Papa Leo amelaani kile alichokiita mazingira “ya kutia wasiwasi” ya kuwashikilia wafungwa nchini Equatorial Guinea, akitaka kuheshimiwa zaidi kwa uhuru na utu wa binadamu.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alitoa kauli hiyo katika Basilica ya Immaculate Conception mjini Mongomo, mji alikozaliwa Rais wa muda mrefu Teodoro Obiang Nguema.
Katika mahubiri yake, alisisitiza umuhimu wa kulinda maisha ya binadamu, akisema ni wajibu na dhamira ya kila mmoja.
“Fikra zangu ziko kwa watu maskini zaidi, familia zinazopitia changamoto, na wafungwa ambao mara nyingi hulazimika kuishi katika mazingira ya kiafya na usafi yanayotia wasiwasi,” alisema Papa Leo.
Kauli hiyo inakuja wakati akijiandaa kutembelea gereza katika mji wa bandari wa Bata baadaye leo, ambalo mashirika ya haki za binadamu yanasema linajulikana kwa kuwashikilia wapinzani wa kisiasa na wanaopinga serikali.
Rais Obiang Nguema, ambaye alichukua madaraka mwaka 1979 kupitia mapinduzi, amekuwa akishutumiwa kuongoza nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta kwa mkono wa chuma. Pia anashutumiwa kwa rushwa, huku serikali yake ikikabiliwa na madai ya kuelekeza mapato ya mafuta kwa manufaa ya tabaka la juu.
Wakati huohuo, Papa Leo amesisitiza tena wito wake wa haki na matumizi ya rasilimali za nchi kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi wote, si wachache waliobahatika pekee.
“Muumba amewajalia utajiri mkubwa wa asili. Nawahimiza mshirikiane ili uwe baraka kwa wote,” alisema, akionya kuwa mustakabali wa nchi unategemea maamuzi ya wananchi wake.
“Bwana awasaidie kuwa jamii ambayo kila mmoja, kwa mujibu wa majukumu yake, anafanya kazi zaidi kwa manufaa ya wote badala ya maslahi binafsi, na kuziba pengo kati ya waliobahatika na wasio na bahati,” aliongeza Papa huyo.
Papa Leo amekuwa akitoa kauli kali dhidi ya ukosefu wa uadilifu katika utawala wakati wa ziara zake barani Afrika, jambo ambalo limevutia hisia za wachunguzi wa kimataifa. Mbinu yake inaonekana kama juhudi za kuendeleza uinjilisti barani humo na pia kuhimiza maadili katika jamii zinazokabiliwa na changamoto mbalimbali.