Uchunguzi wa siri wa BBC wabaini kuwa wahamiaji hujifanya wapenzi wa jinsi moja ili kupata hifadhi

v
Muda wa kusoma: Dakika 11

Mtandao wa siri wa taasisi za mawakili na washauri inatoza maelfu ya pauni kuwasaidia wahamiaji kujifanya kuwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsi moja ili waweze kubaki Uingereza, uchunguzi wa siri wa BBC umebaini.

Katika sehemu ya kwanza ya uchunguzi mkubwa wa siri, imefichuliwa jinsi wahamiaji ambao visa zao zinakaribia kuisha wanavyopewa hadithi za uongo na kufundishwa jinsi ya kupata ushahidi wa kughushi, ikiwa ni pamoja na barua za kuunga mkono, picha na ripoti za kitabibu.

Kisha wanawasilisha maombi ya hifadhi wakidai kuwa ni wapenzi wa jinsi moja na kwamba maisha yao yako hatarini endapo wata watarudishwa Pakistan au Bangladesh.

Kujibu matokeo hayo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza ilisema: "Mtu yeyote atakayebainika kujaribu kutumia vibaya mfumo huu atakabiliwa na mkono mkali wa sheria, ikiwa ni pamoja na kuondolewa Uingereza."

Mchakato wa hifadhi wa Uingereza unatoa ulinzi kwa watu ambao hawawezi kurudi katika nchi zao kwa sababu watakuwa hatarini, kwa mfano katika nchi kama Pakistan na Bangladesh ambako ngono ya jinsia moja ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo, uchunguzi wa BBC News unaonesha kuwa mchakato huo unatumika vibaya kwa kiwango kikubwa na washauri wa kisheria wanaowatoza wahamiaji fedha ili kuwasaidia kubaki nchini.

Mara nyingi hawa ni watu ambao visa zao za masomo, kazi au utalii zimekwisha muda wake, kuliko wale walioingia nchini hivi karibuni kwa boti ndogo au kupitia njia nyingine zisizo halali.

Kundi hili sasa linachangia asilimia 35 ya maombi yote ya hifadhi, ambayo yalizidi 100,000 mwaka 2025.

Baada ya kukusanya ushahidi wa awali, ikiwemo taarifa za siri kutoka kwa watu, tuliwatuma waandishi wetu wa habari waliokuwa chini ya upelelezi wa siri kuchunguza jinsi washauri wa uhamiaji walivyokuwa tayari kusaidia watu kubuni madai ya uongo ya hifadhi.

Waandishi hao walijifanya kuwa wanafunzi wa kimataifa kutoka Pakistan na Bangladesh ambao visa zao zilikuwa zinakaribia kuisha muda wake.

Uchunguzi huo uligundua yafuatayo:

  • Kampuni moja ya mawakili ilitoza hadi pauni 7,000 kuwasilisha ombi la hifadhi la kughushi na ikaahidi kuwa nafasi ya kukataliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ilikuwa "ndogo sana".
  • Waombaji wa hifadhi wa kughushi waliwatembelea madaktari (GPs) wakijifanya wana msongo wa mawazo ili kupata ushahidi wa kitabibu wa kutilia nguvu madai yao, huku mmoja akidanganya hata kuwa ana maambukizi ya HIV.
  • Mshauri mmoja wa uhamiaji alijivunia kuwa ametumia zaidi ya miaka 17 kusaidia kuandaa madai ya uongo, na akasema anaweza kupanga mtu ajifanye kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi wa jinsia moja na mteja.
  • Mwandishi wetu wa siri hata aliambiwa anaweza kumleta mke wake kutoka Pakistan baada ya kupata hifadhi Uingereza, na mke huyo anaweza pia kutoa ombi la uongo akijifanya mtu anayejihusisha na mapenzi ya jinsi moja.
  • Wakili anayehusishwa na kampuni nyingine alimwambia mwandishi wetu kuwa amewahi kusaidia watu kujifanya wapenzi wa jinsi moja au wasioamini dini ili wapate hifadhi kwa mafanikio. Alijitolea kusaidia kwa ada ya pauni 1,500, na akasema alitumia pauni 2,000 hadi 3,000 zaidi kuandaa ushahidi wa kughushi.

'Hakuna mpenzi wa jinsi moja hapa'

Jioni ya Jumanne katika kituo cha jamii kilichopo sehemu tulivu ya Beckton, mashariki mwa London, zaidi ya watu 175 wamekusanyika kwa ajili ya tukio.

Baadhi yao wamesafiri kutoka mbali kama South Wales, Birmingham na Oxford kuhudhuria mkutano ulioandaliwa na Worcester LGBT, ambalo linajieleza kama kundi la msaada kwa waomba hifadhi wa mapenzi ya jinsi moja.

Zaidi ya watu 175 walikusanyika katika tukio lililoandaliwa na Worcester LGBT.
Maelezo ya picha, Zaidi ya watu 175 walikusanyika katika tukio lililoandaliwa na Worcester LGBT.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tovuti ya kundi hilo inasema kuwa ni waomba hifadhi wa mapenzi ya jinsi moja walio halisi pekee wanaokaribishwa.

Lakini wanaume waliokuwa wakitoka nje ya milango ya kituo hicho na kumiminika kwenye njia ya watembea kwa miguu walikiri kwa urahisi kwa mwandishi wetu wa siri kuwa mambo si kama yanavyoonekana.

"Mara nyingi watu walioko hapa si wa mapenzi ya jinsi moja," alisema mwanaume mmoja aliyejitambulisha kama Fahar.

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Zeeshan alienda mbali zaidi:

"Hakuna mtu hapa ni anayejihusisha na mapenzi ya jinsi moja. Hata asilimia 1. Hata asilimia 0.01 si wa namna hiyo."

Safari ya mwandishi wetu wa siri kwenda kwenye mkutano wa kundi hilo ilianza mwishoni mwa Februari alipomfuata Mazedul Hasan Shakil, msaidizi wa kisheria katika kampuni ya Law & Justice Solicitors, kampuni ya sheria za uhamiaji yenye makao yake Birmingham na London.

Mbali na kazi yake ya kisheria, Shakil pia ni mwanzilishi na mwenyekiti wa Worcester LGBT. Hadi hivi karibuni, alitumia tovuti ya kundi hilo la kijamii kutangaza huduma zake za kisheria.

Katika mazungumzo mafupi ya simu, Shakil alimwambia mwandishi wetu kuwa alihitaji kuwa katika hofu ya kuteswa ili aweze kuomba hifadhi, na hakuonekana kuwa na sababu zozote za kufanya hivyo.

Lakini ndani ya saa chache, bila kutarajiwa, mwandishi alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kama Tanisa.

Mazungumzo yalipobadilishwa kwenda kwa lugha ya Kiurdu, alionekana kuwa na shauku zaidi ya kumsaidia mwandishi kubaki nchini, akielezea jinsi atakavyoweza kuomba hifadhi kwa misingi kwamba yeye ni mtu wa mapenzi ya jinsi moja.

Alipomwambia kuwa si mpenzi wa jinsi moja, alimjibu: "Nisikilize. Hakuna mtu aliye halisi. Kuna njia moja tu ya kubaki hapa sasa, na hiyo ndiyo njia ambayo kila mtu anatumia."

Hakutaka kufafanua nani aliyempa namba yake, lakini tuliweza kulinganisha picha yake ya wasifu wa WhatsApp na jina lake la kwanza na Tanisa Khan, ambaye anafanya kazi kama mshauri wa Worcester LGBT.

Jioni hiyo mwandishi wetu wa siri alisafiri kwenda Forest Gate, mashariki mwa London, kwa ajili ya mashauriano ya awali na Tanisa.

Mkutano wa kwanza haukufanyika katika ofisi za kampuni ya sheria ambazo baadaye angezitumia, bali ulifanyika nyumbani kwake. Aliingizwa ndani na kupelekwa ghorofani katika chumba cha kulala.

"Kwa sasa kuna njia moja tu ambayo unaweza kupata visa, na iko wazi," Tanisa alieleza akiwa ameketi pembeni ya kitanda.

"Ni visa ya hifadhi… inahusiana na haki za binadamu na inaitwa kesi ya mapenzi ya jinsi moja. Hakuna matumaini ya visa nyingine yoyote."

Tanisa alisisitiza kuwa kile alichokuwa akipendekeza kingehitaji kazi, kwani mwombaji angelazimika kukariri hadithi ya uongo kwa ajili ya mahojiano na Wizara ya Mambo ya Ndani.

"Wewe ndiye utakayekwenda kufanya mtihani. Mimi niko hapa kuandaa kila kitu kwa ajili yako, lakini hatimaye ni wewe utakayeenda huko," alimwambia.

Kilichofuata katika kipindi cha dakika 45 ndani ya chumba cha Tanisa kilikuwa ufahamu wa jinsi udanganyifu unaohusika katika baadhi ya madai ya hifadhi ya uongo ulivyo wa hali ya juu, na hivyo jinsi inavyoweza kuwa vigumu kwa maafisa kuugundua.

Mahojiano ya awali na Tanisa, mshauri wa Worcester LGBT, yalifanyika katika chumba cha kulala.
Maelezo ya picha, Mahojiano ya awali na Tanisa, mshauri wa Worcester LGBT, yalifanyika katika chumba cha kulala.

Waomba hifadhi hupitia mahojiano ya awali ya uchunguzi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza, kisha hufanyiwa mahojiano ya kina sana yanayoweza kudumu kwa saa kadhaa, ambapo madai yao huchunguzwa kwa undani.

Uamuzi wa Wizara ya Mambo ya Ndani kukataa ombi la hifadhi unaweza kupingwa na huenda ukabatilishwa mahakamani.

"Hakuna ukaguzi wa moja kwa moja wa kubaini kama mtu anajihusisha na mapenzi ya jinsi moja," Tanisa alimwambia mwandishi wetu wa siri.

"Kitu cha msingi ni kile unachosema. Unachotakiwa kufanya ni kuwaambia kwamba 'mimi ni shoga na huo ndio ukweli wangu'."

"Kuna mashirika mengi hapa ambapo kuna watu kama wewe ambao si wapenzi wa jinsi moja lakini wanaomba visa. Si wewe peke yako," alimhakikishia.

Kisha akaeleza jinsi udanganyifu huo unavyofanyika.

"Njia tutakayotumia ni hii: nitakuandaa kikamilifu kwa mahojiano kwa kukutengenezea kifurushi kamili, ikiwemo picha zako kwenye vilabu, ushahidi mbalimbali wa ziada, barua ya taasisi, na barua nyingine za uthibitisho, ili uwe tayari kabisa nitakapokupeleka."

Tanisa, ambaye alisema amekuwa akisaidia kuandaa madai ya uongo kwa zaidi ya miaka 17, alieleza kuwa picha za mwombaji zikichukuliwa katika matukio ya mikutano ya LGBT na tiketi atakazonunua zitatumika kama ushahidi katika ombi lake.

"Nitakupa barua kutoka kwa mtu mmoja na pamoja nayo tutapiga picha kadhaa, na huyo mtu ataandika kwamba amewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wewe," aliongeza.

Huduma ya Tanisa ilikuwa na gharama ya pauni 2,500, pamoja na onyo kwamba gharama itaongezeka iwapo ombi litakataliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani na kupelekwa kwenye rufaa mahakamani.

Alieleza kuwa ombi lililofanikiwa lingekuwa na faida kubwa.

"Unaweza kuishi hapa na kufanya kazi na pia unastahiki kupata misaada ya serikali."

Lakini kama ombi la hifadhi litafanikiwa, hilo litamaanisha nini kwa mke wake aliyeko Pakistan, mwandishi wetu aliuliza, ikiwa tayari alikuwa ameiambia Wizara ya Mambo ya Ndani kuwa yeye ni mpenzi wa jinsi wa jinsi moja?

"Ukimleta hapa, basi tutamuombea hifadhi pia," Tanisa alijibu.

"Akishafika hapa, tunaweza kumfanya awe mpenzi wa jinsi moja."

Kuwasilisha ushahidi

Tanisa si mshauri wa masuala ya uhamiaji aliyeidhinishwa, na kwa hiyo ni kinyume cha sheria kwake kutoa ushauri wa uhamiaji.

Aliendelea kuwa na majibu yasiyo wazi kuhusu uhusiano wake na yule msaidizi wa kisheria ambaye mwandishi wetu alikuwa amemtafuta asubuhi hiyo, akisema tu kwamba anafanya kazi naye.

"Mawakili na watu kama wao wanatakiwa kukuonesha njia. Hata hivyo, kazi ya mahojiano si kitu wanachoshughulikia," alieleza, akionekana kurejelea kazi ya kubuni ushahidi.

"Sisi tunashughulikia kazi ya uwanjani."

Lakini uhusiano wake na Shakil ulianza kuwa wazi zaidi katika mikutano miwili iliyofuata, ambayo yote ilifanyika katika ofisi za Ilford za Law & Justice, kampuni ya sheria anayofanyia kazi Shakil.

"Nafanya kazi na wakili, hivyo natumia ofisi yake," alieleza.

Katika mkutano mmoja, mwandishi wetu wa siri aliomba atambulishwe kwa Shakil ili kumshukuru kwa kumtambulisha kwa Tanisa, na alipelekwa katika chumba cha karibu ambapo alimsalimia Shakil kwa kupeana naye mkono.

Tanisa pia alieleza nafasi ya Worcester LGBT, ambayo aliielezea kama "shirika letu" na ambalo linadai kwenye tovuti yake kuwa "limetambuliwa rasmi na Wizara ya Mambo ya Ndani… likitambua mchango wetu unaoendelea katika kusaidia waomba hifadhi wa LGBT+ kote Uingereza."

Alimwambia mwandishi kwamba lazima ahudhurie mkutano ujao, uliopangwa mapema Aprili, na akasema baadhi ya watu huko watakuwa kama yeye na wanaofuata madai ya uongo, na pia "kutakuwa na wa kweli pia".

"Mkutano huu ni wa muhimu sana kwa sababu unatakiwa kutoa ushahidi kwa Wizara ya Mambo ya Ndani unaoonesha kwamba, kama wewe ni wa mapenzi ya jinsi moja, basi kweli unahusishwa na kundi la hilo," alimwambia.

Alisema Worcester LGBT itaweza kutoa barua ambayo ataitumia kama ushahidi kwa maombi yake.

"Tutasema kwa upande wetu kwamba wewe… ni mwanachama wetu, wa kweli, unahusiana nasi, na tunakufahamu binafsi. Aina hii ya ushahidi ni yenye nguvu sana."

Tulionesha picha na video zetu kwa Ana Gonzalez, wakili wa uhamiaji mwenye uzoefu wa miaka 30. Alisema Tanisa alikuwa wazi kuvunja sheria, "akifanya udanganyifu kwa kutengeneza madai ya kumpa mtu huyu."

"Watu kama hao wanawafanya kuwa vigumu zaidi kwa waomba hifadhi halali na wakimbizi waliopo nje," Gonzalez alisema.

"Haswa kwa jambo ambalo ni la kutokuwa na uthibitisho wa moja kwa moja kama kuwa LGBT, kwa sababu unapokuwa mwathiriwa wa mateso, mara nyingi kuna njia ya kuthibitisha hilo kwa ushahidi wa moja kwa moja.

"Lakini linapokuja suala la jamii ya mapenzi ya jinsi moja, sivyo. Linategemea mawasiliano na jinsi unavyojitokeza na jinsi unavyoweza kushawishi kwa siku hiyo husika, bila kujali kama unasema ukweli au la."

Baada ya BBC News kumwendea Tanisa kuhusu maoni yake kwa mwandishi wa siri, alidai kulikuwa na "kutokuelewana" kutokana na changamoto za mawasiliano na akasema hafahamu Kiurdu vizuri. Alikana kumshauri mwandishi huyo kutoa madai ya uongo au kutoa au kupanga ushahidi wa kughushi.

Shakil alisema kwamba alimpa Tanisa taarifa za mwandishi wa siri bila kujua au kushuku kuwa angependekeza kutengeneza madai ya hifadhi ya uongo.

Alisema Worcester LGBT haikutengeneza wala kuunga mkono ushahidi wa kughushi katika madai ya hifadhi, na si jukumu la shirika hilo kuamua kama mtu ni wa mapenzi ya jinsi moja.

Pia alisema Worcester LGBT ilikuwa inaendesha uchunguzi kuhusu mwenendo wa Tanisa na kwamba hakuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi ndani ya kundi hilo.

Law & Justice Solicitors ilisema Tanisa hana uhusiano wa kikazi na kampuni hiyo na kwamba inachunguza "uwezekano wa matumizi yasiyoidhinishwa" ya ofisi yake ya London.

Iliongeza kuwa mwandishi wetu wa siri hakuwahi kusajiliwa kama mteja wa kampuni hiyo.

Wakati huo huo alipokuwa akikutana na Tanisa, mwandishi wetu wa siri pia alipanga miadi na mshauri katika kampuni ya sheria Connaught Law, ambayo ina ofisi zake katikati ya eneo la kisheria la London.

Huko alikutana na Aqeel Abbasi, mshauri mkuu wa kisheria katika Connaught.

Abbasi alimwambia mwandishi wetu kuwa angeweza kumsaidia kubaki nchini na alionekana kuwa tayari kumwelekeza jinsi ya kutengeneza ushahidi wa kughushi kwa madai ya uongo.

Aliahidi kuwa uwezekano wa kukataliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ulikuwa "mdogo sana".

Alisema ada yake ingekuwa pauni 7,000, na baada ya malipo hayo kufanyika, ofisi yake ingewasiliana na mwandishi wetu ili kumwelekeza katika mchakato na aina ya ushahidi unaohitajika.

Hii ingejumuisha kumshauri "wapi pa kwenda au hatua gani maalum za kuchukua".

"Ushahidi lazima utolewe na kuwasilishwa kutoka kwa mashirika na vilabu vyao," Abbasi alisema.

"Wanakokwenda, vilabu vyao vya jamii hiyo vilipo."

Wakati mmoja, mwandishi aliuliza kama angelazimika kwenda kwenye klabu.

"Ndiyo, utalazimika," Abbasi alimwambia.

"Lakini mimi si wa aina hiyo," mwandishi alijibu.

Abbasi alionekana kufurahia hilo na akasema: "Nitachukua picha kutoka huko."

Mshauri huyo wa kisheria pia alipendekeza kuwa mwandishi angelazimika kupata mtu atakayekubali kujifanya kuwa mpenzi wake wa kiume.

Mwandishi aliposema ana mke nchini Pakistan, Abbasi alitoa haraka wazo la hadithi ya kuficha ukweli huo, akisema kuwa mambo yako "wazi zaidi" nchini Uingereza kuliko Pakistan na kwamba sasa ana mpenzi wa kiume.

"Tutaandaa maelezo (taarifa) kwa ajili yako, na ukisha yasoma utaelewa vizuri jinsi ilivyo," alisema Abbasi.

''Ni tatizo kubwa sana''

Worcester LGBT hufanya mikutano ya kila mwezi inayowavutia washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, wengi wao wakionekana kuwa waombaji wa hifadhi wa kughushi.

Lakini si kundi hilo pekee linalotumiwa na waomba hifadhi wanaojifanya kuwa mashoga.

Ejel Khan, mwanzilishi mzaliwa wa Uingereza wa Muslim LGBT Network yenye makao yake Luton, alisema: "Ni tatizo kubwa sana.

"Watu hunipa ofa ya kunilipa fedha ili niwape barua za mapendekezo kutoka shirika langu, lakini sikubali kamwe. Kazi yangu yote ni ya kujitolea."

Alisema baadhi yao hata wamemwambia: "Mimi si shoga lakini nataka kubaki katika nchi hii."

Ni vigumu kujua kwa usahihi ni maombi mangapi ya hifadhi (asylum) yanaweza kuwa ya kubuniwa.

Hata hivyo, takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani zinaonesha kuwa raia wa Pakistan wanachangia idadi kubwa isiyo sawia ya maombi yanayowasilishwa kwa misingi ya mwelekeo wa kijinsia.

Mwaka 2023, ambao ni mwaka wa hivi karibuni wenye takwimu kamili, kulikuwa na maamuzi ya awali kuhusu maombi 3,430 ya hifadhi ya LGBT, na karibu maombi mapya 1,400 yaliwasilishwa kwa msingi wa mwelekeo wa kijinsia.

Takribani asilimia 42 ya maombi hayo yalifanywa na raia wa Pakistan, na wamekuwa wakiongoza kwa idadi ya maombi kama hayo katika kila moja ya miaka mitano iliyopita.

Katika mwaka huo huo, raia wa Pakistan walikuwa nafasi ya nne kwa wingi wa waombaji wa hifadhi kwa ujumla, wakichangia takribani asilimia 6 tu ya maombi yote ya hifadhi.

Hakuna takwimu mpya zaidi kuhusu maombi ya hifadhi yanayotokana na mwelekeo wa kijinsia.

Hata hivyo, wanatakwimu wa Wizara ya Mambo ya Ndani wamebainisha ongezeko kubwa la maombi ya hifadhi kwa ujumla kutoka kwa raia wa Pakistan, pamoja na wahamiaji kutoka Bangladesh na India, ambao hapo awali walikuwa nchini kwa visa za masomo au kazi katika miaka ya hivi karibuni.

Karibu theluthi mbili ya waomba hifadhi waliodai mateso kwa misingi ya mwelekeo wa kijinsia walikubaliwa maombi yao katika hatua ya awali mwaka 2023.

Ali, si jina lake halisi, awali alikuja Uingereza kama mwanafunzi kutoka Pakistan mwaka 2011.

Alimtembelea wakili kwa ushauri kabla ya visa yake kuisha miaka mitatu baadaye, na anasema wakili huyo alimshauri kubuni hadithi kwamba yeye ni mpenzi wa jinsi moja ili aweze kuomba hifadhi na kubaki nchini humo.

Alisema wakili huyo "alinishauri nimtembelee daktari wangu (GP) na kuonesha kuwa nilikuwa nasumbuliwa na msongo wa mawazo, hasa kutokana na hali ya visa yangu."

Aliongeza: "Kwa kweli sikutumia dawa hizo, lakini alisisitiza nipate dawa hizo ili tuweze kuwasilisha ushahidi kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ukionesha kwamba nilikuwa nimeingia katika hali ya msongo wa mawazo."

Mahojiano ya awali na Wizara ya Mambo ya Ndani hayakwenda vizuri, na rufaa zilizochukua muda mrefu zilisababisha gharama zake kuongezeka hadi zaidi ya pauni 10,000.

Alishiriki katika maandamano ya Pride na kutembelea vilabu vya watu wa mapenzi ya jinsi moja zaidi ya mara 10, akipiga picha ili kuwasilisha kama ushahidi kwa maelekezo ya wakili wake.

BBC News pia imeona ushahidi kwamba alijaribu bila mafanikio kupata barua ya kumuunga mkono kutoka shirika la kusaidia watu wanaoishi na HIV, baada ya kuhudhuria mikutano yao na kudanganya kwamba alikuwa na virusi hivyo.

Hatimaye alirejea Pakistan mwaka 2019 kutokana na kuongezeka kwa gharama za kisheria, miaka minane baada ya kuwasili Uingereza.

Mke wake alipokuja Uingereza kama mwanafunzi wa kimataifa mwaka 2022, alizuiwa kuungana naye kutokana na jaribio lake lililoshindikana la kuomba hifadhi.

Lakini alituambia kuwa marafiki zake watatu walifanikiwa kupata hifadhi kwa kudanganya kuhusu mwelekeo wao wa kijinsia.

"Wao hata walifunga ndoa Pakistan na kuwaleta wake zao hapa, na sasa wana watoto," alisema.