Tommy Thompson: Aligundua dhahabu tani 14 kwenye meli iliyozama baharini

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 3

Tommy Thompson, ambaye amekuwa akitumikia kifungo cha karibu miaka 10 jela kwa kushindwa kufichua mahali zilipo sarafu za dhahabu alizotoa kutoka kwa mabaki ya meli maarufu, ameachiwa huru.

Mwanamme huyo raia wa Marekani alikuwa anajihusisha na utafutaji wa hazina katika kina kirefu cha bahari.

Sarafu 500 za dhahabu alizotoa kwenye meli hiyo bado hazijulikani zilipo.

Tommy Thompson, ambaye sasa ana umri wa miaka 73, aligundua mabaki ya meli iliyozama mwaka wa 1857 iitwayo SS Central America karibu na pwani ya South Carolina mwaka 1988.

Meli hiyo ilikuwa inajulikana kama "Ship of Gold."

Alipata hazina yenye thamani ya mamilioni ya dola kutoka kwenye meli hiyo.

Hata hivyo, kulikuwa na madai kwamba Tommy Thompson aliwalaghai washirika wake kwa kutowapa kipato alichowaahidi baada ya kuwekeza katika safari hiyo ya kutafuta hazina.

Aliishi mafichoni kwa miaka kadhaa, na mwaka 2015 alikamatwa na kufungwa jela kwa kosa la kuidharau ahakama.

Meli ya SS Central America ilizama mwaka wa 1857 ikiwa imebeba takriban pauni 30,000 (tani 14 ) za dhahabu zilizozalishwa katika kituo cha San Francisco Mint.

Wakati wa kusafirisha dhahabu hiyo kuelekea pwani ya Mashariki ya Marekani kwa ajili ya kuhifadhiwa kwenye benki, meli hiyo ilizama kwenye kina cha futi 7,000 baharini.

Watu 425 walipoteza maisha yao katika ajali hiyo. Tukio hilo lilisababisha mgogoro mkubwa wa kiuchumi.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vipande vya dhahabu kutoka meli ya SS Central America, vikionyeshwa kwenye hifadhi ya Makumbusho ya Historia ya Fedha ya Marekani mjini New York mwaka 2003.

Nini hasa kilitokea?

Tommy Thompson, akiwa na imani kwamba uchunguzi wake ungeleta faida, alipata ufadhili wa takriban dola milioni 12.7 kutoka kwa wawekezaji 161.

Wakati huo, Thompson alikuwa mhandisi wa baharini katika Battelle Memorial Institute huko Ohio.

Kama sehemu ya misheni hiyo, yeye na timu yake walifanikiwa kuokoa maelfu ya vipande vya dhahabu na sarafu kutoka chini ya bahari mwaka wa 1988.

Sehemu kubwa ya hazina hiyo iliuzwa kwa kundi la mauzo mwaka wa 2000 kwa takriban dola milioni 50.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Nini kilitokea mahakamani?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wawekezaji walimshtaki Tommy Thompson mwaka wa 2005, wakidai kwamba hawakupokea faida yoyote kutoka kwenye mauzo ya hazina hiyo.

Malalamiko ya wawekazaji hao yalidai kuwa jumla ya thamani ya hazina aliyogundua ilikuwa takriban dola milioni 400.

Thompson alienda mafichoni mwaka 2012 baada ya kuamrishwa kufika mahakamani. Baada ya kuwa mafichoni kwa miaka mitatu, yeye na mshirika wake walikamatwa na polisi katika hoteli moja huko Florida mwaka 2015.

Ili kuepuka kukamatwa na polisi, Thompson aliishi hotelini akitumia majina bandia, alisafiri kwa teksi na mabasi, na alifanya malipo yote kwa pesa taslimu.

Kulingana na CBS News, Tommy Thompson alidai kwamba sarafu hizo zilihamishiwa kwenye mfuko wa amana huko Belize, na kwamba faida kutoka sehemu ya kwanza ya hazina hiyo zilitosha kugharamia gharama za mahakama na madeni ya benki.

Mwezi Desemba 2015, mahakama ilimhukumu kifungo cha miaka miwili jela kwa kukataa kufichua mahali zilipo sarafu 500 za dhahabu zilizopotea. Kwa kawaida, katika kesi kama hizi, kifungo huendelea hadi amri ya mahakama itakapotekelezwa.

Hata hivyo, CBS News iliripoti kwamba jaji, aliyekuwa na mtazamo kuwa Thompson huenda asingefichua siri hiyo bila kujali muda atakaokaa gerezani, alikubali kusitisha kifungo chake mwaka jana.