Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Makombora ya Iran yanaweza kufika hadi Ulaya Magharibi?
Makombora ya Iran yamejaribu kulenga kambi ya pamoja ya kijeshi ya Marekani na Uingereza huko Diego Garcia katika Bahari ya Hindi.
Makombora mawili yalirushwa Ijumaa iliyopita, moja lilishindwa na moja lilidunguliwa, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza John Healey anasema.
Diego Garcia iko karibu kilomita 4,000 (maili 2,500) kutoka Iran na jaribio la Iran limezua tahadhari kuhusu umbali wa makombora ya nchi hiyo na kuchochea hofu kwamba Iran sasa inaweza pia kulenga sehemu kubwa ya Ulaya, hata London.
Bado kuna mashaka kuhusu uwezo wa makombora ya Iran kufikia malengo yaliyo mbali sana. Lakini moja lililoshindwa Ijumaa iliyopita lilifanikiwa kusafiri takribani kilomita 3,000 kutoka kambi yake ya kurusha makombora.
Kwa hivyo tishio hili la Iran ni kubwa kiasi gani?
Nchi za Magharibi zinafuatilia kwa karibu njia za makombora
Marekani na Uingereza zitakuwa zinaona wazi kwamba Iran ilikuwa ikijaribu kuilenga Diego Garcia. Watakuwa wakiangalia makombora yakiruka.
Kikosi cha Anga za Juu cha Marekani kinaweza kugundua kila kombora lililorushwa kutoka Iran kutoka Kituo cha Kikosi cha Anga za Juu cha Buckley huko Colorado.
Mwaka jana BBC ilipewa nafasi ya ndogo ya kutazama picha mjongeo ndani ya kituo cha udhibiti ambapo waliweza kutazama mkondo wa kombora lolote linalorushwa kote ulimwenguni.
Wanatumia mkusanyiko wa setilaiti kutoka angani na rada zenye nguvu ardhini, ikiwa ni pamoja na RAF Fylingdales nchini Uingereza, ambazo zinaweza kufuatilia kombora hilo kuanzia urushaji wake hadi shabaha.
Je, Iran ina uwezo wa makombora ya masafa marefu?
Hata hivyo, urushaji huo haukufanikiwa, unaonesha kwamba Iran haijawa wazi kuhusu mpango wake wa makombora.
Tehran imesema hapo awali kwamba ilikuwa imepunguza umbali wa makombora yake kwa upande mmoja hadi kilomita 2,000. Lakini Israel sasa inadai kwamba makombora ya Iran yana umbali huo maradufu, hadi kilomita 4,000. Hilo linafanya Diego Garcia ionekane si sehemu pekee inayolengwa, bali pia sehemu kubwa ya bara la Ulaya.
Licha ya madai yake, Iran imekuwa ikijulikana kwa muda mrefu kuwa na makombora ya masafa mafupi, yenye umbali wa juu wa kilomita 3,000. Ni kile ambacho wamekuwa wakirusha mara kwa mara kwa Israel na mataifa jirani ya Ghuba katika wiki tatu zilizopita.
Kabla ya vita, Iran iliaminika kuwa na akiba ya makombora zaidi ya 2,000 ya masafa mafupi. Licha ya Marekani na Israel kulenga makombora haya, bado yanarushwa.
Haijulikani sana ni mpango wa makombora ya masafa mafupi wa Iran,wenye umbali wa kati ya kilomita 3,000 hadi kilomita 5,500.
Sidharth Kaushal, mtafiti mwandamizi katika taasisi ya ushauri ya Royal United Services Institute (Rusi) yenye makao yake makuu London, anasema kwamba "ilieleweka kwa muda mrefu kwamba Wairani walikuwa na mpango wa makombora ya masafa ya kati kabla ya vita hivi kuanza".
Alielezea dhana hiyo kwa msingi wa sababu mbili zinazowezekana. Kwanza, makombora ya masafa marefu yangehitajika ikiwa Iran ilitaka kutengeneza silaha ya nyuklia, ambayo imekanusha kila mara, licha ya shutuma za Magharibi. Pili ni kwamba Iran imehitaji kutengeneza makombora ya masafa marefu kwa ajili ya mpango wake wa anga za juu.
Ni makombora gani ambayo Iran ilifyatua kuelekea Diego Garcia?
Bado haijulikani ni aina gani ya makombora yaliyofyatuliwa kwenye kambi ya Marekani na Uingereza katika Bahari ya Hindi.
Kaushal anasema inaweza kuwa toleo la kombora la Khorramshah la Iran, ambalo linategemea mfumo wa hatua moja wa Korea Kaskazini.
Hilo lilikuwa na umbali wa zaidi ya kilomita 2,000 na kichwa cha tani 1.5.
Hata hivyo, Kaushal anasema "ungeweza kuongeza maradufu masafa hayo kwa urahisi kwa kutumia kichwa cha silaya ya kivita chepesi zaidi", ingawa kufanya hivyo kungesababisha uharibifu mdogo kwenye kambi ya Diego Garcia.
Kaushal pia alisema inawezekana kwamba Iran imekuwa ikibadilisha roketi kutoka kwa mpango wake wa anga za juu. Baada ya yote, Tehran imefanikiwa kuweka satelaiti angani na roketi kama Qaem 100 "zilieleweka kila wakati kuwa na uwezo wa matumizi mawili".
Hata hivyo, Iran haiwezekani kuwa na idadi kubwa ya makombora ya balestiki ya kati au hata ya masafa marefu.
Marekani na Israel tayari zimelenga mpango wa makombora ya balestiki wa Iran mwaka jana walipotaka kuharibu mpango wake wa nyuklia. Kilichobaki sasa ni kuwindwa.
Ukweli kwamba Iran ilirusha makombora mawili pekee kuelekea Diego Garcia unaonesha uwezo wake wa makombora ya masafa marefu ni mdogo.
Je, London inaweza kufikiwa?
Ikiwa Iran itachagua kulenga Ulaya, tayari kuna tahadhari kadhaa zilizowekwa ili kukabiliana na tishio hilo.
Marekani imekuwa na wasiwasi kwa muda mrefu kuhusu hatari za makombora ya masafa marefu yanayorushwa kutoka eneo la Mashariki ya Kati.
Chini ya Rais Barack Obama, Marekani ilianzisha mifumo ya ulinzi wa makombora ya masafa marefu nchini Poland na Romania, yote ikiwa ni sehemu ya mwavuli wa ulinzi wa anga wa Nato. Mifumo hii ya Aegis Ashore inarusha makombora yaleyale ya kuzuia yanayotumiwa na Jeshi la Wanamaji la Marekani kwa sasa kuangusha makombora ya masafa marefu ya Iran.
Uingereza yenyewe haina ulinzi mwingi wa makombora ya masafa marefu, pengo linaloonekana wazi lililotambuliwa katika Mapitio ya Ulinzi wa Kimkakati ya hivi karibuni ya serikali.
Lakini, kwa sasa, tishio hilo linaonekana kuwa mbali.
Kaushal anasema "inawezekana" kwamba roketi ya Iran "inaweza kufika London".
"Safu ya makombora ni kitu kinachoweza kunyumbulika kwa kuwa ukiweka kichwa chepesi cha kivita kwenye kombora, unaweza kupanua safu yake ya masafa," aliiambia BBC.
Kutumia makombora machache ya balistiki juu ya maeneo yenye ulinzi mkali wa anga ni vigumu, na hayana usahihi mkubwa yanapopigwa kutoka umbali mrefu sana''.
Mchambuzi wa utafiti Decker Eveleth wa Shirika la CNA, shirika lisilo la faida la utafiti na uchambuzi lenye makao yake makuu Washington DC, aliunga mkono.
Kuna "mambo mengi yasiyojulikana kuhusu muundo huo," aliiambia BBC.
kombora linaposafiri umbali mrefu zaidi, hupaa juu zaidi angani na hurudi chini kwa kasi kubwa zaidi, hivyo linahitaji kinga bora zaidi dhidi ya joto'', alisema.
Aliongeza kuwa ''kadiri kombora linavyosafiri kwa muda mrefu zaidi, ndivyo makosa madogo yanavyoongezeka katika mfumo wake wa uelekezaji, hivyo linakuwa na usahihi mdogo zaidi''.
"Ni kweli kwamba kombora linaweza kufika London," alihitimisha, lakini akaongeza: "Halitakuwa na uwezo wa kulenga hasa."
"Ninaweza kusema kuwa kiwango cha hatari kwa London ni cha chini sana," Eveleth alihitimisha.
Justin Crump wa kampuni ya ujasusi ya Sibylline alisema somo muhimu kutoka kwa jaribio la kushambulia Diego Garcia huenda lisiwe kuhusu uwezo wa makombora, bali wa vikosi vinavyoyafyatua.
"Iran bado inaweza kuishangaza Marekani na Israel baada ya wiki tatu za mabomu. Vikosi vyao vinaweza kuharibiwa, lakini hawako kwenye hali ya kushindwa," Crump aliambia BBC.