Eid ul-Fitr: Sherehe hii ina umuhimu gani kwa waumini wa dini ya Kiislamu?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Sherehe za Eid ul-Fitr mwaka huu zitafanyika siku ya Ijumaa, tarehe 20 au tarehe 21 Jumamosi kwa mataifa mengine.

Sherehe hizi ni mojawapo wa sherehe muhimu katika kalenda ya Kiislamu, na huadhimisha kutamatika kwa mwezi wa Ramadhan.

Katika mataifa ya Afrika, Eid ul-Fitr husherehekewa na maombi, mlo, na utamaduni wa familia kujumuika pamoja.

Eid ul-Fitr ni nini?

Eid ul-Fitr inamaanisha "sherehe ya kumaliza mfungo" ni mojawapo wa sherehe muhimu pamoja na ile ya Eid ul-Adha.

Ni sherehe ya kumaliza mfungo, maombi na kumrejeshea mungu shukran na wakati na kuadhimisha umoja wa jamii.

Kidini, sherehe hizi zinaashiria kuwa mpya kiroho, msamaha na ukarimu kwa wasiojiweza.

Eid ul-Fitr sio Eid ul-Adha

Eid ul-Fitr husherehekewa mwisho wa mwezi wa Ramadhan ikiendana na mwezi wa tisa ya kalenda ya kiislamu.

Siku za sherehe hizi hubadilika kila mwaka kutokana na ni lini mwezi utaonekana mwanzo wa mwezi wa Shawwal.

Eid ul-Adha hufanyika miezi miwili baadaye katika kuhiji kule Mecca.

Inaadhimisha kujitolea kwa Abraham na ina utamaduni wa kuchinja mnyama kama kondoo,mbuzi au ngombe.

Eid ul-Fitr haijumuishi kuchinja mnyama. Kitovu cha sherehe hizo ni maombi, kuwasaidia wasiojiweza, na mlo.

Kwanini siku za Eid ul-Fitr hubadilika kila mwaka?

Kalenda ya kiislamu, ina miezi 12 ambazo huwa na siku 29 au 30, na huwa fupi kwa siku 11 ikilinganishwa na kalenda ya jua.

Kwa hivyo siku ya Ramadhan husonga mbele na siku 11 kila mwaka na inaweza kutokea msimu wowote.

Siku ya Eid ul-Fitr huamuliwa vipi?

Siku hii huamuliwa baada ya kuonekana kwa mwezi, ambayo huashiria mwanzo wa mwezi wa Shawwal unaofuata baada ya Ramadhan.

Iwapo mwezi utaonekana majira ya jioni, basi sherehe hizo zitafanyika tarehe 29 na iwapo mwezi hautaonekana, mfungo utaendelea hadi siku ya thelathini.

Kwa hivyo waislamu wanafaa kusubiri hadi jioni ya Eid ili kuwa na uhakika wa mwezi kuonekana.

Wanaofuatilia mwezi huanza kuangalia angani baada ya jua kutua siku ya 29 ya mwezi wa Ramadhan.

Tunasherehekea lini Eid ul-Fitr?

Siku za Eid ul- Fitr hazifanani kote duniani, ila huwa na utofauti wa siku moja au mbili.

Mwaka huu wa 2026 sherehe hizi zinatarajiwa kufanyika kati ya tarehe 20 hadi 21 mwezi Machi.

Kwa mfano, mamlaka nchini Saudi Arabia nchi yenye Waisunni wengi na waanzilishi wa uislamu hutangaza mwanzo na mwisho wa Ramadhani kulingana na ushuhuda wa wanaotazama mwezi kwa jicho la kawaida na wakati mwingine kwa msaada wa vifaa vya kisasa.

Waislamu kutoka mataifa mengine hufanya vivyo hivyo.

Lakini Iran, ambayo ina wananchi wengi wa Ki Shiite, wanafuata kile kinachotangazwa na serikali baada ya mwezi kuonekana kwa jicho la kawaida.

Iraq, ambayo nayo ina waislamu wengi wa Ki Shiite na wachache wa Ki Sunni, hutumia mchanganyiko wa maelezo mawili, Waishiite hufuata tangazo la mkuu wa kidini (awali alikuwa Ayatolla Khamenei), huku Wasunni wakifuata viongozi wa kidini nchini humo.

Ulaya, waislamu wengi hufuata maelekezo ya viongozi wao wa kidini, na pia hufuatilia uamuzi wa mataifa ya kiislamu.

Kinachofanyika siku ya Eid

Siku hiyo huanza kwa maombi ya pamoja.

Mapema asubuhi, waumini wa dini ya kiislamu hushiriki katika maombi ya pamoja yanayojulikana kama Salat al-Eid, yanayofanyika katika misikiti au maeneo ya umma.

Kutoa sadaka (Zakat ul-Fitr)

Kabla ya sala, Waislamu hutoa sadaka inayolenga kuwasaidia watu maskini ili kila mtu aweze kusherehekea sikukuu kwa heshima.

Chakula cha Eid

Mlo wa Eid ul-Fitr husherehekewa mwishoni mwa Ramadhani kwa karamu kubwa. Baada ya mwezi wa kufunga, chakula kizuri kinawakilisha furaha na thawabu ya kimungu. Inapendekezwa kushiriki mlo huo na familia na majirani, na kutoa chakula kwa wale wanaohitaji.

Kujumuika kwa familia

Watoto hupokea nguo mpya, zawadi, na wakati mwingine pesa.

Kutembeleana kama familia na kushiriki milo ya jamii ni kitovu cha sherehe hizi.

Waumini Waislamu huutakiana kila mmoja "Eid Mubarak" ("Eid Njema").

Eid ul-Fitr inasherehekewa vipi maeneo mengine duniani?

Ingawa sala ya asubuhi ndiyo muhimu kwa siku hiyo, utamaduni wa siku hii hubadilika kulingana na mila na desturi za taifa fulani.

Nchini Senegal, Eid mara nyingi huitwa Korité. Maelfu ya waumini hukusanyika kwa ajili ya sala ya asubuhi, mara nyingi hufanyika katika maeneo ya umma.

Siku hiyo huendelea kwa milo ya kifamilia,kuku, ng'ombe au kondoo hupewa kipaumbele, ikifuatwa na nafaka kama wali.

Familia hutembelea wazee, kuomba baraka zao na kuimarisha uhusiano wa kizazi hadi kizazi.

Nchini Nigeria, sala ya Eid huvutia umati mkubwa wa watu, hasa katika miji mikubwa ya kaskazini. Sherehe hii huadhimishwa kwa kuvaa nguo mpya aina ya (boubous) ambazo hutengenezwa mahususi kwa ajili ya sherehe hizo.

Familia hutayarisha vyakula kama wali wa jollof na suya (kebab zenye pilipili). Katika baadhi ya maeneo, sherehe hii huwavutia watu wengi wanaoshiriki katika mikutano ya kijamii na maonyesho ya kitamaduni.

Nchini Ivorian Coast, Eid ni wakati wa kukutana kwa familia. Familia hukusanyika kula vyakula vya wali vikichanganywa na michuzi mbalimbali wa kienyeji.

Watoto hununuliwa nguo mpya, kupewa zawadi, na pesa kuashiria furaha na urithi wa mila.

Nchini Chad, milo hujumuisha mihogo, wali, na nyama iliyochomwa. Kipaumbele ni umoja na ukarimu, ikizingatia maadili ya Ramadhani.

Misaada pia hutolewa kwa watu wasiojiweza, hii ni kutokana na ukarimu aliyojijingea mtu msimu wa Ramadhan.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula