Trump atangaza ushuru mpya wa 10% kujibu uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Marekani

Majaji sita walipiga kura dhidi ya ushuru huo, hatua ambayo ni pigo kubwa kwa sera ya kiuchumi ya utawala wake.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Elizabeth Kazibure

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Chama tawala Ujerumani chaunga mkono vikwazo vya mitandao ya kijamii kwa watoto

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Chama tawala cha kihafidhina nchini Ujerumani Jumamosi kilipitisha azimio la kupiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya miaka 14 na kuanzisha ukaguzi mkali zaidi wa uthibitishaji wa umri kwa vijana, hatua inayoongeza msukumo wa vikwazo kama hivyo nchini humo na kote Ulaya.

    Katika mkutano wa chama mjini Stuttgart, chama cha Kansela Friedrich Merz, Christian Democratic Union, pia kilitaka kutozwa faini kwa majukwaa ya mtandaoni yatakayoshindwa kutekeleza masharti hayo, pamoja na kuweka viwango vya umri vinavyofanana katika Umoja wa Ulaya.

    Nchi kadhaa zikiwemo Uhispania, Ugiriki, Ufaransa na Uingereza zinatazama marufuku au vikwazo kama hivyo, zikifuata mfano wa Australia ambayo mwaka jana ililazimisha majukwaa kuwazuia watoto kutumia mitandao hiyo.

    “Tunaiomba serikali ya shirikisho kuanzisha sheria ya kikomo cha umri wa miaka 14 kwa matumizi ya mitandao ya kijamii na kushughulikia uhitaji uliopo wa ulinzi katika ulimwengu wa kidijitali hadi pale watakapofikia umri wa miaka 16,” lilisema azimio hilo.

    Washirika wa muungano wa Merz, chama cha Social Democrats, pia wameunga mkono vikwazo hivyo, hali inayoongeza uwezekano wa serikali kusukuma mbele hatua hizo.

    Hata hivyo, chini ya mfumo wa shirikisho wa Ujerumani, udhibiti wa vyombo vya habari ni jukumu la majimbo, ambayo lazima yakubaliane kuhusu sheria za kitaifa.

    Baadhi ya wanafunzi mjini Bonn walikuwa na maoni mseto. Moritz mwenye miaka 13 alisema uamuzi unapaswa kuwa wa wazazi, huku Emma akisema marufuku itakuwa “kitu kisicho cha kawaida”. Mwalimu Till Franke alisema mwanzoni itakuwa mshtuko, lakini baadaye wanafunzi watazoea.

    Soma pia:

  3. Trump atangaza ushuru mpya wa 10% kujibu uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Marekani

    Trump

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump ameweka ushuru mpya wa kimataifa wa 10% ili kuziba nafasi ya ule uliobatilishwa na Mahakama ya Juu, akiita uamuzi huo “mbaya” na kuwakosoa majaji waliokataa sera yake ya biashara.

    Katika uamuzi wa 6-3, mahakama ilisema rais alivuka mamlaka yake, ikifungua njia ya marejesho ya mabilioni ya dola kwa biashara na majimbo yaliyopinga ushuru huo.

    Akizungumza Ikulu, Trump alisema marejesho hayatakuja bila mapambano ya kisheria na alitarajia suala hilo kuendelea mahakamani kwa miaka mingi. Aliongeza atatumia sheria nyingine kuendeleza ushuru huo.

    Ushuru huo uliotangazwa mwaka jana ulilenga karibu kila nchi, ukianzia Mexico, Canada na China kabla ya kupanuliwa kwa washirika wengi wa biashara.

    Ikulu ilitegemea sheria ya mwaka 1977 (IEEPA), lakini wapinzani walisema haikutaja ushuru wala kumpa rais mamlaka ya wazi ya kutoza kodi hizo. Jaji Mkuu John Roberts alisema Bunge hutoa mamlaka ya ushuru kwa masharti ya wazi na yenye mipaka.

    Baada ya uamuzi huo, Trump alisaini tamko la kuweka ushuru mpya wa 10% chini ya kifungu cha 122 kwa siku 150 kuanzia 24 Februari, ukiwa na misamaha kadhaa ikiwemo kwenye baadhi ya madini, bidhaa za kilimo, dawa na vifaa vya kielektroniki.

    Masoko ya Wall Street yalipanda kufuatia tangazo hilo huku baadhi ya biashara zikikaribisha uamuzi huo, ingawa wachambuzi walisema hali imekuwa tata zaidi.

    Nchi washirika zilisema zinafuatilia uamuzi huo, huku baadhi zikisisitiza umuhimu wa mizania ya madaraka katika demokrasia.

    Maelezo zaidi:

  4. Familia ya Mpalestina raia wa Marekani aliyeuawa Ukingo wa Magharibi yataka uwajibikaji

    .

    Chanzo cha picha, Ammar Awad via Reuters

    Familia ya kijana wa miaka 19 ambaye ni Mpalestina na raia wa Marekani wanayedai alipigwa risasi na mkaazi wa makazi ya Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi wametaka uwajibikaji kuhusu kifo chake.

    Nasrallah Abu Siyam alipigwa risasi karibu na Ramallah Jumatano, akiwa angalau raia wa sita wa Marekani kuuawa na walowezi au wanajeshi wa Israel katika eneo hilo ndani ya miaka miwili iliyopita.

    Utawala wa Trump ulisema uko tayari kutoa msaada wa kibalozi, lakini haukujibu madai kuwa sera zake zimeshindwa kuzuia kuongezeka kwa vurugu za walowezi.

    Ubalozi wa Israel mjini Washington ulisema tukio hilo linachunguzwa na “uchunguzi wa kiutendaji lazima ukamilike haraka iwezekanavyo”.

    Familia yake ilisema alikuwa miongoni mwa wakaazi takriban 30 wa kijiji cha Mukhmas waliokuwa wakijaribu kuwazuia walowezi wenye silaha kuiba mbuzi wao. Shahidi mmoja alisema pande zote zilirushiana mawe na walowezi walifyatua risasi, huku Abu Siyam akipigwa risasi na kufariki.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema inafahamu kifo cha raia wake na “inafuatilia kwa makini hali hiyo”.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema wanajeshi walifika eneo la tukio na kutumia mbinu za kutawanya umati kurejesha utulivu, na kuongeza kuwa hakuna risasi zilizofyatuliwa na IDF wakati wa tukio hilo.

    IDF imethibitisha tukio hilo linachunguzwa na kutakuwa na uwepo wa kijeshi katika eneo hilo siku zijazo kuzuia matukio zaidi.

  5. Serikali yafikiria kumuondoa Andrew katika orodha ya urithi wa ufalme

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Uingereza inafikiria kutunga sheria ya kumuondoa Andrew Mountbatten-Windsor katika orodha ya urithi wa ufalme.

    Waziri wa Ulinzi Luke Pollard aliiambia BBC kuwa hatua hiyo, ambayo itamzuia Andrew kuwa Mfalme ni “jambo sahihi kufanya”, bila kujali matokeo ya uchunguzi wa polisi.

    Kwa sasa Andrew, ndugu wa Mfalme, bado ni wa nane katika orodha ya kurithi kiti cha ufalme licha ya kuvuliwa hadhi na majukumu ya kifalme mwaka jana, kufuatia shinikizo kubwa kuhusu uhusiano na mfadhili wake na mtu aliyedaiwa kujihusisha na watoto kimapenzi, Jeffrey Epstein.

    Alikamatwa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma na kuachiwa chini ya uchunguzi, akikanusha makosa yote.

    Pollard alisema serikali imekuwa ikifanya kazi na kasri la Buckingham kuzuia hali ya Andrew “kurithi kiti cha ufalme”, lakini akasisitiza hatua hiyo inapaswa kusubiri hadi pale uchunguzi wa polisi utakapo kamilika.

    Pendekezo hilo litahitaji kupitishwa na Bunge na kuidhinishwa na Mfalme, pamoja na kuungwa mkono na nchi 14 za Jumuiya ya Madola ambako Charles III ni mkuu wa jumuiya ya madola.

    Mara ya mwisho orodha ya urithi kubadilishwa na sheria ya Bunge ilikuwa mwaka 2013, huku mwaka 1936 ikiwa mara ya mwisho mtu kuondolewa rasmi kufuatia kujiuzulu kwa Edward VIII.

    Baadhi ya wabunge wa vyama vya Liberal Democrats na SNP wameunga mkono wazo hilo, huku wengine wakisema ni suala la kusubiri matokeo ya uchunguzi.

    Kasri la Buckingham halijatoa maoni rasmi kuhusu mpango huo.

    Soma pia:

  6. Guardiola: 'Sijali' kutetereka kwa Arsenal katika mbio za ubingwa

    Guardiola

    Chanzo cha picha, Pep Guardiola

    Maelezo ya picha, Meneja wa Manchester City Pep Guardiola

    Pep Guardiola amesisitiza kuwa “hajali hata kidogo” kuyumba kwa Arsenal ambako kumeipa Manchester City nafasi ya kurejea katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England.

    City walikuwa katika hatari ya kuachwa mbali baada ya kiwango chao kisicho thabiti kuipa Arsenal nafasi ya juu.

    Hata hivyo, City wanaoshikilia nafasi ya pili wamepata nafuu kufuatia sare za Arsenal dhidi ya Wolves na Brentford.

    Sasa wana alama tano nyuma ya Arsenal wakiwa na mchezo mmoja mkononi na watacheza nyumbani dhidi ya kikosi cha Mikel Arteta mwezi Aprili.

    Iwapo City watashinda mechi zao 12 zilizosalia, watachukua ubingwa kwa mara ya tano katika misimu sita. Lakini Guardiola hakutaka kubebwa na hali hiyo.

    Badala yake, anajikita katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Newcastle, ambapo ushindi utapunguza pengo kabla ya Arsenal kukutana na Tottenham Jumapili.

    “Sijali hata kidogo,” alisema Guardiola. “Sikuzungumzia kuhusu hatua hiyo hata kwa sekunde moja. Ni Newcastle tu.

    “Ukiniuliza swali hili ikiwa imesalia mechi mbili au tatu, nitakupa jibu. Zimebaki mechi 12, ni nyingi sana.”

    Guardiola alisema mambo mengi yatatokea kabla ya msimu kumalizika na kusisitiza wachezaji wake wanapaswa kuzingatia kushinda mechi inayofuata.

    Wakati huohuo, alisema ubaguzi wa rangi bado ni tatizo la jamii, sio la soka pekee, baada ya nyota wa Real Madrid Vinicius Junior kudai alitukanwa kwa misingi ya rangi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa wiki hii.

    “Kuna kazi kubwa bado ya kufanya. Ubaguzi wa rangi uko kila mahali,” alisema Guardiola.

    “Ni pale unapodhani wewe ni bora kuliko mwingine.”

    Pia unaweza kusoma:

  7. Shirikisho la Soka Senegal lapinga hukumu ya mashabiki wao Morocco

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limelaani hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Morocco dhidi ya mashabiki 18 wa Senegal waliokutwa na hatia ya kufanya vurugu kufuatia fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON.

    Mashabiki hao walihukumiwa Alhamisi kifungo cha kati ya miezi mitatu hadi mwaka mmoja jela, baada ya kuwa rumande tangu Januari 18, siku ya fainali ya AFCON iliyochezwa Morocco, ambapo Senegal iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji.

    Mwishoni mwa mchezo huo, baadhi ya mashabiki wa Senegal walijaribu kuingia uwanjani, huku wachezaji wa Senegal wakisimamisha mchezo huo kwa takribani dakika 20 wakipinga penalti ya dakika za mwisho iliyotolewa kwa Morocco. Pia kulikuwa na ripoti za mashabiki kurusha vitu uwanjani, ikiwemo kiti.

    Mashabiki hao walifikishwa katika mahakama ya Rabat wakikabiliwa na mashtaka ya kufanya vurugu katika mchezo huo, ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu dhidi ya vyombo vya usalama, uharibifu wa vifaa vya michezo, kuvamia uwanja na kurusha vitu.

    Rais wa kamati ya mawasiliano ya FSF, Bacary Cisse, amesema uamuzi huo umeleta mshangao na huzuni kubwa.

    “Tumesikitika na kushangazwa sana na hukumu hiyo,” alinukuliwa akisema. “Uamuzi huu usioeleweka umeibua hasira kali.”

    Kwa mujibu wa hukumu hiyo, mashabiki tisa wamehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na kutozwa faini ya dirham 5,000 (takribani dola 545 za Marekani). Wengine sita wamepewa miezi sita jela na faini ya dirham 2,000, huku watatu wakihukumiwa miezi mitatu na faini ya dirham 1,000.

    Cisse amesema matukio ya vurugu hutokea katika viwanja mbalimbali duniani, ikiwa ni pamoja na Morocco, bila kupelekea adhabu kama hizo.

    “Hatua iliyochukuliwa dhidi ya mashabiki hawa yanaoonekana kuwa kubwa kupita kiasi,” alisema.

    Wakili wa utetezi, Patrick Kabou, pia alieleza hukumu hiyo kuwa “isiyoeleweka”, akidai mashabiki hao ni waathirika.

    Maelezo zaidi:

  8. Watu 12 wauawa katika shambulizi la anga la Israel nchini Lebanon

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Takriban watu 12 waliuawa siku ya Ijumaa katika mashambulizi ya anga ya Israel yaliyolenga Mmaeneo ya mashariki na kusini mwa Lebanon, huku vyombo vya habari vikiripoti kuwa 10 kati ya waliouawa ni pamoja na "afisa mkuu wa Hezbollah".

    Jeshi la Israel lilisema lililenga kundi la "Hezbollah na mshirika wake wa Kipalestina Hamas."

    Hezbollah imetangaza kifo cha mmoja wa viongozi wake katika mashambulizi ya Israel mashariki mwa nchi hiyo na kusema katika taarifa kwamba, "Hezbollah inawatangazia wafuasi wao kwamba kiongozi aliyeuawa ni Hussein Muhammad Yaghi Sadiq."

    Wizara ya Afya ya Lebanon imethibitisha kuwa "mashambulizi ya Israeli katika maeneo kadhaa katika Bonde la Bekaa yalisababisha vifo vya watu 10 na wengine 24 kujeruhiwa," ikiongeza kuwa watoto watatu walikuwa miongoni mwa waliojeruhiwa.

    Awali Shirika la Habari la Taifa la Lebanon liliripoti kwamba mashambulizi ya anga ya Israel katika Bonde la Bekaa yalisababibisha vifo vya watu sita na kuwajeruhi wengine 25.

  9. Trump awasuta majaji wa Mahakama ya Juu kwa kuharamisha ushuru wa kimataifa

    Trump

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amewashutumu majaji sita wa Mahakama ya Juu ambao wameuwekea kizingiti kikubwa katika muhula wake wa pili madarakani kwa kuondoa ushuru wa kimataifa wa utawala huo.

    Uamuzi wa mahakama ya Ijumaa ulikuwa "wa kukatisha tamaa sana". Majaji wanaoshabikia mkumbo wa wengi wanapaswa "kujitafakari" kwani wamekosa ujasiri wa "kufanya jambo sahihi", Trump alisema, katika majibu yake yaliyogeuka kuwa mashambulizi makubwa dhidi ya mhimili huru wa serikali iliyo na haki sawa.

    Uamuzi huo ulikuwa ushindi mkubwa kwa wafanyabiashara na mataifa ya Marekani ambayo yamepinga majukumu hayo, na kufungua mlango kwa uwezekano wa kurejeshewa ushuru wa mabilioni ya dola, huku pia ikizua msukosuko mpya katika mazingira ya biashara ya kimataifa.

    Kujibu amuzi wa Mahakama hiyo hata hivyo Rais Donald Trump ameweka ushuru mpya wa asilimia 10 wa kimataifa kuchukua nafasi ya zile zilizotupiliwa mbali na Mahakama ya Juu, akiitaja uamuzi huo kuwa "mbaya" na kuwakashifu majaji waliokataa sera yake ya biashara kama "wajinga".

    Rais alizindua mpango huo muda mfupi baada ya majaji kuharamisha ushuru mwingi wa kimataifa ambao Ikulu ya White House ilitangaza mwaka jana.

    Alipozindua ushuru huu uliotupiliwa mbali na mahakama Aprili iliyopita alisema "nchi yetu na walipakodi wake wameibiwa kwa zaidi ya miaka 50". Akihoji kwamba Marekani inanunua bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi kuliko inazouza, fedha za Wamarekani zinatumika nje ya nchini bila sababu za msingi.

    Soma pia:

  10. Tunatumai hujambo.

Trending Now