Uingereza yakataa kujiingiza katika vita vya Mashariki ya Kati
Starmer amesema Mlango Bahari wa Hormuz lazima ufunguliwe tena ili "kuhakikisha utulivu katika masoko".
Muhtasari
- Uingereza haitaingizwa kwenye 'vita vikubwa', Starmer
- Raia wa Nigeria ajeruhiwa katika mashambulizi ya Umoja wa Falme za Kiarabu
- Kenya na Urusi zakubali kusitisha usajili wa Wakenya
- Iran yaminya mtandao zaidi
- Uingereza inashirikiana na washirika wake kupata njia muafaka ya kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz
- Israel yaanza 'wimbi kubwa' la mashambulizi nchini Iran
- Starmer anapaswa kufikiria kutuma meli za kivita Mashariki ya Kati, mkuu wa zamani wa ulinzi wa Uingereza anasema
- EU kujadili namna ya kufanya kuweka wazi Mlango Bahari wa Hormuz wazi
- China yamjibu Trump kuhusu kusitishwa mara moja kwa operesheni za kijeshi, baada ya maoni ya Trump
- Nchi za Ghuba zaripoti mashambulizi zaidi ya Iran usiku kucha
- Tuzo za Oscar 2026: Orodha ya washindi kamili
- Trump: Ikiwa washirika hawatasaidia kufungua mlango wa bahari wa Hormuz, itakuwa mbaya sana kwa mustakabali wa NATO.
- Kiongozi wa upinzani nchini Uganda asema alikimbilia nje ya nchi akihofia maisha yake
- Trump: Iran inataka kufanya mazungumzo
- Habari za kijasusi za Marekani zinaonyesha Khamenei alikuwa anahofia mwanawe kumrithi
- Israel yasema bado ina maeneo mengi ya kushambulia nchini Iran, huku Trump na Starmer wakijadili Mlango wa Hormuz
Moja kwa moja
Abdalla Seif Dzungu & Asha Juma
Uingereza haitaingizwa kwenye 'vita vikubwa', Starmer

Chanzo cha picha, PA Media
Waziri Mkuu Sir Keir Starmer amesema Uingereza inashirikiana na washirika wake katika "mpango wa pamoja na wenye tija" wa kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz.
Hii inakuja baada ya Rais Trump kuihimiza Uingereza na nchi zingine kutuma meli za kivita katika Ghuba ili kusaidia kulinda njia ya usafirishaji, ambayo ni muhimu kwa usambazaji wa mafuta duniani.
Sir Keir aliambia mkutano na waandishi wa habari kwamba Uingereza tayari ina meli za kutafutaji mabomu baharini katika eneo hilo lakini bado hakuna uamuzi kuhusu hatua gani zichukuliwe.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba hataruhusu Uingereza kuingizwa katika "vita kubwa".
Mlango Bahari umefungwa hivyo, tangu vita vya na Iran vilipoanza, na kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta.
Iran imetishia kushambulia meli zozote inazoona zina uhusiano na Marekani, huku pia kukiwa na hatari kutokana na mabomu ya baharini.
Soma zaidi:
Raia wa Nigeria ajeruhiwa katika mashambulizi ya Umoja wa Falme za Kiarabu

Chanzo cha picha, Reuters
Raia wa Nigeria amejeruhiwa kufuatia mashambulizi ya hivi majuzi ya makombora na ndege zisizo na rubani zinazohusiana na mzozo unaohusisha Iran, Marekani na Israel, kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Nigeria.
Msemaji Kimiebi Ebienfa aliambia BBC siku ya Jumatatu kwamba raia huyo wa Nigeria alipata jeraha dogo la mkono.
"Alitibiwa katika kituo cha matibabu na ameruhusiwa kwenda nyumbani," Bw Ebienfa alisema.
Hakutoa maelezo zaidi kuhusu ni wapi au lini tukio hilo lilitokea.
Mwishoni mwa wiki, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ulisema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilinasa makombora tisa ya balistiki na ndege zisizo na rubani 33 zilizorushwa kutoka Iran.
Wizara ya Ulinzi ya UAE ilisema tangu kuanza kwa mashambulizi hayo, vikosi vyake vimenasa makombora 294 ya balestiki, makombora 15 ya baharini na ndege zisizo na rubani 1,600.
Mamlaka zinasema kuwa mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu sita, wakiwemo raia kutoka UAE, Pakistan, Nepal na Bangladesh na kujeruhi wengine 141.
Miongoni mwa waliojeruhiwa ni raia wa Afrika kutoka Nigeria, Ghana, Ethiopia, Misri na Uganda.
Soma zaidi:
Kenya na Urusi zakubali kusitisha kuajiri Wakenya kupigana vita Ukraine

Chanzo cha picha, Kuloba family
Kenya inasema raia wake hawatasajiliwa tena kujiunga na jeshi Urusi katika vita vya Ukraine, kufuatia mazungumzo kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili mjini Moscow.
Akizungumza pamoja na Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi Jumatatu alisema serikali hizo mbili zimefikia maelewano baada ya wasiwasi mkubwa nchini Kenya kuhusu ripoti za raia wake kujiunga na mzozo huo.
"Raia wa Kenya hawatastahili tena kusajiliwa kupitia Wizara ya Ulinzi kuhusiana na operesheni maalum za kijeshi," Bw Mudavadi aliambia wanahabari.
"Kutokana na wasiwasi ulioonyeshwa na familia za Wakenya huko Nairobi, tunaamini tumepata maelewano ili kusiwe na usajili zaidi." Aliongeza kuwa Kenya pia imepata hakikisho kwamba raia walioko Urusi kwa sasa wataweza kupata usaidizi wa kibalozi ikihitajika.
Aliongeza kuwa Kenya pia imepata hakikisho kwamba raia walioko Urusi kwa sasa wataweza kupata usaidizi wa kibalozi ikihitajika.
Bw Mudavadi alisisitiza suala hilo lisiathiri uhusiano mpana kati ya Kenya na Urusi.
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi alisema baadhi ya raia wa Kenya walikuwa wamejiunga na jeshi la Urusi kwa hiari.
"Raia wa Kenya, kama raia wa nchi nyingine, wametia saini mikataba na jeshi la Urusi kwa hiari," Lavrov alisema, akiongeza kuwa Moscow iliheshimu maelewano yaliyofikiwa na Nairobi.
Suala hilo limesababisha hisia zaidi baada ya ripoti ya kijasusi iliyowasilishwa kwa wabunge mwezi Februari kusema zaidi ya Wakenya 1,000 wamesajiliwa kupigana upande wa Urusi katika vita dhidi ya Ukraine.
Soma zaidi:
Iran yaminya mtandao zaidi

Chanzo cha picha, Netblocks
BBC Verify imeshuhudia kupungua kwa idadi ya video zinazosambazwa kutoka ndani ya Iran hiyo ikiwa dokezo kwamba mamlaka zimeminya sana matumizi ya intaneti.
Mwanamke mmoja kutoka Tehran aliiambia BBC kwamba baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumia huduma ya intaneti ya setilaiti ya Elon Musk ya Starlink ili kuepuka vikwazo hivyo wamekamatwa.
Mwanamume mmoja wa Iran ambaye amewasiliana na BBC alisema viunganishi vya Starlink vilikuwa vikikatwa.
Kundi la ufuatiliaji la Netblocks linasema limefuatilia "kuporomoka kwa muunganisho" kwenye mtandao muhimu wa mawasiliano ambao ulikuwa umebaki mtandaoni kwa kiasi fulani.
Tunajua Iran imeendelea kuwa na "baadhi ya watu" kama maafisa, vikundi vinavyohusiana na serikali na waandishi wa habari ufikiaji wa intaneti - lakini hatua ya hivi karibuni inaonyesha hata baadhi ya miunganisho hiyo imepunguzwa.
Mamlaka ya Iran ilichukua hatua ya kuzuia muunganisho wa intaneti mnamo tarehe 28 Februari baada ya Marekani na Israeli kuanzisha mashambulizi yao ya kwanza ya angani.
Ufikiaji wa waandishi wa habari wa kimataifa nchini Iran umezuiliwa sana kwa hivyo kupata picha na ujumbe ni njia muhimu ya kuripoti vita kutoka ndani ya nchi.
Kuzuia intaneti kutakuwa na athari katika jinsi na wakati tunapopata taarifa mpya kutoka Iran.
Soma zaidi:
Uingereza inashirikiana na washirika wake kupata njia muafaka ya kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz

Chanzo cha picha, EPA
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema ni wazi kwamba operesheni ya Marekani "imedhoofisha kwa kiasi kikubwa" uwezo wa kijeshi wa "utawala wa kuchukiza nchini Iran".
Lakini baada ya mzozo huo Starmer amesema kutakuwa na haja ya kuwa na aina fulani ya "makubaliano ya mazungumzo" kupunguza uwezo wa Iran wa kujenga upya mpango wao wa nyuklia na usalama wa meli za kimataifa.
Amesema Mlango Bahari wa Hormuz lazima ufunguliwe tena ili "kuhakikisha utulivu katika masoko".
"Hiyo si kazi rahisi," amesema, na ndiyo maana Uingereza inafanya kazi na "washirika wetu wote" kupata "mpango unaofaa" wa kurejesha uhuru wa urambazaji kwenye eneo hilo.
Soma zaidi:
Israel yaanza 'wimbi kubwa' la mashambulizi nchini Iran

Chanzo cha picha, Reuters
Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) limeanza wimbi "pana" la mashambulizi katika sehemu za Iran.
Katika chapisho kwenye programu ya ujumbe ya Telegram, inasema: "IDF imeanza tu wimbi kubwa la mashambulizi yanayolenga miundombinu ya utawala wa kigaidi wa Iran huko Tehran, Shiraz, na Tabriz."
Marekani na Israel zimekuwa zikiendelea na mashambulizi dhidi ya Iran na kumekuwa na ripoti za mabomu makubwa mjini Tehran usiku kucha.
Nchi za Ghuba pia zimekuwa zikiripoti mashambulizi zaidi ya Iran usiku kucha
Soma zaidi:
Starmer anapaswa kufikiria kutuma meli za kivita Mashariki ya Kati, mkuu wa zamani wa ulinzi wa Uingereza asema

Chanzo cha picha, PA Media
Waziri mkuu wa Uingereza anapaswa kuwa tayari kutuma meli za kivita, pamoja na ndege zisizo na rubani, Mashariki ya Kati ili kuiunga mkono Marekani katika vita vyake na Iran, anasema Mkuu wa zamani wa Wafanyakazi wa Ulinzi wa Uingereza.
Jenerali Sir Nick Carter anaambia kipindi cha BBC Radio 4 cha Today kwamba ni kwa "maslahi ya kitaifa" ya Uingereza kuweka Mlango-Bahari wa Hormuz wazi, na pia ni muhimu kwa uchumi wa dunia.
Alipoulizwa kuhusu uwezo wa Iran, anasema jeshi la majini la Iran linaweza kuwa dhaifu kuliko ilivyokuwa lakini jeshi la majini la Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) "bado liko tena imara".
Jenerali Carter ameongeza kuwa silaha za IRGC zinajumuisha makombora yanayoegemea ufukweni, ndege zisizo na rubani, boti za mwendo kasi zenye silaha, meli zisizo na rubani na mabomu. "Wamekuwa wataalamu wa kudhibiti Mlango Bahari huo," anasema.
"Nadhani kile tunachotaka kukiona ni operesheni iliyoratibiwa vizuri, inayoongozwa na Wamarekani wenye mataifa mengi yanayohusika nayo," Jenerali Carter pia alisema.
Aliendelea kwa kusema "huwezi kufanya hivi peke yako; itahitaji uwezo wa kila mtu kuungana ili kufanikisha hili na itakuwa operesheni ngumu sana na ya makusudi".
Soma zaidi:
EU kujadili namna ya kufanya kuweka wazi Mlango Bahari wa Hormuz wazi

Chanzo cha picha, EPA
Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zitazungumzia kile kinachoweza kufanywa kutoka upande wa Ulaya ili kuweka Mlango-Bahari wa Hormuz wazi, mkuu wa sera za kigeni wa kambi hiyo amesema.
"Ni nia yetu kuweka Mlango-Bahari wa Hormuz wazi," Kaja Kallas amesema kabla ya mkutano wa mambo ya nje wa EU huko Brussels, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Meli kadhaa zimeripotiwa kushambuliwa tangu mgogoro huo uanze walipojaribu kupitia njia nyembamba, ambayo kwa kawaida 20% ya mafuta duniani hupitia.
Kama tulivyoripoti muda mfupi uliopita, Rais wa Marekani Donald Trump amesema hali "itakuwa mbaya sana kwa mustakabali wa Nato" ikiwa washirika wa Marekani hawatasaidia kuulinda.
Siku ya Jumapili, Uingereza ilisema Trump alizungumza na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer kuhusu umuhimu wa kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz "ili kukomesha usumbufu kwa usafirishaji wa kimataifa".
Soma zaidi:
China yamjibu Trump kuhusu kusitishwa mara moja kwa operesheni za kijeshi, baada ya maoni ya Trump

Chanzo cha picha, Getty/ Reuters
Maelezo ya picha, Rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa Marekani Donald Trump China imejibu baada ya Rais Trump hapo awali, katika mahojiano na gazeti la Uingereza la Financial Times, kutishia kuchelewesha mkutano wa kilele na kiongozi wa China Xi Jinping ikiwa Beijing haitatuma msaada wa kusaidia kufua mlango wa bahari wa Hormuz.
Alipoulizwa kuhusu maoni ya rais wa Marekani, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China alisema "diplomasia ya mkuu wa nchi ina jukumu la kimkakati lisiloweza kubadilishwa katika uhusiano wa China na Marekani", kabla ya kuongeza "pande hizo mbili zimedumisha mawasiliano kuhusu ziara ya Rais Trump".
Akijibu swali kuhusu Trump akitaka meli za kivita zipelekwe kwenye Mlango wa Bahari, Lin Jian anasema kuwa mivutano ya hivi karibuni imevuruga njia za biashara na kudhoofisha amani ya kikanda na kimataifa.
"China inasisitiza wito wake kwa pande zote kusitisha mara moja operesheni za kijeshi," msemaji huyo anasema na kuongeza "tumejitolea kuzuia kuendelea kwa vita".
Nchi za Ghuba zaripoti mashambulizi zaidi ya Iran usiku kucha

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Uwanja wa ndege wa Dubai Mamlaka zinasema kuwa sasa zimedhibiti moto katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai na kwamba hakuna majeraha yaliyoripotiwa baada ya ndege isiyo na rubani kushambulia tangi la mafuta.
Iran imerusha takriban makombora na ndege zisizo na rubani 2,000 katika Umoja wa Falme za Kiarabu wakati wa vita - huku mengi yakinaswa na walinzi wa anga.
Saudi Arabia inasema ilidungua makumi ya ndege zisizo na rubani usiku kucha na Iraq na Kuwait ziliripoti mashambulizi mapya.
Huku Marekani na Israel zikiendelea na mashambulizi dhidi ya Iran, kuna ripoti za mashambulizi makali ya mabomu mjini Tehran.
Kulikuwa na mlipuko mkubwa katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, ambapo jeshi la Israel linasema lililenga miundombinu ya Hezbollah.
Huko Israel, ving'ora vilisikika kutokana na makombora ya Hezbollah yanayoingia kaskazini na makombora ya Iran upande wa kusini.
Tuzo za Oscar 2026: Orodha ya washindi kamili

Chanzo cha picha, Getty Images
Nyota bora zaidi wa Hollywood wametunukiwa tuzo zinazotamaniwa zaidi katika tasnia ya filamu, Oscars.
Pambano moja baada ya lingine liliongoza huku Jessie Buckley wa Hamnet na Michael B Jordan wa Sinners wakinyakua tuzo bora zaidi. Tazama orodha ya washindi hapa chini.
Picha Bora
- Mshindi: One Battle After Another
- Bugonia
- Frankenstein
- F1
- Hamnet
- Marty Supreme
- The Secret Agent
- Sentimental Value
- Sinners
- Train Dreams
Muigizaji bora wa kike
- Mshindi: Jessie Buckley - Hamnet
- Rose Byrne - If I Had Legs I'd Kick You
- Kate Hudson - Song Sung Blue
- Renate Reinsve - Sentimental Value
- Emma Stone - Bugonia
Muigizaji bora wa kiume
- Mshindi: Michael B Jordan - Sinners
- Timothée Chalamet - Marty Supreme
- Leonardo DiCaprio - One Battle After Another
- Ethan Hawke - Blue Moon
- Wagner Moura - The Secret Agent
Muigiza msaidizi bora wa kike
- Mshindi: Amy Madigan - Weapons
- Elle Fanning - Sentimental Value
- Inga Ibsdotter Lilleaas - Sentimental Value
- Wunmi Mosaku - Sinners
- Teyana Taylor - One Battle After Another
Muigizaji msaidizi bora wa kike
- Mshindi: Sean Penn - One Battle After Another
- Benicio del Toro - One Battle After Another
- Jacob Elordi - Frankenstein
- Delroy Lindo - Sinners
- Stellan Skarsgård - Sentimental Value
Mkurugenzi bora wa filamu
- Mshindi: Paul Thomas Anderson - One Battle After Another
- Ryan Coogler - Sinners
- Josh Safdie - Marty Supreme
- Joachim Trier - Sentimental Value
- Chloé Zhao - Hamnet
Trump: Ikiwa washirika hawatasaidia kufungua mlango wa bahari wa Hormuz, mustakabali wa NATO utakuwa mbaya sana

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Mkondo wa bahari wa Hormuz Donald Trump aliliambia gazeti la Financial Times kuwa ni "kawaida" kwa nchi zinazonufaika na Mlango-Bahari wa Hormuz kusaidia kuufungua tena, kwa sababu, alisema, Ulaya na China zinategemea sana mafuta yanayotoka Ghuba ya Uajemi.
Alionya kwamba ikiwa nchi zingine hazitajibu, inaweza kuwa "mbaya sana kwa mustakabali wa NATO," akiongeza kuwa Marekani imekuwa "mkarimu sana" kwa washirika wake wa Ulaya.
Bw. Trump aliendelea: "Hatukuhitaji kuisaidia Ukraine. Ukraine iko maelfu ya maili kutoka kwetu ... lakini tuliwasaidia.
Sasa tutaona kama watatusaidia au la. Kwa sababu nimekuwa nikisema kwa muda mrefu kwamba tuko kwa ajili yao, lakini hawatatusaidia, na sina uhakika kwamba wako kwa ajili yetu."
Maoni ya Bw Trump yanakuja siku moja baada ya kuzitaka China, Ufaransa, Japan, Korea Kusini na Uingereza kuungana na "juhudi za pamoja" za kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz.
Mlango wa bahari wa Hormuz ndio njia ya bahari yenye shughuli nyingi zaidi kwa usafirishaji wa mafuta duniani, na takriban asilimia 20 ya usambazaji wa mafuta ulimwenguni hupitia humo.
Baada ya kuanza kwa vita kati ya Marekani na Israel na Iran, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi limetishia mara kwa mara kutoruhusu meli za mafuta kupita kwenye mkondo huo wa bahari na kulenga meli kadhaa za mafuta ambazo zilikuwa zikijaribu kupakia na kupita kwenye mkondo huo wa bahari.
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda asema alikimbilia nje ya nchi akihofia maisha yake

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Robert Kyagulani Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine ameiambia BBC kwamba aliondoka nchini baada ya uchaguzi wa Januari uliokumbwa na utata kwa sababu alihofia maisha yake.
Aliiambia Newshour kutoka eneo lisilojulikana baada ya miezi miwili kujificha: "Ilikuwa wazi kwamba serikali ilitaka kuniondoa."
Mwanamuziki huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa mapema alitangaza kuikimbia nchi katika video iliyotumwa kwenye mtandao wa X.
Ndani yake, alirudia madai yake kwamba uchaguzi huo uliibiwa kwa kumpendelea Rais wa Uganda Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu 1986.
Museveni, 81, alishinda kwa asilimia 72 ya kura na kushutumu upinzani kwa kutaka kupindua matokeo kupitia vurugu.
Wine, 44, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu, aliambia BBC kwamba katika muda wa miezi miwili akiwa mafichoni alikuwa amehifadhiwa na wafuasi, akisema: "Watu walinipa chakula, watu walinipa nguo na kila kitu kingine."
Alisema Museveni alijaribu "mara nyingi" kumuua na kwamba mtoto wa rais "ameweka wazi zaidi bila kuchuja maneno yake".
Mtoto wa Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye anaongoza jeshi la Uganda, alisema Wine "alitafutwa akiwa hai au akiwa hai", bila kumshtaki kwa makosa yoyote maalum, na pia alitishia kuhasiwa.
Ujumbe huo umefutwa kutoka kwa akaunti yake ya X. Wakati huo huo, baadhi ya wanachama wa serikali wamekanusha kuwa vyombo vya usalama vimekuwa vikimsaka.
BBC imewataka polisi kutoa maoni yao. Wine alisema katika mahojiano siku ya Jumapili: "Hata nikiwa nje ya Uganda, bado siko salama kwa sababu najua kwamba ninafuatiliwa na utawala... ambao unaweza kuwasaka maadui wake wa kisiasa popote walipo."
Trump: Iran inataka kufanya mazungumzo

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Trump akiwa katika Airforce One Akiwa ndani ya Air Force One, Trump pia alizungumza kwa ujumla zaidi kuhusu vita.
Alisema Iran inataka kufanya mazungumzo na inatumia AI kupotosha wakati akiwasilisha msimamo mmoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Trump alirudia madai yake kwamba Iran inataka makubaliano, akisema kuhusu mazungumzo ya kidiplomasia kwamba "tunazungumza nao lakini sidhani kama wako tayari, lakini wanakaribia sana".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema kuwa Tehran "haijawahi kuomba kusitishwa kwa mapigano, hatujawahi kuomba hata mazungumzo"
Alipoulizwa kama yuko tayari kutangaza ushindi dhidi ya Iran alisema "hakuna sababu" na kuongeza kuwa Marekani imesababisha uharibifu mkubwa ili "tukiwaacha sasa hivi ingewachukua miaka 10 kuijenga upya"
Trump alidai kuwa picha za maelfu ya watu waliokusanyika katika katika bustani kuonyesha kumuunga mkono Mojtaba Khamenei, pamoja na ripoti kuhusu "boti za kamikaze" na mashambulizi kwenye USS Abraham Lincoln zote zilitokana na AI, lakini hakutoa ushahidi.
Alipoulizwa ikiwa aligombana na Netanyahu, Trump alisema: "Hapana, kwa kweli tunaelewana." Alisema atauita uhusiano wake na Netanyahu "wa ajabu"
Trump pia alisema bei ya mafuta "itashuka mara tu vita vitakapomalizika na vita vitaisha haraka sana"
Habari za kijasusi za Marekani zinaonyesha Khamenei alikuwa anahofia mwanawe kumrithi

Chanzo cha picha, Tasnim News Agency
Maelezo ya picha, Mojtaba Khamenei Habari mpya za kijasusi kutoka Marekani zinasema kwamba aliyekuwa kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alikuwa na mashaka kuhusu mtoto wake kuchukua nafasi yake, vyanzo vingi vimeiambia BBC mshirika wa vyombo vya habari vya Marekani CBS News.
Inaripotiwa kwamba Khamenei alikuwa na wasiwasi kuhusu mtoto wake Mojtaba Khamenei kuchukua madaraka kwani alionekana kuwa "si mkali sana" na "hajahitimu" kuwa kiongozi.
Vyanzo vya habari pia vililiambia chapisho hilo kwamba marehemu kiongozi mkuu alikuwa anajua kuwa mtoto wake alikuwa na "matatizo katika maisha yake ya kibinafsi".
CBS inaripoti kwamba taarifa hizo tayari zimesambazwa kwa Rais wa Marekani Donald Trump na "watu wachache wanaomzunguka". Ayatollah Mojtaba Khamenei, 56, alichaguliwa kuwa kiongozi mkuu wa Iran wikendi iliyopita.
Israel yasema bado ina maeneo mengi ya kushambulia nchini Iran, huku Trump na Starmer wakijadili Mlango wa Hormuz

Chanzo cha picha, Reuters
Effie Defrin, msemaji wa jeshi la Israel, ametoa taarifa kwa njia ya televisheni. Anasema jeshi la Israel bado lina "maelfu" ya shabaha za kushambulia Iran.
Defrin's alinukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema: "Tunatambua shabaha mpya kila siku."
Wakati huohuo Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Rais wa Marekani Donald Trump wamejadili "hali inayoendelea katika Mashariki ya Kati na umuhimu wa kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz ili kumaliza usumbufu wa usafirishaji wa mafuta duniani".
Simu hiyo na Trump ilidumu kwa dakika 15, kulingana msemaji wa Downing Street.
Zaidi ya kujadili Mlango-Bahari wa Hormuz na rais wa Marekani, Starmer "pia alitoa rambirambi zake kwa wanajeshi wa Marekani ambao walipoteza maisha wakati wa vita".
Natumai hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja
