Risasi zasikika Washington, Trump aokolewa na walinzi

Chanzo cha picha, Reuters
Rais Donald Trump na mkewe Melania Trump waliondolewa haraka kwenye hafla ya kila mwaka ya chakula cha jioni ya waandishi wa habari (White House Correspondents’ Dinner) mjini Washington DC baada ya mtu mwenye silaha kuvamia na kufyatua risasi karibu na eneo la usalama.
Kwa mujibu wa maafisa wa usalama, mshukiwa huyo alifyatua risasi kuelekea maafisa wa usalama katika eneo la ukaguzi kabla ya kuingia ukumbini. Afisa mmoja alipigwa risasi lakini hakupata madhara makubwa kutokana na kuvaa kuizuia risasi na hali yake inaelezwa kuwa nzuri.

Washiriki wa hafla hiyo, wakiwemo viongozi wa serikali na wanahabari, walilazimika kujificha chini ya meza huku vikosi vya usalama vikichukua hatua za haraka kumdhibiti mshukiwa huyo.
Mshukiwa huyo, aliyekuwa na silaha kadhaa, alikamatwa na mamlaka na anaaminika kuwa alitenda tukio hilo akiwa peke yake. Hakuna viongozi wa serikali walioumia katika tukio hilo.
Baada ya tukio hilo, Trump aliwashukuru maafisa wa usalama kwa hatua zao za haraka na kusema tukio hilo linachunguzwa zaidi huku sababu za mshambulizi bado hazijajulikana.
Hafla hiyo, iliyokuwa imehudhuriwa na mamia ya watu wakiwemo viongozi wakuu wa serikali, ilisitishwa kufuatia tukio hilo la ghafla la kiusalama.

Chanzo cha picha, Getty Images
