Chanzo cha uhasama kati ya Marekani na Cuba

Chanzo cha picha, Bettmann Archive / Getty Images
Ni mojawapo ya mvutano wa muda mrefu zaidi katika historia ya siasa za sasa. Ni kati ya nchi yenye nguvu zaidi duniani dhidi ya kisiwa chenye wakazi chini ya milioni 10.
Marekani na Cuba zimekuwa katika mvutano tangu mapinduzi ya kijamaa ya Fidel Castro zaidi ya miongo sita iliyopita. Katika kipindi hiki kumekuwa na uvamizi unaoungwa mkono na CIA, tishio la vita vya nyuklia, na migogoro kadhaa ya uhamiaji.
Vizazi vya Wakuba na Wamarekani vimeishi katika uadui wa kisiasa ambao bado haujatatuliwa. Katika miongo michache iliyopita, nchi zote mbili zimedumisha utulivu na mvutano wa kupanda na kushuka.
Lakini kurudi kwa Donald Trump katika Ikulu ya White House mwaka 2025 kumeongeza mvutano.
Serikali yake imeimarisha vikwazo vya kiuchumi vilivyokuwepo tangu miaka ya 1960, ambavyo Havana inasema vinaleta changamoto nyingi, na kuifanya iwe vigumu zaidi kwa Cuba kupokea mafuta kutoka nje ya nchi.
Hilo linaongeza mgogoro wa nishati, kiuchumi na kijamii ambao kisiwa hicho tayari kinapitia, na umezidi kuwa mbaya baada ya kuanguka kwa utawala wa Venezuela kufuatia kukamatwa kwa Nicolás Maduro katika operesheni ya kijeshi ya Marekani mapema Januari.
Trump anaonya kwamba Cuba "inakaribia kuanguka," huku akisema utawala wake na Havana wanajadiliana njia ya kutoka katika mkwamo huo.
Bado kuna kutoaminiana, ingawa rais wa Cuba, Miguel Díaz-Canel, amekiri uwepo wa mawasiliano kati ya serikali zote mbili.
Uhasama kati ya majirani hao wawili ulianzaje?
Haki ya kuingilia kati
Februari 15, 1898, meli ya kivita ya Marekani inayoitwa Maine ililipuka katika bandari ya Havana. Zaidi ya wafanyakazi 260 walifariki.
Baada ya kuzama, Uchunguzi wa Mahakama ya Kijeshi ya Wanamaji wa Marekani ilihitimisha kwamba meli hiyo iliharibiwa na bomu la chini ya maji.
Tuhuma zilielekezwa kwa Uhispania, kisha zikahusisha vita dhidi ya waasi wa Cuba ambao walikuwa wakipigania uhuru wao tangu 1895.
Mwezi Aprili, Marekani iliingilia kijeshi mapigano hayo, ikianzisha Vita dhidi ya Uhispania ambavyo viliondoa umiliki wa Uhispania juu ya Cuba baada ya zaidi ya karne nne za ukoloni.
1976, uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Wanamaji la Marekani ulihitimisha kwamba mlipuko huo ulisababishwa na moto wa ndani uliolipua silaha za meli hiyo, na sio bomu la Uhispania au hujuma.

Chanzo cha picha, CORBIS/Corbis via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kufuatia kushindwa kwa Uhispania, uchumi wa Cuba, miundombinu, na viwanda viliharibiwa na vita. Nchi ilihitaji kujengwa upya, na Marekani ilikuwa na jukumu muhimu katika hili.
"Wafanyabiashara wa Marekani walipata fursa. Marekani iliingia moja kwa moja katika uchumi wa Cuba," Profesa Michael Bustamante wa Chuo Kikuu cha Miami nchini Marekani ameiambia BBC Mundo.
Kati ya 1898 na 1902, Cuba ilijiendesha kama nchi inayolindwa na Marekani. Haikupata uhuru wake rasmi hadi 1902.
Hata hivyo, Katiba yao ya kwanza ilikuja na maandishi kidogo, na kukiweka kisiwa hicho chini ya ushawishi wa moja kwa moja wa Washington.
"Ilikuwa jamhuri huru, lakini ikiwa na kiwango dhahiri cha udhibiti wa nje wa siasa kutoka Marekani, ambayo ilidai haki ya kuingilia mambo ya ndani ya Cuba," anasema Bustamante.
Kifungu cha 3 cha katiba kiliipa Marekani haki ya wazi kuingilia kati. Katiba hiyo kwa mfano iliruhusu, kuwekwa kwa kituo cha jeshi la majini cha Guantanamo, ambacho bado kinafanya kazi na chini ya udhibiti wa Marekani hadi leo.

Chanzo cha picha, Hulton Archive/Getty Images
Mapinduzi ya Castro
Kufikia miaka ya 1950, viwanda vya ndani na mitaji ya wa Cuba – vilikuwa na uzito katika uchumi wa taifa, lakini viwanda na mitaji hiyo iliendelea kuathiriwa sana na makampuni ya Marekani.
Viwanda muhimu kama vile nikeli, umeme, mawasiliano ya simu, na fedha vilidhibitiwa sana na Marekani.
Uhusiano wa kiuchumi na kisiasa kati ya majirani hao wawili ulikuwa wa karibu. Mabango ya Coca-Cola na magari ya Marekani, ambayo bado yanaonekana barabarani hadi leo, yalionekana katika mitaa ya miji mikuu.
Katika kisiwa hicho, ustawi na anasa viliambatana na ukosefu wa usawa na ufisadi.
Mwaka 1952, Fulgencio Batista, mwanajeshi ambaye aliitawala Cuba kidemokrasia kati ya 1940 na 1944, alifanya mapinduzi na kunyakua madaraka.

Chanzo cha picha, Hulton Archive/Getty Images
Serikali yake ilijulikana kwa ubabe na mateso na unyanyasaji dhidi ya upinzani.
Kutoridhika miongoni mwa watu kuliongeza matatizo ya kisiwa hicho na kule kuingiliwa na Marekani. Marekani ilimuunga mkono Batista pamoja na serikali zingine za kimabavu za Cuba kama ile ya Gerardo Machado kati ya 1925 na 1933.
"Marekani ilitekeleza ukoloni mamboleo huko Cuba kwa njia nyingi. Hisia za chuki dhidi ya utawala wa Marekani haikuwepo tu kwa wale wa mrengo wa kushoto, bali pia wale wenye itikadi mbalimbali," anasema Bustamante.
Miongoni mwa waliochukizwa na hali hiyo, wapo waliotaka hali irudi kabla ya mapinduzi ya Batista, huku wengine wakitaka mageuzi ya kitaifa ya uchumi ambayo yatapunguza utegemezi wa Marekani

Chanzo cha picha, Bettmann Archive/Getty Images
Katika kundi hili la pili ndipo Fidel Castro akajitokeza, mwanasheria kijana na kiongozi wa kisiasa mwenye mawazo ya kijamaa ambaye aliamini katika uhuru wa nchi na aliona silaha kama njia ya kufanya mapinduzi.
Baada ya uasi wa kwanza wa kutumia silaha ulioshindwa mwaka 1953, ambapo alitumikia kifungo cha karibu miaka miwili gerezani na kisha kwenda uhamishoni Mexico, Castro alirudi mwishoni mwa mwaka 1956 pamoja na mwanamapinduzi mwingine kijana wa Argentina, aliyeitwa Ernesto "Che" Guevara, na wanaume wengine 80.
Waasi walipanga vita vya msituni mashariki mwa nchi. Katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili, uasi ulienea kote kisiwani. Asubuhi ya mapema, Januari 1, 1959, Batista alichukua ndege na kukimbilia Jamhuri ya Dominika.
Siku saba baadaye, Castro na watu wake waliingia Havana kwa ushindi wakiwa na uungwaji mkono mkubwa wa watu, na mapinduzi yalianza.
Wimbi la utaifishaji na vikwazo
Talaka kati ya Cuba na Marekani haikuwa ya moja kwa moja.
"Kulikuwa na watu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani walioamini Castro ni mzalendo tu na alitaka uhusiano mzuri na Marekani," Bustamante anakumbuka.
Hata hivyo, mwanzoni mwa miaka ya 1960, matukio mawili yalivunja uhusiano huo.
Kwanza, mageuzi ya kilimo yaliyoanzishwa na Castro ambayo yalipendekeza kutaifisha baadhi ya ardhi inayodhibitiwa na Marekani.

Chanzo cha picha, PhotoQuest/Getty Images
Bustamante anafafanua kwamba halikuwa wazo la kikomunisti kwa sababu hakuwa na nia ya kunyakua kila kitu. "Ilikuwa zaidi ni maono ya kurekebisha ubepari," anaelezea.
Lakini sauti za tahadhari kutoka Marekani zilianza kusikika, huku mwanadiplomasia wa Usovieti Anastas Mikoyan akitembelea Cuba ili kusaini makubaliano na serikali.
Mpinzani mkubwa wa Marekani katika siasa za kijiografia na kiuchumi, Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti (USSR), ulikuwa ukipata umaarufu.
Mojawapo ya makubaliano kati ya Havana na Moscow ilikuwa kubadilishana sukari ya Cuba na mafuta ghafi ya Urusi.
Tatizo? Viwanda kadhaa vya kusafisha mafuta nchini Cuba vilikuwa vinamilikiwa na Wamarekani.
"Marekani ilipoamuru makampuni yake kukataa kusafisha mafuta ya Urusi, serikali ya Cuba iliingilia kati na kuvitaifisha viwanda vya kusafisha mafuta," Bustamante anasema.
Washington ilijibu kwa kupunguza mgao wa sukari kwa Cuba katika soko la Amerika Kaskazini, na Moscow ilijibu kwa kuwa mnunuzi mkuu wa sukari ya Cuba.
Hii ilisababisha awamu ya kwanza ya vikwazo vya kiuchumi vya Marekani, ambapo Havana ilijibu kwa kutaifisha viwanda na biashara za Marekani.
Kufikia Januari 1961, mahusiano yalivunjika kabisa na Castro akaanza mapinduzi ya kijamaa.
Miaka ya mvutano zaidi
Miezi iliyofuata ilikuwa na mvutano mkubwa sana.
Aprili 1961, wapiganaji wapatao 1,500, wengi wao wakiwa Wakuba waliokuwa uhamishoni kwa kumpinga Castro, walifika Cuba kwa usaidizi wa CIA katika meli ili kumpindua Castro.
Ni uvamizi unaoitwa Bay of Pigs, uliozuiwa na vikosi vya Cuba katika siku tatu kusini mwa nchi baada ya Rais wa Marekani John F. Kennedy kuondoa usaidizi wa anga dakika za mwisho.
Kushindwa huko kulimwimarisha Castro, ambaye alizidisha pendekezo lake la kijamaa. Hilo lilimfanya Kennedy atathmini upya sera yake kuelekea Cuba.
Kutoka Washington, mpango mpya wa siri unaoitwa Operesheni Mongoose ulitekelezwa ili kufanikisha kile ambacho uvamizi wa Bay of Pigs ulishindwa kutimiza.
Misheni hiyo ilijumuisha shughuli za kisiasa, kisaikolojia, kijeshi, hujuma na ujasusi, pamoja na majaribio ya mauaji dhidi ya viongozi wakuu wa kisiasa, akiwemo Castro.
"Operesheni Mongoose ilikusudiwa kuunda uasi nchini Cuba ambao ungeiweka nchi katika ukingo wa maafa, lakini ikawa wazi kwamba hakukuwa na uwezekano wa kutokea harakati za ndani zitakazo sababisha mapinduzi na kuanguka kwa utawala," anasema Oscar Zanetti, mtafiti katika Chuo cha Historia cha Cuba.
"Kwa hivyo, Machi 1962, Marekani ilichukua chaguo la kuingilia kati moja kwa moja kwa kutumia njia zote muhimu za kijeshi," Zanetti anaongeza.
Cuba ambayo ni ndogo ilihitaji kujilinda, na USSR, wakati huo ikiwa chini ya uongozi wa Nikita Khrushchev, ilikuwa tayari kuiunga mkono.
Katika majira ya joto ya 1962, ripoti za ujasusi za Marekani zilionyesha ongezeko la usafirishaji wa silaha za Usovieti kwenda Cuba. Mwezi Oktoba, ndege moja ilipiga picha na kugundua mfumo wa kurushia makombora kwenye kisiwa hicho.
Kwa siku 13, dunia ilikuwa ukingoni mwa mzozo wa nyuklia kati ya mataifa makubwa ya wakati huo huku Cuba ikiwa katikati ya vita. Baada ya mazungumzo makali, mgogoro huo ulitatuliwa na USSR ikaondoa makombora yake kutoka Cuba.
Lakini jeraha la kurithi na kutoaminiana lilikuwa kubwa sana.
Serikali ya Cuba iliimarisha uhusiano wake na kambi ya kijamaa ya USSR na Ulaya Mashariki, ikijitenga zaidi na jirani yake wa kaskazini.

Chanzo cha picha, Photo12/Universal Images Group via Getty Images
Miongo kadhaa ya msuguano
Marais kadhaa wa Democratic na Republican walipitia Ikulu ya White House, na huko Havana mfumo wa kijamaa wa chama kimoja ulioongozwa na Fidel Castro uliimarishwa.
Mapinduzi ya Cuba pia yalichochea harakati za mrengo wa kushoto katika eneo hilo: kuanzia waasi wa Colombia miaka ya 1960, hadi Sandinismo huko Nikaragua miaka ya 1980 na mapinduzi ya Bolivarian huko Venezuela mwishoni mwa miaka ya 1990.
Katika kipindi hiki, uhamiaji ulikuwa sehemu ya migogoro na ushirikiano.
Tangu mwaka 1959, Marekani imekuwa ikiwapa upendeleo wahamiaji kutoka wa Cuba, ikihimiza kuondoka kwa wapinzani na wale wanaotafuta hali mbadala ya maisha.
Watu 125,000 waliondoka Cuba kwenda Florida baada ya Castro kufungua milango kwa yeyote aliyetaka kuondoka.
Na baada ya kuanguka kwa USSR mwaka 1991 Cuba ilitumbukia katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi.
Mgogoro huo ulisababisha maandamano makali na yasiyo ya kawaida. Akikabiliwa na shinikizo, Castro alifungua tena mipaka na watu wapatao 35,000 wakaondoka kwenda Marekani.
Hii ilisababisha Washington kurekebisha sera yake ya uhamiaji na kuanzisha sera ambayo; yeyote anayefika Marekani kwa njia ya ardhini atabaki, huku yeyote anayekamatwa akiingia kupitia baharini atarudishwa.
Miaka ya 1990 pia ilishuhudia kuimarishwa kwa sera dhidi ya Cuba. Kulikuwa na vikwazo zaidi kwa uchumi. Ikikabiliwa na vikwazo na upungufu wa uzalishaji, nchi hiyo ilitegemea sana utalii na hadi leo haijaweza kuondoa kabisa pigo la miaka ya 90.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hali ya sasa

Chanzo cha picha, ADALBERTO ROQUE/AFP via Getty Images
Kuanzia mwaka 1994 hadi sasa, uhusiano bado ni wa mashaka, ingawa kumekuwa na vipindi vya ukaribu na mvutano.
Fidel Castro aliachia madaraka mwaka 2006 baada ya kuugua sana, na kaka yake Raúl akamchukua nafasi yake.
Chini ya serikali ya Raúl Castro na rais Barack Obama, nchi zote mbili zilichukua hatua kuelekea kurekebisha uhusiano mwaka 2015.
"Mapema mwaka 2013, kufuatia hatua mabadiliko ya sera za kiuchumi zilizochukuliwa na Raúl, Marekani na Cuba zilianza kujadiliana kupitia Papa Francis na Kanisa Katoliki la Cuba," anakumbuka mwanahistoria Rojas, kutoka Chuo cha Mexico.
Mwaka 2015, balozi zilifunguliwa tena, vikwazo vya usafiri viliondolewa, na uhuru wa kiuchumi ulitoa matumaini.
Lakini kuwasili kwa Donald Trump katika Ikulu ya White House 2017, miezi kadhaa baada ya kifo cha Fidel Castro, kulimaanisha kuvurugika kwa ufunguzi huo.
Na kufikia mwaka 2025, vikwazo na shinikizo dhidi ya kisiwa hicho vimeongezeka zaidi, kama vile mvutano kati ya nchi hizo mbili.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah.











