Hapa ndipo tunatamatisha matangazo yetu. Kwaheri.
Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waziri wa Ulinzi wa Marekani aiambia Iran “kufanya maamuzi ya busara”
Pete Hegseth ameonya kuwa Marekani iko na nguvu ya kuanza tena mashambulizi dhidi ya Iran, iwapo watakataa kuafikia makubaliano ya kusitisha vita.
Muhtasari
- Israel na Lebanon wakubaliana kusitisha mapigano kwa siku 10, asema Trump
- Lissu azungumza na Chakwera, ataka kufutwa kwa kesi ya uhaini dhidi yake
- Kamanda wa Centcom asema jeshi la Marekani linakarabati mbinu zake za kivita na utendaji
- "Fanyeni maamuzi ya busara"- Waziri wa Ulinzi wa Marekani aionya Iran
- Papa Leo aitaka Cameroon kupambana na ufisadi ili kupata amani
- Mwanaharakati Kemi Seba akamatwa Afrika Kusini kwa kuchochea mapinduzi nchini Benin
- Wimbi la mashambulizi ya Urusi yasababisha maafa Ukraine
- "Mimi ni mtu niliyedhihakiwa zaidi mitandaoni" - Meghan Markle
- Raia wa China ahukumiwa mwaka mmoja jela kwa kusafirisha mchwa kutoka Kenya
- Mwanasiasa wa Afrika Kusini Julius Malema, ahukumiwa miaka tano jela
- Rais Samia na ujumbe wa Jumuiya ya Madola wazungumza Ikulu Dar es Salaam
- Lebanon yatilia shaka madai ya mazungumzo ya Trump
- Marekani yakamata meli yenye bendera ya Iran
- Uingereza yasema mzozo wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran ulikuwa kosa
- Idara ya Hazina ya Marekani yatangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran
- Mohsen Rezaei: Sikubaliani na kuongeza muda wa usitishaji mapigano
- Israel yaendelea na operesheni dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon - Netanyahu
- Papa Leo akemea ufisadi, aihimiza Cameroon kuheshimu haki za binadamu
- Marekani na Iran zajadili duru ya pili ya mazungumzo kukiwa na wasiwasi wa muda wa usitishaji mapigano
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid & Beldeen Waliaula
Israel na Lebanon wakubaliana kusitisha mapigano kwa siku 10, asema Trump
Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa Lebanon na Israel wamekubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa siku 10, makubaliano ambayo yataanza kutekelezwa saa saba usiku saa za Afrika Mashariki.
Katika taarifa, Trump amesema amezungumza na Rais wa Lebanon Joseph Aoun pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Taarifa ya Trump haijajumuisha Hezbollah, kundi la wapiganaji linaloungwa mkono na Iran nchini Lebanon, ambalo limekuwa likijibizana kwa mashambulizi na Israel.
Taarifa ya Trump ilisema hivi:
"Nilikuwa na mazungumzo mazuri sana na Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu."
"Viongozi hawa wawili wamekubaliana kwamba ili kuwa na amani katika nchi zao, wataanza rasmi kutekeleza usitishwaji mapigano kwa muda wa siku 10."
"Siku ya Jumanne, nchi hizi mbili zilikutana kwa mara ya kwanza baada ya miaka 34 mjini Washington, D.C., na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio."
"Nimemwagiza Makamu wa Rais JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje Rubio, kushirikiana na mnadhifu mkuu wa Majeshi, Dan Caine, kushirikiana na Israel na Lebanon ili kupata amani itakayodumu"
"Imekuwa heshima yangu kumaliza vita 9 kote duniani, na hii itakuwa ya 10, hivyo basi, tuifanikishe"
Lissu azungumza na Chakwera, ataka kufutwa kwa kesi ya uhaini dhidi yake
Kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu amekutana na Lazurus Chakwera mjumbe maalum wa Commonwealth nchini Tanzania na kujadili mustakabali wa sheria na utawala nchini humo, Taarifa ya chama hicho imeeleza.
Katika majadiliano yao, Lissu, aliwasilisha hoja tofauti kwa rais huyo wa zamani wa Malawi ambazo angetaka ziangaziwe.
Hoja hizo ni kama vile:
- Kufutwa kwa kesi ya uhaini inayomkabilu Pamoja na kesi zinazoikabli chama chake
- Kufanyika uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29 kupitia taasisi ya SADC
- Kuwepo na mazingira wezeshi ya kufanya mazungumzo ya kweli
- Uwajibikaji wa kitaasisi ya yaliyotokea Oktoba mwaka wa 2025 hususan kwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, INEC, TCRA na kurejelea ripoti ya jaji Nyalali ya 1992.
- Kufanyika kwa mageuzi ya vyombo vya ulinzi na usalama
- Mabadiliko ya mfumo mzima wa uchaguzi,ikiwemo kuundwa kwa chombo kipya huru cha kusimamia uchaguzi kwa kuzingatia ripoti mbali mbali za waangalizi wa uchunguzi
- Kupatikana kwa katiba mpya.
Ni mwaka mmoja sasa tangu Tundu Lissu, Mwenyekiti wa (CHADEMA), kukamatwa na kuwekwa gerezani kwa mashtaka ya uhaini na uchochezi.
Kesi yake imekuwa ya kivutio kimataifa, ikichochea mjadala kuhusu haki za kikatiba, uwazi wa mahakama, na uhuru wa kisiasa nchini Tanzania.
Hii kesi ni mojawapo ya kesi kubwa zaidi za kisiasa nchini Tanzania tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Unaweza kusoma;
Kamanda wa Centcom asema jeshi la Marekani linakarabati mbinu zake za kivita na utendaji
Admiral Brad Cooper, kamanda wa kituo cha kuendesha oparesheni za kijeshi za Marekani (Centcom) amesema majeshi ya Marekani yanajipanga upya na “kurekebisha mbinu za kiutendaji” kipindi hiki ambacho mapigano yamesitishwa.
Cooper alisema wanaendelea kufanya mazungumzo na washirika wao kanda ya Mashariki ya Kati ili kudumisha usalama na kusema kuwa hakuna “mshirika bora zaidi” kuliko Israel.
Mnadhimu mkuu wa jeshi la Marekani, jenerali Dan Caine amesema kwa sasa wanafuata maelekezo ya Rais Trump ya kusitisha mapigano ila wako tayari kutekeleza mashambulizi “baada ya kupewa taarifa ya muda mfupi”
Jenerali huyo alifafanua kuwa kizuizi cha kijeshi cha Marekani ni cha kudhibiti bandari na pwani ya Iran ila haijaegemea sana katika mlango bahari wa Hormuz.
Kizuizi hicho kinalenga meli zote zinazotoka au kuingia bandari za Iran bila kujali taifa linalomiliki meli hiyo na kuonya kuwa meli itakayokataa kufuata masharti itakabiliwa vikali.
Pia unaweza kusoma :
"Fanyeni maamuzi ya busara"- Waziri wa Ulinzi wa Marekani aionya Iran
Waziri wa ulinzi wa Marekani Pete Hegseth, amesema kuwa kizuizi cha kijeshi cha Marekani ni “njia staha zaidi” ya kukabiliana na hali ilivyo kwa sasa, na kuongezea kuwa sekta ya nishati ya Iran bado haijaharibiwa.
Kiongozi huyo amesema kuwa Iran inapenda kujigamba kuwa imedhibiti mlango bahari wa Hormuz, ila haina jeshi la wanamaji. “Hamuwezi kudhibiti kitu” alisema Hegseth.
Aidha aliongezea kuwa Iran imetishia kurusha makombora kwa meli za biashara, ila wamedhibiti hali hiyo na kusema kuwa “huo ni uharamia na ugaidi”
Waziri huyo amesema jeshi la wanamaji la Marekani linadhibiti safari za meli zinazoingia na kutoka katika mlango bahari wa Hormuz, na linafanya hivyo kwa kutumia chini ya 10% ya uwezo wake wa kijeshi.
Hegseth pia ameionya Iran na kuwaambia kuwa “tunawafuatilia kwa karibu” na kuongezea kuwa uwezo wa Marekani na Iran si sawa, na kwamba haya “sio mapambano ya haki.”
“Tunazidi kuwa na nguvu zaidi. Nyinyi mnaendelea kutumia makombora yenu yaliyobaki bila uwezo wa kuyatengeneza tena,” alisema.
Kiongozi huyo alisema Marekani inaishauri serikali ya Iran “ifanye maamuzi ya busara,” akiongeza kuwa Marekani ina uwezo wa kuanza tena operesheni za kijeshi iwapo serikali hiyo itafanya maamuzi “mabaya” na kukataa kuafikia makubaliano.
Pia unaweza kusoma:
Papa Leo aitaka Cameroon kupambana na ufisadi ili kupata amani
Papa Leo, ameiambia utawala wa Cameroon ikabiliane na ufisadi, katika ziara yake nchini humo.
Akiwahutubia waliohudhuria mkutano katika ikulu ya rais mjini Yaoundé, akiwemo Rais Paul Biya, Papa alisema,
“Ili amani na haki itawale, minyororo ya ufisadi inayoharibu mamlaka na kuinyima uaminifu lazima ivunjwe.”
Paul Biya, mwenye umri wa miaka 93, alishinda muhula wake wa nane wa urais mwaka uliopita katika uchaguzi uliopingwa na wapinzani wake, na serikali yake imekumbwa na tuhuma za rushwa, utawala mbaya na kushindwa kuimarisha usalama.
Papa yuko katika maeneo yanayozungumza Kiingereza nchini Cameroon, ambako makundi ya kujitenga yamedumu eneo hilo kwa karibu muongo mmoja.
Kiongozi huyo wa dini ya katoliki anatarajiwa kuombea amani katika misa itakayofanyika mjini Bamenda, kitovu cha ghasia ambazo zimesababisha vifo vya watu wasiopungua elfu 6,000 na kuwafanya wengi kuhama makazi yao.
Pia unaweza kusoma:
Mwanaharakati Kemi Seba akamatwa Afrika Kusini kwa kuchochea mapinduzi nchini Benin
Maafisa wa polisi Afrika Kusini wanasema kuwa wamemkamata “mtoro” ambaye ni mwanaharakati wa Benin aliyekuwa akitafutwa.
Kemi Seba, anasemekana alikuwa akijaribu kukimbilia ulaya kupitia Zimbabwe.
Seba ambaye jina lake kamili ni Stellio Gilles Robert Capo Chichi, anatafutwa na mamlaka nchini Benin “kwa kuchochea uasi” baada ya kuunga mkono mapinduzi ya serikali yaliyotibuka mwaka uliopita.
Mwanaharakati huyo alikamatwa siku ya Jumatatu na mwanawe kijana mwenye umri wa miaka 18 mjini Pretoria. Mtu aliyekuwa amelipwa kuwasaidia kuenda nchini Zimbabwe, pia anazuiliwa na polisi.
Seba mwenye umri wa miaka 45, anajulikana kwa kupinga ushawishi wa Ufaransa barani Afrika.
Kemi Seba alizaliwa nchini Ufaransa na wazazi wake ni wazaliwa wa Benin na anawafuasi zaidi ya millioni 1.5 kwenye mitandao ya kijamii.
Amehukumiwa mara kadhaa nchini Ufaransa kwa kuchochea chuki, ukabilia na chuki dhidi ya wayahudi.
Mwaka wa 2024, alinyanganywa uraia wake wa Ufaransa, na akajibu hatua hiyo kwa kuchoma pasipoti yake hadharani na kusema kuwa “amekombolewa kutoka kwa kubeba mzigo wa kuwa raia wa Ufaransa.”
Pia unaweza kusoma:
Wimbi la mashambulizi ya Urusi yasababisha maafa Ukraine
Urusi imetekeleza mfulululizo wa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani nchini Ukraine usiku wa kuamkia leo, na kuwauwa watu 16 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 100.
Watu 8 waliuawa katika mji wa Odesa, mkuu wa jeshi katika mji huo Sergiy Lysak aliandika kwenye mtandao wa Telegram huku mashambulizi yakiendelea kuripotiwa.
Upande wa pili wa mpaka wa Ukraine, eneo la Krasnodar Krai nchini Urusi, watoto wawili waliuawa na ndege zisizo na rubani za Ukraine.
Mashambulio haya yanakuja baada ya kipindi kifupi cha kusitisha mapigano wakati wa sherehe za pasaka za Orthodox wikendi iliyopita.
Mashambulio ya Urusi pia yalilenga mji wa Kyiv, Kharkiv, Dnipro,Mykolaiv na Kherson.
Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky amesema vikosi vya ulinzi vya taifa lake vimedungua ndege zisizo na rubani 636 kutoka Urusi katika muda wa siku moja.
Kwenye mtandao wa X rais huyo aliandika kuwa “huu ni usiku mwingine unaodhibitisha kuwa Urusi haistahili kulegezewa sera za kimataifa au kuondolewa vikwazo”
Pia unaweza kusoma:
"Mimi ni mtu niliyedhihakiwa zaidi mitandaoni" - Meghan Markle
Mke wa mwanafalme Harry, Meghan Markle, amesema kwa kipindi cha miaka 10 alikuwa “mtu aliyedhihakiwa zaidi duniani” kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza mjini Melbourne nchini Australia, kuhusu madhara ya mitandao ya kijamii akiwa ameambatana na mumewe mwanamfalme Harry, Meghan alisema amenyanyaswa mitandaoni kwa kipindi cha muongo mmoja, na kwamba “kampuni za teknlojia zinazomiliki mitandao hiyo, hazijakuwa na motisha ya kuzuia mitandao yao kutotumiwa vibaya.”
Katika mkutano huo, Meghan aliwaambia waliohudhuria kuwa “nikiwafikiria nyinyi nyote na kila ambacho mnapitia, nawaza jinsi sekta hii yenye thamani ya mabillioni ya dola imejengwa kwa ukatili na kupata mibofyo na hilo huenda halitabadilika”
“Hivyo basi lazima muwe na ujasiri zaidi” alisema Meghan.
Mwanamfalme Harry pia aliipongeza Australia kwa kuzuia watoto kuwa na mitandao ya kijamii.
Pia unaweza kusoma:
Raia wa China ahukumiwa mwaka mmoja jela kwa kusafirisha mchwa kutoka Kenya
Raia mmoja wa China, Zhang Kequn, amepewa kifungo cha mwaka mmoja jela, kwa jaribio la kutaka kuwasafirisha maelfu ya malkia wa mchwa kutoka Kenya.
Mahakama moja mjini Nairobi pia ilimpa faini ya shillingi millioni moja ($ 7,737).
Jaji wa mahakama hiyo Irene Gichobi alisema raia huyo wa China kwa jina Zhang hakuwa mkweli, na alikosa “huruma”
Zhang alikamatwa mwezi uliopita katika uwanja wa ndege akiwa amepanga safari kurudi China akiwa amebeba zaidi ya mchwa 2000 kwenye begi lake.
Mamlaka za Kenya zimeonya watu dhidi ya kuwakamata mchwa hao, ambao uhitaji wake umeongezeka bara Ulaya na Asia na huuzwa takriban $ 220 kila mmoja.
Soma pia:
Mwanasiasa wa Afrika Kusini Julius Malema, ahukumiwa miaka mitano jela
Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) Julius Malema, mwenye umri wa miaka 45, amepewa kifungo cha miaka mitano jela hii leo katika mahakama moja nchini Afrika Kusini.
Hakimu Twanet Oliver wa mahakama ya East London nchini humo, aliamuru kuwa kiongozi huyo ana hatia dhidi ya mashtaka matano yanayomkabili.
Kiongozi huyo alipatikana na hatia mwaka uliopita baada ya kushtakiwa kwa kumiliki risasi, matumizi mabaya ya bunduki katika eneo la umma na kuhatarisha maisha ya watu.
Timu yake ya wanasheria imeanza mchakato wa kukata rufaa ili kumuepusha kiongozi huyo kuenda jela.
Soma pia:
Chakwera akutana na ujumbe wa CCM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola ambaye pia ni Rais wa zamani wa Malawi, Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika muendelezo wa ziara hiyo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Asha-Rose Migiro, pia amefanya mazungumzo na Chakwera katika Ofisi za CCM Lumumba, jijini humo.
Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Jumuiya ya Madola, huku Mhe. Chakwera akiwa nchini kwa niaba ya Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Mhe. Shirley Ayorkor Botchwey.
Haya yanajiri baada ya Jumuiya ya Madola kuanza rasmi mchakato wa kusaidia juhudi za maridhiano nchini Tanzania, na imemtuma Rais wa zamani wa Malawi, Dkt Lazarus Chakwera, kama Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu.
Tutaendelea kukutaarifu yanayoendelea na mazungumzo yalizingatia vipengele vipi.
Lebanon yatilia shaka madai ya mazungumzo ya Trump
Afisa katika ofisi ya rais wa Lebanon ameiambia BBC kuwa nchi hiyo haina taarifa yoyote kuhusu mawasiliano yajayo na Israel, kufuatia ujumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump uliodokeza uwezekano wa mazungumzo kati ya viongozi wa mataifa hayo mawili.
Trump alisema usiku uliopita kuwa mazungumzo kati ya viongozi wa Israel na Lebanon yanatarajiwa kufanyika “leo”.
Siku ya Jumanne, maafisa wa Israel na Lebanon walifanya mazungumzo mjini Washington, D.C., ikiwa ni mara ya kwanza kwa pande hizo kufanya mazungumzo ya moja kwa moja tangu mwaka 1993.
Lebanon ilielezea mazungumzo hayo kuwa “yenye tija”, huku Israel ikisema kuwa pande zote ziko “upande mmoja wa mlinganyo”, ingawa mashambulizi ya Israel dhidi ya kundi la Hezbollah yanaendelea.
Marekani yakamata meli yenye bendera ya Iran
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imesema kuwa imekamata meli ya mizigo yenye bendera ya Iran iliyokuwa ikijaribu kukwepa marufuku iliyowekwa kwa meli zote zinazoingia au kutoka katika bandari za Iran.
CENTCOM ilisema meli hiyo ilikamatwa Jumanne baada ya kuondoka katika mji wa bandari wa Bandar Abbas na kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Pia iliongeza kuwa meli ya Jeshi la Wanamaji la Marekani, USS Spruance, ilifanikiwa kuigeuza mwelekeo meli hiyo, ambayo sasa inarejea Iran.
CENTCOM ilisema pia kuwa imezirudisha nyuma meli 10 kuelekea Iran, na kwamba hakuna meli iliyokiuka zuio hilo tangu lilipoanza kutekelezwa Jumatatu.
Uingereza yasema mzozo wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran ulikuwa kosa
Waziri wa Fedha wa Uingereza Rachel Reeves amesema kuwa kumalizika kwa mazungumzo ya kidiplomasia na Iran na kuanza kwa mzozo wa kijeshi ni kosa lililofanywa na Marekani.
Akizungumza na kipindi cha CNBC cha Invest in America, Rachel Reeves alisema kwamba “sera bora ya kiuchumi kwa sasa, si tu kwa Uingereza bali kwa dunia nzima, ni kupunguza mvutano.”
Serikali ya Uingereza imesema kuwa haitashiriki katika kizuizi cha kijeshi cha Marekani katika Mlango-Bahari wa Hormuz ili kuongeza shinikizo kwa Iran.
Alipoulizwa kama tofauti zinazoongezeka kati ya Marekani na Uingereza kuhusu mzozo huo zimeathiri uhusiano maalum kati ya nchi hizo mbili, Rachel Reeves alikataa hilo, akisema halijawa na athari.
Hata hivyo, alisema pia kwamba “kuna nafasi ya kutofautiana kati ya marafiki.”
Idara ya Hazina ya Marekani yatangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran
Idara ya Hazina ya Marekani imetangaza msururu wa vikwazo vipya dhidi ya watu binafsi, mashirika na meli zinazohusishwa na Iran.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya idara hiyo, vikwazo vimewekwa dhidi ya watu watatu, meli tisa na taasisi 17, ambapo neno “taasisi” linaweza kujumuisha kampuni au mashirika mbalimbali.
Katika taarifa yake, Idara ya Hazina ya Marekani imesema imeweka vikwazo dhidi ya mtandao wa usafirishaji mafuta unaoendeshwa na Mohammad Hossein Shamkhani, mtoto wa afisa wa zamani wa usalama wa Iran Ali Shamkhani.
Anatuhumiwa kuhusika katika usafirishaji na uuzaji wa mafuta ya Iran kupitia mtandao mpana wa majini.
Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, mtandao huo umeingiza mapato ya mabilioni ya dola.
Idara hiyo pia imeweka vikwazo dhidi ya malengo yanayohusishwa na mpango tata wa kifedha unaohusishwa na kundi la Lebanon la Hezbollah, unaodaiwa kupangwa kupitia vituo vya kubadilisha dhahabu na hatimaye kunufaisha utawala wa kijeshi wa Iran.
Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, mpango huo unahusisha kubadilisha akiba ya dhahabu kuwa fedha taslimu, ambazo hutumika kufadhili shughuli za Hezbollah huku ukikwepa vikwazo kupitia mitandao ya biashara na usambazaji.
Soma zaidi:
Mohsen Rezaei: Sikubaliani na kuongeza muda wa usitishaji mapigano
Mohsen Rezaei, mwanachama wa Baraza la Uamuzi wa Maslahi ya Mfumo nchini Iran, amesema: “Hatutauacha Mlango wa Hormuz hadi haki zetu zitakapopatikana kikamilifu.”
Rezaei, ambaye pia aliwahi kuwa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC), amesema katika mahojiano yake mapya yaliyoripotiwa na vyombo vya habari vya ndani ya Iran: “Tofauti na Wamarekani wanaoogopa vita vya muda mrefu, sisi tumejiandaa kikamilifu na tumezoea vita vya muda mrefu.”
Katika mahojiano hayo, akirejelea kauli za Donald Trump na Waziri wa Vita wa Marekani Pete Hegseth kuhusu kuharibiwa kwa Jeshi la Wanamaji la Iran, alihoji: “Ikiwa Jeshi la Wanamaji la Iran limeharibiwa, kwa nini Marekani haijathubutu kupita katika Mlango wa Hormuz?”
Rezaei pia amesisitiza kuwa licha ya kufuata maamuzi ya viongozi wa nchi, maoni yake binafsi ni kwamba Iran haipaswi kukubali kurefushwa kwa usitishaji mapigano wa wiki mbili na Marekani.
Soma zaidi:
Israel yaendelea na operesheni dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon - Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Jeshi la nchi yake linaendelea na operesheni dhidi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran Hezbollah nchini Lebanon licha ya shinikizo la kimataifa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Bwana Netanyahu amesema majeshi ya Israel yako karibu kuudhibiti mji wa kusini mwa Lebanon wa Bint Jbeil ambao anautaja kuwa ngome ya Hezbollah.
Baraza la Mawaziri la Israel linaripotiwa kukutana kujadili uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano lakini bado hakujatangazwa uamuzi wao kuhusiana na hilo.Iran inasisitiza kuwa Lebanon sharti ijumuishwe katika makubaliano yoyote ya kuvimaliza vita vya Mashariki ya Kati.
Soma zaidi:
Papa Leo akemea ufisadi, aihimiza Cameroon kuheshimu haki za binadamu
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Leo ametoa wito kwa Serikali ya Cameroon kupambana dhidi ya ufisadi.
Baada ya kukaribishwa kwa vifijo na nderemo na maelfu ya waumini waliojitokeza katika Mji Mkuu Yaounde, Papa Leo aliwahutubia viongozi wa Serikali akiwemo Rais wa muda mrefu wa Cameroon Paul Biya akiwataka viongozi wa nchi hiyo kuzisuta nafsi zao, kuvunja minyororo ya ufisadi na kuheshimu haki za binadamu.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki amesema viongozi wanapaswa kuwa madaraja na sio chanzo cha migawanyiko.
Asasi za kiraia zimelaani ukandamizaji unaofanywa na Serikali dhidi ya wanaopinga kuchaguliwa tena kwa muhula wa nane kwa Rais Biya katika uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana.
Soma zaidi:
Marekani na Iran zajadili duru ya pili ya mazungumzo kukiwa na wasiwasi wa muda wa usitishaji mapigano
Marekani imesema inajadili uwezekano wa kufanyika duru ya pili ya mazungumzo ya kutafuta amani na Iran.
Gazeti la Wall Street Journal limeripoti kuwa pande hizo mbili zimefikia makubaliano ya awali ya kukutana tena, ingawa muda na mahali pa mkutano huo havijabainishwa. Hata hivyo, Tehran imesema kuwa “misimamo ya Marekani inayobadilika na kukinzana inafanya kuwa vigumu kudumisha uaminifu wa makubaliano yoyote.”
Msemaji wa Ikulu ya White House amekanusha taarifa kwamba Marekani iliomba kurefushwa rasmi kwa usitishaji mapigano na Iran, akisema madai hayo “si ya kweli.”
Caroline Leavitt amesema, “tunaendelea kushiriki kikamilifu katika mazungumzo haya,” na kuongeza kuwa mazungumzo hayo ni “ya kujenga na yanaendelea.”
Akijibu taarifa kuhusu uwezekano wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, Leavitt alisema: “Majadiliano haya yanaendelea, lakini hakuna jambo lililo rasmi hadi litakapotangazwa hapa Ikulu ya White House.”
Aliongeza kuwa iwapo mazungumzo yatafanyika, kuna uwezekano mkubwa yakafanyika katika eneo lile lile la duru ya kwanza, yaani Islamabad, mji mkuu wa Pakistan.
Leavitt pia alisema kuwa kutekeleza matakwa ya Donald Trump, ambayo aliyataja kuwa “wazi na yasiyo na utata,” kutakuwa “kwa manufaa ya Iran.”
Ujumbe kutoka Pakistan ukiongozwa na mkuu wa majeshi Asim Munir uko Tehran kama sehemu ya juhudi za upatanishi.
Duru ya kwanza ya mazungumzo iliyofanyika mwishoni mwa juma lililopita mjini Islamabad, ilifeli kufikia makubaliano yoyote ya kuumaliza mzozo wa Mashariki ya Kati uliozuka tangu mwishoni mwa mwezi wa Februari.
Soma zaidi: