Viongozi wakuu 20 wa Iran waliouawa ndani ya siku 20 za vita

s
Maelezo ya picha, (Kutoka kushoto) Mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) Mohammad Pakpour, Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa Ali Larijani, na Waziri wa Ulinzi Aziz Nasrzadeh. Wote wameuawa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepoteza viongozi wake wengi tangu Marekani na Israel zilipoanza vita dhidi yake wiki tatu zilizopita.

Na ndani ya siku 20 tu za vita, idadi kubwa ya maafisa wa kijeshi, usalama na kisiasa wameuawa katika mashambulizi ya mfululizo ndani na nje ya Iran. Hata hivyo, orodha hii inaangazia takriban viongozi 20 waandamizi zaidi waliouawa, miongoni mwa wengi waliopoteza maisha katika vita hiyo.

Iran ilimpoteza Kiongozi wake Mkuu, Ayatollah Ali Khamenei, pamoja na viongozi wengine wa juu kabisa katika siku ya kwanza ya vita, tukio lililoishtua dunia. Baada ya hapo, Iran ilianza kujibu mashambulizi hayo huku ikiapa kulipiza kisasi.

Jeshi la Marekani limesema kuwa licha ya pigo hilo, utawala wa Iran bado haujaanguka kabisa kwa sababu baadhi ya viongozi waliouawa wamebadilishwa. Wakati huo huo, Israel imeendelea na mashambulizi yake, hata ikitangaza kuwaua maafisa watatu wa usalama ndani ya siku moja.

Hawa hapa ni baadhi ya vifo vya viongozi wakuu vilivyoshtua dunia:

 Ayatollah Ali Khamenei

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ya Ayatollah Ali Khamenei

Februari 28: Siku ya kwanza ya vita ilivyoangamiza uongozi wa juu

Viongozi wengi waandamizi wa Iran waliuawa katika siku ya kwanza ya vita, Februari 28, 2026. Mashambulizi hayo ya awali yalilenga moja kwa moja safu ya juu ya uongozi wa kijeshi na kisiasa wa nchi hiyo.

Miongoni mwa waliouawa ni Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei, pamoja na Katibu wa Baraza la Majeshi na mshauri wake wa usalama Ali Shamkhani, na Mkuu wa Majeshi Abdolrahim Mousavi. Vifo vya viongozi hawa vilionekana kuwa pigo kubwa kwa mfumo wa uongozi wa Iran.

Pia waliouawa ni Mkuu wa wafanyakazi wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) Mohammad Pakpour na Waziri wa Ulinzi Aziz Nasirzadeh, ambao walikuwa na nafasi muhimu katika kupanga na kusimamia operesheni za kijeshi za nchi hiyo.

Aidha, maafisa wengine wa juu waliopoteza maisha ni Brigedia Jenerali Mohammad Shirazi, Brigedia Jenerali Saleh Asadi, Meja Jenerali Mohsen Darehbaghi, Brigedia Jenerali Akbar Ibrahimzadeh na Brigedia Jenerali Hassan Ali Tajik, hali inayoonyesha ukubwa wa pigo lililopata uongozi wa kijeshi wa Iran katika siku ya kwanza ya vita.

Machi 3–10: Mashambulizi yaenea nje ya mipaka ya Iran

Abanya-Irani

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Baadhi ya maafisa wa Iran waliuawa katika shambulio lililotokea kwenye Hoteli ya Ramada mjini Beirut, Lebanon
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika siku zilizofuata, mashambulizi hayakuishia ndani ya Iran pekee, bali yalienea hadi nchi jirani kama Lebanon. Machi 3, Israel ilitangaza kumuua Seyid Majid Ibn al-Reza, ambaye alihusishwa na wizara ya ulinzi ya Iran, katika hatua iliyoonyesha kupanuka kwa uwanja wa vita.

Siku hiyo hiyo, kamanda wa Kikosi cha Quds, Reza Khazai, aliuawa katika shambulizi mjini Beirut. Kikosi cha Quds kinahusika na operesheni za nje ya Iran, hivyo kifo chake kilionekana kama pigo kwa shughuli za Iran nje ya mipaka yake.

Machi 10, mashambulizi makubwa yalifanyika katika hoteli moja Beirut ambapo viongozi kadhaa waliokuwa wakikutana waliuawa. Jeshi la Israel lilisema limewaua watu watano, akiwemo Alireza Bi-Azar na Ahmed Rasouli.

Wengine waliotajwa kuuawa ni Majid Hassani, aliyekuwa akisimamia fedha za Iran nchini Lebanon, pamoja na Hussein Ahmadlou na Abu Muhammad Ali. Iran, kwa upande wake, ilisema wanadiplomasia wake wanne pia waliuawa katika tukio hilo, jambo lililoongeza mvutano wa kidiplomasia.

Machi 14–19: Viongozi wa juu waliendelea kushambuliwa

Ali Larijani,

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Ali Larijani, mbunifu wa itikadi na usalama wa Iran naye ameuawa ndani ya siku 20 za vita

Kadri vita ilivyoendelea, mashambulizi yaliendelea kulenga viongozi muhimu zaidi wa usalama na kijeshi. Machi 14, Israel ilitangaza kumuua Abu Dar Mohammed, aliyedaiwa kuwa mkuu wa operesheni za makombora wa Hezbollah anayehusishwa na Iran.

Siku chache baadaye, Machi 17, Katibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Iran, Ali Larijani, aliuawa katika shambulizi la anga. Larijani alikuwa mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa, akiwa pia amewahi kuwa Spika wa Bunge kwa muda mrefu. Ndiye alikuwa mbunifu wa itikidadi na masuala ya usalama wa nchi hiyo.

Minisitiri w’ubutasi wa Irani Esmail Khatiba

Chanzo cha picha, IRNA

Maelezo ya picha, Waziri wa Ujasusi Esmail Khatib aliuawa

Katika tukio hilo hilo, kamanda wa Basij Gholamreza Soleimani pia aliuawa, tukio lililoongeza shinikizo kwa Iran kujibu mashambulizi hayo. Serikali ya Iran ikaapa kulipiza kisasi dhidi ya waliotekeleza mashambulizi hayo.

Machi 18, Israel ilitangaza kumuua Waziri wa Ujasusi Esmail Khatib, hatua inayodhihirisha kuwa mashambulizi yanalenga moja kwa moja mfumo wa ujasusi wa Iran.

Hata hivyo wachambuzi wanasema mfululizo huu wa mauaji unaweza kuongeza zaidi mvutano na kuifanya vita hiyo kudumu kwa muda mrefu zaidi.