Tunachojua kuhusu usitishwaji mapigano kati ya Marekani na Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Kelly Ng, Singapore, Khashayar Joneidi & Daniel De Simone
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Iran na Marekani zimekubaliana kusitisha mapigano kwa wiki mbili, ambapo usafiri wa meli utaruhusiwa kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Hii inakuja zaidi ya mwezi mmoja baada ya Marekani na Israeli kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran, na saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kuiharibu Iran yote ikiwa Iran haitafungua Mlango-Bahari wa Hormuz.
Waziri Mkuu wa Pakistani Shehbaz Sharif, ndiye mpatanishi, alisema mapema Jumatano usitishaji mapigano umeanza mara moja.
Trump amesema amekubali "kusimamisha mashambulizi na Iran kwa muda wa wiki mbili" kwa Tehran kukubali kufungua Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na mauzo mengine ya nje kutoka Ghuba.
Katika chapisho kupitia Truth Social, Trump alisema alikubali kusitisha mapigano kwa muda kwa sababu "tayari tumetimiza na kuzidi malengo yote ya Kijeshi".
Hii inakuja baada ya kuonya hapo awali kwamba Marekani inaweza kuiharibu Iran "kwa usiku mmoja."
Vitisho vilivyosababisha kulaaniwa na mkuu wa Umoja wa Mataifa na Papa.
Iran imekubali kuruhusu meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz kwa wiki mbili, huku jeshi la Iran likisimamia safari hizo. Nchi hiyo pia imetoa mpango wa vipengele 10.
Mapendekezo ya Iran
Vipengele kumi kutoka Iran, bado havijakubaliwa na Marekani. Ni katika sehemu ya juhudi za Iran kuweka matakwa yake kuelekea mazungumzo kamili.
Maelezo ya mpango wa vipengele kumi kulingana na Iran
- Kukomesha vita nchini Iraq, Lebanon, na Yemen
- Kukomesha kabisa vita na uhasama dhidi ya Iran bila ukomo wa muda.
- Kukomesha kabisa migogoro yote katika eneo hilo
- Kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz
- Itifaki na masharti ili kuhakikisha uhuru na usalama wa Mlango-Bahari wa Hormuz.
- Malipo kamili ya fidia kwa ujenzi mpya wa Iran
- Kuondoa vikwazo dhidi ya Iran
- Kutolewa kwa fedha na mali za Iran zinazozuiliwa nchini Marekani
- Iran imejitolea kikamilifu kutounda silaha zozote za nyuklia
Kulingana na Sharif, usitishaji mapigano huo pia utaanza kutekelezwa nchini Lebanon, ambapo Israel inasema imekuwa ikipambana na kundi la wanamgambo la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.
Israeli imekuwa ikisema haitaondoka Lebanon hadi tishio kutoka kwa Hezbollah litakapomaliza.
Hakuna dalili yoyote kutoka kwa Israel kwamba imekubali kusimamisha shughuli zake nchini Lebanon au kwengineko mbali na Iran.
Israeli imesema nini?

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ving'ora vilisikika nchini Israeli muda mfupi baada ya tangazo la Trump, huku Jeshi la Ulinzi la Israeli likisema lilikuwa likizuia makombora yaliyorushwa kutoka Iran. Milio kadhaa mikubwa ilisikika Yerusalemu usiku wa Jumanne.
Saa chache baada ya Trump kutangaza kusitisha mapigano, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema: "Israel inaunga mkono uamuzi wa Rais Trump wa kusimamisha mashambulizi dhidi ya Iran kwa wiki mbili ikiwa Iran itafungua mara moja njia ya mkondo wa bahari na kusimamisha mashambulizi yote dhidi ya Marekani, Israel na nchi katika eneo hilo."
Taarifa hiyo iliongeza kuwa "kusitishwa kwa mapigano hakuijumuishi Lebanon," ambapo Israeli ina wanajeshi wa ardhini.
Haijulikani wazi jinsi Netanyahu alivyohusika katika uamuzi wa Trump.
Pakistan, ambayo imekuwa ikipatanisha pande hizo, imewaalika wajumbe kukutana jijini Islamabad siku ya Ijumaa "ili kujadili zaidi makubaliano ya mwisho ya kutatua mizozo yote."
Msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt alikiri kuwepo kwa majadiliano yanayoendelea kuhusu mazungumzo ya ana kwa ana, lakini akasema "hakuna kauli ya mwisho hadi Rais au Ikulu ya White House itangaze.”
Vyovyote itakavyo kuwa, mazungumzo yatakuwa magumu sana.
Tayari, nchi hizo mbili zinaonekana kuwa na misimamo inayokinzana kuhusu maana ya kusitisha mapigano huku.
Na Iran na Marekani zimefanya mazungumzo ya raundi mbili katika mwaka uliopita. Nyakati zote mbili zilishuhudia mvutano wa kijeshi ukiongezeka katikati ya mazungumzo.















