'Tutawafuata popote wanapojificha': Mapambano dhidi ya Dola la Kiislamu Somalia

Chanzo cha picha, BBC/Amensisa Ifa
- Author, Sahnun Ahmed
- Nafasi, BBC News Somali
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Katika milima ya al-Miskad nchini Somalia, kundi la wanajeshi limekusanyika kuzunguka runinga ndogo inayoshikiliwa kwa mkono, likiwafuatilia wapiganaji wa kundi la Islamic State kwa ndege zisizo na rubani.
Mtu anaonekana kwenye runinga, akitembea katika bonde. "Anatafuta maji kwa ajili ya marafiki zake," anasema mwendeshaji wa ndege zisizo na rubani. "Anakimbia na amebeba kitu mgongoni mwake," anaongeza askari mwingine.
Mwanaume aliye kwenye skrini yuko karibu na pango, ambalo jeshi linaamini ni maficho ya wapiganaji 50 hadi 60 wa IS.
Kikosi cha Ulinzi cha Puntland kina takriban wanajeshi 500 waliowekwa katika kambi hii kaskazini-mashariki mwa Somalia. Miaka kumi iliyopita, eneo hilo lilikuwa makazi ya jamii za kuhamahama, lakini hilo limebaadilika baada ya IS kuvamia hapa, ikielekeza nguvu zake Afrika huku wapiganaji wake wakifukuzwa kutoka ngome zao nchini Syria na Iraq.
Kufikia Aprili 2025, Jenerali Michael Langley, ambaye wakati huo alikuwa kamanda wa Kamandi ya Marekani ya Afrika (Africom), aliliambia Bunge la Marekani "ISIS inadhibiti mtandao wao wa kimataifa kutoka Somalia".
Na katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imeunga mkono mapambano ya Somalia dhidi ya IS, ikishambulia mara kwa mara waasi waliojificha kwenye mapango ya Somalia - 2025 Pentagon ilitekeleza mashambulizi 60 dhidi ya IS-Somalia.

Chanzo cha picha, BBC/Amensisa Ifa
"Uwezo wa IS wa kufanya mashambulizi nchini Somalia umepungua" na "hautoi tishio kubwa kwa Puntland au Somalia leo", anasema Tricia Bacon, mkurugenzi wa Kituo cha Kupambana na Ugaidi katika Chuo Kikuu cha Marekani huko Washington DC.
Hata hivyo, IS-Somalia bado "ina jukumu muhimu katika kutoa rasilimali, usaidizi, na uwezeshaji kwa washirika wengine wa Dola ya Kiislamu, barani Afrika na mbali zaidi, kama vile Afghanistan", anaelezea.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
IS-Somalia, yenye makao yake makuu katika eneo lenye uhuru wa ndani la Puntland kaskazini-mashariki mwa nchi, ilianzishwa na raia wa Somalia, Abdulqadir Mumin. Aliwahi kuishi Sweden na Uingereza na alikuwa na uraia wa Uingereza.
Mwaka 2015 alionekana pamoja na wanaume 17 katika video wakiahidi utii kwa IS. Mumin hapo awali alikuwa mwanachama wa kundi la wanamgambo la al-Shabab, ambalo linapigana na serikali kwa miongo miwili na bado linadhibiti sehemu kubwa za kusini mwa Somalia.
IS-Somalia iliwafukuza al-Shabab kutoka milima ya al-Miskad ya Puntland, na kuwaleta wapiganaji wa kigeni na polepole kuwa kitovu cha mafunzo na kifedha kwa mtandao mpana wa IS.
Kundi hilo lilikuwa na ushawishi katika mji wa bandari wa Bosaso na ripoti ya serikali ya Marekani inasema mwaka 2022 IS-Somalia "ilikusanya dola milioni 2 [pauni milioni 1.5] kutokana na malipo ya biashara za ndani, uagizaji, mifugo, na kilimo".
Vikosi vya Puntland vilifanikiwa kuwafukuza IS-Somalia kutoka Bosaso mwanzoni mwa 2025, lakini kundi hilo la wanamgambo bado lilidhibiti vijiji na miji midogo katika milima ya al-Miskad iliyo karibu.

Chanzo cha picha, BBC/Amensisa Ifa
Sheria za IS Somalia
Mojawapo ya miji hiyo ni Dardar, yenye wakaazi 600. Uwepo wa IS ulileta ukatili na hofu.
Watu wanaoishi hapa wanasema sheria kali ziliandikwa kwenye ubao mweusi katika kijiji kilicho zikiwakataza wanaume na wanawake kuchanganyika hadharani, zikiwakataza wanaume kuvaa suruali ndefu chini ya vifundo vya miguu au kukata nywele kwa mtindo wa kisasa.
Wanawake walilazimika kuvaa aina maalum ya hijabu wakiwa na glavu na soksi ili kufunika mikono na vifundo vya miguu, na muziki haukuruhusiwa.
Utawala mkali na itikadi uliacha makovu makubwa.
"Maisha yakawa magumu sana," anasema Said Mohamud Ibrahim, imamu wa eneo hilo, akiwa ameketi sakafuni mwa msikiti wake. "Watu waliogopa. Baadhi walitekwa nyara na bado hawajulikani walipo."
Huku baadhi ya watu wakikimbia kijiji, yeye alibaki, lakini anasema IS walimfukuza msikitini. "Walisema: 'Sisi ndio imamu sasa. Na usipofuata maagizo yetu na kuondoka msikitini sasa hivi, utapata unachostahili.'
"Nilielewa hilo kwamba wangenikata kichwa au wangeniteka nyara."
Miongoni mwa waumini katika msikiti huo ni Mahad Jama. Miaka miwili iliyopita mpwa wake, Shukri, alitekwa nyara na kuuawa na wapiganaji wa IS.
"Alikuwa msichana mzuri, binti mwenye upendo sana, alimtunza mama yake. Alikuwa Mwislamu anayefanya kazi," anasema.
Shukri alikuwa mjamzito alipouawa. Aliacha watoto wawili na mama mmoja mgonjwa.
"Huwezi kufikiria jinsi ninavyohisi kumpoteza mpwa... na hata hujui ni kwa nini aliuawa. Unapopokea habari za kifo cha mtoto wake, ni vigumu kuamini," Jama anaongeza.
Shukri alikuwa na mtoto wa kiume wa miaka saba anayeitwa Said. Mvulana huyo mdogo alikuwa kiziwi na mara nyingi alikuwa karibu na mamake. Usiku ule IS walipokuja nyumbani kwao alikuwa pamoja naye. Naye pia aliuawa.
Baada ya miezi mingi ya mapigano, kijiji hicho kilitekwa na Jeshi la Ulinzi la Puntland Februari 2025. Wamarekani walikuwa wamesaidia, wakiwalenga na kuwaua wanamgambo watatu wa IS Mei 2024.

Chanzo cha picha, BBC/Amensisa Ifa
Hata hivyo, IS bado ina vituo katika eneo hilo.
Muna Ali Dahir, ni afisa mwenye umri wa miaka 32, ni mmoja wa wanawake wachache miongoni mwa wanajeshi hapa.
Amepigana vitani hapo awali: "Tulipigana kwa bidii na tukashinda… kwa sababu hii ni nchi yetu," anasema.
Hata hivyo, wakati huu, anakaa kwenye kambi, akijiandaa kwa majeruhi wanaoweza kutokea.
Askari mmoja kijana anatuonyesha picha kwenye simu yake akiwa ameshika mkono wa mpiganaji wa IS ambaye alimkamata. Mfungwa huyo ni mrefu na mkubwa kuliko yeye, mwenye ndevu nyeusi nene na nywele ndefu. Askari mwingine ameshika mkono mwingine.
"Huyu ni Hassan. Mwanaume wa Kituruki tuliyemkamata," anasema Abdikhair Abdiriza Jama mwenye umri wa miaka 24.
Juni 2025, Umoja wa Mataifa ulikadiria kwamba kundi la Islamic State lina wapiganaji hadi 800 nchini Somalia, zaidi ya nusu yao ni wageni.
Vikosi vya Puntland vinadai kuwaua mamia ya wanachama wa IS katika kipindi cha miezi 16 iliyopita, na vimetoa picha za zaidi ya wapiganaji 50 wa kigeni waliokamatwa, kutoka nchi ikiwemo Ethiopia, Morocco na Syria.
Mamlaka ya Puntland inasema wale wanaozuiliwa wanakabiliwa na mashtaka, na katika baadhi ya matukio, adhabu ya kifo.

Chanzo cha picha, BBC/Amensisa Ifa
Abddikhair Jama alikuwa na umri wa miaka 14 wakati IS walipokuja katika eneo hili kwa mara ya kwanza. "Sikuamini kwamba walikuwepo. Mwanzoni, nilidhani ni propaganda tu," anasema. "Lakini nilipomshikilia mmoja wao ... niligundua kuwa wapiganaji wa kigeni walikuwa wakishambulia nchi yetu."
Wakati tukizungumza nao, mlipuko mkali unasikika. Bunduki nzito na vifaa vinapakiwa kwenye ngamia na wanajeshi wanatoka nje ya kambi hiyo katika vikundi vidogo kwa ajili ya kushambulia ngome za IS.
Kamanda wa jeshi anaelezea kwamba ndege isiyo na rubani ya Marekani iko angani ikikusanya taarifa za kijasusi, na kusaidia kubaini wapi pa kufyatua risasi.
Baada ya mapigano droni inatumwa tena, wakati huu ili kutathmini uharibifu, na kwenye runinga ndogo, mlango wa pango unaonekana umeungua.
Mwanaume aliyeonekana akikimbia bondeni hapo awali haonekani tena, ukiangalia chini kutoka mlimani, haiwezekani kujua jinsi shambulio lilivyoleta ufanisi.
Jeshi la Ulinzi la Puntland liligundua kuwa ndege zisizo na rubani za Marekani baadaye zilihusika na kuwapiga wapiganaji ndani ya mapango - haijulikani ni wangapi.
Mapambano dhidi ya IS nchini Somalia hayajaisha.
Tricia Bacon katika Chuo Kikuu cha Marekani anaonya kwamba ingawa IS-Somalia "imedhoofika... ila imethibitika kuwa ni shirika lenye uwezo wa kupona na kujipanga upya."
Na Abddikhair Jama anasema: "Hatutasimama hadi mpiganaji wa mwisho atakapokamatwa."
"Iwe inachukua miaka 10 au 15, tutakwenda popote wanapohamia au kujificha. Ni pale tu ardhi itakaposafishwa kikamilifu ndipo tutapumzika."
Wakati huo huo, yeye na wanajeshi wengine wanaendelea kuishi katika mazingira magumu. Hakuna maji ya bomba au umeme na wanalala katika mahema ya muda yaliyotengenezwa kwa matawi, maturubai na mawe. Wanaishi na mbuzi wanaowafuga na vifaa vinavyoletwa mara mbili kwa siku kwa helikopta.
Katika nyakati tulivu katikati ya vita, Dahir huipigia simu familia yake - ana watoto wanane lakini amewaona mara mbili tu katika mwaka uliopita. Anasema watoto wake ndio motisha yake.














