kufanya hivyo, hakuna shaka tutajilinda ipasavyo".

    Anasema kwamba vituo, mali au vifaa vinavyolenga Iran vitachukuliwa kuwa "maeneo halali ya kulengwa".

    Pia unaweza kusoma:

  4. Iran yarusha makombora nchini Israel- lasema jeshi la Israel

    xcv

    Chanzo cha picha, Reuters

    Jeshi la Israel linasema limegundua makombora yaliyorushwa kutoka Iran kuelekea Israel.

    "Mifumo ya ulinzi inafanya kazi ili kuzuia tishio hilo," IDF inasema, ikiongeza kuwa hatua za tahadhari zimetangazwa zikiwaagiza wakazi kukaa katika maeneo salama yaliyotengwa.

    Katika hatua nyingine wizara ya ujasusi ya Iran inaonya kwamba itachukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote anayechapisha picha au video za maeneo yaliyoshambuliwa katika mashambulizi ya Marekani na Israel.

    Katika taarifa yake, wizara hiyo imesema kuwa watu wanaopiga picha za maeneo yaliyoathiriwa na kisha kuzituma kwenye mitandao ya satelaiti inayodaiwa kuwa ya kigaidi, kurasa za mtandaoni, au vyombo vya habari vinavyodaiwa kuwa vya maadui wanachukuliwa kama “mamluki” wanaofanya kazi kwa niaba ya Israel.

    Wizara hiyo imeongeza kuwa itafuatilia kwa karibu vitendo vya watu hao waliowaita “vibaraka wa Israel”, na kwamba watachukuliwa hatua za kisheria.

    Pia imewataka wananchi kuripoti mara moja mtu yeyote anayefanya shughuli za kupiga au kusambaza picha za maeneo yaliyolengwa na mashambulizi hayo.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Idadi ya waliopoteza maisha kutokana na mafuriko Kenya yafikia 23

    xcv

    Polisi jijini Nairobi wamesema watu 23 wamefariki dunia kufikia sasa,huku uharibifu wa mali, kufungwa kwa baadhi ya barabara pamoja na wakazi wengi kulazimika kuhama makazi yao kutokana na hali hiyo.

    Aidha zoezi la uokoaji bado linaendelea kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku kucha na kusababisha mafuriko makubwa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

    Taarifa ya polisi inaeleza kwamba watu 29 waliokolewa kutoka maeneo mbalimbali na kwa sasa wanapokea msaada unaohitajika.

    Vikosi vya uokoaji bado vimeendelea kuwepo katika maeneo yaliyoathirika zikijibu simu za dharura na kuendeleza operesheni za utafutaji na uokoaji.

    Mamlaka zinaendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu ili kuhakikisha usalama na ustawi wa wananchi , wakazi na raia wa kigeni.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Ghana yataka uchunguzi wa UN baada ya wanajeshi wake kujeruhiwa Lebanon

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ghana imewasilisha rasmi malalamiko kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, baada ya shambulio kusini mwa Lebanon kuwajeruhi wanajeshi wake wawili wa kulinda amani.

    Waziri wa Mambo ya nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, amesema serikali inadai uchunguzi kamili, wa haraka, usio na upendeleo na wa wazi kuhusu tukio hilo.

    Amesema shambulio hilo linakiuka sheria za kimataifa na linaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.

    Wanajeshi hao wa Ghana wako nchini Lebanon kama sehemu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kinachoitwa United Nations Interim Force in Lebanon (UNIFIL), ambacho kimepelekwa kufuatilia mpaka kati ya Israel na Lebanon.

    Kwa mujibu wa Jeshi la Ghana, makao makuu ya kikosi cha Ghana kusini mwa Lebanon yalilengwa na makombora Ijumaa jioni.

    Hadi sasa haijulikani ni nani aliyetekelezwa shambulio hilo.

    Serikali ya Ghana imelilaani vikali tukio hilo na pia imesisitiza kuwa wale wote waliohusika lazima watambuliwe na kuwajibishwa.

    Tukio hili linatokea wakati mvutano unaongezeka sana kwenye mpaka wa Israel na Lebanon. Mapigano yameongezeka kati ya jeshi la Israel na kundi la wanamgambo la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.

    Hezbollah imeanza kushambulia kaskazini mwa Israel kwa roketi na ndege zisizo na rubani karibu kila siku, ingawa Israel inasema mashambulizi hayo yanazuiwa na mifumo yake ya ulinzi wa anga.

    Wakati huo huo, Israel imetoa amri ya kuwataka watu kuhama katika baadhi ya maeneo ya kusini mwa Lebanon, umbali wa takribani kilomita 27 ndani ya nchi hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Iran haitashambulia mataifa jirani, asema rais wa Iran

    XCV

    Chanzo cha picha, IRNA

    Rais wa Iran Masoud Pezeshkian ametangaza ujumbe wa video kwenye televisheni ya taifa ya Iran akisema: “Naona ni muhimu kuomba msamaha kwa nchi jirani ambazo zilishambuliwa.”

    Amesisitiza pia kwamba Iran haina nia ya kuvamia nchi Jirani na kutaka mataifa y a ukanda huo kuhakikisha amani na utulivu.

    Pezeshkian aliongeza kuwa amri imetolewa kwa majeshi ya Iran:

    “Kuanzia sasa, msishambulie nchi jirani isipokuwa kama Iran itashambuliwa kwanza.”

    Aidha alionya kwamba: “Wale wanaofikiria kutumia fursa ya wakati huu kushambulia Iran hawapaswi kuwa vibaraka wa ubeberu.”

    Mwisho, rais huyo alisema kuwa kuunga mkono Israel au Marekani haitafsiri heshima na uhuru.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Watu 10 wafariki kwa mafuriko Nairobi

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Watu 10 wamethibitishwa kufariki jijini Nairobi kufuatia mafuriko makubwa yaliyokumba jiji hilo siku ya Ijumaa.

    Kamanda wa Polisi jijini Nairobi George Seda alisema watu nane walisombwa na maji ya mafuriko yanayoongezeka kwa kasi, huku wengine wakifariki wakiwa ndani ya magari yaliyobebwa na mkondo wa maji.

    Seda aliongeza kuwa waathiriwa wengine wawili walifariki katika matukio tofauti ya umeme wakati wa mafuriko katika sehemu tofauti za kaunti.

    Aidha ameongeza kuwa, takriban magari 71 yalikwama jijini Nairobi baada ya barabara kuu kutopitika kutokana na mafuriko makubwa.

    Kamanda Seda alionya kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka huku shughuli za utafutaji na uokoaji zikiendelea katika maeneo kadhaa yaliyoathiriwa vibaya na mafuriko.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Tumetekeleza mashambulizi zaidi ya 3,000 nchini Iran: Marekani

    cvb

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kamati ya usalama ya Marekani, ambayo inaongoza shughuli za kijeshi za nchi hiyo, inasema imetekeleza mashambulizi zaidi ya 3,000 nchini Iran.

    Meli zipatazo 43 pia zimeshambuliwa au kuharibiwa kama sehemu ya Operesheni Epic Fury, ilitangaza katika chapisho lake katika X.

    Mashambulizi hayo yanapewa kipaumbele kulingana na "maeneo ambayo yanasababisha uwezekano wa kuwa na tishio" kwa lengo la "kubomoa vifaa vya usalama vya utawala wa Iran".

    Uchambuzi wa BBC wa picha na video za setilaiti umeonyesha kuwa shule za Iran, hospitali na mengine muhimu ni miongoni mwa maeneo ya raia ambayo yameathiriwa na mashambulizi ya Marekani na Israeli.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Qatar yafungua anga kuruhusu safari chache za ndege

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Shirika la ndege la Qatar Airways linatoa huduma chache za ndege za kuwarejesha nyumbani kwenda London, Rome, Paris, Madrid na Frankfurt

    Qatar imetangaza kuanza tena kwa safari chache za ndege kwa mara ya kwanza tangu vita vilipoanza wiki moja iliyopita.

    Mamlaka ya usafiri wa anga ya nchi hiyo ilisema kuwa anga ya Qatar itafunguliwa kwa sehemu ili kuruhusu tu safari za uokoaji na ndege muhimu za mizigo.

    Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hamad umefafanua kuwa safari nyingine katika siku zijazo zitategemea tathmini inayoendelea ya hali ya usalama.

    Maafisa wa Qatar walisema mapema wiki hii kuwa jeshi lilifanikiwa kuzuia jaribio la mashambulizi ya Iran dhidi ya uwanja huo wa ndege.

    Wizara ya ulinzi iliripoti kuwa Qatar ilidungua ndege tisa zisizo na rubani siku ya Ijumaa.

    Moja ya hizo ilianguka katika eneo lisilo na watu bila kusababisha majeruhi.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Mashuhuda waripoti milipuko katika uwanja mkubwa wa ndege Tehran

    XCV

    Chanzo cha picha, AFP

    Kumeshuhudiwa shambulio kubwa katika moja ya viwanja vikuu vya ndege vya kibiashara mjini Tehran.

    Ndege inayowaka moto pamoja na moshi mkubwa unaonekana katika uwanja wa ndege wa Mehrabad, ambao ni uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi zaidi nchini Iran na kitovu kikuu cha safari za ndani.

    Hali hiyo inaonekana katika video zilizochapishwa na mashuhuda kwenye mitandao ya kijamii.

    Picha za satelaiti zilizopigwa Ijumaa zinaonyesha kuwa kulikuwa na ndege kadhaa katika uwanja huo.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran pia vinaripoti kuwa baadhi ya sehemu za uwanja wa ndege zimelengwa katika shambulio hilo.

    Tukio hili linakuja baada ya jeshi la Israel kusema kuwa linaanzisha “wimbi jipya la mashambulizi makubwa” nchini Iran.

    Hapo awali lililenga uwanja huo tarehe 4 Machi, likisema mashambulizi yake yalibomoa mifumo ya ulinzi na ilikuwa tishio kwa Jeshi la anga la Israel, ikiwemo sehemu ya kutengeneza helikopta katika uwanja huo.

    Bado haijafahamika ni sehemu gani hasa za uwanja wa ndege zimepigwa katika shambulio jipya, lakini mashuhuda wanasema mashambulizi ya usiku huu yamekuwa makali zaidi.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Trump aitaka Iran ijisalimishe bila masharti, Putin azungumza na rais wa Iran

    a

    Chanzo cha picha, Getty Images/BBC

    Rais wa Marekani Donald Trump ameitaka Iran kujisalimisha bila masharti huku mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel yakiendelea. Trump amesema baada ya Iran kuchagua uongozi mpya unaokubalika na Washington, Marekani na washirika wake wataisaidia nchi hiyo kuimarisha uchumi wake.

    Kauli hiyo imekuja wakati vita vinaingia wiki ya pili tangu kuuawa kwa kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei katika mashambulizi ya hivi karibuni. Hata hivyo bado haijulikani nani ataIongoza Iran baada ya tukio hilo.

    Ikulu ya Marekani imesema operesheni za kijeshi zinaweza kudumu kati ya wiki nne hadi sita, huku lengo likiwa kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa Iran.

    Wakati huo huo, rais wa Urusi Vladimir Putin amezungumza kwa simu na rais wa Iran Masoud Pezeshkian, akitoa pole kwa vifo vilivyotokea katika mashambulizi hayo.

    Urusi imesisitiza kuwa mapigano yanapaswa kusitishwa mara moja na kutafutwa suluhisho la kidiplomasia. Iran nayo imeishukuru Urusi kwa kuendelea kuiunga mkono.

    Wakati huo huo, mapigano yameongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati baada ya kundi la Hezbollah kushambulia Israel, huku mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora yakiripotiwa katika nchi kadhaa zenye kambi za kijeshi za Marekani.

Trending Now