Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Marekani na Israel wana malengo sawa kuhusu vita dhidi ya Iran?
Rais wa Marekani Donald Trump, alitoa taarifa yenye "maneno makali" baada ya shambulio lililolenga kituo cha gesi cha Iran na Qatar siku ya Jumatano.
Israel iliishambulia Iran South Pars, eneo lililo na gesi asili na Tehran ilijibu shambulio hilo kwa kushambulia kituo cha nishati nchini Qatar, na hili lilimkasirisha Trump.
Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump aliitishia Iran, ila hakujua kuwa Israel ilikuwa imepanga kutekeleza shambulio hilo.
Kwa hivyo, semi za Trump zinaelezea nini kuhusu vita hivi, na kwa kiwango gani Israel na Marekani wanafungamana ikija katika mkakati wa kutekeleza mashambulizi?
Wacha tuchambue.
Marekani haikujua lolote kuhusu shambulio hilo
Rais wa Marekani alisema "sikujua lolote kuhusu shambulio hilo"
Matamshi yake yalisambaa katika magazeti ya Israel.
"Shambulio hilo lilifanyika kwa ushirikiano wa mapema na Marekani.. baada ya makubaliano kati ya Waziri mkuu Benjamin Netanyahu na Rais Trump wa Marekani," gazeti la Yedioth Ahronoth iliripoti.
Ila kwa kawaida katika matamshi ya Rais ni vigumu kujua ukweli.
Maneno aliyoyatumia kuelezea shambulizi la Israel yalikuwa ya hasira kwa kusema "Israel ilifanya shambulio hilo kwa kukurupuka" dhidi ya kituo cha gesi cha Iran.
Je, Trump anadokeza kwamba Israel ilitekeleza shambulio hilo bila busara?
Israel haitafanya "mashambulizi zaidi" kwenye vituo vya gesi
Kwa kawaida Donald Trump hutumia herufi kubwa katika maandishi yake, lakini katika chapisho la hivi karibuni, ametumia herufi kubwa mara moja tu.
"HAITAWEZEKANA TENA MASHAMBULIZI YOYOTE KUFANYWA NA ISRAEL kuhusu eneo muhimu la gesi la South Pars," aliandika, "isipokuwa Iran itaamua kwa kukosa busara kushambulia taifa lisilo na hatia, la Qatar."
Kwa rais anayependa kuonekana kuwa na udhibiti, je, hii ilikuwa ishara ya makubaliano yaliyokwisha kuafikiwa, au onyo kwa Benjamin Netanyahu?
Kama ilivyo kawaida kwa machapisho ya Trump ya kuandika mawazo yake kwenye mtandao wa Truth Social, si rahisi kuelewa moja kwa moja.
Hata hivyo, kuna ripoti zinazosema kuwa Trump alikasirishwa na mashambulizi ya Israel dhidi ya maghala ya mafuta ya Iran siku za kwanza za vita hivyo.
Je, malengo ya vita ya Israel na Marekani yanaanza kutofautiana?
Maafisa wa Israel wanasisitiza kuwa nchi hizo mbili zina shirikiana kikamilifu, hata kama mara kwa mara, , wanaonyesha dalili za utofauti.
Siku ya Alhamisi,Netanyahu alifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo alirudia kauli ya Trump, akisema kuwa Israel "ilitekeleza shambulio hilo kivyake" katika kushambulia eneo la gesi la Iran, na kwamba Trump aliomba vikosi vya Israel "visitishe" mashambulizi zaidi kama hayo.
Alijaribu kuonyesha picha kwamba yeye na Trump wako pamoja kuhusu Iran.
Alex Gandler, msemaji wa ubalozi wa Israel mjini London, aliiambia BBC, "Kwa kiasi kikubwa tunafungamana katika malengo yetu mengi au yote kuhusu utawala wa Kiislamu nchini Iran, Kikosi cha jeshi la Mapinduzi, pamoja na mipango yao ya makombora ya balistiki na nyuklia."
Lakini ingawa washirika hao wawili wanaonekana kukubaliana katika mambo mengi, Israel imekuwa ikisisitiza zaidi nia yake ya kutaka mabadiliko ya utawala nchini Iran.
Maafisa walionukuliwa katika vyombo vya habari vya Israel wameelezea shambulio la South Pars kama sehemu ya juhudi zinazoendelea kudhoofisha mamlaka ya utawala wa Iran.
"Usambazaji wa gesi kwa raia umekatizwa, na hilo litaleta uasi," afisa mmoja alimwambia mwandishi wa habari wa Yedioth Ahronoth.
Netanyahu hajawahi kuficha azma yake ya muda mrefu ya kutaka kuiangusha utawala wa Kiislamu, ambao yeye na Waisraeli wengi wanaiona kama tishio kwa wayahudi.
Wakati Marekani imeelekeza juhudi zake za kijeshi katika kudhoofisha uwezo wa Iran wa makombora na ndege zisizo na rubani na kuzamisha jeshi lake la majini, Israel imechukua hatua kubwa ya kuwaua viongozi wa Iran na kushambulia mifumo ya dola, ikiwa ni pamoja na vikosi vya kijeshi vya Basij ambavyo vilihusika kwa kiasi kikubwa katika kudhibiti maandamano mapema mwaka huu.
David Satterfield, aliyewahi kuwa mjumbe maalum wa Marekani Mashariki ya Kati, alisema malengo ya Israel na Marekani yanafanana isipokuwa inapokuja katika suala la wakati wa kusitisha mapigano hayo.
"Naamini kwamba Trump anatamani kupata njia ya kutangaza ushindi unaoaminika" aliiambia BBC. "Yeye hatafuti kubadilisha utawala wa Iran, hilo halina uhalisia wa kutokea"
Kuhusu Netanyahu, Satterfield alisema kuanguka kwa Iran na kuzuka kwa machafuko ni "lengo linalotamanika litokee" na Israel.
Iran "haikujua" ukweli kuhusu shambulio
Katika chapisho lake, Rais Trump anasisitiza kwamba Qatar haikuhusika wala haikuwa na taarifa ya mapema kuhusu mashambulizi hayo.
Lakini "kwa bahati mbaya," anaandika, "Iran haikujua hili" kabla ya kulipiza kisasi .
Tishio la kulipua uwanja wa gesi wa Iran
Iwapo Iran itashambulia tena miundombinu ya LNG (gesi asilia iliyoyeyushwa) ya Qatar, anaonya kuwa Marekani "ikiwa na au bila msaada au idhini ya Israel, italipua kwa kiwango kikubwa kabisa uwanja mzima wa gesi wa South Pars kwa nguvu na uwezo ambao Iran haijawahi kuona au kushuhudia."
Trump pamoja na Waziri wake wa Ulinzi, Pete Hegseth, wanajulikana kwa kauli kama hizi za vitisho vikali.
Donald Trump, anayejitaja kuwa "rais wa amani," mara nyingi hutumia lugha ya aina hii.
Kurejelea idhini ya Israel kutekeleza mashambulizi ni usemi unaoshangaza.
Je, hii ilikuwa ni kumkosoa Netanyahu na kumkumbusha, umuhimu wa kushauriana kwa karibu siku zijazo?
Huku baadhi ya wanachama wa harakati ya MAGA (Make America Great Again) ya Donald Trump tayari wakiamini kwamba ni Israel, si Marekani, inayoshika hatamu katika vita hivi, kuna hatari kwamba baadhi ya wakosoaji wa rais wanaweza kuona hili kama "kuteleza kwa ulimi"
Lakini huku bei za mafuta na gesi zikiongezeka tena,vita hivi vinaendelea kumpa Trump changamoto ambazo hakutarajia, ambazo utawala wake unaonekana haukuwa umejiandaa nazo.
Uungwaji mkono wa vita, ambao bado uko juu sana nchini Israel, uko chini ya 50% nchini Marekani. Mgogoro huu unaweza kumsaidia Netanyahu kupata muhula mwingine kama waziri mkuu, huku ukimgharimu pakubwa Donald Trump katika uchaguzi wa katikati ya muhula wa mwezi Novemba.
Israel na Marekani ni washirika wa karibu katika masuala ya ulinzi, lakini hii ndiyo mara ya kwanza wanapigana vita pamoja.
Kwa pamoja, wamepata mafanikio kadhaa chini ya muda wa wiki tatu.
Lakini kadri siku zinavyopita, vita hivi vinaonekana kuwa vigumu zaidi kuliko Donald Trump alivyotarajia.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula