Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mabaharia waliokwama karibu na Iran
- Author, Mohammad Zubair Khan
- Nafasi, BBC News Urdu
- Author, Aye Thu San
- Nafasi, BBC News Burmese
- Author, Hyojung Kim
- Nafasi, BBC News Korean
- Author, Andrew Webb
- Author, Grace Tsoi
- Nafasi, BBC World Service
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Droni, makombora na ndege za kivita zimekuwa jambo la kawaida kwa mabaharia wengi waliokwama kwenye meli za mafuta na meli za mizigo katika eneo la Ghuba.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la visa vya mashambulizi dhidi ya meli katika eneo la Ghuba, huku Iran ikijibu mashambulizi ya Marekani na Israel kwa kutishia kufyatulia risasi meli zozote zinazojaribu kuvuka Mlango Bahari wa Hormuz.
Mlango Bahari ni muhimu kwa meli, kwa ajili ya mafuta na vyombo vya kubeba bidhaa nyingine. Kuzuka kwa ghafla kwa vita kumeziacha meli nyingi - na mabaharia wao wakiwa wamekwama baharini huku wakitazama mashambulizi yanavyoendelea kwenye maeneo karibu na wao na yale ya juu ya anga.
"Nimeona ndege zisizo na rubani za Iran na makombora yakipaa kwenye mwinuko wa chini," anasema Amir, baharia wa Pakistani ndani ya meli ya mafuta katika Umoja wa Falme za Kiarabu ambayo haiwezi kuondoka eneo hilo. "Pia nasikia sauti za ndege za kivita, lakini hatuwezi kujua ni za nchi gani."
Kinachompa hofu zaidi ni ndege isiyo na rubani au kombora lililozuiwa kuangukia kwenye chombo chake.
Hein, baharia kutoka Myanmar, hushuhudia mapigano kila siku. "Asubuhi ya leo tu, ndege mbili za kivita zilifyatuliwa risasi tukiwa bado tunafanya kazi," anasema. "Hakuna mahali pa kujificha kwenye meli, na ilibidi tuingie ndani."
Tumebadilisha majina yao kuwa Amir na Hein, pamoja na yale ya mabaharia wengine baharini na familia zao, ili kulinda usalama wao.
Ingawa ni vigumu kupata takwimu sahihi ya idadi ya mabaharia waliokwama kwenye meli Mashariki ya Kati, Kapteni Anam Chowdhury, rais wa Chama cha Maafisa wa Baharini wa Merchant Marine wa Bangladesh, anakadiria kwamba idadi hiyo ni karibu 20,000.
Baadhi wako baharini na wengine wamekwama bandarini, lakini anasema ni vigumu kutathmini ni eneo gani hatari zaidi.
"Ndani ya bandari, watu wanaweza kudhani ni salama, lakini kumekuwa na meli ambazo zimeshambuliwa kwa mabomu zilipokuwa zimetia nanga," anaelezea.
Shirika lake limefuatilia angalau meli saba ambazo linasema zimeshambuliwa na makombora na kuharibiwa katika vita hadi sasa.
Anasema mnamo Machi 1, baharia aliuawa ndani ya meli ya Skylark, meli ya mafuta iliyosajiliwa na Jamhuri ya Palau.
Chowdhury anasema mabaharia walionusurika wameathiriwa na shambulizi hilo, ambapo chumba cha injini kilishika moto na wafanyakazi wakaondoka.
Kapteni M Mansoor Saeed anasafirisha meli za mafuta, na anaambia BBC News anaamini kwamba linapokuja suala la kuepuka mashambulizi, hakuna tofauti kubwa kati ya kuwa bandarini au baharini: "Ikiwa wanataka kulenga meli yangu watailenga tu."
Lakini, anasema, kwa ujumla meli kubwa zinaweza kuwa salama zaidi zikiwa mbali na pwani. "Katika hali mbaya ya hewa huwa tunakimbia baharini, ambapo tuna maji na kina zaidi cha kuendesha kwa uhuru. Katika bandari na maji yaliyofungwa, hali ya hewa inaweza kuharibu chombo kwa kutua au kugonga kuta za gati."
Uchanganuzi wa mawasiliano na urambazaji
Hali hiyo isiyotabirika imezifanya familia za mabaharia kuwa na wasiwasi.
Kwa sababu mamlaka nchini Iran zimefunga mitandao ya intaneti na simu kwa watu wengi nchini Iran, imekuwa vigumu kwa wanafamilia wa mabaharia kupata habari kuhusu mahali walipo. Ingawa wakati mwingine mawasiliano hurudi, haitabiriki na kwa kawaida ni kwa muda mfupi sana.
Mwana wa Ali Abbas yuko ndani ya meli katika bandari ya Iran karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz. Mara ya mwisho alizungumza na mwanawe siku kadhaa zilizopita, alipokuwa akimwambia kuhusu shambulio la kombora. Mwanawe alifanikiwa kutoroka, lakini baharia mmoja wa Kihindi alijeruhiwa.
"Nimemficha hili mke wangu na mkwe wangu," anasema huku akilia.
Jumanne usiku, kulikuwa na shambulio lingine kali bandarini na Ali hajaweza kuzungumza na mwanawe. "Kwa ajili ya Mungu, tafadhali nisaidie," anasema, huku akihuzunika. Ali anatumai mwanawe bado yuko hai na mzima wa afya, na kushindwa kwa mfumo wa mawasiliano ndio sababu ya ukosefu wa mawasiliano.
Seo-jun anaongoza boti yenye wafanyakazi zaidi ya 20 kutoka Korea Kusini na Myanmar. Anasema urambazaji wa satelaiti umekuwa mbaya - na kusababisha hatari zaidi.
"Tangu vita vianze, kuingiliwa kwa GPS kumetokea mara kwa mara, lakini hali imekuwa mbaya zaidi katika siku tatu au nne zilizopita," anasema.
Boti yao ilipoingia Dubai, mabaharia walilazimika kusafiri bila GPS.
"Kuna msemo wa Kikorea unaoeleza 'kama mtu kipofu anayehisi kitasa cha mlango," anasema.
Chakula kimepungua
Mbali na kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wao, mabaharia wengi wanaogopa kwamba maji na chakula vitaisha hivi karibuni.
Kwenye meli ya Seo-jun wana chakula cha siku 15, lakini maji ya kunywa yamekuwa haba kupatikana.
"Meli inaweza kuwa na maji safi kwa kuyasafisha na kuondoa chumvi maji ya baharini, lakini hilo linakuwa vigumu ikiwa hatusafiri," anasema.
"Tayari imepita miezi miwili tangu tupate mahitaji muhimu," anasema baharia wa Pakistani, Masood.
Kabla ya vita, Hein anasema ndani ya meli yake, chakula kilikuwa kinaandaliwa kisha wanajigawanyia wenyewe na wafanyakazi wangepata chakula kama mayai, na maji wakati wowote walipotaka.
Lakini sasa mfumo wa mgao umewekwa kwenye meli ya Hein na wanapata mlo mmoja tu wa vipande vinne vidogo vya nyama na bakuli moja la mboga za kukaanga kila siku. Vyakula vyao vitadumu kwa mwezi mmoja tu.
"Maisha yetu yanatia huruma na tuna mafuta na chakula kidogo sana," anasema baharia mwingine wa Pakistani, Zeeshan.
"Hakuna mtu anayeweza kuwa na furaha na amani katika hali hii," Amir anasema. "Tunajishughulisha na kazi za kawaida za kila siku. Mazoezi na mafunzo ya usalama."
Hein, ambaye anafanya kazi kama mhandisi mkuu kwenye meli, anakubali. "Sijiruhusu kukata tamaa kwa sababu ninasimamia wafanyakazi wengine 20 wa Myanmar."
Pia ameandaa mpango wa wakati wa dharura ikiwa hali itazidi kuwa mbaya. "Nimearifu timu yangu jinsi ya kukimbia, wapi pa kuruka na nini cha kubeba ikiwa chochote kitatokea."
Hakuna bima inayoweza kukurejeshea uhai wako
Hata kama mabaharia watafika nchi kavu baada ya meli zao kutia nanga katika bandari salama, huenda kusiwe na njia rahisi kwao kufika nyumbani au kuondoka katika eneo hilo.
Hamza anasema mwanawe, ambaye amekwama kwenye meli, ni miongoni mwa mabaharia "wasioruhusiwa kuondoka" kwa sababu kampuni zao zina pasipoti zao.
Wakati huo huo, mabaharia wenye hofu ambao hawatimizi mikataba yao kwa kuacha meli watapata shida kupata ajira za baadaye kwani kampuni za meli zinaweza kuwaorodhesha kwenye orodha ya wasiofaa kikazi.
Hali ni mbaya sana, na Amir anasema anaweza tu kutumainia mema na kuombea usalama wa mabaharia wote.
Pia anahimiza makampuni ya meli kutowalazimisha wafanyakazi wao kupita Mlango-Bahari wa Hormuz.
Hofu hizo ni za kufikirika, lakini ana wasiwasi kwamba shinikizo la kifedha linaweza kuzidi usalama. Anasema ikiwa chombo chochote kitashambuliwa na ndege isiyo na rubani au kombora, mabaharia ndio wanaolipa gharama kwa makosa ya kibinadamu, huku mizigo na meli zikiweza kulipwa na bima. "Maisha ya binadamu hayawezi kuwa na mbadala kwa bima yoyote," anasema.
Anaamini kwamba vita hivyo vitabadilisha pakubwa sekta ya ubaharia.
"Mtindo na madhumuni ya vita hivi ni tofauti sana na yale tuliyoyaona katika miaka michache iliyopita. Vita hivi vitakuwa na athari za muda mrefu kwenye biashara katika eneo la Ghuba ya Uajemi."
Chowdhury anaamini mabaharia wanajikuta katika matukio ambayo hawajukumiki nayo.
"Watu hawapaswikushambulia meli. Unaposhambulia meli, unashambulia pia mabaharia, ambao ni watu wasio na hatia," anasema.
Imefasiriwa na Asha Juma