Ni nchi gani ya Kiislamu ambayo bunge la Israel linapiga kura kuitangaza kuwa adui?

Chanzo cha picha, Reuters
Bunge la Israel, Knesset, litapiga kura, kuhusu usomaji wa awali wa mswada uliowasilishwa na kiongozi wa upinzani Yair Lapid, wenye mada: "Kuitangaza Qatar kuwa taifa adui."
Maandishi ya pendekezo hilo ambayo yana kifungu kimoja tu, yanaifafanua Qatar kuwa "taifa adui," na inaeleza kuwa vifungu vyote vya sheria za Israel kuhusu mataifa adui, aina zote za sheria, vitatumika kwake.
Chama cha Yesh Atid kinauita mradi huo "Sheria ya Urich," baada ya mshauri wa Benjamin Netanyahu, na unalenga kutoa ufafanuzi wa kina wa neno "nchi adui," ambalo kwa sasa halipo katika sheria za Israel.
Mswada huo unajumuisha marejeleo ya maandishi ya awali kama vile "Biashara na Sheria ya Adui ya 1939" na vifungu katika Kanuni ya Adhabu vinavyofafanua adui na kutoa adhabu kwa ajili ya kusaidia au kumsaidia adui.
Pia inajumuisha kipengele kinachokataza watahiniwa wa Knesset kuunga mkono serikali ya adui au kuishi kinyume cha sheria katika nchi kama hiyo .
Sababu kuu inayozifanya nchi za Ghuba ikiwemo Qatar kukumbwa na mashambulio ya Iran ni kwamba zina kambi za Marekani jambo ambalo Iran inalipiza kisasi.
Qatar pia ilikuwa moja ya nchi zinazopatanisha Israel na Hamas wakati wa mazungumzo hayo, huku maafisa wengi wa Hamas wakiishi huko.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliionya Qatar mwaka jana kwamba ifikapo 2025 lazima "iwafukuze maafisa wa Hamas au kuwafikisha mahakamani".

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Ninaiambia Qatar na nchi zote ambazo zina ugaidi: lazima uwafukuze au uwafikishe kwenye vyombo vya sheria, au tutafanya vivyo hivyo," Netanyahu alisema katika matangazo ya video kutoka ofisi yake.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi Israel Katz alisema wakati huo, "Sera ya usalama ya Israel iko wazi: mkono mrefu wa Israel utachukua hatua dhidi ya maadui wake kila mahali, hakuna mahali pa kujificha."
Aliongeza kuwa iwapo viongozi wa Hamas hawatakubali masharti ya Israel ya kusitisha vita, ambayo ni pamoja na kuachiliwa kwa mateka wote na kuwapokonya silaha, wataangamizwa, na Gaza itaangamizwa," alisema.
Wakati huo huo, Qatar ni miongoni mwa nchi ambazo ni marafiki wa karibu na Marekani, hasa Trump, kwani tayari ameshatembelea huko, na Rais Trump pia ni rafiki wa karibu wa Israel.
Ikiwa bunge la Israel litapiga kura kuhusu suala hili, baadhi wanaamini litakuwa na athari, kwani linakuja wakati mgumu ambapo mgogoro wa Mashariki ya Kati unaonekana kutokuwa na uhakika.











